DECEMBA 17, WIKI
YA 3 YA MAJILIO
Somo: Mwa 49:2, 8-10
Zab: 72:2, 3-4ab, 7-8, 17
Injili: Mt 1: 1-17
Nukuu:
“Kusanyikeni, msikie, enyi wana wa Yakobo, Msikilizeni
Israeli, baba yenu,” Mwa 49:2
“Fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda, Wala mfanya sheria
kati ya miguu yake, Hata atakapokuja Yeye, mwenye milki, Ambaye mataifa
watamtii,” Mwa 49:10
“Kitabu cha ukoo wa Yesu Kristo, mwana wa Daudi, mwana
wa Ibrahimu,” Mt 1:1
“Yakobo akamzaa Yusufu mumewe Mariamu aliyemzaa YESU
aitwaye Kristo,” Mt 1:16
“Basi vizazi vyote tangu Ibrahimu hata Daudi ni vizazi kumi
na vinne; na tangu Daudi hata ule uhamisho wa Babeli ni vizazi kumi na vinne;
na tangu ule uhamisho wa Babeli hata Kristo ni vizazi kumi na vinne,” Mt 1:17
TAFAKARI: “Hata
atakapokuja Yeye, mwenye milki, Ambaye mataifa watamtii.”
Wapendwa wana wa Mungu, tu karibu kupokea tunda la haki na
Bwana mwenye milki, Masiha wetu na Mkombozi wetu. Huu ni wakati wa kusikiliza
kwa makini habari zake, siyo zile tu zitokazo nje, bali zile zitokazo ndani ya
mioyo yetu. Swali ni hili: Je, ajapo Masiha huyu atapata nafasi ndani ya moyo
wangu? Kama nafasi ipo, Je, nimejiandaa vizuri? Tusisahau kwamba Masiha huyu
ndiye mwenye milki yote, na hakuna chochote kile katika uwepo wake ambacho
hakikufanyika kupitia yeye. Mwinjili Yohane anasema, “Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho
chote kilichofanyika,” Yoh 1:3. Je, ninakilicho changu? Kama kipo ni nini zaidi
ya dhambi zangu?
Bila
shaka ili Mwokozi wetu akija akute nafasi ndani ya moyo wangu, sina budi kutoa
kile kilicho changu, yaani, dhambi zangu ili Mwokozi apate nafasi ndani yangu.
Atakapo kuja hataondoka ikiwa nitampa nafasi. Mwokozi huyu anachohitaji kingine
kutoka kwangu ni utii. Utii huu ni kielelezo sahihi cha kuyapokea mapenzi yake
kwa sababu yeye ni UTII. “Fimbo ya enzi haitaondoka
katika Yuda, Wala mfanya sheria kati ya miguu yake, Hata atakapokuja Yeye,
mwenye milki, Ambaye mataifa watamtii,” Mwa 49:10. Utii huu ndiyo siri ya
Kristo na mafanikio yake ya kuupokea msalaba na kukubali kuwambwa juu yake kwa
hiari yake. “Tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza
akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba,” Flp 2:8
Wapendwa wana wa Mungu, ili Mwokozi wetu alipate umbo hili
la mwanadamu, atamwilishwa na kuzaliwa kama sisi tulivyo na kuwa na asili kama
sisi tulivyo, yaani, kutoka kwenye familia, koo, kabila, na taifa. “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye
Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Naye Neno alifanyika
mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee
atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli,” Yoh 1:1-2, 14.
Ndiyo “Alifanyika mwili, akakaa kwetu:”-hapa ndipo alipochukua
hali yetu ya kibinadamu, ikiwa ni pamoja na mazingira yetu isipokuwa hakutenda
dhambi. “Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake,” 1Pet
2:22. Hata hivyo anakubali kuzaliwa katika hali na mifumo ya kwetu katika asili
zetu. Hivi ndivyo ilivyokuwa, “Kitabu cha ukoo wa Yesu Kristo, mwana wa
Daudi, mwana wa Ibrahimu. Yakobo akamzaa Yusufu mumewe Mariamu aliyemzaa YESU
aitwaye Kristo,” Mt 1:1, 16. Historia ya familia ya Yesu, Ukoo, Kabila na
Taifa, unaufunua mpango mzima wa Mungu katika historia hii ya wokovu wetu.
Wapendwa wana wa Mungu, hakuna hata mmoja wetu aliyechagua kuzaliwa katika
familia hiyo aliyopo. Hii ni pamoja na ukoo wake, kabila lake na Taifa lake.
Yote ni mapenzi na mpango wa Mungu. Tusema vipi basi pale tunapowaona baadhi
yetu wakizisifia familia zao, koo zao, makabila yao na Mataifa yao? Hivi kweli
kuna sababu yoyote ile ya kujisifia? Jibu ni HAPANA! Basi kama ni kujisifu,
Yesu angekuwa wa kwanza kufanya hivyo.
Lakini Yesu, “ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna
ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana
nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu,
akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu,” Flp 2:6-7
Wapendwa katika Kristo, kwa tendo la Neno kufanyika mwili na
kukaa kwetu akichukua hali yetu ya kibinadamu na mazingira yetu, ni heshima
kubwa sana kwetu. Pili, Mwokozi huyu anatufundisha unyenyekevu uliotukuka. Nasi
tujifunze kwa mwalimu wetu Yesu Kristo kwani kwake kuna ufahamu wote.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Msitende
neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu
na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake,” Flp 2:3
Tusali:-Ee Yesu, tujalie
fadhila ya Unyenyekevu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario