Sikukuu ya Watoto Mashahidi
DECEMBA 28
Somo: 1Yoh 1:5:2:2
Zab: 124:2-3, 4-5, 7cd-8
Injili: Mt 2:13-18
Nukuu:
“Tukisema ya
kwamba twashirikiana naye, tena tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatuifanyi
iliyo kweli,” 1Yoh 1:6
“bali tukienenda nuruni, kama yeye
alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu, Mwana wake,
yatusafisha dhambi yote,” 1Yoh 1:7
“Na
hao walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika
ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko
hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize,” Mt 2:13
“Ndipo Herode, alipoona
ya kuwa amedhihakiwa na wale mamajusi, alighadhabika sana, akatuma watu akawaua
watoto wote wanaume waliokuwako huko Bethlehemu na viungani mwake mwote, tangu
wenye miaka miwili na waliopungua, kwa muda ule aliouhakikisha kwa wale
mamajusi,” Mt 2:16
TAFAKARI: “Tuushinde uovu kwa wema. Kama wafuasi wa Krito tu mwanga wa ulimwengu.”
Wapendwa
wana wa Mungu, Mama Kanisa leo anashereherekea Sikukuu ya Watoto Watakatifu
Mashahidi, waliomwaga damu zao pasipo hatia yoyote ile. Huu ni mtikiso wa
kwanza pale nguvu na mamlaka za kibidamu zinapoingiwa na hofu. Mtoto Yesu
anakuwa tishio kwa utawala na milki ya Mfalme Herodi. Yesu ni Mfalme wa AMANI!
Neno na mtazamo wa nyakati ule kuhusu MFALME, unamtia hofu Herodi Mfalme.
Ukweli
huu unakuwa hofu kwa wale wote wenye kung’ang’ania madaraka na ukuu. Ni tishio
kwa uwepo wa Amani hii anayotupatia Kristo. Kuwa na Amani ndani na katika
Kristo Yesu ni kujisalimisha kwake. Aliye kwenye madaraka ni vigumu
kujisalimisha kwani kutamwondolea ukuu wake. Hivyo Yesu anatuambia, “Mtu
ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila
siku, anifuate,” Lk 9:23. Je, ni nani aliyetayari kuyaacha yale yanayomtukuza
na kupokea Amani anayotupatia Kristo Yesu? Wapo wengi wanaouwawa kila dakika
ulimwenguni na hasa nchi zetu za kiafrika kwa sababu ya hofu ya madaraka
yaliyobebwa na utawala dhalimu.
Hivyo
kuhakikisha anamwangamiza Mtoto Yesu, tangazo linatolewa mara moja baada ya
kujua wale Mamajusi wamemdanganya kadiri ya maagizo aliyokwisha wapa, yaani, “Shikeni njia, mkaulize sana mambo ya mtoto; na
mkiisha kumwona, nileteeni habari, ili mimi nami niende nimsujudie,” Mt 2:8.
Wakijua nia yake mbaya juu ya mtoto Yesu, Mamajusi walishika njia nyingine
baada ya kumsujudu mtoto Yesu na kutoa zawadi zao.
Hapa ndipo lilipotolea tangazo la kuwaangamiza watoto wasio
na hatia. “Ndipo Herode, alipoona ya kuwa amedhihakiwa na wale
mamajusi, alighadhabika sana, akatuma watu akawaua watoto wote wanaume
waliokuwako huko Bethlehemu na viungani mwake mwote, tangu wenye miaka miwili
na waliopungua, kwa muda ule aliouhakikisha kwa wale mamajusi,” Mt 2:16. Nguvu
ya Mungu na mpango wake kwa wale aliorithia nao ni tofauti na mipango yetu
ambayo kwayo haina uzima ndani yake.
Kama
Mungu ndiye mweza wa vyote hakuna chochote kitakachozuia mpango huo, kwani nasi
kama tulivyo na mamlaka tuliyonayo humtegemea Mungu huyu huyu. “Na hao
walipokwisha kwenda zao, (Mamajusi) tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu
katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri,
ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto
amwangamize,” Mt 2:13. Ni nani kama Mungu wetu? Leo tunajionea wenyewe baadhi
ya tawala ambazo hazipo tayari kuachia dola kwa AMANI, na hivyo kuleta maafa
makubwa ya mauaji ya watu wasio na hatia. Pamoja na ukatili huu, uovu hauwezi
kudumu katika umilele wake, kwa sababu uovu hauna umilele. Wale wote wauteteao
na kuulinda uovu ujichosha kure. Hivyo, “Bwana
asipoijenga nyumba Waijengao wafanya kazi bure. Bwana asipoulinda mji Yeye
aulindaye akesha bure,” Zab 127:1
Wapendwa
wana wa Mungu, Kristo kama Mwanga wa
limwengu, uwepo wake ni vita dhidi ya giza na uovu wote. Hili ndilo alisemalo
Mwinjili Yohane, Yoh 1:9, 8:12. Wakristo, yaani, wafuasi wa Kristo, ni
washiriki wa mwanga huu. “Ninyi ni nuru ya
ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima,” Mt 5:14. Wakristo ni
mwanga unaoangaza duniani, unaojionyesha katika maisha ya Mkristo kupitia Makuu
ya Mungu, katika unyenyekevu na kuusifu utukufu wa Mungu Baba aliye mbinguni.
“Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu
mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni,” Mt 5:16.
Mwanga huu wa utukufu wa Mungu hujidhihirisha katika miale
ya UPENDO. Katika miale hii ya upendo kwa Mungu na jirani ndiyo utambulisho
wetu kwamba sisi tu wanafunzi wa Kristo. “Hivyo watu wote watatambua ya kuwa
ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi,” Yoh 13:35. Ni
kwa namna hii basi kama tukiwa na umoja sisi kwa sisi tutajenga umoja ndani na
katika Kristo, ambao umoja huo ndiyo alama kubwa ya kukabili na kuubadilisha
ulimwengu huu kwa kuushinda uovu kwa wema. “Mimi ndani yao, nawe
ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa
ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi,” Yoh 17:23
Wapendwa
katika Kristo, umoja huu ndani na katika Kristo, na Kristo ndani ya Baba wa
Mbinguni ndio unaotuwezesha kusafishwa dhambi zetu, kwa nguvu ya utakaso wa
damu ya Kristo. “Na
kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki, naye ndiye kipatanisho kwa dhambi
zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote,” 1Yoh
2:1b-2. Kama yeye anatujua hata idadi ya
nywele zetu, Mt 10:30, hatuna cha kudanganya na kujihesabia haki kwamba tu
wema. “Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo
mwetu,” 1Yoh 1.8.
Tiba yako na
kupona yako kutoka majeraha haya ya dhambi ni kuziungama dhambi zako zote bila
kuficha. “Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata
atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote,” 1Yoh 1:9. Je! wataka
tiba ya Upungufu wa Kinga Rohoni-“UKIRO.”? Basi ijongee sakramenti ya
upatanisho pasipo shaka na ukutane na Baba wa HURUMA na MSAMAHA. Mungu ni
huruma. Twende basi tukajisalimisha kwa Jemedari wetu aliye Upendo, Huruma na
Msamaha.
Tumsifu Yesu
Kristo!
“Ee
Bwana, kwa ajili ya jina lako, Unisamehe uovu wangu, maana ni mwingi,” Zab
25:11
Tusali: Ee Yesu na
Mkombozi wetu, tuondolee tufanye vyombo vya haki na amani yako. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario