JUMAPILI YA 4 YA MAJILIO YA MWAKA-A
Somo
I: Isa 7:10-14
Zab: 24:1-2, 3-4, 5-6
Rum 1:1-7
Injili: Mt 1:18-24
Nukuu:
“Naye akasema,
Sikilizeni sasa, enyi nyumba ya Daudi; Je! Ni neno dogo kwenu kuwachosha
wanadamu, hata mkataka kumchosha Mungu wangu pia?” Isa 7:13
“Kwa hiyo Bwana
mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanaume,
naye atamwita jana lake Imanueli,” Isa 7:14
“Kuzaliwa kwake Yesu
Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla
hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu,” Mt 1:18
“Naye Yusufu, mumewe,
kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri,”
Mt 1:19
“Basi alipokuwa
akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema,
Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa
uweza wa Roho Mtakatifu,” Mt 1:20
“ambaye katika yeye
tulipokea neema na utume ili mataifa yote wapate kujitiisha kwa imani, kwa
ajili ya jina lake,” Rum 1:5
“ambao
katika hao ninyi mmekuwa wateule wa Yesu Kristo,” Rum 1:6
TAFAKARI: “Yusufu, Mumewe Bikira Maria, Mtu wa
haki.”
Wapendwa wana wa Mungu, Mama Kanisa leo anapoadhimisha
Dominika ya nne ya Majilio ya Mwaka “A” wa Kanisa, tunaalikwa kutafakari
“Mpango wa Mungu wa wokovu wa mwanadamu; kupitia wanyenyekevu wa Moyo.” Mungu
aliye kusudi la mwanadamu, alikuwa na mpango na mwanadamu tangu kabla ya kuumba
ulimwengu. Hakuna shaka kwamba uumbaji wa ulimwengu huu pamoja na uzuri wake ni
kwa mafaa ya mwanadamu na ufunuo wa Utukufu wa Mungu.
Binadamu huyu aliyekuwa
kusudi la Mungu tangu kabla ya kuumbwa ulimwengu, kwa bahati mbaya tendo hili
ya pekee kwake hulichukulia la kawaida tu, na wakati mwingine kama mastahili
yake. Kiburi hiki cha mwanadamu ndicho kimtiacho majaribuni na kujitenda na
Mungu kwa kutenda dhambi.
Hata baada ya kuanguka
kwa sababu ya dhambi, Mungu kwa upendo wake hakuacha mpango wake wa kumkomboa
mwanadamu. Huu ni upendo wa ajabu sana wa Mungu kwetu. Mungu kwa mara hii,
anakubali kuchukua umbo letu na kufanana nasi-“Kumwilishwa,” ili awe karibu
zaidi nasi. Mpango huu anaufunua kwa njia ya Ishara kupitia Nabii Isaya, na
kusema, “Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua
mimba, atazaa mtoto mwanaume, naye atamwita jana lake Imanueli,” Isa 7:14.
Ishara hii inakuwa wazi kupitia wale waliojawaliwa maisha ya unyenyekevu.
Bikira Maria anakuwa
kati ya wanyenyekevu wa Moyo wa Mungu na aliyempendeza kwa namna ya pekee.
Bikira Maria anachukua jukumu la mzazi wetu wa kwanza-Eva, aliyeshindwa kwa
anguko la dhambi. Bikira Maria anapewa mastahili haya kwa unyenyekevu wake, na
siyo kwa sababu alikuwa mzuri sana au binti wa pekee sana katika mtaa wake au
kijiji chake, au maarufu yake binafsi na familia yake. Mastahili haya anapewa
Bikira Maria kwa sababu ya udogo wake na unyenyekevu wake.
Malaika anatoa siri hii na mpango huu wa Mungu
kwa Mama Bikiria Maria. Tendo hili linampa Bikira Maria hofu kubwa sana.
Anapata hofu kwa kuona mpango mkubwa kama huu utakuwaje na yeye ni nani hata
Mungu ayafanye hayo yote kwake? Malaika anapoona hofu hii, anamwambia,
“Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba
na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu,
ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba
yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna
mwisho,” Lk 1:30-33
Ndugu yangu, kama hili
lingetokea kwako, ungelibeba moyoni kwa unyenyekevu kama wa Bikira Maria? Leo
mmoja wetu anapochaguliwa kwa nafasi mfano ya Ubunge, tena wakati mwingine kwa
wizi wa kura, ona anavyojipambambanua kwa sifa bungeni. Nusu saa nzima kutoa
shukrani zilizojaa majigambo, mbwembwe nyingi, na mwisho wa siku hakuna
anachofanya kwa kujitoa kwa wale waliomchagua. Ipo mifano mingi sana ya
kutokuwa na unyenyekevu kama huu wa Bikira Maria. Tujifunze kwa Mama yetu
Bikira Maria.
Yesu Kristo, ambaye
anabeba dhambi za sisi wanadamu, analo jambo moja tu la kufanya. Nalo ni
kufanya mapenzi ya Mungu, na si yake. Huu pia ni unyenyekevu wa hali ya juu. Ni
sadaka kubwa sana mtu anapoazimia kuutoa uhuru wake wote kwa sababu ya mtu
mwingine. Kuwa tayari kufanya yote bila kujibakiza kwa maelezo ya mtu mwingine
bila kuhesabu faida ni sadaka kubwa sana. Hii ni sadaka kubwa sana isiyo na
kipimo. “Ndipo aliposema, Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako. Aondoa la
kwanza, ili kusudi alisimamishe la pili,” Ebr 10:9. Utii ni sadaka kubwa sana
unayeweza kutoa. Huwezi kuwa mtii kama si mnyenyekevu.
Ndugu yangu,
tunatafakari makuu haya ya Mungu kupitia mjakazi wake Mama Bikira Maria,
tujifunze kuwa wanyenyekevu kama Mama yetu Bikira Maria. Anza zoezi hili pale ulipo.
Lianze kwenye familia yako na lifanye kadiri ya nafasi yako katika hiyo familia
kwa kuyatimiza yote yanayokuhusu kwa unyenyekevu. Pili, lifanye jambo hili
katika sehemu yako ya kazi, na sehemu yeyote unapowajibika kwa ajili ya
wengine. Ndugu yangu, ukilifanya hili kwa moyo mkunjufu hakika Mungu atatenda
mambo makuu kwako.
Wapendwa
wana wa Mungu, sehemu hii ya Injili tuliyoisoma leo, na hasa, Mt 1:18-19,
inatufanya tujiulize swali hili. Kwa nini Yusufu alikusudia kumwacha Mariamu
ikiwa walikuwa bado kuoana? Ukweli ni kwamba, mila na desturi za Kiyahudi
zilikuwa tofauti na zetu. Mwanaume na mwanamke waliunganishwa pamoja wakati
wanapopeana miadi ya kuoana (uchumba), ingawa hawakuruhusiwa kuhusiana kimwlili
hadi baada ya harusi. Yusufu alikuwa anapanga kuuvunja uchunba wao rasmi baada
ya kugundua kuwa Mariamu ana mimba ili hali hakuwahi kukutana naye kimwili.
Yusufu anataka
kulifanya jambo hili kuwa siri ili kumnusuru Mariamu kifo cha aibu ambacho
kingempata kama jambo lile lingegundulika katika jamii. Kama Yusufu angetaka
kutafuta haki yake, sheria ilisema hivi kuhusu ubikira; “Mtu akitwaa mke, akamwingilia na
kumchukia, kisha akamshitaki
mambo ya aibu kumzushia jina baya, akasema, Nimemtwaa mwanamke huyu, nami
nilipomkaribia sikuona kwake alama za ubikira; Lakini likiwa ni kweli neno hili, la
kutoonekana kwake yule kijana alama za ubikira; na wamtoe nje yule kijana (kike)
mlangoni pa nyumba ya baba yake, na waume wa mji wake wampige kwa mawe hata
afe; kwa vile alivyofanya upumbavu katika Israeli, kwa kufanya ukahaba katika
nyumba ya baba yake; ndivyo utakavyoondoa uovu katikati yako,” Kumb 22:13-14,
20-21. Kwa hali aliyokuwa nayo Mariamu si tu tatizo la ubikira, ila alionekana
ana mimba. “Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama yake
alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa
uweza wa Roho Mtakatifu,” Mt 1:18
Kwa vile Yusufu
alimpenda sana Mariamu aliona ni vyema kumwondoa katika aibu ile, ili asife kwa
kupigwa mawe. “Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake
kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri,” Mt 1:19. Hapa ndipo tunapoona utu wa
Yusufu. Utu huu ndio unaomfanya kuhesabiwa haki na Mungu kama mtu wa haki.
Yusufu hakupenda kulihukumu jambo lile asilolijua.
Yusufu alimjua vizuri
Mariamu ikiwa ni pamoja na malezi aliyopata kutoka kwa wazazi wake. Hata hivyo
tukio hili la mimba lilibaki kitendawili kikubwa kwa Yusufu. Kwa upande
mwingine hapa tunafundishwa kwamba ukiwa na mashaka na kitu fulani usitende
chochote. Jambo au kitu kile kipe kwanza Muda. Kitendo cha Yusufu kutaka
kumwacha kwa siri Mariamu ilikuwa kulipa jambo lile muda. “Basi alipokuwa
akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema,
Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa
uweza wa Roho Mtakatifu,” Mt 1:20. Je, ingetokea kwako au kwangu kwa namna
yoyote ile ungelipa jambo hili muda?
Pamoja na hakikisho
hilo la Mungu kuhusu mimba ile, Yusufu anapewa ufahamu juu ya kile
kitakachozaliwa ambacho kinaonyesha wazi makusudi na upendo wa Mungu kwa
wanadamu. Mama Bikira Maria “atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana,
yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao,” Mt 1:21. Huyu atakayezaliwa
atakuwa upatanisho, daraja, na mahusiano mapya kati yetu sisi wanadamu na
Mungu. Jambo hili linamtia ujasiri Yusufu na hivyo kuacha mpango wake ule wa
kumwacha Mariamu kwa siri. “Naye Yusufu alipoamka katika usingizi, alifanya
kama malaika wa Bwana alivyomwagiza; akamchukua mkewe.” Mt 1:24
Swali lingine ambalo
linatujia katika habari hii, Mt 1:18, ni hili; Je Mariamu alikuwa na mimba kwa
uwezo wa Roho Mtakatifu, au Yesu alikuwa uzao wa viuno vya Daudi kwa mujibu wa
Mdo 2:30?-(“Basi kwa kuwa ni nabii, akijua ya
kuwa Mungu amemwapia kwa kiapo, ya kwamba katika uzao wa viuno vyake
atamketisha mmoja katika kiti chake cha enzi”). Mariamu alikuwa bikira;
Biblia inasema Roho Mtakatifu "alimfunika" Mariamu, si kwa jinsi ya
kuhusiana kimwili. Yusufu alikuwa baba pekee wa kisheria aliyemuasili Yesu,
hakuwa baba halisi.
Lakini Yesu alikuwa
mzao halisi wa ukoo wa Daudi kupitia Mariamu, kama orodha ya vizazi yenye
kupitia kwa Mariamu ya Lk 3:23-37 inavyoonyesha. Aya nyingine zenye kusema kuwa
Yesu ni mtoto (mzao wa ukoo) wa Daudi ni Mat 12:23; 15:22; 20:30; 21:9,15;
Marko 10:47-48; 12:35; Luka 10:41; 18:38-39; Yoh 7:42; 2 Tim 2:8; Ufu 5:5;
22:16. Je, Mat 1:23 (Tazama, bikira atachukua
mimba, Naye atazaa mwana; Nao watamwita jina lake Imanueli; Yaani, Mungu pamoja
nasi) inatafsiri Isa 7:14 (Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira
atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli)
kimakosa kwa kutumia jina "bikira?"
Jibu ni hapana. Si tu kwamba neno la Kiebrania lililotumiwa
hapa linamaanisha amaa "bikira" ama "msichana", lakini pia
tafsri ya Kigiriki ya Agano la Kale (Septuagint) imelitafsiri neno hili kuwa
“parthenos,” yaani bikira. Swali lingine ambalo tunaweza kujiuliza ni hili:
Kwenye Mat 1:23 na Lk 1:26-35, inawezekanaje Yesu aliyezaliwa na bikra awe mzao
wa ukoo wa Daudi? Hapa kuna mambo matatu ya kuzingatia;
1. Yesu hakuwa mtoto halisi wa Yusufu. Kama angekuwa, Yer
29:32 ingekuwa ni unabii wa uongo.
2. Yesu
alikuwa mtoto wa Yusufu kisheria. Leo hii, mwanaume anayemuoa mwanamke aliye na
mtoto anakuwa baba wa mtoto huyo kisheria, ingawa si baba halisi.
3. Yesu alikuwa mtoto
halisi wa Mariamu. Yesu alikuwa wa ukoo wa Daudi kisheria kupitia Yusufu, na
Yesu alikwa wa ukoo wa Daudi kiuhalisi kupitia Mariamu. Kadiri ya Mat 1:25, “asimjue
kamwe hata alipomzaa mwanawe; akamwita jina lake YESU,” Mt 1:25”. Je Mariamu alikuwa na watoto wengine wowote?
Mstari huu hautakuwa na maana yeyote na wenye kupotosha kama Yusufu na Mariamu
hawakuwa wamewahi kuwa na uhusiano wa kimwili.
Zaidi ya hapo, Mat 13:55-56; Mak 6:4; Gal 1:19; na Yuda 1 pia
zimerekodi kuwa Yesu alikuwa na wadogo wake wa kiume (ndugu). Eusebius, katika
kitabu chake kiitwacho Ecclesiastical History (karibu mwaka 360 BK) 2:23 na d
3:20 pia anasema kuwa wadogo wane wa kiume wa Yesu walikuwa Yakobo aliyeitwa
mwenye haki), Yose (au Yusufu), Yuda na Simoni.
Moja ya majibu yatolewayo na Kanisa Katoliki ni kuwa Yusufu
alikuwa na watoto kupitia ndoa yake ya awali, lakini si kupitia kwa Mariamu.
Hata hivyo, hakuna ushahidi toka kwenye historia ya Kanisa kuwa Yusufu aliwahi
kuwa na ndoa nyingine kabla ya ile na Mariamu, au mdogo wake yoyote wa kiume
hakutokana na Yusufu na Mariamu.
Jibu lingine la Kanisa Katoliki ni kuwa kwenye jamii za
Kimediteraniani neno "ndugu" linaweza kumaanisha binamu na
ndugu/jamaa wa karibu wenye umri unaofanana, na si tu kaka au wadogo wa mtu.
Hata hivyo, Ambrose wa Milani alikuwa wazi kuwa Yesu hakuhitaji msaada wowote
ili aweze kuwaunganisha watu na Mungu, na Mariamu hakupaswa kusujudiwa (On the
Holy Spirit kitabu cha 3 sura ya 11 na.80 mwaka 381 BK). Alisema, "Na mtu
yeyote asihamishie jambo hili kwa Bikira Mariamu; Mariamu alikuwa hekalu la
Mungu. Na kwa hiyo Yeye (Mungu) pekee ndiye anayepaswa kuabudiwa Yeye afanyaye
kazi katika hekalu lake (mwenyewe)."
Wapendwa wana wa Mungu,
pamoja na kuona ukweli huo hatuwezi kupinga kwamba yote hayo yalifanyika chini
ya mpango mzima wa Mungu. Mungu hawezi kujikanganya mwenyewe. Hivyo Nabii
Yeremia anasema, “Tazama siku zinakuja, asema
Bwana, nitakapomchipushia Daudi Chipukizi la haki; naye atamiliki mfalme,
atatenda kwa hekima, naye atafanya hukumu na haki katika nchi,” Yer 23:5. Huyu ndiye Bwana wa haki na utawala wake ni
utawala wa hekima na hukumu zake ni za haki. Ujio wa Masiha ni habari ya wokovu
na kuwekwa huru mwili na roho. “Katika siku zake Yuda ataokolewa, na
Israeli atakaa salama, na jina lake atakaloitwa ni hili, Bwana ni haki yetu,”
Yer 23:6. Basi na tuwe watu wa haki, tukitenda yaliyo kweli na haki, na
kuhukumu kwa haki.
Wapendwa wana wa Mungu,
ulimwengu wetu wa leo pamoja na maendeleo yake, binadamu amefikia hatua ya
kufikiri na kuishi bila Mungu. Watu walio wengi leo sio kwamba hawataki kuamini
kuwa Mungu yupo bali hawataki kusikia kabisa kuhusu Mungu. Leo walio wengi
uweka umuhimu wao katika kazi zao, namna ya kupata pesa, namna ya kupata
umaarufu, na mwisho wa siku namna ya kuyafurahia maisha. Tupo kwenye ulimwengu
wa vitu na kuviabudu vitu hivyo ndiyo imekuwa
sanamu ya kila siku.
Lakini pamoja na hayo
yote tunashindwa kuelewa ukweli huu, kwamba,
“Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, Dunia na wote wakaao ndani
yake,” Zab 24:1. Na uthibitisho wa kweli hii ni kwamba ‘hakuna binadamu ye yote
katika ulimwengu huu pamoja na utajiri aliokwisha kuwa nao mwisho wa siku
alifanikiwa kuondoka nao.’
Maisha ya mwanadamu
bila Mungu hayana maana yoyote. Uwepo wako hapa duniani ni kwa sababu Mungu
alipenda uwe hivyo na alikuwa na mpango nawe hata kabla ya kutungwa mimba
kwako. Hivyo hakuna mtu anayeishi kwa ajili yake mwenyewe. Kwa maana,
“mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni
jiwe kuu la pembeni,” Efe 2:20. Yesu Kristo ndiyo msingi wa yale yote
tuyafanyayo kwa sababu kwa kupitia Yeye yote tuyaonayo kwa macho yetu
yalifanyika. “Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho
chote kilichofanyika,” Yoh 1:3. Hapa ndipo tunapouona Umungu wa Yesu na uwezo
wake juu ya vitu vyote.
Je,
wa mwamini Yesu Kristo? Mtume Paulo anatuambia wazi kwamba, ni katika Yesu
Kristo, “ambaye katika yeye tulipokea neema na utume ili
mataifa yote wapate kujitiisha kwa imani, kwa ajili ya jina lake,” Rum 1:5.
Katika jambo hili la msingi, Yesu Kristo ndiye njia ya safari yetu ya maisha ya
umilele na hakuna mbadala wake. Kwa kuuishi ukweli huu, na kuufanya wengine
wauishi kwa kujitoa kwetu pasipo kujibakiza ndiko kunakotufanya sisi kuwa
wateule wa Kristo.
Hivyo kwa kupitia hawa
tuliojitoa kwao bila kujibakiza ili wamjue Mungu, wampende, wamtumikie na
mwisho warudi kwake kwenye uzima wa milele, “katika hao ninyi mmekuwa wateule
wa Yesu Kristo,” Rum 1:6. Usifikiri hata mara moja unapoteza muda wako kwa
kuwalisha neno watu wa Mungu. Usisikitike hata mara moja unapotumia muda wako
kwa ajili ya wokovu wa watu. Kuna furaha kubwa sana kwa Mungu ikiwa kwa kupitia
kwako mtu mmoja alipata wokovu na kwenda Mbinguni kwenye maisha ya umilele.
Ndugu yangu uliyesafari nami katika tafakari hii, maisha bila Kristo Yesu ni
sawa na safari bila kuijua njia.
Baada ya miaka 15 ya
ndoa ya Bwana na Bibi Msanje, walibahatika kupata watoto wawili, Yoseph na
Maria, ambaye kwa sasa, yaani, Maria, ana miaka miwili na nusu. Mzee Msanje ni
mtu wa kusafiri sana kutokana na kazi yake ya udereva, na kwa mwezi aweza
kuwepo nyumba kama siku tatu tu.
Ndugu na marafiki zake
wa karibu walimweleza mambo mengi kuhusu mke wake, yaani, hakuwa ametulia, na
ufanya hovyo hovyo wakati yeye akiwa safarini. Basi siku mmoja alifika nyumbani
kutoka safarini na kumkuta binti yake Maria nyumbani akiwa na furaha, na wakati
huo mke wake alikuwa bado hajarudi kutoka kazini.
Basi Mzee Msanje
alianza kumdadisi binti yake kama huwa kuna mtu anafika nyumbani pale mara kwa
mara. Mara binti yake akamwambia Baba yake, “ukininunulia baiskeli ya matairi
matatu nitakuambia ni nani anayelala na Mama chumbani mwake kila siku wakati
wewe haupo.” Kwa habari hii Mzee Msanje aliunganisha na maneno ya ndugu zake na
kusema moyoni, ‘huu ni wakati wa kujua ukweli.’
Hivyo kesho yake
alienda kununua baiskeli ya miguu mitatu, na kuwaita wazazi wa pande zote
mbili, yaani, kwa wakwe zake, na wazazi wake, ili wapata kujua ukweli wa mke
wake asiye mwaminifu. Mzee Msanje aliwaeleza wazazi wale alichowaitia, na
mwisho alimwita binti yake aliyekuwa nje anacheza na watoto wenzake aje asema
ukweli ule wa nani anaye lala chumbani mwake wakati yeye akiwa safarini.
“Maria, kabla sijakupa
zawadi yako hii, niambie ni nani huwa analala chumbani na Mama wakati mimi
sipo?” Mzee Msanje alimuuliza mwanaye kwa hali ya uchangamfu ili kumfanya awe
huru kujibu. Kwa huzuni Maria alimjibu Baba yake, “Baba mimi najisikia vibaya
tangu jana kwa sababu nalala mwenyewe. Ukiwa haupo huwa nalala na Mama chumbani
mwake. Asante Dady kwa zawadi ya baiskeli. Kesho naenda nayo shule.” Wote
walitazamana, huku Mzee Msanje akiinamisha kichwa chake chini kwa aibu. Mke
wake aliinuka na kuelekea chumbani kimya huku machozi yakimtoka.
Ndugu yangu, usikiapo
jambo tafakari kwa kina, na lipe muda.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Kicho cha Bwana
ni kitakatifu, Kinadumu milele. Hukumu za Bwana ni kweli, Zina haki kabisa,”
Zab 19:9
Tusali: Ee Yesu Mwema, tujalie moyo wa subira na uvumilivu kwa yale tusiyoyajua vizuri. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario