IJUMAA WIKI YA 1
YA MAJILIO
Somo: Isa 29:17-24
Zab: 27:1, 4, 13-14
Injili: Mt 9:27-31
Nukuu:
“Na
katika siku hiyo viziwi watasikia maneno ya hicho chuo, na macho ya vipofu
yataona katika upofu na katika giza,” Isa 29:18
“Wanyenyekevu
nao wataongeza furaha yao katika Bwana, na maskini katika wanadamu watafurahi
katika Mtakatifu wa Israeli,” Isa 29:19
“vipofu wawili
wakamfuata wakipaza sauti, wakisema, Uturehemu, Mwana wa Daudi,” Mt 9:27
“Naye
alipofika nyumbani, wale vipofu walimwendea; Yesu akawaambia, Mnaamini kwamba
naweza kufanya hili? Wakamwambia, Naam, Bwana,” Mt 9:28
“Ndipo
alipowagusa macho, akasema, Kwa kadiri ya imani yenu mpate,” Mt 9:29
TAFAKARI:
“Mnaamini kwamba naweza kufanya hili? Kwa kadiri ya imani yenu mpate.”
Wapendwa
wana wa Mungu, tukiachana na yote yale mazuri yaletwayo
na Masiha wetu kama tuonavyo katika somo letu la kwanza, kutoka kitabu cha
Nabii Isaya, ni vyema tukajikita leo kwa undani juu ya haya yafuatayo:
kuviondoa vilema vyetu na mapungufu, kujifunza ustahimilivu kwa yale
tusiyoyajua, kujifunza katika shida na mateso, na kutokuchukulia vitu kwa mzaa
mzaa au mazoea ili tuufaidi ujio wa Masiha. Huu ndio wito wa kipindi hiki cha
Majilio. Hivyo leo tuangalie kwa undani juu ya mahangaiko yetu na mateso ambayo
kwa kiasi kikubwa yanatutoa katika mwelekeo mzima wa Imani ya kweli. Ni kwa
kadiri ya Imani yako utapata yale uyaombayo.
Bila
shaka wewe ni mmoja wa wale ambao kwa namna mmoja au nyingine umekuwa
ukizunguka kila kona ukitafuta suluhu la tatizo lako bila mafanikio. Hakuna shaka
pia kwa tatizo hilo au matatizo hayo umeshasali kila aina ya sala na novena
bila mafanikio. Kwa mtiririko huu naona pia unavyoangaika kutafuta majibu ya
matatizo yako kutoka nyumba moja ya sala (vijikanisa vya majina ya watu) kwenda nyingine, toka mchungaji mmoja kwenda
mwingine bila mafanikio yenye utulivu wa kutosha. Naona unavyoshawishika
kufanya ibada za giza kwa maagizo ya waganga wa kienyeji kupitia marafiki zako
unaowaamini.
Wapendwa
katika Kristo, leo Yesu anakuambia wewe na mimi maneno haya ya uzima kama
alivyowaambia wale vipofu waliotaka kuona tena; “Mnaamini kwamba naweza kufanya
hili? Kwa kadiri ya imani yenu mpate.” Swali hili analotuuliza leo Yesu ni
swali la msingi sana. Wengi wetu ni wakristo wa majina na zaidi sana ni wakrito
wa jumapili. Dini na Imani ya wengi imekuwa kama kautaratibu fulani kitumikacho
kama utambulisho wa kawaidi katika matukio fulani ya maisha, na kisicho sema
chochote kuhusu undani wa maisha wa mtu husika.
Licha
ya kwamba mtu akiwa amebanwa na tatizo kubwa huweza kutekeleza ushauri wowote
apewao, ni vyema kusimama katika Imani thabiti bila kuterereka. “Naye alipofika
nyumbani, wale vipofu walimwendea; Yesu akawaambia, Mnaamini kwamba naweza
kufanya hili? Wakamwambia, Naam, Bwana,” Mt 9:28. Yote
hutendwa ndani yetu kwa uzito ule ule
tulionao kuhusu kile tuaminicho. “Ndipo
alipowagusa macho, akasema, Kwa kadiri ya imani yenu mpate,” Mt 9:29.
Mungu ana lengo kwa
kila tatizo. Yeye hutumia mazingira kukuza tabia yetu ya kweli. Yeye
hutegemeza zaidi mazingira katika kutufanya tufanane na Kristo. Ukweli ni
kwamba unakabiliwa na mazingira masaa ishirini na nne kila siku. Yesu alituonya
kwamba tutakuwa na matatizo ulimwenguni. “Hayo
nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini
jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu,” Yoh 16:33.
Hakuna aliye sugu kwa
matatizo au amefunikwa asipatwe na mateso, wala hakuna aliye huru mbali na
matatizo katika maisha. Maisha ni mfululizo wa matatizo. Kila unapotatua moja,
jingine linasubiri kutokea. Si yote makubwa, lakini yote yana maana kwa Mungu
katika kukuza tabia yako. Petro anatuhakikishia kwamba mtatizo ni ya kawadia, “Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba ulio
kati yenu, unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni
kiwapatacho,” 1Pet 4:12.
Mungu anatumia matatizo
kukusogeza karibu naye. “Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo, Na waliopondeka roho
huwaokoa,” Zab 34:18. Ndugu yangu, wakati wako mzuri wa kuwa na ibada ya karibu
na Mungu unaweza kuwa siku zile za giza sana, moyo wako unapokuwa umepondeka,
unapohisi kuachwa, unapokuwa huna uchaguzi, maumivu yanapokuwa makubwa, na
unamgeukia Mungu peke yake.
Ni wakati wa taabu
ndipo tunajifunza kusali sala za kweli na uaminifu kutoka moyoni. Tunapokuwa
katika maumivu, hatuna nguvu za sala za juu juu. Maisha yakiwa ya raha,
tunaweza kumfahamu Yesu juu juu tu, tukimwiga na kumnukuu na kusema juu yake.
Lakini ni katika taabu ndipo tutamjua Yesu. Tunajifunza mambo katika mateso,
mambo ambayo hatuwezi kujifunza kwa njia nyingine yoyote.
Mungu angeweza kuzuia
Yusufu asitiwe gerezani, Mwa 39:20-22. Mungu angezuia Danieli asitupwe kwenye
shimo la simba, Dan 6:16-23. Mungu angezuia Yeremia asitupwe katika shimo la
matope, Yer 38:6. Mungu angezui Paulo asivunjikiwe na jahazi mara tatu, 2Kor
11:25. Na Mungu angewazuia vijana watatu Waebrania wasitupwe katika tanuru la
moto, Dan 3:1-26. Pamoja na hali hiyo Mungu hakufanya hivyo. Aliruhusu matatizo
hayo kutokea, na matokeo yake kila mmoja wao alimsogelea Mungu karibu zaidi.
Matatizo hutulazimisha
kumtazama Mungu na kumtegemea badala ya nafsi zetu wenyewe. Mtume Paulo
anashuhudia faida hii. “Naam, sisi wenyewe tulikuwa na hukumu ya mauti katika
nafsi zetu ili tusijitumainie nafsi zetu, bali tumtumaini Mungu, awafufuaye
wafu,” 2Kor 1:9. Kamwe hutajua kwamba unachohitaji ni Mungu tu mpaka pale
utakapojikuta umebaki na Mungu tu. Bila kujua chanzo, hakuna tatizo lolote
linaloweza kukupata bila ruhusa ya Mungu. Kila kinachotokea kwa mtoto wa Mungu
kinachujwa na Baba, na amekusudia kukitumia kuleta mema ingawa Shetani na watu
wengine wanakusudia mabaya.
Kwa kuwa Mungu
anatawala yote, ajali ni matukio tu katika mpango mzuri wa Mungu kwa ajili
yako. Kwa sababu kila siku ya maisha yako iliandikwa kwenye kalenda ya Mungu
kabla hujazaliwa. “Macho yako yaliniona kabla
sijakamilika; Chuoni mwako ziliandikwa zote pia, Siku zilizoamriwa kabla
hazijawa bado,” Zab 139:16. Hivyo kila kinachotoka kwako kina umuhimu wa
kiroho. Kila kitu! “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya
kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa
kusudi lake. Maana wale aliowajua
tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili
yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi,” Rum 8:28-29
Wengi wetu hiki kifungu (Rum 8:28-29)
hukinukuu na kukieleza vibaya. Hakisema, “Mungu husababisha kila kitu kufanya
kazi kama ninavyopenda mimi.” Wala hakisemi, “Mungu husababisha kila kitu
kufanya kazi ili kuleta maisha ya furaha duniani.” Hii si kweli pia kuna miisho
ya huzuni duniani. Tunaishi katika ulimwengu ulioanguka. Ni mbinguni tu ndiko
mambo yanatendeka kikamilifu kama Mungu alivyokusudia. Ndiyo maana katika sala
ya Baba Yetu tumeelezwa kusali, “Mapenzi
yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni,” Mt 6:10. Ili kuelewa vyema
kifungu hicho kutoka Barua ya Mtume Paulo kwa Warumi ni vyema tuangalie kwa
makini kila fungu la maneno.
“Twajua:”
Tumaini letu wakati wa magumu hutegemea kufikiri chanya, kufikiri kwa
kutarajia, au kule kutegemea mazuri kwa kawaida. Huu ni uhakika uliojengwa
kwenye kweli ya kwamba Mungu anatawala kikamilifu ulimwengu na kwamba
anatupenda.
“Katika
mambo yote:” Mpango wa Mungu kwa maisha yako unahusisha yote
yanayokutokea-pamoja na makosa yako, dhambi zako, na maumivu yako. Pia ni
pamoja na magonjwa, madeni, majanga, talaka, kifo cha uwapendao. Mungu anaweza
kuleta mema kutokana na jambo ovu sana. Alifanya hivyo pale Kalvari.
“Mungu
hufanya:” Kuna mbunifu nyuma ya kila kitu. Maisha yako siyo matokeo ya bahati
mbaya, ajali, au bahati nzuri. Kuna msanifu nyuma. Historia ni hadithi yake.
Mungu anavuta nyuzi. Tunafanya makosa, lakini Mungu hakosei kamwe. Mungu hawezi
kufanya kosa-kwa sababu yeye ni Mungu.
“Hufanya kazi pamoja:”
Siyo kwa kipekee au kwa kujitegemea. Matukio katika maisha yako hufanya kazi
pamoja katika mpango wa Mungu. Siyo matukio yaliyojitenga, lakini matukio
yanayotegemeana katika machakato mzima wa kukufanya ufanane na Kristo. Ili
kutengeneza keki lazima utumie unga wa ngano, chumvi, yai bichi, sukari, na
mafuta. Kama kila kimoja kikiliwa peke yake hakina ladha nzuri au hata ni
kichungu. Lakini ukivioka pamoja vinakuwa chakula kitamu. Na hiyo ndiyo keki.
Kama ukimpa Mungu maono yako yote mabaya, matukio yasiyopendeza, atayaunganisha
pamoja kuwa kitu chema.
“Wale wampendao katika
kuwapatia mema:” Hii si kwamba kila kitu maishani ni chema. Mengi yanayotokea
katika ulimwengu ni maovu na mabaya, lakini Mungu ni mtaalam wa kutoa mema
kutokana na hayo. Katika ukoo wa Yesu Kristo, Mt 1:1-6, wanawake wanne
wameorodheshwa: Tamari, Ruthu, Rahabu, na Bethsheba. Tamari alimhadaa baba mkwe
wake. Rahabu alikuwa kahaba. Ruthu hakuwa Myahudi na alivunja sheria kwa
kuolewa na Myahudi. Bethsheba alitenda uzinzi na Daudi, jambo lililopelekea
mauaji ya mume wake. Hizi hazikuwa ni sifa nzuri, lakini Mungu alileta mema
kutokana na mabaya, na Yesu akaja kupitia ukoo wao. Kusudi la Mungu ni kubwa
kuliko matatizo yetu, maumivu yetu na
hata dhambi yetu. Neema na huruma ya Mungu ni kubwa kuliko dhambi zetu.
“Wale walioitwa:” Ahadi
ya Mungu ni kwa watoto wa Mungu tu. Si kwa kila mmoja. Kila kitu hufanya kazi
pamoja kwa ubaya kwa wale wanaoishi wakimpinga Mungu na kukazia kufuata njia
zao.
“Kwa kusudi lake:”
Kusudi hilo ni lipi? Ni kwamba sisi “tufananishwe na mfano wa Mwana wake,” Kila
kitu Mungu anachokiruhusu kutokea katika maisha yako kinaruhusiwa kwa kusudi
hilo.
Wapendwa wana wa Mungu,
sisi ni kama lulu, tumechongwa kwa nyundo na tezo ya taabu nyingi. Kama nyundo
ya sonara haina nguvu sana kuweza kuondoa mikwaruzo, Mungu atatumia nyundo
nzito zaidi. Kama sisi ni jeuri zaidi, anatumia nyundo nzito ya kunyanyuliwa na
chombo maalum. Atatumia chochote kile.
Hivyo, kila tatizo ni
nafasi ya kujenga tabia, na kadiri linavyokuwa gumu zaidi, ndivyo kunakuwa na
matokeo makubwa katika kujenga msuli wa kiroho na uadilifu. “Wala
si hivyo tu, ila na mfurahi katika dhiki pia; mkijua ya kuwa dhiki, kazi yake
ni kuleta saburi; na kazi ya
saburi ni uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini,” Rum 5:3-4.
Kila kinachotokea kwa maisha yako ya nje si cha muhimu sana kama kile
kinachotokea ndani yako. Mazingira yako ni ya muda mfupi, lakini tabia yako
itadumu milele.
Maandiko Matakatifu
hufananisha majaribu na moto wa kusafisha madini ambao huchoma takataka zote.
Mtume Petro anasema, “ili kwamba kujaribiwa kwa imani yenu, ambayo ina thamani
kuu kuliko dhahabu ipoteayo, ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa
kwenye sifa na utukufu na heshima,” 1Pet 1:7a-d. Mfua fedha aliulizwa, “Je,
unafahamu vipi kwamba sasa fedha ni safi? Alijibu, “ninapoona sura yangu ndani
yake.” Unapokuwa umesafishwa kwa majaribu, watu wanaweza kuiona sura ya Kristo
ndani yako. Yakobo anasema, “mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta
saburi,” Yak 1:3.
Kwa kuwa Mungu
anakusudia ufanane na Kristo, atakupitisha katika yale Yesu aliyopitia. Hii ni
pamoja na upweke, majaribu, dhiki, kulaumiwa, kukataliwa, na matatizo mengine
mengi. “Alijifunza kutii kwa njia ya mateso” na alikamilishwa kwa njia ya
mateso,” Ebr 5:8-9. Kwa nini Mungu atuepushe kutoka yale aliyomruhusu Mwana
wake kuyapata? Mtume Paulo anasema, “na
kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo;
naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye,” Rum 8:17.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Mateso ya mwenye haki ni mengi, Lakini Bwana humponya nayo
yote,” Zab 34:19
Tusali:-Ee Yesu, tujalie
ustahimilivu wako katika mahangaiko na mateso yetu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario