domingo, 4 de diciembre de 2016

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 2 YA MAJILIO





JUMATATU WIKI YA 2 YA MAJILIO

Somo: Isa 35:1-10

Zab: 85:9ab-10, 11-12, 13-14

Injili: Lk 5:17-26

Nukuu:
Nyika na mahali palipo ukiwa patafurahi; jangwa litashangilia na kuchanua maua kama waridi,” Isa 35:1
Na hao waliokombolewa na Bwana watarudi, watafika Sayuni wakiimba; na furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao; nao watapata kicheko na furaha, huzuni na kuugua zitakimbia,” Isa 35:10
Naye alipoiona imani yao, alimwambia, Ee rafiki, umesamehewa dhambi zako,” Lk 5:20 
Lakini, mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (alimwambia yule mwenye kupooza). Nakuambia, Ondoka, ujitwike kitanda chako, ukaende zako nyumbani kwako,” Lk 5:24

TAFAKARI: “Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi.”

Wapendwa wana Mungu, leo katika Injili tunaona baadhi ya watu walivyokuwa na Imani juu ya Yesu na wengine wakiwepo Mafarisayo na Waandishi wakimbeza kwa kile anachofundisha na kutenda. Hata hivyo Yesu anastaajabia Imani ya watu hasa pale ilipobidi kulitoboa dari ya nyumba na kumwingiza mgonjwa ili apate kuponywa kwani hapakuwa na nafasi ya kumpitisha. Naye alipoiona imani yao, alimwambia, Ee rafiki, umesamehewa dhambi zako,” Lk 5:20.

Maneno haya na tendo hili yanazua zogo kubwa katika ya Yesu, Mafarisayo na Walimu wa torati. Zogo hili linazuka kwa sababu ya mitazamo waliyokuwa nayo Wayahudi juu ya Masiha waliokuwa wakimsubiri, ikiwa ni pamoja na namna ya kufanya na kutenda Masiha huyo. Kwa ujumla walikuwa na mashaka na Yesu. Walimtazamia Masiha ambaye angewatoa na kuwaweka huru kutoka kwenye dola ya Kirumi. Masiha huyo walimtegemea labda angeshughulikia sana mambo ya kisiasa na kifalme katika maana kiutawala. Kumbe yote yalikuwa kinyume.

Yesu kabla ya kifo chake anauweka ukweli huu mbele ya Pilato alipomuuliza kama Yeye ni Mfalme wa Wayahudi, Yoh 18:33. “Yesu akajibu, Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa Wayahudi. Lakini ufalme wangu sio wa hapa,” Yoh 18:36. Yesu hakujihusisha na mambo ya leo na kesho. Alikuja ili tuupate uzima wa Milele na hilo ndilo lengo la kuumbwa kwetu. Duniani hapa tunajiandaa kwa ajili ya uzima huo wa milele. Naye Yesu anasema, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi,” Yoh 11:25. Nasi kama wafuasi wa Kristo, mambo ya leo na kesho yasitupotezee muda wetu na kuukosa uzima wa milele.

Leo Yesu anaudhihirisha Umungu wake bila kupepesa Macho. Ni mtu mwenye kiburi tu itamgharibu kuelewa ukweli huu. Naye Yesu anasema, Lakini, mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (alimwambia yule mwenye kupooza). Nakuambia, Ondoka, ujitwike kitanda chako, ukaende zako nyumbani kwako,” Lk 5:24.
Mamlaka haya Yesu aliyakabidhi kwa mitume wake kabla ya kupaa kwenda mbinguni. Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa,” Yoh 20:22-23. Kanisa limeratibu ukweli huu Kiimani na Kisakramenti-“Sakramenti ya upatanishi/kitubio” tangu nyakati hizo  na kubaki hata leo katika Kanisa Katoliki.

Hivyo wapendwa wana wa Mungu, tusione haya kwenda kuziungama dhambi zetu. Mama Kanisa yupo muda na wakati wowote kutupokea kwa huruma na upendo kupitia Sakramenti hii ya upatanisho. Ni wakati wa kupatanishwa na upendo wa Mungu Baba ambaye yupo tayari kutukomboa kutoka utumwa wa dhambi. Ni huyu tumsubiriaje ambaye, Nyika na mahali palipo ukiwa patafurahi; jangwa litashangilia na kuchanua maua kama waridi,” Isa 35:1.
Anakuja kuuleta uzima pale palipodhoofu, na furaha palipo na ukiwa. Na hao waliokombolewa na Bwana watarudi, watafika Sayuni wakiimba; na furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao; nao watapata kicheko na furaha, huzuni na kuugua zitakimbia,” Isa 35:10. Ndugu yangu uliyesafiri nami katika tafakari hii usiziache neema zikupite bure. Nenda kapatanishwe na Mungu aliye hai.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma,” Yoh 17:3

Tusali:-Ee Yesu Mwema, tujalie unyenyevu na moyo wa kusamehe. Amina
 
 

No hay comentarios:

Publicar un comentario