Sikukuu ya Mt. YOHANA MTUME na mwinjili
DECEMBA 27
Somo: 1Yoh 1:1-4
Zab: 97:1-2, 5-6, 11-12
Injili: Yoh 20:1, 2-8
Nukuu:
“Lile
lililokuwako tangu mwanzo, tulilolisikia, tuliloliona kwa macho yetu, tulilolitazama,
na mikono yetu ikalipapasa, kwa habari ya Neno la uzima,” 1Yoh 1:1
“hilo tuliloliona na kulisikia, twawahubiri na
ninyi; ili nanyi pia mpate kushirikiana nasi: na ushirika wetu ni pamoja na
Baba, na pamoja na Mwana wake Yesu Kristo,” 1Yoh 1:3
“Basi akaenda mbio, akafika kwa Simoni Petro
na kwa yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda, akawaambia, Wamemwondoa
Bwana kaburini, wala hatujui walikomweka,” Yoh 20:2
“Basi Petro akatoka, na
yule mwanafunzi mwingine, wakashika njia kwenda kaburini,” Yoh 20:3
“Basi akaja na Simoni Petro, akaingia ndani ya
kaburi,” Yoh 20:6
“Basi ndipo alipoingia
naye yule mwanafunzi mwingine aliyekuwa wa kwanza wa kufika kaburini, akaona na
kuamini,” Yoh 20:8
TAFAKARI: “Na
haya twayaandika, ili furaha yetu itimizwe.”
Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Mtume
Yohane na Mwinjili. Yohane mwana wa Zebedayo alikuwa mmojawapo kati ya Mitume wa
Yesu, ambaye alipendwa na mwalimu wao kuliko wenzake wote. Mapokeo
ya Kanisa yanamuona kuwa mwandishi wa Injili ya
Yohane, wa barua tatu (Waraka wa kwanza wa Yohane, Waraka wa pili wa Yohane, Waraka wa tatu wa Yohane) na wa Kitabu cha
Ufunuo.
Mtume Yohane alizaliwa
na Salome baada ya Yakobo Mkubwa
mwanzoni mwa karne ya 1 B.K. akafa mkongwe mwishoni mwa karne hiyo huko Efeso (katika Uturuki
wa leo). Kabla ya kumfuata Yesu Kristo alikuwa mvuvi na mfuasi wa Yohane Mbatizaji Ndiye shahidi mkuu wa miaka mitatu hivi ya utume wa Yesu, akiwa wa kwanza
kumfuata (pamoja na Mtume Andrea), mshiriki wa matukio ya pekee ya
mwalimu wake (kama alipogeuka sura mlimani), mtume pekee aliyesimama chini ya msalaba,
wa kwanza kusadiki ufufuko wa Yesu hata kabla hajamuona.
Kutokana na
udhati wa teolojia
yake alifananishwa na Tai (Ndege) mwenye kuruka juu zaidi angani, na kuyaona yaliyo
yote vizuri chini. Yohane Mtume anaheshimiwa na madhehebu karibu yote ya
Kikristo kama Mtakatifu, hasa tarehe 27 Decemba.
Mpendwa katika Kristo, pamoja na Injili ya leo kuelezea tukio la
ufufuko wa Bwana Yetu Yesu Kristu, Yoh 20:1, imekazia mambo makuu mawili. Kwanza, nafasi ya Kanisa, na pili, nafasi ya Mtume Petro, ikiwa
ni pamoja na kujitambua kwake Mtume Yohana ambaye leo kwa namna ya pekee
tunaadhimisha sikukuu yake. Kwa namna ya pekee leo naomba tuyatafakari mambo
haya.
Tuelewe
kwamba Yesu Kristo alikwisha weka mfumo fulani wa uongozi kabla ya mateso, kifo
na ufufuko wake. Ni katika mfumo huyo wafuasi wake wapaswa kuufuata. “Nami
nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba wako huu nitalijenga Kanisa
langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda,” Mt 16:18. Jambo hili na nafasi
hii ya Petro inajitokeza na kujionyesha wazi wakati wa Ufufuko wa Bwana wetu
Yesu Kristo. “Basi akaja na Simoni Petro, akaingia ndani ya
kaburi,” Yoh 20:6.
Licha ya kwamba Mtume
Yohani ambaye Yesu alimpenda sana kuliko Mitume wote, ikiwa ni moja ya sifa
yake na uhusiano wake na Yesu Kristo, pia alikuwa ni kijani kuliko wote; hakuwa
wa kwanza kuingia katika kaburi licha ya kwamba alikimbia kuliko Mtume Petro na
kufika wa kwanza Kaburini baada ya kupata taarifa ya Kristo Mfufuka.
Yohane Mtume anatambua
nafasi ya Petro kama kiongozi halali aliyepewa mamlaka na Kristo mwenyewe. Hapa
ndipo tunapoona nafasi ya Baba Mtakatifu kama HALIFA wa Kristo. Huyu ndiye
Petro, yaani mwamba ambapo Kanisa lake limeoteshwa na kukua. Na hapa ndipo
tunapoona umoja wa Baraza la Maaskofu na Mwenyekiti wao kama msemaji Mkuu wa Kanisa
mahalia.
Kwa sababu hiyo, Mtume
Petro anakuwa wa kwanza kuingia Kaburini. Na baada ya Petro, Mtume Yohane
anaingia na kuona na kuamini. “Basi ndipo alipoingia naye yule mwanafunzi
mwingine aliyekuwa wa kwanza wa kufika kaburini, akaona na kuamini,” Yoh 20:8.
Kuona na kuamini kwa Mtume Yohane, kunachukuliwa kwa namna mbili;
Moja, Mtume Yohane mwenyewe kwa upendo
aliokuwa nao Kristo juu yake, na upendo wa Mtume Yohane juu ya Kristo. Kwa kuonyesha
furaha na upendo wake kwa Kristo, Yohana Mtume anaongea kwa niamba ya Kanisa,
na kusema, “Na haya twayaandika, ili furaha
yetu itimizwe,” 1Yoh 1:4
Pili, Yohane Mtume
katika jambo hili la kuona na kuamini, anasimama badala ya Kanisa kama
mshuhudia na mshuhuda wa kweli wa ufufuko wake Yesu Kristo. “Lile lililokuwako tangu mwanzo, tulilolisikia,
tuliloliona kwa macho yetu, tulilolitazama, na mikono yetu ikalipapasa, kwa
habari ya Neno la uzima,” 1Yoh 1:1. Ndugu yangu tunaye safiri sote katika tafakari
hii, huwezi kutoa ushuhuda wa Neno kama huna uwezo wa kulishirikisha Neno.
Huwezi lishirikisha Neno kama ukuweza kulitafakari Neno hilo. Huwezi litafakari
Neno kama ukuweza kulipokea Neno hilo. Na hutoweza kulipokea Neno kama
ukulisikia Neno. Na “hilo tuliloliona na kulisikia, twawahubiri na ninyi; ili
nanyi pia mpate kushirikiana nasi: na ushirika wetu ni pamoja na Baba, na
pamoja na Mwana wake Yesu Kristo,” 1Yoh 1:3
Kumbe kuwa shuhuda wa Neno kutanipasa haya
yafuatayo; kulisikia Neno, kulipokea Neno, kulitafakari (ikiwa ni pamoja na
kulitafiti) Neno, na kulishirikisha Neno. Hatua hizi ndizo ziletazo uzima kwa
Neno lile tuishilo. “(Na uzima huo ulidhihirika, nasi tumeona, tena
twashuhudia, na kuwahubiri ninyi ule uzima wa milele, uliokuwa kwa Baba,
ukadhihirika kwetu),” 1Yoh 1:1
Kanisa tuishilo leo na
sasa linaishi katika ushuhuda huu wa Ufufuko. Kanisa halipo kama hakuna Imani hii
ya Ufufuko. Je, jambo hili linasema nini kuhusu vipaumbele vyako katika Imani?
Ndugu yangu, yale
ambayo yanachukua muda wako mwingi katika maisha yako, ndiyo hayo yanayo akisi
maisha yako baada ya kifo. Yawezekana hadi sasa huna mpangilio wa maisha yako.
Mambo ya muhimu kufanya katika maisha
yako mapya ya ufufuko ni haya;
Moja, Mshukuru Mungu
kwa kukutumia vyema, endapo unaishi vyema utume wako kadiri ya wito wako.
Katika jambo hili utafunuliwa siri ya umilele.
Pili, kila mmoja wetu
yampasa kufanya mkataba na Kristo kama ishara ya kuanza maisha mapya ya
ufufuko. Mkataba wako ulenge kufanya
jambo jema kwa ajili ya Kristo kila siku. Hapa haitegemei ukubwa wa jambo au
udogo wake.
Tatu, lifanye jambo
hilo kuwa kiu yako kila siku na usichoke kulifanya. Nakuhakikishia utaanza
kuona mabadiliko makubwa katika maisha yako yakiambatana na Neema na Baraka za
ajabu.
Nne, Sala kuu yako iwe
kushukuru hata kwa yale ambayo bado kuyapata. Hapa ni kumwachia Kristo usukani
wa maisha yako. Yesu Kristo ndiye dereva maarufu kuliko wote waliokwisha
kutokea. Yeye ndiye “Njia, na Ukweli, na
Uzima,” Yoh 14:6
Na mwisho, omba kifo
Chema kila siku na hasa mara uamkapo. Sala hii iambatane na Neema ya kutoa
msamaha bila kujibakiza.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Basi mkiwa
mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono
wa kuume wa Mungu,” Kol 3:1
Ee Yesu, nijalie neema ya kutafuta
yale yakuelekeayo katika maisha yangu kila siku. Amina.
Mtakatifu Yohana Mtume, na
Mwinjili, Utuombee
No hay comentarios:
Publicar un comentario