miércoles, 7 de diciembre de 2016

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 2 YA MAJILIO


 
IJUMAA WIKI YA 2 YA MAJILIO
Somo: Isa 48:17-19
Zab: 1:1-2, 3, 4, 6
Injili: Mt 11:16-19
Nukuu:
Mimi ni Bwana, Mungu wako, nikufundishaye ili upate faida, nikuongozaye kwa njia ikupasayo kuifuata,” Isa 48:17b 
Laiti ungalisikiliza amri zangu! Ndipo amani yako ingalikuwa kama mto wa maji, na haki yako kama mawimbi ya baharí,” Isa 48:18 
Tena wazao wako wangalikuwa kama mchanga, na hao waliotoka katika tumbo lako kama chembe zake; jina lake lisingalikatika, wala kufutwa mbele zangu,” Isa 48:19 
Maana Yohana alikuja, hali wala hanywi, wakasema, Yuna pepo,” Mt 11:18 
Mwana wa Adamu alikuja, akila na kunywa, wakasema, Mlafi huyu, na mlevi, rafiki yao watoza ushuru na wenye dhambi! Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa kazi zake,” Mt 11:19
 
TAFAKARI: “Nitakifananisha na nini kizazi hiki?”
Wapendwa wana wa Mungu, leo tupo kwenye ulimwengu ambao siyo kwamba tu watu wengi hawaamini kuwa Mungu yupo, bali hawataki kusikia kabisa habari za Mungu. Kumbe leo kwa namna ya pekee Yesu anatuambia “nikifananishe na nini kizazi hiki cha leo?” Kwa namna nyingine twaweza kusema tu kizazi kisichokuwa na hofu ya Mungu. Ikiwa hawakumwamini Yesu wakati huo, je leo watamwamini? Historia yajieleza kwamba, “Yohana alikuja, hali wala hanywi, wakasema, Yuna pepo,” Mt 11:18. Na Mwana wa Adamu alikuja, akila na kunywa, wakasema, Mlafi huyu, na mlevi, rafiki yao watoza ushuru na wenye dhambi! Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa kazi zake,” Mt 11:19.
 
Ikiwa tunaamini maisha ni safari kuelekea umilele, bila uwepo wa Mungu kuufikia umilele huo haitawezekana. Kuna faida kubwa kuamini na kuishi tukiwa na hofu ya Mungu. Mungu anasema, “Mimi ni Bwana, Mungu wako, nikufundishaye ili upate faida, nikuongozaye kwa njia ikupasayo kuifuata,” Isa 48:17b. Njia atufundishaye Mungu ndiyo njia salama na yenye uhakika. Usalama wetu ni kuzishika na kuziishi amri za Mungu. “Laiti ungalisikiliza amri zangu! Ndipo amani yako ingalikuwa kama mto wa maji, na haki yako kama mawimbi ya baharí,” Isa 48:18. Mahali popote pale penye utaratibu pana akili. Hivyo tu wacha wake Mungu tunapoishi yale anayotutaka kuishi. Mawazo yake Mungu kwetu ni mawazo ya uzima na mema. “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho,” Yer 29:11.
Faida tuipatayo kwa kumwamini Mungu na kuishi kadiri ya mapenzi yake ni kubwa sana. Mungu anatuambia, “Tena wazao wako wangalikuwa kama mchanga, na hao waliotoka katika tumbo lako kama chembe zake; jina lake lisingalikatika, wala kufutwa mbele zangu,” Isa 48:19. Huku ni kuhesabiwa haki mbele ya Mungu pale tunapoishi kwa uaminifu na hofu juu yake.
Tumsifu Yesu Kristo!
Wewe, Bwana, ndiwe utakayetuhifadhi, Utatulinda na kizazi hiki milele,” Zab 12:7
 
Tusali:-Ee Yesu, tujalie imani thabiti. Amina
 

No hay comentarios:

Publicar un comentario