JUMATATU WIKI YA 3
YA MAJILIO
Somo: Hes 24:2-7, 15-17a
Zab: 25:4-5ab, 6-7bc, 8-9
Injili: Mt 21:23-27
Nukuu:
“Namwona,
lakini si sasa; Namtazama, lakini si karibu;
Nyota itatokea katika Yakobo Na fimbo ya enzi itainuka katika Israeli; Nayo
itazipiga-piga pembe za Moabu, Na kuwavunja-vunja wana wote wa ghasia,” Hes
24:17
“Ni kwa amri gani
unatenda mambo haya? Naye ni nani aliyekupa amri hii?” Mt 21:23b
“Yesu
akajibu akawaambia, Na mimi nitawauliza neno moja; ambalo mkinijibu, nami
nitawaambia ni kwa amri gani ninatenda haya,” Mt 21:24
“Ubatizo
wa Yohana ulitoka wapi? Ulitoka mbinguni, au kwa wanadamu?” Mt 21:25
“Wakamjibu
Yesu wakasema, Hatujui. Naye akawaambia, Wala mimi siwaambii ninyi ni kwa amri
gani ninatenda haya,” Mt 21:27
TAFAKARI:
“Ni kwa amri gani unatenda mambo haya?”
Wapendwa wana wa Mungu,
Taifa la wana wa Israeli linaingiwa hofu juu ya Mfalme Balaki wa Moabu. Balaamu
akiwa amejawa na Roho wa Mungu aliyaandaa maombi kuhusu sintofahamu ile waliyokutana
nayo jangwani. Mungu anampa maono naye anayatafsiri kama ifuatavyo; “Namwona, lakini si sasa; Namtazama, lakini si karibu; Nyota itatokea katika Yakobo Na fimbo ya
enzi itainuka katika Israeli; Nayo itazipiga-piga pembe za Moabu, Na
kuwavunja-vunja wana wote wa ghasia,” Hes 24:17. Je, maono haya ni ashirio la
kuja kwake Masiha, hasa Nyota hii kutoka katika Yakobo?
Hakika
nyota hiyo na yote yanayoambatana nayo ni ashirio la kuja kwa Masiha, ambaye
atawaweka huru wana wa Taifa hili teule la Mungu. Utabiri huu unathibitishwa na
Malaika Gabrieli alipompasha habari
Bikira Maria na kusema, “Tazama, utachukua mimba
na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa
mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi,
baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake
utakuwa hauna mwisho,” Lk 1:31-33. Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo,
tunaona Malaika anazungumzia kazi ya
yule atakaye zaliwa na Bikira Maria na
kusema, “Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu,
maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao,” Mt 1:21. Hivyo tendo
hili ni mpango mahususi wa wokovu wa mwanadamu.
Hata hivyo pamoja na
tabiri zote hizi na uthibitisho wa kweli kwa Neno kufanyika Mwili na kukaa
kwetu, Yoh 1:14, bado Taifa hili Teule hawakutaka kuachana na
mitazama yao ya kibinadamu, wakabaki kushikilia sheria za kibinadamu na tafsiri
zao zilizokuwa na mwelekeo wa ubinadamu.
Kwa maana hiyo, waliingiwa upofu wa kiroho na kutokuona ishara zilizokuwa zinaufunua
Umungu wa Yesu Kristo. Hivyo Wayahudi, na hasa Wakuu wa Makuhani na wazee
wanahoji Mamlaka ya Yesu na kumwambia, “Ni kwa amri gani unatenda mambo haya?
Naye ni nani aliyekupa amri hii?” Mt 21:23b.
Yesu hakuhitaji mamlama yoyote kutenda aliyoyatenda kwa sababu licha ya kuwa na
hali ya ubinadamu, Yeye ni Mungu pasipo shaka, Yoh 1:1-3.
Hivyo kwa kutambua udhaifu wao, naye
Yesu anawauliza swali, “Ubatizo
wa Yohana ulitoka wapi? Ulitoka mbinguni, au kwa wanadamu?” Mt 21:25. Jibu lao liliwaweka katika mtego mkubwa kwa
sababu wangalijibu ubatizo huo ulitoka mbinguni wataonekana hawana imani, hasa
kile alichokitabiri Yohani kuhusu Yesu. Na wakisema ulikoka mwa mwanadamu
waliogopa kwani watu wote waliujua utakatifu wa Yohani Mbatizaji. Kuepukana na
hoja hii ya msingi waliamua kusema hatujui ingawa ukweli waliujua. Naye Yesu
aliwaacha jinsi walivyo kwa sababu ujumbe uliwafikia bara’bara. Pasipo shaka
yoyote, Wakuu wa Makuhani na Wazee wanahoji mamlaka ya Yesu kwa sababu
wanahofia nafasi zao na hasa maslahi yao kutokana sheria kandamizi
walizojitungia wenyewe, kutoka amri kumi za Mungu hadi kufikia sheria 613.
Uwepo wa Yesu, Nguvu, na Mamlaka yake katika kufundisha na kutenda kuliwatia
hofu kubwa sana. Kitumbua chao kilianza kuingia mchanga!
Hivyo ndugu zangu, katika Kristo
tunawekwa huru, na yatupasa kutokunaswa katika kongwa la utumwa wa dhambi. “Katika
ungwana huo Kristo alituandika huru; kwa hiyo simameni, wala msinaswe tena
chini ya kongwa la utumwa,” Gal 5:1. Maisha mapya ndani ya Kristo na katika
Kristo hayatulazimu tena kuhofia au kuwajibika kwa sheria za kibinadamu, na
zisizokuwa na mwelekeo wa kweli, haki, na upendo. Tunawajibika kufanya yote
katika imani itendayo kazi kwa upendo. “Maana
katika Kristo Yesu kutahiriwa hakufai neno, wala kutokutahiriwa, bali imani
itendayo kazi kwa upendo,” Gal 5:6. Kuyatumikia haya ni kujitia hofu pasipo
sababu.
Yesu Kristo hakuacha
kukemea mambo haya yasiyo ya msingi kuhusu imani ya kweli. Wayahudi nyakati za
Yesu walionekana kufuata zaidi tafsiri ya torati kuliko torati yenyewe. Tafsiri
hii, yaani, TALMUD, ulikuwa ukweli wa Mungu uliopotoshwa kwa maslahi ya
kibinadamu. Mambo muhimu ya kuzingatia yalikuwa kuhusu adili, rehema, na imani
ya kweli. Yesu anatoa karipio kwa Waandishi na Mafarisayo na kuwaambia, “Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa
kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu ya
sheria, yaani, adili, na rehema, na imani; hayo imewapasa kuyafanya, wala yale
mengine msiyaache,” Mt 23:23. Sheria hizi ambazo kwa kiasi kikubwa
zilikuwa kandamizi zikiendana na utoaji wa sadaka ulionyambuliwa kwa manufaa
yao binafsi. Sheria hizi hazikuwa na mwelekeo wa uzima wa milele. Ukweli ni
kwamba, “kumpenda yeye (Mungu) kwa moyo wote, na kwa ufahamu wote, na
kwa nguvu zote, na kumpenda jirani kama nafsi yako, kwafaa kuliko sadaka nzima
za kuteketezwa na dhahibu zote pia,” Mk 12:33. Mtakatifu Agustino anasema,
‘ukipenda kweli, utafanya yote.’
Wapendwa
katika Kristo, ni vyema tukatambua wajibu wetu na mapaswa yetu ili tuweze
kutumika vyema kadiri ya mpango wa Mungu. Mungu anakila sababu na wewe ikiwa ni
pamoja na maisha yako. Hivyo pigania cheo chako ambacho ni UTAKATIFU wako. Bila
huo huwezi kumwona Mungu.
Tusifu
Yesu Kristo!
“Tafuteni
kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu
atakayemwona Bwana asipokuwa nao,” Ebr 12:14
Tusali:-Ee
Yesu, tufanye vyombo vyako vya kweli, haki, na upendo popote pale tulipo,
kadiri ya nafasi na wito wetu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario