viernes, 23 de diciembre de 2016

TAFAKARI: KIPINDI CHA KUZALIWA BWANA, NOELI-MISA YA MCHANA


KIPINDI CHA KUZALIWA BWANA

NOELI: MISA YA MCHANA

Somo I: Isa 52:7-10

Zab: 98: 1, 2-3, 3-4, 5-6

Somo II: Ebr 1:1-6

Injili: Yoh 1:1-18

Nukuu:

Pigeni kelele za furaha, imbeni pamoja, Enyi mahali pa Yerusalemu palipokuwa ukiwa; Kwa kuwa Bwana amewafariji watu wake, Ameukomboa Yerusalemu,” Isa 52:9

“Bwana ameweka wazi mkono wake mtakatifu Machoni pa mataifa yote; Na ncha zote za dunia Zitauona wokovu wa Mungu wetu,” Isa 52.10

Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu,” Ebr 1:1-2

“Yeye kwa kuwa ni mng'ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu; amefanyika bora kupita malaika, kwa kadiri jina alilolirithi lilivyo tukufu kuliko lao,” Ebr 1:3-4

“Hata tena, amletapo mzaliwa wa kwanza ulimwenguni, asema, Na wamsujudu malaika wote wa Mungu,” Ebr 1:6

“Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu.Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika,” Yoh 1:1-3

“Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu,” Yoh 1:12-13

“Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli,” Yoh 1:14

TAFAKARI: “Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu.”

Wapendwa wana wa Mungu, “Pigeni kelele za furaha, imbeni pamoja, Enyi mahali pa Yerusalemu palipokuwa ukiwa; Kwa kuwa Bwana amewafariji watu wake, Ameukomboa Yerusalemu,” Isa 52:9. Leo katika adhimisho hili la Misa Takatifu, siku hii ya kuzaliwa Mwokozi na Mkombozi wetu Yesu Kristo, Misa hii ya Mchana,  Mama Kanisa kwa furaha kubwa, anatuzamisha ndani kabisa tutafakakari juu ya Umungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, ikiwa ni asili yake ya pili. Jana usiku kwenye Misa ile ya Kesha la Noeli, Mama Kanisa alifanya tafakari ya kina kuhusu ubinadamu wa Yesu Kristo. Hivyo asili hizi mbili ndizo alizokuwa nazo Yesu hapa duniani kwa ajili ya kile alichokijia, yaani, kutukomboa kutoka katika utumwa wa dhambi, na kuturudishia hadhi yetu tena ya kuwa wana na warithi wa ufalme wa mbinguni, na kuviratibisha vyote katika kweli na haki, kuelekea ukamilifu na upendo wa Mungu Baba.

Hivyo kadiri ya Injili ya leo, Mwinjili Yohane anatutafakarisha kwa undani kabisa asili hii ya Umungu wa Mwokozi na Mkombozi wetu Yesu Kristo. Ni kwenye sehemu hii ya Injili pia tunaona nani ni Yesu, na  nafasi yake ilikuwa wapi kabla ya kuumbwa kwa ulimwengu na vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. Siku hii ya leo Tukufu ya Mungu, kuzaliwa kwake Yesu Kristo, imeufunua ukweli ambao haukuwahi kujulikana tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Ukweli huo ni huu kwamba, “Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua,” Yoh 1:18. Huu ndio msingi na ufupisho wa hayo yote aliyoyasema Mwinjili Yohane.

Ufupisho huu unagusa subira yote katika historia nzima ya wokovu wetu, kama asemavyo Nabii Isaya, “Bwana ameweka wazi mkono wake mtakatifu Machoni pa mataifa yote; Na ncha zote za dunia Zitauona wokovu wa Mungu wetu,” Isa 52.10. Kwa hiyo, “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli,” Yoh 1:1, 14. Ni kwa sababu hiyo katika Mwili ni Mungu kama Baba.

Kwa uwezo wake wa Kimungu, hakuna chochote kilichokuwa pasipo Yeye, yaani,  neno huyu aliyefanyika mwili. “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu.Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika,” Yoh 1:1-3. Ni kwa maana hii na ukweli huu kwamba, ye yote amwonaye Kristo, amemwona Baba. Yesu kauthibitisha ukweli huu, kuiondoa shaka aliyokuwa nayo Filipo pale alipomtaka amwonyeshe Baba. Naye, “Yesu akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuonyeshe Baba?” Yoh 14:9. Lakini “kuona” huku kunawezeshwa tu kwa yule anayelisikia neno, yule ambaye kwa imani anaona zaidi ya “mwili,” yaani, utukufu wa Baba alioupokea. Kwa hiyo kuja kwake Mwokozi wetu ulimwenguni huku ni “utengano”: kuwatenga watu katika mwanga na giza, kama mwanga ambao ni wa ulimwengu. “Huyo hakuwa ile nuru, bali alikuja ili aishuhudie ile nuru. Kulikuwako Nuru halisi, amtiaye nuru kila mtu, akija katika ulimwengu,” Yoh 1:8-9. Mwilinjili Yohana hapa anamnukuu Yohana Mbatizaji kama mtengeneza njia.

Hivyo wapendwa katika Kristo, wote watakaoupokea mwanga huo wanaupokea kwa Imani ikiwa ndiyo zawadi kubwa aliyetuletea Mwokozi na Mkombozi wetu. “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu,” Yoh 1:12-13. Mwokozi na Mkombozi wetu leo hii anahitaji nafasi ndani ya Moyo wako. Bila shaka wengi wetu hii siyo Noeli ya kwanza kusherehekea. Basi nikuombe ufanye mabadiliko mwaka huu kama tendo la shukrani kwa Mungu. Yakupasa kufanya mkataba na Mungu kuhusu maisha yako, na iwe tendo lako la kudumu muda wote uwapo hapa duniani. Fanya hivyo na Mungu atakutumia vizuri kadiri ya mpango na hitaji lake.

Huna wakati mwingine tena katika maisha yako wa kufanya jambo hili ninalokuwambia. Kama Mungu ilifika mahali akasema basi na inatosha, kwa nini wewe usiseme pia basi inatosha kwa kuanza upya na Mungu? Ni Mungu huyu, “ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu,” Ebr 1:1-2. Leo tunapewa nafasi ya kuongea naye moja kwa moja na bila chenga.

Wapendwa katika Kristo, katika Ukuu na Umungu wake Mwokozi na Mkombozi wetu, “Yeye… ni mng'ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu; amefanyika bora kupita malaika, kwa kadiri jina alilolirithi lilivyo tukufu kuliko lao,” Ebr 1:3-4. Hivyo mwisho wa maisha yetu hapa duniani utakuwa na maana na uhakika wa umilele ndani na katika Kristo Yesu. Jamani Mungu yupo na huyu ndiye tunayemshangilia na kumsheherekea leo. Hatuna uzima pasipo Yeye.

Mwana falsafa, mwana mashairi, mwanamziki na mtaalamu wa lugha,  aliyejulikana sana, Friedrich Wilhelm Nietzche (1844-1900), hakuamini kuwa Mungu yupo. Nietzche alikuwa mzaliwa wa Urusi ya Zamani, ila maisha yake karibia yote aliishi Ujerumani. Falsafa yake ilijulikana kama “Nihilism and death of God,” kwa maana ya kwamba, “Vyote ni ubatili na kifo cha Mungu.”

Katika moja ya maandishi yake yaliyobeba falsafa hii alithubutu kusema “Mungu amekufa kwa hiyo hakuna Mungu.” Watu wengi wasioamini uwepo wa Mungu walishabikia sana falsafa yake na hasa eneo la Ulaya. Ila jambo la ajabu, tarehe 25 mwezi wa Agosti, 1900, Mungu alitangaza kuwa “Mwafalsa mashuhuri Friedrich Wilhelm Nietzche amefariki,” kwa ugonjwa wa Neumonia katika umri wa miaka 55.

Ndugu yangu uliyesafiri nami katika tafakari hii, kati ya Nietzche na Mungu, ni nani aliye mkweli? Tusisahau jambo hili: “Bwana huua, naye hufanya kuwa hai; Hushusha hata kuzimu, tena huleta juu. Bwana hufukarisha mtu, naye hutajirisha; Hushusha chini, tena huinua juu,” 1Sam 2:6-7

Tumsifu Yesu Kristo!

Bwana ameweka wazi mkono wake mtakatifu Machoni pa mataifa yote; Na ncha zote za dunia Zitauona wokovu wa Mungu wetu,” Isa 52.10

Tusali:-Ee Yesu na Mkombozi wetu, tuondolee upofu wetu wa Imana na kuacha kuona Umungu na Ubinadamu wako. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario