lunes, 19 de diciembre de 2016

TAFAKARI: DECEMBA 20, WIKI YA 4 YA MAJILIO


DECEMBA 20, WIKI YA 4 YA MAJILIO

Somo: Isa 7:10-14

Zab: 24:1-2, 3-4ab, 5-6

Injili: Lk 1:26-38

Nukuu:

Jitakie ishara ya Bwana, Mungu wako; itake katika mahali palipo chini sana, au katika mahali palipo juu sana,” Isa 7:11

 Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli,” Isa 7:14 

Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe,” Lk 1:28

 “Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho,” Lk 1:30-33

“Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume?” Lk 1:34

TAFAKARI: “Litakuwaje neno hili, maana sijui mume?”

Wapendwa wana wa Mungu, Nabii Isaya na Mfalme Ahazi wanakabiliana uso kwa uso juu ya hatma ya Taifa na wana wa Israeli. Mfalme Ahazi anaomba ushauri ili aweze kuwashinda maadui zake. Badala yake Nabii Isaya anachokonoa dhamiri, mawazo, na mtazamo wao juu ya yule wanao paswa kumwamini na kumtumikia. “Naye akasema, Sikilizeni sasa, enyi nyumba ya Daudi; Je! Ni neno dogo kwenu kuwachosha wanadamu, hata mkataka kumchosha Mungu wangu pia?” Isa 7:13. Nabii Isaya mtu wa Mungu na mtu wa imani, anawapa ishara ya kweli. “Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli,” Isa 7:14. Mungu pamoja nasi! Katika utabiri huu, Mtoto huyu aweza kuwa kihistoria kadiri ya nyakati zile kuwa ni mtoto wa Mfalme, atarajiwaye kuzaliwa. 

Ila katika maudhui ya Kinabii na hasa nyakati tarajiwa, ilimaanisha kuwa ni Masiha. “Jitakie ishara ya Bwana, Mungu wako; itake katika mahali palipo chini sana, au katika mahali palipo juu sana,” Isa 7:11. Mtoto huyu ni zawadi ya wazi kabisa wakati ulipotimia na wa Imani. Ishara hii ndiyo tunayoiona ikisemwa na Nabii Isaya, 9:5-6, Nabii Mika, 1:18-25, Mwinjili Mathayo, 1:18-25.

Kutangazwa kwa Yohana kulitokea katika hekalu kule Yerusalemu, na mpokeaji wa ujumbe huu alikuwa kuhani, yaani, Zakaria Baba yake. Hapa tunaona nyumba ya unyeyekevu, kijiji kisichojulikana na nchi isiyojulikana na kudharauliwa. Mungu haitaji chochote kutoka kwa kiumbe chake alichokiumba ikiwa kiumbe hicho hujifunua kwake. Ni kwa maana hiyo basi tunaona kazi kubwa za Mungu hufanyika katika ukimya na kwa kujificha sana. Bikira Maria anakuwa muhimili wa fumbo zima hili kwa matendo haya Makuu ya Mungu.  Malaika “Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe,” Lk 1:28. Maneno haya hayakusemwa kwa Zakaria wala Elizabeti katika kutangazwa kwake Yohana.

Kama binadamu kwenye mipaka yake kadiri ya kuumbwa kwake, na maumbile yake, Bikira Maria anamuuliza Malaika uhalisa wa jambo lile. “Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani?” Lk 1:29. Mungu huyakamilisha yote kadiri ya mapenzi yake licha ya udhaifu wa yule anayependa na kuchagua kufanya naye kazi hiyo au mpango huo. “Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho,” Lk 1:30-33.

Huyu ni Mungu asiyeshindwa na mweza wa yote. Akiujua mfadhaiko na mahangaiko ndani ya Maria, “Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu,” Lk 1:35. Kuthibitisha Ukuu wa Mungu na mpango mzima wa wokofu wa mwanadamu, Malaika anaifichua siri kuhusu hali ya binamu yake Elizabeti na kusema, “Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu,” Lk 1:36-37

Huu ni wakati wa Kimasiha utarajiwao kuwasili. Ishara zilizobeba uwepo huu wa Kimasiha ni pamoja na unyenyekevu, ukamilifu, na furaha. Bwana na Mungu wetu anakuwa jirani wetu wa karibu. Bikira Maria anakuwa Yerusalemu mpya, hekalu jipya; Utukufu wa Mungu una kaa ndani yake. Kwa Imani ya Bikira Maria, agano jipya linaanza. “Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake,” Lk 1:38. Kama Tusomavyo habari hii kutoka katika kitabu cha Mwazo sura ya 12, na Barua ya Mtume Paulo kwa Warumi sura ile ya 4. Huu ni wakati wa kuanza upya na Mungu kwa kila mmoja wetu kadiri ya nafasi yake na wito wake.

  Tumsifu Yesu Kristo!

Matendo ya Bwana ni makuu, Yafikiriwa sana na wapendezwao nayo,” Zab 111:2

Tusali:-Ee Yesu na Mkombozi wetu, anza nasi upya na iandike tena historia yetu upya. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario