JUMANNE WIKI YA 3
YA MAJILIO
Somo: Sef 3:1-2, 9-13
Zab: 34:2-3, 6-7, 17-18, 19, 22
Injili: Mt 21:28-32
Nukuu:
“Siku ile hutatahayarikia matendo yako yote uliyoniasi; maana
hapo nitawaondoa watu wako wanaotakabari na kujivuna, wasiwe kati yako, wala
hutatakabari tena katika mlima wangu mtakatifu,” Sef 3:11
“Lakini nitasaza ndani yako watu walioonewa na maskini, nao
watalitumainia jina la Bwana,” Sef 3:12
“Mabaki ya Israeli hawatatenda uovu, wala kusema uongo; wala
ulimi wa hadaa hautaonekana kinywani mwao; kwa maana watakula na kulala, wala
hapana mtu atakayewaogofya,” Sef 3:13
“Basi
Yesu akawaambia, Amin nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanatangulia mbele
yenu kuingia katika ufalme wa Mungu,” Mt 21:31b
“Kwa sababu Yohana alikuja kwenu kwa njia ya haki, ninyi
msimwamini; lakini watoza ushuru na makahaba walimwamini, nanyi hata mlipoona,
hamkutubu baadaye, ili kumwamini,” Mt 21:32
TAFAKARI: “Watoza ushuru na makahaba
wanatangulia mbele yenu kuingia katika ufalme wa Mungu.”
Wapendwa
wana wa Mungu, kutangulia au kuchelewa kwa kuwa na ufahamu wa Mungu hakuna
maana yoyote kama katika tendo hilo hatutimizi mapenzi ya Mungu. Mfano alioutoa
Yesu kwenye Injili ya leo unathibitisha ukweli huo niliousema. Mtoto wa kwanza
katika familia ile aliambiwa na Baba yake kwenda kufanya kazi shambani
akakubali hata hivyo hakwenda. Mtoto wa pili alikataa kwenda kufanya kazi
shambani, ila baada ya kujifikiria akafanya toba na kwenda kufanya kazi
shambani. Mtoto huyu wa pili anawakilisha watoza ushuru na makahaba ambao kwa
uhakika kwa kutubu kwao kadiri ya Injili ya leo wataingia katika ufalme wa
Mungu.
Watoza
ushuru na Makahaba hawakuwa na mwono mzuri nyakati zile za Yesu kutokana na
matendo yao. Watoza ushuru walichukiwa sana kutoka na kodi waliyoitoza ambayo
kwa kiasi kikubwa haikuhakisi maisha ya watu. Ilikuwa kodi ya dhuluma na
iliyojaa unyanyasaji hasa kwa wanyonge. Makahaba hawakupendwa kutokana na
mtindo wa maisha yao. Kwa ujumla makahaba walionekana kuwa najisi kabisa, na
wachafu kupindukia. Kumbe kwa kutubu kwao bado wananafasi ya kuhesabiwa haki na
Mungu. Na hii ndiyo sababu ya Yesu kuyasema maneno haya, “Amin nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanatangulia mbele
yenu kuingia katika ufalme wa Mungu,” Mt 21:31b.
Yesu
hayasemi maneno haya kwa Wakuu wa Makuhani, Waandishi, na Mafarisayo kwa
kuwasingizia, bali hali halisi ilijionyesha pale walipojiinua kupita kiasi na
hata kuchukua nafasi ya Mungu. Watu hawa walionekana kama miungu watu. Walikuwa
wepesi kusema maneno mengi na mazuri bila wao wenyewe kutenda. Hakika walikuwa
wanafiki sana. Yesu anasema, “Waandishi na
Mafarisayo wameketi katika kiti cha Musa; basi,
yo yote watakayowaambia, myashike na kuyatenda; lakini kwa mfano wa matendo
yao, msitende; maana wao hunena lakini hawatendi,” Mt 23:2-3.
Mtazamo
huu wa Dini ulipoteza msingi wake ambao ni maisha kuelelea uzima wa milele. Kila
kitu kilionekana kubeba mitazamo ya kibinadamu na kusahau kwamba yote bila
Mungu ni ubatili mtupu. Ni kwa maana hiyo basi siku ya mwisho mimi na wewe
tutapigwa mshangao kama asemavyo Yesu, “ Yohana alikuja kwenu kwa njia ya haki,
ninyi msimwamini; lakini watoza ushuru na makahaba walimwamini, nanyi hata
mlipoona, hamkutubu baadaye, ili kumwamini,” Mt 21:32. Ni vyema
kila mmoja wetu akachunguza njia zake na mahusiano yake na Mungu.
Wapendwa wana wa Mungu,
ufuasi wetu kwa Kristo siyo kitu cha majaribu. Jambo hili halina lelemama. Ni
aheri kuwa baridi au joto kuliko kuwa vuguvugu katika imani ndani na katika
Kristo. Yesu anaweka wazi kweli iliopo tunapotaka kumfuata na kuwa wanafunzi
wake. Mambo yalikuwa kama ifuatavyo; “Mwingine katika
wanafunzi wake akamwambia, Bwana, nipe ruhusa kwanza, niende nikamzike baba
yangu. Lakini Yesu akamwambia,
Nifuate; waache wafu wazike wafu wao,” Mt 8:21-22. Ufuasi wetu ndani na katika
Kristo utasababisha wakati mwingine kuachana na mazoea yaliyojengeka kadiri ya
mila na desturi zetu.
Kumfuata
Kristo ni kufuata utamaduni mwingine usio wa kawaida. Hakuna mfananano wa
tamaduni nyingine za kibinadamu. Na hakuna tamaduni au mila fulani inayoweza kujigamba kwamba kwayo ni zoefu katika
tamaduni hii mpya ya Kristo. Sote tu wanafunzi wa Yesu hadi kifo. Kila siku ni
siku ya kujifunza yaliyo mapya anayotufunulia Kristo mwenyewe. Yesu analisema
hili kama ifuatavyo: “Mtu mwingine pia akamwambia, Bwana, nitakufuata;
lakini, nipe ruhusa kwanza nikawaage watu wa nyumbani mwangu. Yesu akamwambia, Mtu aliyetia mkono
wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu,” Lk 9:61-62.
Hivyo ni kuanza upya na Kristo, na kuwa wapya kila siku tunapoongozana naye.
Ufuasi
huu unatulazimu kwa hiari yetu kuyakabidhi yote mikononi mwa Kristo. Hatuendi
kwake nusunusu na kubaki na yaliyo yetu. Kumfuata Yesu ni kujisalimisha bila
kujibakiza. Yesu anasema, “Wala mtu
asiyechukua msalaba wake akanifuata, hanistahili. Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza;
naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona. Mt 10:38-39. Kumbe
sharti la kwanza tena la hiari ni kuchukua msalaba wako, yaani, kuyajua
madhaifu yako na kuyachukua kama sehemu muhimu ya kuupata wokovu wako utakapo
yashinda ndani na katika Kristo. Pili, kujiachia kwa Kristo bila kujibakiza ili
kuiona nafsi yako.
Ufuasi huu pia unatutaka kuishi katika mfumo wa moja na
ibaki kuwa moja, katika maana ya kujua ni nani hasa upasaye kumtumikia. Hapa
Michanganyo hairuhusiwi hata kidogo. Kweli na uongo hapa haviivi chungu kimoja.
Hivyo Yesu anasema, “Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana
atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu.
Hamwezi kumtumikia Mungu na mali,” Mt 6:24. Kumbe kumfuata Yesu yakupasa kuamua
kati ya haya yanayoonekana na kushikika ila ni ya muda tu, au kisichoonekana
kwa urahisi na kisichoshikika ila kina uzima wa milele.
Ufuasi huu unatulazimu kutobandukana na Kristo hadi mwisho
wa kiama. Kumbe ufuasi wangu usiwe ule wa jumapili tu na matukio mengine ya
Kanisa. Siku zote na majira yote yanipasa kuishi ndani na katika Kristo. Naye
Yesu anasema, “Mtu ambaye si pamoja nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya
pamoja nami hutawanya,” Lk 11:23. Kumbe kuwa Mkristu wa jina tu bila kuishi
ahadi zako za ubatizo, ukristo wako hauna maana yoyote wala faida yoyote. “Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka;
watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea,” Yoh 15:6. Hatuna uzima wa
kiroho bila kuwa ndani na katika Kristo Yesu. Hatuwezi pia kukua kiroho na
kimwili kama hatuna muunganiko ndani na katika Kristo Yesu.
Wapendwa
wana wa Mungu, huyu ndiye Masiha tunayemsubiri. Ujio wake watupasa kuwa tayari,
yaani katika hali isiyo ya dhambi. Leo yako isisubiri kesho ili ujiandae. Kesho
hiyo hujaifikia, na jana yako ilishapita bila kufanya chochote. Hivyo, “Siku ile hutatahayarikia matendo yako yote uliyoniasi;
maana hapo nitawaondoa watu wako wanaotakabari na kujivuna, wasiwe kati yako,
wala hutatakabari tena katika mlima wangu mtakatifu,” Sef 3:11. Aliyejiandaa
ndiye atakaye kuwa mikono salama ya Mungu. Kundi
hili ni lile la wenye hofu ya Mungu, Masikini na walioonewa. “Lakini
nitasaza ndani yako watu walioonewa na maskini, nao watalitumainia jina la
Bwana,” Sef 3:12
Wenye hofu ya Mungu na wanyenyekevu wa moyo, hawana woga wala
hofu kwa sababu maisha yao yapo mikononi mwa Mungu. Nabii Sefania anawataja
watu hawa kwa kusema, “Mabaki ya Israeli hawatatenda uovu, wala kusema uongo;
wala ulimi wa hadaa hautaonekana kinywani mwao; kwa maana watakula na kulala,
wala hapana mtu atakayewaogofya,” Sef 3:13. Hawa wanajua ni nani
wanayemtumikia. Mungu huyu wa kweli na hai hatotuangusha kamwe tunapojitoa
kwake bila kujibakiza. Ndugu yangu tuliye safiri wote katika tafakari hii, Hakika hakuna lisilowezekana kwa Mungu! Yote yawezekana kwa
IMANI.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Mwe
na hofu wala msitende dhambi, Tafakarini vitandani mwenu na kutulia,” Zab 4:4
Tusali:-Ee Yesu Mwema na Mwokozi wangu, usijitenge nami hata katika
udhaifu wangu. Nakupenda Mungu wangu na yote yangu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario