viernes, 2 de diciembre de 2016

TAFAKARI: JUMAPILI YA 2 YA MAJILIO YA MWAKA-A


JUMAPILI YA 2 YA MAJILIO YA MWAKA-A

Somo I: Isa 11:1-10

Zab: 72:1-2, 7-8, 12-13, 17

Somo II: Rum 15:4-9

Injili: Mt 3:1-12

Nukuu:

Basi litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda,” Isa 11:1 

 Na itakuwa katika siku hiyo, shina la Yese lisimamalo kuwa ishara kwa kabila za watu, yeye ndiye ambaye mataifa watamtafuta; na mahali pake pa kupumzikia patakuwa na utukufu,” Isa 11:10

“Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia,” Mt 3:2.

 “Kwa sababu huyo ndiye aliyenenwa na nabii Isaya, akisema, Sauti ya mtu aliaye nyikani, Itengenezeni njia ya Bwana, Yanyosheni mapito yake,” Mt 3:3.

 “Na Mungu mwenye saburi na faraja awajalie kunia mamoja ninyi kwa ninyi, kwa mfano wa Kristo Yesu; ili kwa moyo mmoja na kwa kinywa kimoja mpate kumtukuza Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo,” Rum 15:5-6

 “Kwa maana nasema, ya kwamba Kristo amefanyika mhudumu wa agano la kutahiriwa kwa ajili ya kweli ya Mungu, kusudi azithibitishe ahadi walizopewa baba zetu; tena ili Mataifa wamtukuze Mungu kwa ajili ya rehema zake; kama ilivyoandikwa, Kwa hiyo nitakushukuru kati ya Mataifa, Nami nitaliimbia jina lako,” Rum 15:8-9

TAFAKARI: “Kristo amefanyika mhudumu wa agano la kutahiriwa kwa ajili ya kweli ya Mungu, kusudi azithibitishe ahadi walizopewa baba zetu.”

Wapendwa wana wa Mungu, Leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya pili ya Majilio ya Mwaka “A” wa Kanisa. Masomo yetu yote matatu ya leo yanaufunua mpango mzima wa Mungu kumkomboa mwanadamu kutoka hali yake ya utumwa, mwili na roho. Ikiwa wewe na mimi ni tokeo la upendo wake, na tendo hilo kuufunua Utukufu wake, na hivyo kuibeba chapa yake ndani yetu, Mungu asingependa tupotee katika hali ya dhambi.

Na kulikamilisha hili, yaani, kumkomboa mwanadamu kutoka hali yake ya mateso, mahangaiko na dhambi, Mungu huyu aliye Kweli, Haki, Amani, na Upendo kwa makusudi makubwa anapenda kuanzisha uhusiano na yule aliyemuumba kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27. Tendo hili la kuujenga uhusiano wa karibu nasi linamshusha Mungu chini kabisa katika hali ya mwanadamu. Huu ni upendo mkubwa sana kwetu. Kipindi hiki cha majilio ni kipindi cha kutafakari upendo huu wa ajabu Mungu anaokwenda kutufanyia. Ikiwa zawadi hii ni kubwa sana kwetu hatuna budi kujiandaa vizuri mwili na roho ili atakapokuja atukute tupo safi na wenye afya njema hasa roho zetu.

Kufanikisha mpango huu, Mungu huyu aliye Alfa na 0mega atachukua hali yetu ya kibinadamu, na hivyo atazaliwa ikiwa ni moja ya kushiriki hali yetu ya kibinadamu. Jambo hili linatabiriwa na Nabii Isaya. Basi litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda,” Isa 11:1. Je huyu atakayezaliwa ataongozwa na mamlaka gani? Hakika kwa vile anakuja kuusimika ufalme wa kweli, haki, amani, na upendo, roho ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana,” Isa 11:2. Hivi ndivyo vitendea kazi vyake. Ujio wake kwetu ni hukumu pia ambayo itasimama katika haki. Hivyo, kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili; naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, na kwa pumzi ya midomo yake atawaua wabaya,” Isa 11:4 

Ujio wa mfalme huyu ni ujio wa neema na baraka. Anakuja na kusimika ‘mfumo wema’ na kuufifisha ‘mfumo uovu.’ Anakuja kuondoa sintofahumu zetu kati yetu wanadamu na viumbe vingine alivyoviumba. Huyu hakika ni Mfalme wa Amani. Hakutakuwa tena na sintofahumu kati ya wanyama aliowaumba. Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi; ndama na mwana-simba na kinono watakuwa pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza,” Isa 11:6. Mwanadamu ataishi kwa amani na hofu haitakuwepo tena. Na mtoto anyonyaye atacheza penye tundu la nyoka, na mtoto aliyeachishwa atatia mkono wake katika pango la fira,” Isa 11:8.

Uwepo wa Mfalme huyu wa kweli,  haki, amani na upendo utajidhihirisha kwa utukufu wake. Mataifa yote watamfuata alipo kwa sababu kuna Utukufu. “Na itakuwa katika siku hiyo, shina la Yese lisimamalo kuwa ishara kwa kabila za watu, yeye ndiye ambaye mataifa watamtafuta; na mahali pake pa kupumzikia patakuwa na utukufu,” Isa 11:10. Haya ndiyo atakayoyafanya na kuujenga tena uhusiano wetu ulioharibiwa na dhambi zetu.

Wapendwa wana wa Mungu, pamoja na hayo mazuri yote yaliyotabiriwa na Nabii Isaya kuhusu Mfalme huyu tunayemsubiri kwa hamasa kubwa, yatawezekana tu kama tutakuwa tayari kutoa ushirikiana naye. Mungu atukokoti kama Jemedari katili na mwenye silaha za kutisha. Utawala wake ni utawala wa Upendo. Mungu hapendi kuondoa uhuru na utashi wetu wa kumfuata. Ametuachia haya yote akijua kabisa kwamba kwa kuyatumia vizuri ni njia rahisi ya kumfikia, hata pale tutakapoyatumia vibaya itakuwa njia rahisi pia ya kumrudia tukifanya toba ya kweli na majuto.

Kama ilivyo kwa utawala mpya kuonyesha tofauti na utawala au tawala zilizotangua, tofauti hiyo ujionyesha katika kauli mbiu yake. Mfano: Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kabarage Nyerere, na sasa Mtumishi wa Mungu, alikuwa na kauli mbiu hizi kuonyesha utofauti wa utawala wake na ule wa kikoloni (Uhuru na Umoja, Uhuru na Maendeleo, na Uhuru na Ujamaa). Na alicho kilenga hapa Mwalimu Nyerere ni Uhuru wenye kuleta Umoja, Maendeleo, na Undugu, bila kujali tofauti zetu kiitikadi, kiimani, kifamili, kikoo, kikabila, na hata kijiografia. Dhima hii ndiyo inayotushikamanisha hadi leo kama Taifa licha ya kwamba kwa sasa twaziona nyufa.

Aliye mridhi, yaani, Rais Ali Hassani Mwinyi,  kadiri ya mazingira yake, na mabadiliko ya kiulimwengu katika maana ya kimfumo, yaani, ujio wa soko huria, akawa na kauli mbiu yake, “Ruksa.” Milango na madirisha yalifunguliwa na kila kitu hasa, kiuchumi vilikubaliwa. Mtoto mdogo mwenye pesa nyingi nyakati zile alipewa jina la MZEE, yaani, anazo! Aliye mfuata, ‘Mzee wa Ruksa,’ yaani, Rais Benjamin William Mkapa, naye hakuwa nyuma kuhusu kauli mbiu. Dira yake iliongozwa na haya: (Ukweli na Uwazi, Nguvu za Masikini ni mtaji wake mwenyewe, na ubinafsishaji wa mashirika ya Umma, ingawa vuguvugu hili lilianza kwa mtangulizi wake).

Baada ya kauli mbiu hii kupita, tulipata pia kauli mbiu nyingine kutoka kwa mrithi wa Rais Mkapa, yaani, Rais Jakaya Mrisho Kikwete. Dhamiri yake iliongozwa na upyaisho, yaani, kuleta nguu mpya. Na bila shaka wote tunaikumbuka kauli mbiu hii; “Nguvu mpya, kasi mpya, na hari mpya.” Na leo chini ya Rais wetu John Pombe Magufuli tunaongozwa na kauli mbiu hii; “Hapa kazi tu!”

Ndugu yangu, maisha yale yote yenye mwelekeo chanya hayakosi kuwa na msukumo wake, yaani, kauli mbiu yake. Na leo kwa namna ya pekee, ujumbe wa Yesu umebebwa na kauli mbiu hii: “Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia,” Mt 3:2. Kutubu ni dhamiri ya ndani yenye kukutaka kuyaanza yote upya katika maana ya kukataa kutoka ndani kuongozwa na yale ya kale, na yasiyo na upeo wa huko utakako kufika, na kwa maana hii, maisha yale ya umilele.

Alisemalo Yesu ‘Ufalme wa Mungu umekaribia,’ haikuwa mbwembwe za kisiasa ambazo mara nyingi kile kisemwacho majukwani sicho kimaanishwacho. Yesu anamaanisha kweli kile akisemacho, yaani, ukaribu huo wa ufalme wa Mungu ni uwepo wake mwenyewe kama pendo la Mungu lililo wazi, na Ufunuo wa Mungu usio na shaka. Na hii ndiyo maana ya maneno haya ya Yesu yaliyolandana na kile alichokisema katika kauli mbiu yake, kwamba,Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa,” Lk 4:18-19.

Ndugu yangu tunaye safiri sote katika tafakari hii, ujio wa Yesu sio wa kugushigushi au udanganyifu kama tuonavyo leo kwa wale wote wanaojitwalia mamlaka bila utaratibu. Ujio wa Kristo na Mkombozi wetu, ni mpango wa Mungu mwenyewe ulio jikita katika dhima nzima ya kumkomboa mwanadamu. “Kwa sababu huyo (yaani, Kristo) ndiye aliyenenwa na nabii Isaya, akisema, Sauti ya mtu aliaye nyikani, Itengenezeni njia ya Bwana, Yanyosheni mapito yake,” Mt 3:3. Kuyanyoosha mapita,’ ndicho kilicho beba kauli mbiu ya Yesu. Na hapo tutakapo yanyoosha mapito yetu, yaani, vilema vyetu, ndipo penye, neema na huruma ya Mungu. Nasi tunawajibu wa kufanya ili yale yote aliyoyaazimia Mungu ndani yetu yatimie. “Aliye kuumba wewe pasipo wewe hawezi kukukomboa wewe, pasipo wewe,” Mtakatifu Agustino wa Hippo.

Wajibu huu muhimu kuelekea neema na huruma ile ya Mungu ni kuukiri ukweli na kusimama katika kweli hiyo. Yohana Mbatizaji anawaongoza watu wake katika njia hiyo, kama maandalizi kwa ujio huo wa Mwokozi wetu. “Ndipo walipomwendea Yerusalemu, na Uyahudi wote, na nchi zote za kandokando ya Yordani; naye akawabatiza katika mto wa Yordani, huku wakiziungama dhambi zao,” Mt 3:5-6. Leo na katika mazingira yetu, Mama Kanisa anachukua nafasi hii ya Yohana Mbatizaji katika kuwaongoza wana wake katika kweli na haki, na kusimama katika kweli hili, bila kutetereka na kuishuhudia Imani ya kweli.

Furaha ya Mama Kanisa siyo kuona mtiririko wa watu waikimbiliayo njia hii kama ng’ombe waswagwao kuelekea zizini, bali furaha ya Mama Kanisa ni kuona kila aifuataye njia ya kweli anatambua sababu ya kufanya hivyo, na kuwa tayari kuishuhudia sababu hiyo mbele za watu. Hii ndiyo Imani ya kweli. Ni katika mazingira haya Yohana Mbatizaji anatoa angalizo kwa wale waliofuata mkumbo pasipo kujua maana ya kufanya hivyo. “Hata alipoona wengi miongoni mwa Mafarisayo na Masadukayo wakiujia ubatizo wake, aliwaambia, Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja?” Mt 3:7. Kumbe, lengo siyo kuukimbilia utukufu ule ulio mbele yako, bila kufuata njia ile ikupelekeayo kwenye tamanio hilo la utukufu. Kristo ndiyo mfano wenyewe, kwa sababu katika Kristo Yesu tunajifunza kwamba hakuna Utukufu pasipo Msalaba, na hakuna Pasaka bila Ijumaa Kuu. Na ukitaka kujua Mungu ni nani, Msalaba unasema yote kuhusu Mungu. Utafakari Msalaba!

Hivyo angalizo la Yohana Mbatizaji, na leo Mama Kanisa, ni kufanya toba, ili tuyapate matunda yake, yaani, neema, baraka, na huruma ya Mungu. “Basi zaeni matunda yapasayo toba; wala msiwaze mioyoni mwenu kwamba, Tunaye baba, ndiye Ibrahimu; kwa maana nawaambia ya kwamba Mungu aweza katika mawe haya kumwinulia Ibrahimu watoto,” Mt 3:8-9. Ndugu yangu, ingawa Kristo Yesu kesha inyoosha njia kuelekea maisha yale ya uzima wa milele, safari hiyo siyo mteremko mchirizo, bali kila mmoja lazima afanye sehemu yake, na katika ukamilifu wake, ingawa udhaifu upo.

Bila kufanya hivyo, sahau ndoto na tamaa ya uzuri huo wa umilele. Ukweli ni kwamba, mwenye kuijua siri hii aelewe kwamba, “shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni,” Mt 3:10. Kuijua kweli, na kutokuifanya au kuiishi kweli hiyo, kwa maanisha tarajio la epuko lile ambalo ndilo likutakalo kuifanya kweli hiyo ili uwe huru. Na usipo utaka ukweli huu ni kukubali epuko hilo ambalo katika lugha hii ya picha ni kutupwa motoni, mateso yasiyo na ukomo.

Licha ya kwamba Yohana Mbatizaji anaijua siri hiyo na kuwaongoza watu katika kweli hiyo, kwamwe hajiinui kwa lolote lile. Yohana anafahamu nafasi yake, na anatimiza wajibu wake katika ukamilifu wake. Naye anasema, “Kweli mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala sistahili hata kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto,” Mt 3:11. Ndugu yangu, Kanisa kama nafasi hii ya Yohana Mbatizaji, ni jumuiya ya Wakristo Wabatizwa, na mabao ndani yake wapo wadhambi na Watakatifu. Pamoja na ukweli huu, Kanisa ambalo ni mwili wa Kristo nasi viungo vya mwili huo,  haliachi kuwa Sakramenti ya wokovu wa mwanadamu.

Nguvu na uwepo huo wa Kristo katika udhaifu huu wa wana wa Mungu, yaani, wanadamu, Kristo uliongoza Kanisa katika kweli na haki, naye ubaki kuwa mizania ya kweli, na hakimu mwenye haki, “Ambaye pepeto lake li mkononi mwake, naye atausafisha sana uwanda wake; na kuikusanya ngano yake ghalani, bali makapi atayateketeza kwa moto usiozimika,” Mt 3:12. Huyu ndiye Masiha tunayemsubiri kwa hamu, na huyu ndiye Mkombozi wetu ambaye kila uvutapo pumzi yake Mungu, anakupa fursa ya kumgeukia na kuyaacha yale yote ya kale, na kuanza yote upya pamoja naye. Na hili ndilo tumaini hai, “kwa kuwa yote yaliyotangulia kuandikwa yaliandikwa ili kutufundisha sisi; ili kwa saburi na faraja ya maandiko tupate kuwa na tumaini,” Rum 15:4

Wapendwa katika Kristo, kipindi hiki cha majilio kinatutafakarisha pia kuhusu sala ya utakatifu. Sala ya utakatifu haina ubinafsi wala kujitanguliza. Ni sala inayotambua wengine walio na shida kama yako, na hata zaidi. “Na Mungu mwenye saburi na faraja awajalie kunia mamoja ninyi kwa ninyi, kwa mfano wa Kristo Yesu; ili kwa moyo mmoja na kwa kinywa kimoja mpate kumtukuza Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo,” Rum 15:5-6.

Hata pale tunapojisikia kuwa tumeachwa na kusahauliwa, hatuna sababu ya kulalamika zaidi ya kufurahia utukufu ule ambao tutaupata tukilishida jaribu hilo kwani Mungu anajua lazima tutashinda tunapoutumia uhuru wetu vyema bila kumuasi Mungu.Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili,” 1Kor 10:13.

Na tendo hilo la kuutumia vizuri uhuru aliotupa Mungu bila kumsaliti Mungu, linatuweka karibu zaidi na Mungu tunapojitoa bila kujibakiza kwa wengine na hasa wahitaji wakati huo huo bila kujisahau katika sala na ukaribu na Mungu. “Kwa hiyo mkaribishane ninyi kwa ninyi, kama naye Kristo alivyotukaribisha, ili Mungu atukuzwe,” Rum 15:7.

 Mtindo huu wa maisha ndio aliouishi Yesu Kristo angali hapa duniani ingawa Yeye alikuwa Mungu na Mwanadamu. Alijitoa bila kujibakiza katika mila na desturi ambayo waliokuwa na uwezo walijiinua na kuwasahau wale wote wasio kuwa na sauti katika jamii. Hivyo Yesu alikuwa sauti ya wasio na sauti, yaani, wakoma, wadhambi, viwete, vipofu, wazinzi, wanawake, watoto, na watoza ushuru. Hawa ndio waliokuwa jamaa na rafiki wa karibu wa Yesu. Kuwa kwake karibu hakukumaanisha alifurahia hali yao na hivyo ni utukufu kuwa hivyo, bali alikuwa karibu yao ili awatoe katika mateso na masikitiko yao. Na hili ndilo dhihirisho lililo wazi la Mkombozi wetu. Na kwa maana hiyo, “Kristo amefanyika mhudumu wa agano la kutahiriwa kwa ajili ya kweli ya Mungu, kusudi azithibitishe ahadi walizopewa baba zetu; tena ili Mataifa wamtukuze Mungu kwa ajili ya rehema zake; kama ilivyoandikwa, Kwa hiyo nitakushukuru kati ya Mataifa, Nami nitaliimbia jina lako,” Rum 15:8-9

 Hakina Kristo anatupenda upeo, Yoh 13:1, na kwa tendo hili la kumwilishwa, Yesu anaukubali umasikini ili wewe na mimi tuwe matajiri mwili na roho. “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake,” 2Kor 8:9. Ndugu yangu, utajiri wa kweli ni kumpata Kristo Yesu na kuishi ndani na katika Yeye tu. Na kwake tu, yaani, Kristo Yesu, kuna furaha ya kweli kwa sababu kwake tu tunapata sababu ya furaha, mateso, na mahangaiko yetu.

Daudi Jamali, mzaliwa wa Kigoma, katika kuyatafuta maisha mazuri na yenye hadhi, rafiki yake alimwamba nchini Kongo kuna dhahabu nyingi sana, na kuipata ni rahisi sana kwani watu wa huko Kongo uchimba umbali wa mita mbili tu.

Hivyo Daudi alianza safari yake ingawa hakujua ni sehemu gani huko Kongo kuna hiyo dhahabu. “Nitakwenda tu, na nitawauliza watu wa huko nami nitafika,” Daudi alijipa moyo.

Safari kutoka Kigoma hadi Kongo kwa miguu ilimchukua wiki mbili hivi. Akiwa katikati ya msitu mnene, hakujua mwelekeo wa kufuata. Na hapa aliona ulazima wa kuuliza. Mbele yake kulikuwa na Mzee mmoja, na baada ya kumuuliza Mzee huyo alimjibu, “Ukitaka kufika huko kwenye hiyo dhahabu yakupasa kurudi hadi pale ulipoanza safari yako. Hapa ulipo hutoweza kufika huko,” yule Mzee aliondoka taratibu.

Daudi alijishauri sana, akifikiria safari yake tena ya wiki mbili kurudi hadi Kigoma. Mwisho kwa unyonge alifanya maamuzi magumu na kurudi.

Ndugu yangu, hata wewe waweza kuwa kama Daudi Jamali. Ikiwa ushapotea na hicho ukiangaikiacho hujakipata, ni vyema kurudi pale ulipoanza safari yako, kwani kwa kufanya hivyo kuna uhakika wa kukipata hicho ulichokuwa unakitafuta kwa sababu hapa utapata ramani ya kufika kwenye nia yako. Na hii ndiyo toba ya kweli. Usitazame muda uliokwishapoteza, bali tumaini lile la kweli.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia,” Mt 3:2.

Tusali:-Ee Yesu na Mwokozi wetu, tunakutumainia. Usituache. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario