JUMATANO WIKI YA 3
YA MAJILIO
Somo: Isa 45:6c-8, 18, 21c-26
Zab: 85:9ab-14
Injili: Lk 7: 19-23
Nukuu:
“Mimi naiumba nuru, na kulihuluku giza; mimi
nafanya suluhu, na kuhuluku ubaya; Mimi ni Bwana, niyatendaye hayo yote,” Isa
45:7
“Dondokeni, enyi mbingu, toka juu, Mawingu na yamwage haki;
Nchi na ifunuke, ili kutoa wokovu, Nayo itoe haki ikamee pamoja; Mimi, Bwana,
nimeiumba,” Isa 45:8
“Ni nani aliyeyahubiri hapo zamani? Si mimi, Bwana? Wala
hapana Mungu zaidi ya mimi; Mungu mwenye haki, mwokozi; hapana mwingine zaidi
ya mimi,” Isa 45:21c
“Ndipo Yohana alipowaita wawili katika wanafunzi wake, akawatuma
kwa Yesu akiuliza, Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine?” Lk 7:19
“Na saa
ile ile aliwaponya wengi magonjwa yao, na misiba, na pepo wabaya; na vipofu
wengi aliwakirimia kuona,” Lk 7:21
“Ndipo
alipojibu, akawaambia, Nendeni mkamweleze Yohana hayo mliyoyaona na kuyasikia;
vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakasika, viziwi
wanasikia, wafu wanafufuliwa, maskini wanahubiriwa habari njema,” Lk 7:22
“Naye heri mtu ye yote asiyechukizwa nami,” Lk 7:23
TAFAKARI: “Wewe ndiwe yule ajaye, au
tumtazamie mwingine?”
Wapendwa wana wa Mungu, kadiri ya masomo yetu ya leo, yaani
somo la kwanza kutoka kitabu cha Nabii Isaya, na Injili kama ilivyoandikwa
na Mwinjili Luka tunaona shahuku ya watu
ilivyokuwa kubwa wakisubiri ukombozi. Somo la kwanza tunaona Mungu akijifunua
kwa watu wake kupitia asili ya vitu. Asili hii inathibitisha uweza wa Mungu wa
kuwakomboa watu wake. Asili hii inawajengea watu wake imani naye na kuwaondolea
hofu. Asili hii inajenga tena ukaribu kati ya watu na Muumba wao. “Mimi naiumba nuru, na kulihuluku giza; mimi
nafanya suluhu, na kuhuluku ubaya; Mimi ni Bwana, niyatendaye hayo yote,” Isa
45:7.
Mungu ndiye haki ya watu wake, na ndiye peke yake mwenye
uwezo wa kuwakomboa. “Wala hapana Mungu zaidi ya mimi; Mungu mwenye haki,
mwokozi; hapana mwingine zaidi ya mimi,” Isa 45:21c. Kazi yote ya uumbaji wa ulimwengu na yale yote
yaliyomo ililenga kumkomboa mwanadamu. Vyote hivyo vinadhihirisha ukuu wake na
uweza, na kwa upande mwingine vinaonyesha lengo la kila kimoja vikimwelekea
yule aliyeumbwa kwa sura na mfano wake Mungu, yaani wewe na mimi. “Maana
Bwana, aliyeziumba mbingu, asema hivi; Yeye ni Mungu; ndiye aliyeiumba dunia na
kuifanya; ndiye aliyeifanya imara; hakuiumba ukiwa, aliiumba ili ikaliwe na
watu; Mimi ni Bwana, wala hapana mwingine,” Isa 45:18
Huyu
ndiye Mungu mwenye kuvishurutisha vyote alivyoviumba na humtii. “Dondokeni, enyi mbingu, toka juu, Mawingu na
yamwage haki; Nchi na ifunuke, ili kutoa wokovu, Nayo itoe haki ikamee pamoja;
Mimi, Bwana, nimeiumba,” Isa 45:8. Kazi hii ya ukombozi inakamilishwa na Yesu
Kristo. “Mungu, ambaye alisema zamani na baba
zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi
amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye
aliufanya ulimwengu.Yeye kwa kuwa ni mng'ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi
yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa
dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu,” Ebr 1:1-3.
Hata
hivyo licha ya kwamba Maandiko Matakatifu yalionyesha wazi kuwa Yesu ndiye
atakayeukamilisha ukombozi huu, Yohane Mbatizaji akiwa gerezani anaingiwa na
mashaka. Na hii inaonyesha kwamba umasiha wa Yesu haukulandana na matumaini ya
kibinadamu. “Ndipo Yohana alipowaita wawili katika wanafunzi wake, akawatuma
kwa Yesu akiuliza, Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine?” Lk 7:19.
Yesu hakujibu swali hili moja kwa moja. Hakika hapakuwa na neno la kibinadamu
yenye kusema kwa ujumla kile alicho Yesu.
Maandiko
Matakatifi yanamfunua kama ifuatavyo; Yesu ni Mfalme, Nabii, Kuhani, Mwana wa
Adamu, Mtumishi…; lakini Yesu ni zaidi ya Ibrahimu. “Yesu akawaambia, Amin,
amin, nawaambia, Yeye Ibrahimu asijakuwako, mimi niko,” Yoh 8:58. Yesu ni zaidi
ya Musa na Eliya. Tunaona tukio hili pale aliojeuka sura akiwa mlimani.
“Wakatokewa na Eliya pamoja na Musa, nao walikuwa wakizungumza na Yesu,” Mk
9:4. Yesu ni zaidi ya Yohane Mbatizaji. Yohane anakiri jambo hili na kusema, “Kweli
mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana
nguvu kuliko mimi, wala sistahili hata kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza
kwa Roho Mtakatifu na kwa moto,” Mt 3:11. Kwa mtazamo huu na kile alicho Yesu,
haikuwa rahisi kujibu moja kwa moja kile alicho. Badala yake Yesu anawataka
wale wanafunzi wa Yohane Mbatizaji
washuhudie yale ayatendayo na iwe shuhuda kwao na jibu sahihi kwa Yohane
Mbatizaji.
Yesu
anaendelea na kazi aliyoijia kama shuhuda iliyo hai na yenye kumtambulisha kile
alicho. Na hivi ndivyo iliyotokea mbele ya
wale wanafunzi waliotumwa na Yohani Mbatizaji kwa Yesu; “Na saa ile ile
aliwaponya wengi magonjwa yao, na misiba, na pepo wabaya; na vipofu wengi
aliwakirimia kuona,” Lk 7:21. Baada ya kazi hii ya uzima na yenye
kumtambulisha, Yesu anawaambia wale wanafunzi wa Yohane, “Nendeni mkamweleze
Yohana hayo mliyoyaona na kuyasikia; vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea,
wenye ukoma wanatakasika, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, maskini
wanahubiriwa habari njema,” Lk 7:22. Tofauti
na wale wote waliomtangulia Yesu katika safari hii ya ukombozi, Yeye, yaani,
Yesu, aliufunua Umungu kwake na kuudhihirisha kwa watu na wote waliomridhia
kupitia kazi zake. Basi na “Naye heri mtu ye yote asiyechukizwa nami,”
Lk 7:23. Ukikutana na Yesu hawezi kukuacha
hivi hivi. Lazima tu atakubadilisha na kuyaacha yale yote ya zamani.
Ndugu yangu uliyesafiri nami
katika tafakari hii ungependa kukutana na Yesu? Kama jibu lako ni ndiyo; basi
kukutana na Yesu itakupasa kulisoma neno lake, kulipokea neno lake, kulitafiti
neno lake, kulitafakari neno lake, na kulikumbuka daima neno lake.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Ninyi mkikaa ndani yangu,
na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa,” Yoh
15:7
Tusali: Ee Yesu Mwema,
niondolee mashaka na nisilipoteze tumaini langu kwako hasa nyakati zile
ninapohisi u mbali nami. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario