JUMAMOSI WIKI YA 2
YA MAJILIO-C
Somo: YbS 48:1-4, 9-11
Zab: 80, 2ac, 3b, 15-16,
18-19
Injili: Mt 17:10-13
Nukuu:
Bila shaka wamebarikiwa
wale waliokuona kwa macho, wakafa; lakini wewe umezidi kubarikiwa, kwa maana
unaishi,” YbS 48:11
“Naye akajibu, akawaambia, Kweli Eliya
yuaja kwanza, naye atatengeneza yote,” Mt
17:11
“ila nawaambia, ya kwamba Eliya amekwisha
kuja, wasimtambue, lakini wakamtenda yote waliyotaka. Vivyo hivyo Mwana wa
Adamu naye yuaenda kuteswa kwao,” Mt 17:12
TAFAKARI: “Wewe umezidi
kubarikiwa, kwa maana unaishi.”
Wapendwa wana wa
Mungu, kuuishi ushuhuda katika maisha si kitu cha ajabu. Kuishi ushuhuda ni
kuguswa na habari fulani katika maisha, na habari hiyo ikawa kielelezo na dira
ya maisha yako. Ushuhuda huu waweza kuwa mvuto wa maisha ya mtu yaliyojaa
maadili mazuri na roho ya upendo wa ajabu. Mvuto huu ukawa kioo cha kujitazama
na kuwa kielelezo cha maisha yako. Ushuhuda waweza kuwa wosia anaotoa mtu
uliojaa hekima na busara kwa wale anaowaacha. Hivyo watu wakavutwa na kuishi
wosia huo kama kielelezo cha maisha yao.
Mungu katika safari
ya wokovu wa mwanadamu alitumia watu mbalimbali kujifunua kwake na kuacha jumbe
mbalimbali kama kielelezo katika maisha. Watu hawa walikuwa: Waamuzi, Manabii,
Wafalme, na Mwishoni kabisa Neno aliyemwilishwa na kukaa kwetu. Kumbe baraka na
neema ziliwafikia waja wa Mungu kwa kupitia watu mbalimbali. Lakini pamoja na
neema na baraka hizo, kinachokaziwa hapa ni mwendelezo wa ile roho iliyoachwa
na wale wapeleka jumbe. Kuishi kwa ile roho katika mioyo ya watu ni kuzuri
zaidi kwa sababu ni kuishi katika uzima wa Mungu. Hivyo, “Bila shaka
wamebarikiwa wale waliokuona kwa macho, wakafa; lakini wewe umezidi kubarikiwa,
kwa maana unaishi,” YbS 48:11
Wanafunzi wa Yesu
wanamuuliza Yesu katika Injili ya leo, “kwa nini waandishi hunena ya kwamba
imempasa Eliya kuja kwanza?” Msingi wa swali hili unajijenga au kujikita katika
mwono wa Yesu ulivyo kwa jamii ile iliyomzunguka. Bila shaka kulikuwa na
mfanano mkubwa sana kati ya Yesu na Manabii waliomtangulia ikiwa ni pamoja na
Nabii Isaya. Naye Yesu anawajibu wanafunzi wake, “Kweli Eliya yuaja kwanza,
naye atatengeneza yote,” Mt 17:11. Bila shaka
hapa Yesu anamzungumzia Yohane Mbatizaji kwani ndiye aliyeitoboa siri ya
Masiha, yaani, Yesu Kristo kadiri ya utabiri wa Nabii Isaya. “Kwa sababu
huyo ndiye aliyenenwa na nabii Isaya, akisema, Sauti ya mtu aliaye nyikani,
Itengenezeni njia ya Bwana, Yanyosheni mapito yake,” Mt 3:3. Watu waliishi roho
hii na matumaini haya ingawa hawakujua ni lini itakuwa kweli.
Kwa kuufafanua ukweli huu, Yesu anaenda
mbali zaidi na kusema, “ila nawaambia, ya kwamba Eliya amekwisha kuja,
wasimtambue, lakini wakamtenda yote waliyotaka. Vivyo hivyo Mwana wa Adamu naye
yuaenda kuteswa kwao,” Mt 17:12. Huyu waliyemtenda kama walivyotaka ni Yohani
Mbatizaji ambaye alikatwa kichwa siku ya sherehe ya ukumbusho wa kuzaliwa
Herode, Mk 6:21-29. Mauti yanamfika Yohane Mbatizaji kwa kusimamia kweli na
haki. Yohane Mbatizaji alimkemea Mfalme Herode kwa tendo baya la kumchukua mke
wa ndugu yake Filipo. “Kwa maana Herode mwenyewe alikuwa ametuma watu,
akamkamata Yohana, akamfunga gerezani, kwa ajili ya Herodia, mkewe Filipo ndugu
yake, kwa kuwa amemwoa; kwa
sababu Yohana alimwambia Herode, Si halali kwako kuwa na mke wa nduguyo,” Mk
6:17-18.
Kifo cha Yohane Mbatizaji kinaashiria pia kifo cha Yesu Kristo. Yesu analiona hilo katika maisha
yake. Kwetu ni ushuhuda wa maisha kwamba tunaposimama katika kweli na haki,
maisha hayo yatatugharimu. Hata kama tutakufa kwa kuishi ushuhuda huu, tutaishi
na Kristo milele kwa sababu Yeye ndiyo kielelezo halisi cha maisha yetu. Huyu
ndiye Masiha tunayemsubiri. Tunapomsubiri Masiha wetu kwa hamasa hii kubwa na
matumaini, yatupasa pia kutambua mapaswa yetu katika ufuasi wake.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Na kila mwenye matumaini haya katika yeye hujitakasa,
kama yeye alivyo mtakatifu,” 1Yoh 3:3
Tuombe:-Ee Yesu, wewe tu wapaswa kutukuzwa na
kuhimidiwa milele. Kwako ipo Njia, kweli, na Uzima. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario