DECEMBA 23, WIKI YA 4 YA MAJILIO
Somo: Mal 3:1-4, 4:5-6
Zab: 25:4bc-5ab, 8-9, 10, 14
Injili: Lk 1: 57-66
Nukuu:
“Angalieni, namtuma mjumbe wangu, naye ataitengeneza njia
mbele yangu; naye Bwana mnayemtafuta atalijilia hekalu lake ghafula; naam, yule
mjumbe wa agano mnayemfurahia, angalieni, anakuja, asema Bwana wa majeshi,” Mal 3:1
“Naye ataigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto
wao, na mioyo ya watoto iwaelekee baba zao, ili nisije nikaipiga dunia kwa
laana,” Mal 4:6
“Mamaye
akajibu akasema La, sivyo; bali, ataitwa Yohana,” Lk 1:60
“Akataka
kibao, akaandika ya kwamba, Jina lake ni Yohana. Wakastaajabu wote,” Lk 1:63
“Na wote walioyasikia
wakayaweka mioyoni mwao, wakisema, Mtoto huyu atakuwa wa namna gani? Kwa sababu
mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye,” Lk 1:66
TAFAKARI:
“Kwake vyote vitafanywa upya.”
Wapendwa
wana wa Mungu, mazoea hujenga tabia. Na tabia ya mtu kama ni mbaya huchukua
muda sana kurudi katika njia iliyo sahihi. Kinyume cha kuhani aliyekuwa siyo
mwaminifu, Nabii Malaki anatangaza siku ya Mungu ambayo itakuwa ya kutisha
sana. “Lakini ni nani atakayestahimili siku ya kuja kwake? Au ni
nani atakayesimama atakapoonekana yeye? Kwa maana yeye ni mfano wa moto wa mtu
asafishaye fedha, ni mfano wa sabuni ya mtu afuaye nguo,” Mal 3:2
Tunaweza kusoma habari hii ya kutisha ya siku
ya Bwana pia kutoka kwa Nabii Amosi, 5:18-20, na Namii Joeli, 1:15-20. Katika
hatua hii, Bwana atarudi katika hekalu lake na kulitakatifuza kwa moto, Eze 22:
17.22, na kumweka Kuhani Mtakatifu na sadaka ya haki itakayokubalika. “Angalieni, nitawapelekea Eliya nabii, kabla haijaja siku ile
ya Bwana, iliyo kuu na kuogofya,” Mal 4:5.
Kama ilivyokuwa kwamba huwezi kumwona Mungu bila kufa, Kut 33:20, Mungu alionekana
kwa watu mfano wa Malaika, Mwa 16:7, Kut 3:2. Malaika wa agano ni Bwana ambaye
anawatafuta watu wake, na siyo mjumbe.
Hii
inamaanisha Mungu mwenyewe, anayeonekana, atakuwa muhuri wa agano hili jipya,
Yer 31:31ff, kwenye Hekalu lake. Maneno haya yanamaanisha Yesu mwenyewe, Mt
11:10, Ebr 3:5-6. Ujio wa Bwana unamaanisha upya wa mambo na mtazamo wa maisha
wa watu kuelekea umilele. “Naye ataigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto wao, na mioyo
ya watoto iwaelekee baba zao, ili nisije nikaipiga dunia kwa laana,” Mal 4:6.
Kinyume cha baraka ni laana. Hivyo pona ya watu wake ni kufuata maagizo yake
yenye uhai ndani yake.
Kuzaliwa
kwa Yohana Mbatizaji kunathibitishwa katika uhalisia wake kwa tangazo la
Malaika wa Mungu. Tunda la kwanza katika kuzaliwa kwake ni furaha. Yohana tunda
la muujiza, halina uhusiano na watu; hitimisho lake halipo mikoni mwa familia
yake, limefanywa hivyo na Mungu mwenyewe. Mungu amempa jina ambalo linaelezea
hatma yake, Mwa 17:3-8, Mt 16:17-19. Yohana anauvunja mwendelezo uliokuwepo. Hivyo
hataitwa Zakaria, jina lake litakuwa
Yohane, Lk 1:60.
Elizabeti
kama alivyokuwa Ana mama yake Samuel, anajua mwanaye si mali yake. Mtoto
Samweli alitwaliwa, na kuchaguliwa hata kabla ya kuzaliwa kuwa ni mali yake
Bwana, Yer 1:5. Zakaria Baba yake Yohane anakubali hatma ya mtoto wake, na
mdomo wake unafunguka na kumsifu Mungu. Haya ndiyo maajabu ya Mungu kwa watu
wake. “Na
wote walioyasikia wakayaweka mioyoni mwao, wakisema, Mtoto huyu atakuwa wa
namna gani? Kwa sababu mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye,” Lk 1:66. Kwake
Mungu vyote vitafanywa upya. Hakuna aliyekutana na Mungu katika hali yoyote ile
akabaki kama alivyo kuwa mwanzo.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Si kwa sababu ya matendo ya haki
tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili na
kufanywa upya na Roho Mtakatifu,” Tit 3:5
Tusali:-Ee
Yesu Mwema, yaanze yote upya katika maisha yetu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario