domingo, 25 de diciembre de 2016

TAFAKARI: SIKUKUU YA MT. STEFANO SHAHIDI


Sikukuu ya Mt. Stefano Shahidi

DECEMBA 26

Somo: Mdo 6:8-10, 7:54-60

Zab: 31:3cd-4, 6, 8ab, 16bc, 17

Injili: Mt 10: 17-22

Nukuu:

“Basi waliposikia maneno haya, wakachomwa mioyo, wakamsagia meno,” Mdo 7:54 

 Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu, Bwana, usiwahesabie dhambi hii. Akiisha kusema haya akalala. Na Sauli alikuwa akiona vema kwa kuuawa kwake,” Mdo 7:60

“Jihadharini na wanadamu; kwa maana watawapeleka mabarazani, na katika masinagogi yao watawapiga,” Mt 10:17

“Lakini hapo watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema,” Mt 10:19

“Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu,” Mt 10:20 

TAFAKARI: “Waliposikia maneno haya, wakachomwa mioyo, wakamsagia meno.” 

Wapendwa wana Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Mt. Stefano Shahidi wa kwanza aliyemfia Kristo kadiri ya mapokea ya Kanisa. Shahidi Stefano alikuwa kati ya wale  saba waliochanguliwa, Mdo 6:5,  na Mitume ili kusaidia utowaji wa huduma kutokana na ongezeko la wanafunzi/wafuasi wa Kristo, na manung’uniko ya wayahudi wa Kiyunani juu ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahaulika katika huduma, Mdo 6:1. Hivyo ili kuendelea na kazi ya kulihubiri neno la Mungu, Wale Thenashara wakawaita jamii ya wanafunzi, wakasema, Haipendezi sisi kuliacha neno la Mungu na kuhudumu mezani,” Mdo 6:2

Shahidi Stefano alikuwa mtu aliyejaa Imani na Roho Mtakatifu. Hata pamoja na huduma aliyochaguliwa kuifanya, alilihubiri neno la Mungu kwa ufasaha. Stefano Shahidi hakupindisha ukweli, na alisema lililo kweli mbele ya Mungu na mbele ya macho ya watu. Stefano alionyesha wazi kupotoka kwao Wayahudi na kile walichomfanyia Yesu na kuutoa uhai wake. Hakika maneno na mafundisho yake yalikuwa kama upanga mkali uliopenyeza ndani ya mioyo ya watu.

Watesi wake Shahidi Stefano hawakuweza kuvumilia hali ile na hasa maneno yake ya kuchoma. Kwa hali hii ndipo walipomtungia uongo na kuwasimamisha mashahidi wa uongo ili wamteketeze kama walivyo fanya kwa Bwana wetu Yesu Kristo. “Wakasimamisha mashahidi wa uongo waliosema, Mtu huyu haachi kusema maneno ya kufuru juu ya mahali hapa patakatifu na juu ya torati; maana tumemsikia akisema kwamba Yesu huyo Mnazareti atapaharibu mahali hapa, na kuzibadili desturi tulizopewa na Musa,” Mdo 6:13. Kwa ushahidi huu wa uongo na wakusuka, uliamsha hasira za watu katika sinagogi na kusababisha Stefano kutolewa nje, kisha kushushiwa mvua ya mawe baada ya kuvuliwa nguo na kukabidhiwa Sauli ambaye leo ndiye Mtume Paulo.

Mambo yalikuwa hivi huko ndani ya sinagogi baada ya ushahidi ule wa uongo, “Wakapiga kelele kwa sauti kuu, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja, wakamtoa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa kijana mmoja aliyeitwa Sauli,” Mdo 7:57-58. Hivyo kwa tendo hili, Stefano alikufa kama shahidi mfiadini wa kwanza katika historia ya Kanisa. Kwa damu yake ilitoa ushahidi wa upendo wake na Imani kwa Kristo Yesu.

Akiwa katika hali hii ya mateso makubwa mbingu zinafunguka na huko anamwona Mwana wa Adamu. “Akasema, Tazama! Naona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adamu amesimama mkono wa kuume wa Mungu,” Mdo 7:56. Mahangaiko na mateso yake hayakuwa sababu ya kumwasi Kristo. “Wakampiga kwa mawe Stefano, naye akiomba, akisema, Bwana Yesu, pokea roho yangu,” Mdo 7:59 .Vile vile Stefano hakuchukua nafasi hii ya mateso na mahangaiko yake kuwalaumu watesi wake zaidi ya kuwaombea. “Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu, Bwana, usiwahesabie dhambi hii. Akiisha kusema haya akalala. Na Sauli alikuwa akiona vema kwa kuuawa kwake,” Mdo 7:60. Huku ndiko kufa kifo shahidi na dini, na damu yake ilipelekea kukua kwa Imani na uthabiti wa Kanisa la Mwanzo.

Majaribu, Mateso, na Mahangaiko aliyoyapata Stefano yawezekana kwa namna fulani na nyakati fulani umefikwa nayo ila kwa kiwango tofauti. Swali ni hili: Je, katika nyakati hizo umefanya kufuru kwa kumwasi Kristo? Je, umetumia nafasi hiyo kutoa lawama na hata kuwalaani watesi wako? Na mwisho, katika hali hii ya majaribu, mateso, na mahangaiko umetumia nafasi hiyo kujiombea, na kuwaombea watesi wako wapate wokovu? Bila shaka kabisa matokeo ya sala njema na yenye dhamiri njema ya Stefano ilikuwa nguvu ya wokovu kwa Sauli ambaye tunaambiwa alishuhudia kuuawa kwake, Mdo 7:60b. Tuishi mara zote tukiwa na hofu ya Mungu, na tuepuke mara zote kutoa na kushuhudia  uongo.

Injili ya leo inaweka bayana yatakayojiri pale tunapoamua kwa dhati kuambatana na Kristo, na kuishi kwa ajili yake. “Jihadharini na wanadamu; kwa maana watawapeleka mabarazani, na katika masinagogi yao watawapiga,” Mt 10:17.  Vile vile Injili inaweka bayana kabisa kwamba atakayeambatana na Kristo na kuishi kwa ajili yake, Kristo hatomwacha kamwe. “Lakini hapo watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema. Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu,” Mt 10:19-20. Hivyo hatuna sababu na wala kuwa na hofu tunaposema na kusimama katika kweli. “Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru,” Yoh 8:31b-32 

Kuwa mfuasi wa Kristo ni kutangaza vita vya mwanga dhidi ya giza. Hivyo kusalitiwa na kusalitiana ni mazingira halisi ya kufa kifo dini kila siku. Tendo hili mbaya zaidi hufanyika na wale tunaowajua na wakati mwingine ni ndugu zetu wa damu. “Na ndugu atamsaliti nduguye ili auawe, na baba atamsaliti mwana, na wana watawainukia wazazi wao, na kuwafisha,” Mdo 10:21. Kumfuata Kristo kwa uaminifu ni sababu pia ya kuchukiwa na wale wapendao giza, yaani, watendao matendo maovu na kinyume na Kristo.

Hata hivyo, shinda yetu, okoka yetu, na salama yetu katika hali hii ni uvumilivu ndani na katika Kristo hadi mwisho. “Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka,” Mt 10:22. Je, ndugu yangu tuliyesafiri wote katika tafakari hii, unayo misuli ya Imani ya kuyashinda majaribu haya? Usihofu! Mtazame kwa Imani yule waliyemtundika, Kristo Yesu Mshindi.

Tumsifu Yesu Kristo! Mt. Stefano Shahidi, Utuombee

Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili,” 1Kor 10:13

Tusali: Ee Yesu Mwema, tujalie Imani na ujasiri wa kusimama katika kweli na haki hata pale itakapotugharimu uhai wetu. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario