SIKUKUU YA BIKIRA MARIA MKINGIWA DHAMBI YA ASILI
Desemba 8
Somo I: Mwa 3:9-15, 20
Zab: 98:1, 2-3ab, 3cd-4
Somo II: Efe 1:3-6, 11-12
Injili: Lk 1:26-38
Nukuu:
“Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye
aliyenipa matunda ya mti huo, nikala,” Mwa 3:12
“Bwana Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo,
umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni;
kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako,” Mwa 3:14
“kama vile
alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe
watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo,” Efe 1:4
“Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya
Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake,” Efe 1:5
“Malaika
akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu,” Lk 1:30
“Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake
utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu
atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake,” Lk 1:31-32
TAFAKARI:
“Mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema.”
Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, leo Mama Kanisa
anaadhimisha Sikukuu ya Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya Asili. Basi katika
tafakari hii ya leo ili tuelewe fumbo hili ni vyema kujiuliza maswali
yafuatayo; Ni kwa nini Bikira Maria akingiwe dhambi ya Asili? Kabla ya kujibu
swali hili, ni vyema kujua dhambi ya Asili ni nini? Kadiri ya Maandiko
Matakatifu hasa tuliyoyasoma kutoka somo la kwanza, na mafundisho ya Kanisa,
dhambi hii ya asili ni mwelekeo wa kutenda dhambi ambao chanzo chake ulitokana
na anguko la wazazi wetu wa kwanza, yaani Adamu na Hawa.
Je, pamoja na anguko hili hatukuweza kurudi na
kuuchuchumilia Utakatifu? Jibu ni kwamba tunaweza. Ukweli ni kwamba licha la
anguko hili la wazazi wetu wa kwanza, Mungu hakutuondolea ili hali ya uhuru
ndani mwetu. Hivyo basi, ni kwa kupitia uhuru huu twaweza kumrudia Mungu kwa
njia ya toba na majuto, na vile vile kwa uhuru huu pia twaweza kuasi kabisa. Ni
nini basi kilitokea kule Bustanini Edeni kati ya Adamu na Hawa?
Wapendwa wana wa Mungu, ni kweli kwamba mahali popote
anapoishi zaidi ya mtu mmoja kuna kautaratibu kake ili mawasiliano yaende
vizuri. Utaratibu huu unaweza kuwa kimaandishi, au kimapokea katika hali ya
kuaminiana na kujenga mazoea ya kuishi katika misingi hiyo. Hivyo Mungu
alivyomuumba Adamu na kumpatia msaidizi wake, yaani, Hawa. “Bwana Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke
yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye. Bwana
Mungu akamletea Adamu usingizi mzito, naye akalala; kisha akatwaa ubavu wake
mmoja, akafunika nyama mahali pake, na
ule ubavu alioutwaa katika Adamu Bwana Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa
Adamu,” Mwa 2:18,21-22.
Mungu aliwapa mahali pa kuishi na mahali hapo palijulikana
kama bustani ya Edeni. Mungu aliwapa utaratibu wa kuishi mahali hapo kadiri ya
mpango wake mwenyewe ili uzima uwepo ndani yao milele na kuepuka kifo. “Bwana Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema,
Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula, walakini
matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula
matunda ya mti huo utakufa hakika,” Mwa 2:16-17.
Makatazo haya yanajenga udadisi na ushawishi wa yule mwovu
shetani. Hii ndiyo dhambi ile ya tamaa, ambayo hutujengea hali ya kutojipokea
na kutoridhika kwa kile tulicho. Shetani kwa umbo la nyoka anatumia mwanya huu
kumshawishi Eva. Dhambi hii inashirikishwa kwa wote wawili, yaani, Hawa an
Adamu. Matokeo yake ni anguko kubwa la wazazi wetu wa kwanza. Mungu anapotaka
kujua kilichojiri kila mmoja anamtupia lawama mwenzake. Mwanamke anamlaumu
nyoka, na Adamu anamlaumu mkewe. “Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe
pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala,” Mwa 3:12.
Tukio hili linamfanya Mungu kutoa adhabu kwa yule mwovu-nyoka
na kuvunja agano kati yake na Adamu na Hawa. “Bwana Mungu akamwambia nyoka, Kwa
sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani
wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za
maisha yako,” Mwa 3:14. Tangu hapa Hawa anakuwa Mama wa wote walio hai. “Adamu
akamwita mkewe jina lake Hawa; kwa kuwa yeye ndiye aliye mama yao wote walio
hai,” Mwa 3:20. Na tangu nyakati hizo la anguko hili la wazee wetu wa kwanza,
kifo hakikuepukika tena hadi leo.
Kwa vile Mungu ni Huruma na Upendo, alipenda kuurejesha
uhusiano wake na wale aliowaumba kwa sura na mfano wake. Mpango huu ni tendo
zima la kumwilishwa kwake, yaani Neno kufanyika mwili. Bikira Maria kwa
upendeleo Mkubwa anachukua nafasi ya Hawa aliye dondoka. Bikira Maria katika
mpango huu anakuwa sababu ya kuinuliwa mzazi wetu wa kwanza yaani Hawa. Hivyo kukingiwa
kwa dhambi ya asili Bikira Maria kunaendana na kile kitarajiwacho kuzaliwa,
“Neno kufanyika mwili.”
Mama Bikira Maria anapatwa na mshtuko kwa jambo hili Mungu
analotaka litokee kwake. Malaika Gabrieli anamwambia, “Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu,” Lk 1:30.
Kukingiwa dhambi hii ya Asili Bikira Maria, yaani, ule mwelekeo wa kutenda
dhambi, kuliwezekana pia kwa sababu “alipata neema kwa Mungu.” Akijua ubinadamu wake, Bikira Maria anauliza jambo
hili litawezekanaje? “Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu
yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho
kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu,” Lk 1:35. Kwa hiyo neema
ile kutoka kwa Mungu inajidhihirisha kwa nguvu na uwepo wa Roho Mtakatifu na
kufanya kile kitakachozaliwa kuitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu.
Habari
njema hii kwa Bikira Maria haikuishia hapo tu. Kuthibitisha jambo hilo
linawezekana mbele ya Mungu kwake yeye Bikira Maria kukingiwa dhambi ya Asili
na kumzaa Mwana wa Mungu kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, Malaika anampa yaliyojiri
kwa Elizabeti. “Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya
mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa
tasa; kwa
kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu,” Lk 1:36-37. Mungu wetu aliye hai
siyo Mungu wa kushindwa. Kwa unyenyekevu mkubwa Mama Bikira Maria anaupokea
mpango mzima wa Mungu na kusema, “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe
kwangu kama ulivyosema,” Lk 1:38a
Na kwa vile kile kitakachozaliwa kitakuwa kitakatifu, Mwana
wa Mungu, “ndani yake sisi nasi tulifanywa
urithi, huku tukichaguliwa tangu awali sawasawa na kusudi lake yeye, ambaye
hufanya mambo yote kwa shauri la mapenzi yake,” Efe 1:11. Mungu alichagua
kutuumba kama tulivyo kwa sura na mfano wake “kama vile alivyotuchagua katika
yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na
hatia mbele zake katika pendo,” Efe 1:4.
Tunaupata
ukweli huu kutoka Mwinjili Yohane juu ya huyu atakaye mwilishwa, yaani Mwana wa
Mungu. “Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote
kilichofanyika,” Yoh 1:3. Hivyo kila alifanyalo Mungu linamakusudi yake katika
umilele. Hakuna yeyote katika yetu yupo katika ulimwengu huu kwa bahati mbaya.
Hivyo vyote vinamuunganiko na Kristo Yesu. “Kwa kuwa alitangulia kutuchagua,
ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi
yake,” Efe 1:5.
Wapendwa
katika Kristo, tumshangilie Mama Bikira Maria leo tunapo fanya sikukuu hii ya
kukingiwa dhambi ya Asili. Tunamshangilia kwanza kabisa kwa utayari wake wa
kuupokea mpango mzima wa Mungu kuelekea ukamilisho wa historia ya wokovu wetu.
Pili, kwa utayari wake nasi tunahesabiwa haki na kufanywa wanawe Mungu kwa njia
ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake Mungu.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Kwa kuwa Mwenye
nguvu amenitendea makuu, Na jina lake ni takatifu,” Lk 1:49
Tusali:- Ee Yesu, tufanye
vyombo vya amani yako. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario