miércoles, 14 de diciembre de 2016

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 3 YA MAJILIO


IJUMAA WIKI YA 3 YA MAJILIO

Somo: Isa 56:1-3a, 6-8

Zab: 67:2-3, 5, 6-7

Injili: Yoh 5:33-36

Nukuu:

“Ninyi mlituma watu kwa Yohana, naye akaishuhudia kweli,” Yoh 5:33

 “Lakini ushuhuda nilio nao mimi ni mkubwa kuliko ule wa Yohana; kwa kuwa zile kazi alizonipa Baba ili nizimalize, kazi hizo zenyewe ninazozitenda, zanishuhudia ya kwamba Baba amenituma,” Yoh 5:36

“Bwana asema hivi, Shikeni hukumu, mkatende haki; kwa maana wokovu wangu u karibu kuja, na haki yangu kufunuliwa,” Isa 56:1

 “kila aishikaye sabato asiivunje, na kulishika sana agano langu; Nitawaleta hao nao hata mlima wangu mtakatifu, na kuwafurahisha katika nyumba yangu ya sala; makafara yao na dhabihu zao zitakubaliwa juu ya madhabahu zangu; kwa maana nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote,” Isa 56:6b-7

TAFAKARI: “Kila aishikaye sabato asiivunje, na kulishika sana agano langu; Nitawaleta hao nao hata mlima wangu mtakatifu, na kuwafurahisha katika nyumba yangu ya sala,” Isa 56:6b-7a.

Wapendwa wana wa Mungu, masomo yetu ya leo yanatupa msingi wa kile tuaminicho na malengo yetu kama wafuasi wake Kristo. Kwa wewe uliye Mkristo, uzima na ufufuo wako hauwezekani pasipo kuwa ndani ya Kristo na katika Kristo. Wayahudi hawaukubali ukweli huu, na badala yake wanamdhihaki Yesu Kristo kwa kutokuamini kwao. Naye Yesu anawakumbusha na kusema, “Ninyi mlituma watu kwa Yohana, naye akaishuhudia kweli,” Yoh 5:33. Na kweli hiyo ndiyo hii: “Nendeni mkamweleze Yohana mnayoyasikia na kuyaona; vipofu wanapata kuona, viwete wanakwenda, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa habari njema,” Mt 11:4-5.

Yohana Mbatizaji alikuwa mwandaa njia ya nuru ile kamili, ambaye ndiye Neno aliyefanyika mwili na kukaa kwetu, Yoh 1:14. Na huyu Yohana Mbatizaji katika kazi hii ya uandaaji njia, ndiye Yesu anayemsemea kwamba, “Yeye alikuwa taa iwakayo na kung'aa, nanyi mlipenda kuishangilia nuru yake kwa muda,” Yoh 5:36. Jambo la ajabu ni kwamba ile nuru kamili, ambayo ndiye Kristo Yesu-NENO, Wayahudu hawataki kuiona.  Yohana Mbatizaji “hakuwa ile nuru, bali alikuja ili aishuhudie ile nuru. Kulikuwako Nuru halisi, amtiaye nuru kila mtu, akija katika ulimwengu. Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua,” Yoh 1:8-10.

Kristo Yesu ndiye Nuru Kamili “kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema. Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo. Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua,” Yoh 1:16-18.  Ukweli huu ndio wasioutaka kuusikia Wayahudi na wale wote wampinga Kristo ambao wafunua kweli hiyo juu ya Kristo na upendo wa Mungu katika safari nzima ya historia hii ya wokovu.

Yesu anasema mshitaki wao mkuu ni kazi zake, na yale yote yasemwayo katika Maandiko Matakatifu. Na kazi zake haziitaji ushududa wowote wa wanadamu ili kusadifu kwamba ni Mungu. Kazi zake zimepita uwezo na ufahamu wa mwanadamu. Hivyo Yesu anasema, “mimi siupokei ushuhuda kwa wanadamu; walakini ninasema haya ili ninyi mpate kuokoka,” Yoh 5:34. Lengo la hayo yote, yaani, ishara hizo ni kukupata wewe na mimi. “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake,” 2Kor 8:9. Huu ni upendo na unyenyekevu mkubwa alioufanya Mungu kwa ajili yako na yangu, yaani, kujikatalia yote ili akupate mwili na roho. Mungu hakuhitaji kufanya hivyo kwa sababu hapakuwa na shinikizo lolote lile la kutuumba sisi wanadamu zaidi ya furaha na upendo wake.

 Ndugu yangu tunaye safari sote katika tafakari hii, swali la kujiuliza ni hili; pamoja na kweli hiyo, ni yapi mapaswa yetu ili tubaki katika mikono salama ya Mungu? Kwa vile lengo ni kukupata wewe na mimi mwili na roho, Mungu kwa kupitia Mtumishi wake Nabii Isaya anatuambia hivi, “Shikeni hukumu, mkatende haki; kwa maana wokovu wangu u karibu kuja, na haki yangu kufunuliwa,” Isa 56:1. Wokovu huu ambao u karibu kuja ni NENO huyo atakayefanyika mwili na kukaa kwetu, Yoh 1:14, na kwa namna ya pekee kabisa yakupasa ukubali kwa kuachilia hatia zote ndani mwako ili NENO huyu afanyike mwili ndani mwako.

Huyu NENO ni Mfalme wa Amani, Haki, Kweli, Huruma, Upendo, Msamaha, Unyenyekevu, na Mwenye kujikataliya yote ili akupata mwili na roho. Hivyo ili ayaweke makazi yake kwako na kwangu, yatupasa kuwa watu wa haki, na watenda haki. Ni kutumia vizuri madaraka tuliyopewa na umma kwa mujibu wa Katiba na taratibu zake husika. Madaraka yako na cheo chako visiwe fimbo ya kuwachapa wengine kwa sababu tu hamuendani kiimani, au kiitikadi, au kimitazamo. Nafasi uliyonayo ni alama ya Umoja, na ndiyo moja ya sifa kuu  ya Utatu Mtakatifu, yaani, Umoja usiogawanyika. Katika kweli hii Mungu anasema, “Heri afanyaye haya, na mwanadamu ayashikaye sana; azishikaye sabato asizivunje, auzuiaye mkono wake usifanye uovu wo wote,” Isa 56:2. Cheo, nafasi yako katika jamii, na  kadiri ya wito wako ni DHAMANA na WAJIBU.

Na furaha ya Mungu kwetu ni nguvu ile ya Upendo ndani mwetu yenye kutuleta katika umoja ule wa Kimungu, yaani, Utatu Mtakatifu-UKAMILIFU. Na kufikia ukamilifu huu Mungu hatulazimu kuishi katika hali ya ubunifu, yaani, nje ya ubinadamu wetu na kuwa kitu kingine. Ilimpendeza Mungu tuwe kama tulivyo, na ndiyo maana kwa furaha na pasipo shuruti alituumba kama tulivyo, yaani, kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27. Kumbe yale yote tuliyokubaliana kwa pamoja na kwa faida ya kila mmoja tuyaheshimu kama ilivyokuwa siku ya sabato kwa Wayahudi bila kuingiza mambo yetu binafsi kwa malengo binafsi. Na hii ndiyo maana ya maneno haya ya Mungu; “kila aishikaye sabato asiivunje, na kulishika sana agano langu; Nitawaleta hao nao hata mlima wangu mtakatifu, na kuwafurahisha katika nyumba yangu ya sala; makafara yao na dhabihu zao zitakubaliwa juu ya madhabahu zangu; kwa maana nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote,” Isa 56:6b-7. Je, katika hili tupo salama? Tafakari!

Tumsifu Yesu Kristo!

“Lakini ushuhuda nilio nao mimi ni mkubwa kuliko ule wa Yohana; kwa kuwa zile kazi alizonipa Baba ili nizimalize, kazi hizo zenyewe ninazozitenda, zanishuhudia ya kwamba Baba amenituma,” Yoh 5:36

Tusali:-Ee Yesu na Kiongoze wetu, tukumbushe mara zote cheo ni dhamana na wajibu. Amina

 

No hay comentarios:

Publicar un comentario