ALHAMISI, SIKU YA 5 YA OKTAVA, KIPINDI CHA NOELI
DECEMBA 29
Somo: 1Yoh 2:3-11
Zab: 96:1-2a, 2b-3, 5b-6
Injili: Lk 2: 22-35
Nukuu:
“Na
katika hili twajua ya kuwa tumemjua yeye, ikiwa tunashika amri zake,” 1Yoh 2:3
“Lakini
yeye alishikaye neno lake, katika huyo upendo wa Mungu umekamilika kweli kweli.
Katika hili twajua ya kuwa tumo ndani yake,” 1Yoh 2:5
“Kisha,
zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa walikwenda naye
hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana, (kama
ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba
ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana),” Lk
2:22-23
“Nuru
ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli,” Lk 2:32
“Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama,
huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa
ishara itakayonenewa,” Lk 2:34
“Nawe
mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi,”
Lk 2:35
TAFAKARI:
“Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli. Huyu
amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi.”
Wapendwa
wana wa Mungu, kuishi katika Nuru ya kweli ni kuishi katika KWELI na HAKI. Hii
ndiyo mizania au kipimo halisi ndani na katika Kristo. Mizania hii hutuongoza
katika kuzishika amri zake kwa sababu tunajua kweli juu ya amri hizo na sababu
yake kuelekea umilele. Mizania hii hutupeleka zaidi kwa Kristo, kwani tu huru
katika kweli, Yoh 8:32. Na nuru hii ambayo ndiyo uwepo wa Kristo ndani yetu, ni
vita isiyo na kikomo dhidi ya giza.
Mkristo
amfuataye Kristo Yesu katika kweli na haki ni mtangaza vita dhidi ya mwanga na
giza, wema na uovu. Mtihani mkubwa ambao twapambana nao katika hali hii ni pale
wewe na mimi ‘ninapoishi upendo kati
yangu na Mungu, kati yangu na jirani, na kati yangu na Mazingira
yanayonizunguka.’ Hivyo huu ndio mwaliko wa kuwa chumvi na nuru katika
ulimwengu huu; “Ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika
itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na
watu. Ninyi ni nuru ya ulimwengu.
Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima,” Mt 5:13-14. Wote wale walio chumvi
na nuru katika ulimwengu huu kamwe Mungu hatovunja ahadi na mategemeo yao.
Hivyo
somo letu la kwanza na Injili, yanatutafakarisha juu ya maisha ya nuru ambayo
msingi wake ni kuishi katika kweli na haki. Kweli na haki hutuongoza kuzishika
amri za Mungu kwa uaminifu. “Na katika hili twajua ya kuwa
tumemjua yeye, ikiwa tunashika amri zake,” 1Yoh 2:3. Asiyeishi katika kweli na
haki ni vigumu kumwelewa Kristo aliye Haki na kweli. Hakika tutakuwa waongo
wakubwa. Hivyo, “Yeye asemaye,
Nimemjua, wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake,”
1Yoh 2:4. Kweli na haki hutuongoza
kwenye neno lake ambalo ndilo uzima. Huku ndiko kukamilika ndani na katika
Kristo Yesu. “Lakini yeye alishikaye neno lake, katika huyo upendo wa
Mungu umekamilika kweli kweli. Katika hili twajua ya kuwa tumo ndani yake,”
1Yoh 2:5.
Kukaa ndani na katika Kristo ni ukomavu
wa kiroho. Hatuendi kwake kwa shuruti
wala kulazimishwa mara tunapoutambua ukweli na nafasi ya Kristo ndani ya
maisha yetu. Tunaenda kwake kwa hiari yetu kwa sababu tunajua yeye ndiye kweli,
njia na uzima, Yoh 14:6. Hivyo, “Yeye asemaye ya kuwa
anakaa ndani yake, imempasa kuenenda mwenyewe,” 1Yoh 2:5. Ukomavu wa Imani
ambao ni nuru chini ya msingi wa kweli na haki utuweka karibu sana na Kristo
Yesu. Hivyo kila tunayekutana naye twamwona Kristo ndani yake. Hivyo hatuwezi
kamwe kuishi katika chuki na yeyote yule kwa sababu twaishi katika nuru ya
kweli. “Yeye asemaye kwamba yumo nuruni, naye amchukia ndugu yake, yumo gizani,”
1 Yoh 2:9. Kuishi katika chuki yamaanisha kwamba bado hujakutana na Kristo, na
hivyo bado u gizani.
Matumaini yetu kama binadamu, ingawa hatujui
ni lini yatakuwa kweli, Mungu hawezi kuyasahau kwani twaishi kile
tunachokiamini katika kweli na haki. Injili ya leo inatupa mfano ulio hai wa
yule aliyeishi katika nuru ya kweli chini ya msingi wa kweli na haki. Huyu
ndiye Simeoni.
Simeoni anakutana na
nuru hii ya kweli na haki wakati Yesu anapotolewa hekaluni kama ilivyo desturi
ya Wayahudi kwa kila mzaliwa wa kwanza wa kiume. “Kisha,
zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa walikwenda naye
hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana, (kama
ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba
ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana),” Lk
2:22-23. Hata hivyo, kumkomboa huyu mzaliwa wa kwanza kutoka
hekaluni iliwapasa wazazi wake kumtolea Bwana sadaka kama shukrani. “Wakatoe na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya
Bwana, Hua wawili au makinda ya njiwa wawili,” Lk 2:24. Sadaka hii inaonyesha
umasikini wa Familia hii Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu.
Ni
katika tendo hili pale Hekaluni, Simeoni mtu wa kweli na haki ahadi yake
inatimizwa na Mungu. “Na tazama, pale
Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha
Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake,” Lk
2:25. Yesu Kristo hapa ndiye nuru halisi na
uhuru wa kweli wa wana wa Taifa la Mungu. Kristo ndiye ile nuru aliyokuwa ikisubiriwa, “Nuru
ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli,” Lk 2:32.
Mungu anaifunua nuru
ya Yesu ndani ya moyo wa Simeoni naye anayaona makuu ndani ya Yesu: “Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama,
huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa
ishara itakayonenewa,” Lk 2:34. Kristo ndiye sababu ya kuanguka na kuinuka
wengi, kwa sababu ulimwenguni hapa ni vita dhidi ya mwanga ambaye ndiye Kristo,
na giza ambayo ndiye yule mwovu shetani. Watainuliwa wale watakaoambatana na
mwanga na wataangushwa wale waambatanao na giza, yaani yule mwovu.
Katika
vita hii Mama Bikira Maria hatakuwa salama katika maana ya kufurahia tu uwepo
wa mwanaye. Ni katika uchungu na kushiriki mateso ya mwanaye nuru ya kweli na
haki itafunuliwa ndani yake. Hivyo ni katika msalaba ambao mwanaye anauendea
ndipo utakapokuwepo utukufu wake. “Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako,
ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi,” Lk 2:35. Kwenye Msalaba Mtakatifu na
wenye ushindi wa Bwana Yetu Yesu Kristo ndipo penye Utukufu, kufunguliwa kwa
mioyo yetu kutoka utumwa wa dhambi, na kuuelekea uzima wa milele. Ndugu yangu,
mimi ninao wangu Msalaba. Nawe unao wako Msalaba. Chunguza vizuri. Upo. Hivyo
kwa Mkristo na Mfuasi wa Kristo, hakuna UTUKUFU pasipo MSALABA.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Atamkaye maneno ya kweli hufunua haki; Bali shahidi wa uongo
hutamka hila. Nuru ya mwenye haki
yang'aa sana; Bali taa ya mtu mbaya itazimika,” Mit 12:7, 13:9
Tusali: Ee Yesu
uliyeushinda Msalaba na kuniweka huru, nijalie nami niushinda wangu msalaba ili niurithi uzima wa milele.
Amina
Mungu ni mwema
ResponderEliminar