JUMATANO WIKI YA 2
YA MAJILIO
Somo: Isa 40:25-31
Zab: 103:1-2, 3-4, 8, 10
Injili: Mt 11:28-30
Nukuu:
“Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na
uwezo,” Isa 40:29
“Hata vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana
wataanguka; bali wao wamngojeao
Bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio,
wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia,” Isa 40:30-31
“Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na
mizigo, nami nitawapumzisha,” Mt 11:28
“Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole
na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu,” Mt 11:28
“kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi,”
Mt 11:30
TAFAKARI: “Nira yangu ni laini, na Mzigo wangu ni mwepesi.”
Wapendwa wana wa Mungu, kadiri ya uhalisia wa mambo kama
yanavyoonekana, na hata Maandiko Matakatifu yanavyotuelekeza, maisha ya hapa
duniani ni mafupi sana na yaliyojaa sintofahamu nyingi. Ndiyo maana hata baadhi
yetu utawasikia wakisema “afadhali ya jana kuliko leo.” Wapo wengine kati yetu
licha ya kwamba maisha ni mafupi sana, wanamwomba Mungu azidi kuwapa uhai
wavifaidi walivyokuwa navyo. Pamoja na hali zote hizi mbili hatuwezi kuupinga
ukweli kwamba duniani hapa sote tunapita. Je, Yesu anasema nini kuhusu uhalisia
huu?
Bwana wetu Yesu Kristo kabla ya kuteswa kwake, na akiwa
kwenye mahangaiko makubwa, aliomba kwa kila mmoja wetu na kusema, “Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na
yule mwovu. Wao si wa ulimwengu,
kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Uwatakase
kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli. Na
kwa ajili yao najiweka wakfu mwenyewe, ili na hao watakaswe katika kweli. Wala si hao tu ninaowaombea; lakini na
wale watakaoniamini kwa sababu ya neno lao,” Yoh 17:15-17, 19-20. Kila neno katika sala hii limebeba uzito mkubwa
sana katika maisha yetu.
“Mimi siombi kwamba uwatoe
katika ulimwengu:”-Ili kuurithi ufalme wa Mungu ikiwa ni pamoja na maisha ya
milele, hatuna budi kujiandaa hapa hapa duniani. Kufaulu vizuri katika
mashindano yoyote yale yakupasa kufanya mazoezi ya kutosha na yenye kuendana na
kasi ya mchezo huo. Hivyo, muda uliopewa hapa duniani ni muhimu sana kwa ajili
ya kesho yako, ambayo ni umilele wa maisha yako.
Yesu haombi tuondolewe
katika ulimwengu huu licha ya shida zake na sintofahamu zake. Ulimwenguni hapa
ni sehemu muhimu sana kwa utakaso wako na kwa kukufanya uijongee ile taji ya
utakatifu. Mazoezi haya ya kiroho Mtume Paulo anayafananisha na kuvipiga vita.
“Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda,” 2Tim
4:7. Maisha yetu hapa duniani shabaha
yake iwe kulishika lile lililoshikwa na Kristo Yesu.
Kwa hiyo hakuna sababu
yoyote ya kubweteka na raha za leo na kesho katika ulimwengu huu. Mtume Paulo
anatupa mfano na kusema, “Si kwamba
nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo ili nipate
kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu. Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba
nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma,
nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza
mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu,”
Flp 3:12-14. Kumbe ulimwenguni hapa ni sehemu ya kujiandaa tu katika ukamilifu.
“Bali
uwalinde na yule Mwovu:”-Hapa pia Yesu hatuombei kuondolewa kwa yule mwovu, bali
Mungu atulinde na yule mwovu. Ndugu yangu, hutoweza kamwe kushinda kishawishi
kwa kupigana nacho, bali yakupasa kuelekeza mawazo yako sehemu nyingine penye
usalama zaidi. Vishawishi vyote vile uanza kwenye fikra zako unapoanza kufikiri
juu ya hicho kishawishi.
Kudumu
katika kukipinga na kupigana nacho hutofaulu na mwisho wa siku kitakutawala.
Bali mfumo wako wa kufikiri ikiwa ni pamoja na kuyaelekeza mawazo yako sehemu
nyingine palipo salama ndiyo pona yako. Ni katika hali hii unaweza kudumu na
kukua kiroho hadi mwisho licha ya kusongwa na vishawishi. Naye Yesu anasema, “mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka,”
Mt 10:22b. Hivyo, kulikimbia tatizo ni
kulikwepa kwa muda tu, ila kubadili mwelekeo na mtazamo wako juu ya tatizo hilo
ndiyo njia pekee ya kujinasua.
“Wao si waulimwengu, kama
mimi nisivyo wa ulimwengu:”-Ulimwenguni hapa ni sehemu ya kupita tu. Hapa siyo
makazi yetu ya kudumu. Hivyo, ili upate furaha ya kweli yakupasa kuwa na
mtazamo mpya kuhusu uhusiano uliopo kati ya maisha yako hapa duniani na umiliki
wako wa vitu. Yesu anatupa angalizo kuhusu jambo hili. “Viuzeni mlivyo navyo, mtoe sadaka. Jifanyieni mifuko
isiyochakaa, akiba isiyopungua katika mbingu, mahali pasipokaribia mwivi, wala
nondo haharibu. Kwa kuwa hazina
yenu ilipo, ndipo itakapokuwapo na mioyo yenu,” Lk 12:33-34. Kumbe duniani hapa
siyo mahali salama pa kuwekeza kiroho.
“Uwatakase
kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli”-Furaha ya kweli ni kuishi katika kweli.
Mtu yeyote yule hudondoka katika dhambi kwa kuyaruhusu mambo haya manne
yamtawale; tamaa ikutawale, Mashaka yakutawale, udanganyifu ukutawale, na
mwisho kukosa utii. Kumbe ukiishi katika kweli, hayo yote niliyoyataja
hayatakuwa na nafasi juu ya maisha yako. Wakati nyingine nitayaelezea kwa
undani mambo hayo manne. Naye Yesu anasema haya kuhusu kutakaswa na ile kweli:
“Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli
itawaweka huru. Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli,” Yoh
8:31b-32, 36. Kutakaswa katika kweli ni “kukaa” katika NENO la Mungu. Je, neno
la Mungu lina nafasi gani katika maisha yako? Kweli ni mwanga. Hivyo kama kweli
ni mwanga haiwezi kuchangamana na giza.
“Kwa
ajili yao najiweka wakfu mwenyewe, ili na hao watakaswe katika kweli:”-Maneno
haya ya Yesu yanaonyesha mizania ya upendo wake kwetu. Yesu kwa kujiweka wakfu
kwenyewe kwa sababu yako na yangu ni heshima kubwa sana kwetu na thamani ya
heshima hii haina kipimo. Kristo ndiye aliyetuchagua kwa kujiweka wakfu kwa
ajili yetu, na siyo sisi tuliyemchagua
Yeye. “Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi;
nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba
lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni,” Yoh 15:16. Yote huwa mepesi na
laini tunapoambatana na Yesu aliyejitoa wakfu kwa ajili yetu. Je, hilo
walitambua ndugu yangu?
“Wala si
hao tu ninaowaombea; lakini na wale watakaoniamini kwa sababu ya neno
lao:”-Maneno haya ya Yesu yanathibitisha upana wa sadaka yake pale Msalabani.
Kwa sadaka ya upendo wake pale msalabani kwa kuwa mtii kwa ajili yako na yangu
tulio wadhambi hata kifo cha msalamba, tendo hili ni kufunguliwa pia kwa wale
wasiomjua Kristo ila wanaongozwa kwa dhamiri zao safi na njema. Mtu wa kwanza
kupata baraka na neema hii bila shaka ni Akida yule aliyeshuhudia namna Mwokozi
wetu alivyo isalimu roho yake. “Basi yule akida,
aliyesimama hapo akimwelekea, alipoona ya kuwa alikata roho jinsi hii, akasema,
Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu,” Mk 15:39. Huyu ni mmoja aliyeamini
mwishoni kabisa mwa maisha ya Yesu hapa duniani.
Wapendwa
wana wa Mungu, ni katika mazingira hayo yote niliyoyaelezea tunaweza
tukayaelewa maneno haya mazito ya Yesu katika Injili ya leo: “kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni
mwepesi,” Mt 11:30. Tunapojiandaa mwili na roho kumpokea Masiha wetu tuubebe
ujumbe huu tunapozitazama dhambi zetu. Hata kama dhambi inayokusumbua kwa muda
mrefu huwa inajirudia rudia usikate tamaa kwenda kuiungama huku ukiweka nia
thabiti ya kuiacha. Ni kujisalimisha kwa Kristo aliyekwisha legeza lile kongwa
kwa sadaka ya kifo chake pale msalabani. Sadaka hii imeufanya mzigo kuwa
mwepesi tunaoubeba kila siku kutokana na dhambi zetu. Hivyo pumziko la kweli
lipo kwa Yesu tu. “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na
mizigo, nami nitawapumzisha,” Mt 11:28
Tumejifunza
mengi kupitia ile sala ya Yesu kabla ya mateso yake. Ni Kristo tu mwenye
kutufahamu vizuri kwa sababu alitupenda upeo. “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai
wake kwa ajili ya rafiki zake,” Yoh 15:13. Hivyo salama yetu mwili na roho ipo
kwa Kristo Yesu. Ndugu yangu, natujisalimishe katika mikono salama ya Kristo
kwa kuziungama dhambi zetu. Yesu anakuambia wewe na mimi, “Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole
na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu,” Mt 11:28. Basi
yatupasa kujinyenyekesha kama Kristo alivyofanya, na kutii maagizo yake. Huku
ndiko kujitia nira ya Kristo, yaani kuwa tayari kuongozwa na kongwa lake.
Masiha huyu ndiye aliyetabiriwa na Nambii Isaya kwamba, “Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye
asiyekuwa na uwezo,” Isa 40:29. Uwepo wa Masiha katika maisha yetu ni kuupata
uzima tele ndani yetu. Huku ndiko kupata nguvu mpya kama asemavyo Nabii Isaya.
“Hata vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka; bali wao wamngojeao Bwana watapata
nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka;
watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia,” Isa 40:30-31. Ndugu yangu tuliyesafiri
sote katika tafakari hii, sasa ndio ule wakati wa kupiga mbio kuelekea
Utakatifu. Basi na tujitakase kwenye kisima cha wokovu, yaani, Sakramenti ya
upatanisho.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa
nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera,
zitakuwa kama sufu,” Isa 1:18
Tusali: Ee Yesu na Mwokozi
wangu, usiniache nitoke ndani ya mikono lako salama. Ni kwako tu yote hupata
wepesi katika maisha yangu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario