domingo, 18 de diciembre de 2016

TAFAKARI: DECEMBA 19, WIKI YA 4 YA MAJILIO


DECEMBA 19, WIKI YA 4 YA MAJILIO

Somo: Amu 13:2-7, 24-25a

Zab: 71:3-4a, 5-6ab, 16-19

Injili: Lk 1: 5-25

Nukuu:

Palikuwa na mtu mmoja wa Sora, wa jamaa ya Wadani; jina lake akiitwa Manoa; na mkewe alikuwa tasa, hakuzaa watoto,” Amu 13:2 

Malaika wa Bwana akamtokea yule mwanamke, akamwambia, Tazama, wewe sasa u tasa, huzai; lakini utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume,” Amu 13:3 

 “Na wote wawili walikuwa wenye haki mbele za Mungu, wakiendelea katika amri zote za Bwana na maagizo yake bila lawama,” Lk 1:6

“Nao walikuwa hawana mtoto, maana Elisabeti alikuwa tasa, na wote wawili ni wazee sana,” Lk 1:7

 “Lakini yule malaika akamwambia, Usiogope, Zakaria, maana dua yako imesikiwa, na mkeo Elisabeti atakuzalia mtoto mwanamume, na jina lake utamwita Yohana,” Lk 1:13

 “Zakaria akamwambia malaika, Nitajuaje neno hilo? Maana mimi ni mzee, na mke wangu ni mkongwe wa siku nyingi,” Lk 1:18

TAFAKARI: “Hakuna lisilowezekana kwa Mungu. Mungu anahitaji kilicho bora zaidi kutoka kwako.”

Wapendwa wana wa Mungu, tangu kufariki kwa Nabii Yoshua, hali ya makabila ya Waisraeli haikuwa nzuri na yautulivu. Wafilistia waliyanyanyasa sana makabila haya ya Waisraeli. Katika safari yake ya kumkomboa mwananadamu, Mungu anakisikia kilio chao, na anamsimamisha mmoja kati ya wana wa Israeli, na kuwarudishia furaha tena. Hakika kila afanyacho Mungu kina makusudi yake makubwa ikiwa ni udhihirisho wa Utukufu wake, na furaha na amani kwa waliosetwa. Mungu humuhusisha mwanadamu Mipango yake kwa sababu mwanadamu huyu ndiye kwenye chapa yake, yaani, kamuumba kwa sura na mfano wake, Mwan 1:27.

Hivyo basi, kwa tendo hili lenye matokea makubwa kwanza kabisa linakuwa furaha na amani kwa mke wa Manoa ambaye alikuwa tasa. “Palikuwa na mtu mmoja wa Sora, wa jamaa ya Wadani; jina lake akiitwa Manoa; na mkewe alikuwa tasa, hakuzaa watoto,” Amu 13:2. Malaika wa Bwana akiwa ni mjumbe wa Mungu, wa mambo muhimu ya Mungu, na yamuhusuyo Mungu, anamtokea Mke wa Manoa na kumwambia, “Tazama, wewe sasa u tasa, huzai; lakini utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume,” Amu 13:3. Hakika, lisilowezekana kwa mwanadamu kwa Mungu linawezekana. Mungu anataka kilicho bora kutoka kwetu. Bila shaka familia hii, yaani, Manoa na Mkewe walikuwa na hofu kubwa sana, na nini hatma ya maisha yao. Mungu kamwe hamtupi mja wake hasa pale anapojiachia kwake bila kujibakiza.

Kwa vile kitakachozaliwa lazima kijibu mahangaiko ya watu wa Mungu, Malaika anatoa masharti yake kadiri ya matakwa ya Mungu. Huku ndiko kule kuwa Mnadhiri wa Mungu kama tusomavyo kukoka kitabu cha hesabu 6:2-8. Na haya ndiyo anayoyasema Malaika kwa Mke wa Manoa, kwamba, “Basi sasa, jihadhari, nakuomba, usinywe divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi; kwani tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume; na wembe usipite juu ya kichwa chake; maana mtoto huyo atakuwa mnadhiri wa Mungu tangu tumboni; naye ataanza kuwaokoa Israeli na mikono ya Wafilisti,” Amu 13:4-5. Mtoto huyu anatengwa rasmi kwa kazi ya Mungu na yanayomuhusu Mungu. “Basi yule mwanamke akamzaa mtoto mwanamume akamwita jina lake Samsoni, mtoto huyu akakua, Bwana akambarikia,” Amu 13:24. Samsoni anachukua jukumu kubwa kutoka kwa Mungu, na anashirikishwa kazi Takatifu ya Mungu, yaani, mpango wa wokovu wa mwanadamu. 

Jambo lingine kubwa lenye mfanano kama huu linatokea pia kwenye Injili yetu ya leo. Mungu anavunja ukimya kwa kuingia katika historia ya mwanadamu kwa kuleta furaha na Amani kwa wale waliosetwa, na kuudhihirisha Utukufu wake. Zakaria na Mkewe Elizabeti hawakufanikiwa kupata mtoto kwa muda mrefu sana. Kwa hali ya kibinadamu matumaini yao yalianza kutoweka. Maandiko Matakatifu yanatuambia hivi, “Nao walikuwa hawana mtoto, maana Elisabeti alikuwa tasa, na wote wawili ni wazee sana,” Lk 1:7. Pamoja na hali hii isiyowezekana kutokana na mipaka yetu kibinadamu, bado Mungu anahitaji kilicho bora kutoka kwetu. Kilichobora kutoka kwa Zakari na Elizabeti ilikuwa maisha yao ya uaminifu na Imani thabiti. “Na wote wawili walikuwa wenye haki mbele za Mungu, wakiendelea katika amri zote za Bwana na maagizo yake bila lawama,” Lk 1:6. Hakika, Mungu kamwe hamtupi mja wake anapojiachia kwake bila kujibakiza!

Hivyo Zakaria akiwa katika shughuli zake za kila siku hekaluni, “Akatokewa na malaika wa Bwana, amesimama upande wa kuume wa madhabahu ya kufukizia,” Lk 1:11. Tukio hili linamshtusha sana Zakari. Halikuwa jambo la kawada kwake. “Lakini yule malaika akamwambia, Usiogope, Zakaria, maana dua yako imesikiwa, na mkeo Elisabeti atakuzalia mtoto mwanamume, na jina lake utamwita Yohana,” Lk 1:13. Hii ni habari njema kwa Zakaria na Mkewe Elizabati. Mungu ameamua kuwatoa aibu na kuwapa hadhi yao kama wazazi.

Hadhi hii ambayo kwa msingi na mtazamo katika jamii ni heshima kubwa kwa wazazi wote wawili, na kwa namna ya pekee kwa upande wa mama. Ujumbe huu ni habari njema na siyo adhabu. Ni habari njema kama tusomavyo kutoka kitabu cha Nabii Sefania, “Imba, Ee binti Sayuni; piga kelele, Ee Israeli; Furahi na kushangilia kwa moyo wako wote, Ee binti Yerusalemu. Bwana ameziondoa hukumu zako, Amemtupa nje adui yako; Mfalme wa Israeli, naam, yeye Bwana, yu katikati yako; Hutaogopa uovu tena. Katika siku ile Yerusalemu utaambiwa, Usiogope, Ee Sayuni; mikono yako isilegee. Bwana, Mungu wako, yu katikati yako shujaa awezaye kuokoa; Atakushangilia kwa furaha kuu, Atakutuliza katika upendo wake, Atakufurahia kwa kuimba,” Sef 3:14-17

Malaika anaendelea kuufunua ujumbe wa Mungu kwa kile kitakachozaliwa, ikiwa ni pamoja na kazi atakayoifanya kwa sifa na utukufu wa Mungu. Atakayezaliwa atatengwa kwa kazi ya Mungu, “Kwa sababu atakuwa mkuu mbele za Bwana; hatakunywa divai wala kileo; naye atajazwa Roho Mtakatifu hata tangu tumboni mwa mamaye,” Lk 1:15. Hakika ataongozwa na Roho Mtakatifu kabla hata ya kuzaliwa kwake. Jambo hili litajidhihirisha kwenye maamkio kati ya Mariamu na Elizabeti baadaye.

Huyu atakayezaliwa, yaani, Yohana, na baadaye kama Yohona Mbatizaji, atakuwa na kazi hii ifuatayo, “Naye atatangulia mbele zake katika roho ya Eliya, na nguvu zake, ili kuigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto, na kuwatilia waasi akili za wenye haki, na kumwekea Bwana tayari watu waliotengenezwa,” Lk 1:16-17. Kwa ufupi kazi yake itakuwa kuwaandaa watu na kuiandaa njia ya mwokozi, yaani, Yesu Kristo. “Sikiliza, ni sauti ya mtu aliaye, Itengenezeni nyikani njia ya Bwana; Nyosheni jangwani njia kuu kwa Mungu wetu,” Isa 40:3. Huyu ndiye Yohane Mbatizaji na kazi ile atakayoifanya.

Lakini pamoja na Malaika kumwambia Zakaria asiogope juu ya ujumbe huu, bado anakuwa na mashaka na kumwiya vigumu kuamini. Zakaria anautazama zaidi uchakavu wake wa nje na kusahau utu wake wa ndani. “Zakaria akamwambia malaika, Nitajuaje neno hilo? Maana mimi ni mzee, na mke wangu ni mkongwe wa siku nyingi,” Lk 1:18. Katika mahangiko haya, mazingira na hali yake, Mtume Paulo anatuambia, “Kwa hiyo hatulegei; bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku,” 2Kor 4:16. Hivyo hakuna lisilowezekana kwa Mungu. Mungu anahitaji kilicho bora zaidi kutoka kwako.

Zakaria anashindwa kumpa Mungu kilicho bora zaidi kutoka kwake, yaani, ‘Imani yake ya kweli’. Hivyo jambo hili linakuwa chukizo kwa Mungu, na hivyo “Malaika akamjibu akamwambia, Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele za Mungu; nami nimetumwa niseme nawe, na kukupasha habari hizi njema. Na tazama! Utakuwa bubu, usiweze kusema, mpaka siku ile yatakapotukia hayo, kwa sababu hukuyasadiki maneno yangu; nayo yatatimizwa kwa wakati wake,” Lk 1:19-20.

Hata pamoja na tukio hilo la kutokuamini kwake Zakaria, Mungu hakusitisha mpango wake na nia yake njema katika safari hii ya ukombozi. “Hata baada ya siku zile mkewe Elisabeti alichukua mimba akatawa miezi mitano, akisema, Hivi ndivyo alivyonitendea Bwana katika siku zile alizoniangalia ili kuniondolea aibu yangu mbele ya watu,” Lk 1:24-25. Huyu ndiye Mungu asiyeshindwa. Huyu ndiye Mungu anayetutoa katika vifungo vya mateso na aibu zetu. Ndugu yangu tuliyesafiri wote katika tafakari hii, tunaalikwa wewe na mimi kutokukata tamaa hata pale tunapoona giza tupu mbele ya maisha yetu. Mungu huyaona mahangaiko yetu yote. Bado anahitaji kilicho bora zaidi kutoka kwetu, yaani, ‘Imani thabiti.’

Tumsifu Yesu Kristo!

Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili,” 1Kor 10:13

Tusali:-Ee Yesu, tujalie nguvu na Imani thabiti ya kustahimili majaribu, na kuyashinda. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario