JUMANNE WIKI YA 2
YA MAJILIO
Somo: Isa 40:1-11
Zab: 96:1-2, 3, 10ac, 11-12, 13
Injili: Mt 18:12-14
Nukuu:
“Semeni
na moyo wa Yerusalemu, kauambieni kwa sauti kuu ya kwamba vita vyake
vimekwisha, uovu wake umeachiliwa; kwa kuwa amepokea kwa mkono wa Bwana adhabu
maradufu kwa dhambi zake zote,” Isa 40:2
“Majani
yakauka, ua lanyauka; Bali neno la Mungu wetu litasimama milele,” Isa 40:8
“Atalilisha
kundi lake kama mchungaji, Atawakusanya wana-kondoo mikononi mwake; Na
kuwachukua kifuani mwake, Nao wanyonyeshao atawaongoza polepole,” Isa 40:11
“Mwaonaje?
Mtu akiwa na kondoo mia, mmoja akampotea, je! Hawaachi wale tisa na tisini,
akaenda milimani, na kumtafuta yule aliyepotea?” Mt 18:12
“
“Vivyo hivyo haipendezi mbele za Baba yenu aliye mbinguni kwamba mmoja wa
wadogo hawa apotee,” Mt 18:14
TAFAKARI:
“Haipendezi mbele za Baba yenu aliye mbinguni kwamba mmoja wa wadogo hawa
apotee.”
Wapendwa waamini
wenzangu, huu ndio wakati wa kujinyenyekesha kuliko kwa kweli na kujiachilia
bila kujibakiza katika kiti hiki cha huruma na msamaha wa Mungu, yaani,
Sakramanti ya upatanisho. Mungu huyu aliyekuwa tayari kujipatanisha wa wana wa
Taifa lake Israeli anasema NASI pia leo kwa maneno haya: “Semeni na moyo wa Yerusalemu, kauambieni kwa sauti kuu ya
kwamba vita vyake vimekwisha, uovu wake umeachiliwa; kwa kuwa amepokea kwa
mkono wa Bwana adhabu maradufu kwa dhambi zake zote,” Isa 40:2.
Mwitikio huu mbele ya
Mungu unabeba maana pale tu utakapokuwa tayari kujinyenyekesha na kuukubali
ubinadamu wako kwamba umekosa. Lengo na makusudi ya Mungu ni kumpata kila mmoja
wetu aliye muumba kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27. Na huu ndio mpango mzima wa
historia hii ya wokovu wa mwanadamu. Mungu yu tayari, wewe na mimi tujitazame
mwenendo wa maisha yetu, mwili na roho.
Tutalishwa na Masiha
huyu tunayemtarajia na kuwa sehemu ya kondoo zake tutakapo ukubali ubinadamu
wetu. Ni kwa sababu ya ubinadamu wetu ilimpendeza Mungu sisi kuwa kama tulivyo.
Hivyo kwa namna hii ndivyo tutakavyokombolewa na si vinginevyo. Naye Masiha, “Atalilisha kundi lake kama mchungaji, Atawakusanya wana-kondoo
mikononi mwake; Na kuwachukua kifuani mwake, Nao wanyonyeshao atawaongoza
polepole,” Isa 40:11. Maneno haya ni kweli kabisa kwetu na hakuna lolote
litakalo pita hata kama nyakati zipita na mengi yatabadilika.
Neno
la Mungu litabaki kuwa hai siku zote. “Majani yakauka, ua lanyauka; Bali neno
la Mungu wetu litasimama milele,” Isa 40:8. Ndugu yangu tunaye safiri sote, Je!
una jambo lolote la kujivunia zaidi ya dhambi zako? Kama mimi na wewe hatuna,
basi yatupasa mara zote kujinyenyekesha mbele za Mungu, tukiwa na hofu hiyo
ndani mwetu.
Yesu
anamfananisha mtu unyenyekevu na mtoto mdogo. Mtoto mdogo hana cha kujikuza
zaidi ya kuyaona yote na katika yote kwa wazazi wake. Mtoto huweka uaminifu
mkubwa sana kwa wazazi wake. Wazazi wake huwa kila kitu kwake. Ni katika
mtazamo huu Mungu wetu ni kila kitu kwetu. Hatuna cha kujikweza mbele zake “kwa
sababu upumbavu wa Mungu una hekima zaidi ya wanadamu, na udhaifu wa Mungu una
nguvu zaidi ya wanadamu,” 1Kor 1:25.
Ni
katika ukweli huu Yesu anawaambia wanafunzi wake maneno haya mazito, “akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa
kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni,” Mt 18:3. Tusipojivua
kujua kwetu kusikokuwa na maana yo yote zaidi ya mbwembe zetu, hatutaweza
kufunuliwa siri za mbinguni.
Unyenyekevu
wenye mfano wa utoto ndio huo unaotufanya wakubwa mbele ya uso wa Mungu. Ukubwa
huo siyo ule wa kufanya tutakayo sisi na kuzirithisha nafsi zetu, bali
kuyafanya yote kadiri ya mpango wa Mungu. Na unajua mpango wa Mungu pale
unapokuwa tayari kujinyenyekesha mbele zake. Hivyo, “ye
yote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika
ufalme wa mbinguni,” Mt 18:4. Katika ufalme huu wa mbinguni hakuna maguvu ya
kutalawa au kutawaliwa, bali nguvu ya UPENDO wa KWELI.
Wapendwa
wana wa Taifa la Mungu, wanyenyekevu wana sauti kubwa sana mbele za Mungu. Mtu
ye yote anayemdharau mtu mnyenyekevu kwa vile anayafanya yote hayo kwa
kujishusha yu na hatia kubwa sana mbele za Mungu. Yesu anatuambia, “Angalieni
msidharau mmojawapo wadogo hawa; kwa maana nawaambia ya kwamba malaika wao
mbinguni siku zote huutazama uso wa Baba yangu aliye mbinguni,” Mt 18:10. Hivyo
tujiadhari sana na jeuri yetu ya pesa, madaraka, umaarufu na kutambulika kwetu
katika jamii, na kutumia hali hizo kama fimbo ya kuchapa wengine.
Haya
yote mwisho wa siku hayana msaada wo wote katika umilele wako. “Vivyo hivyo
haipendezi mbele za Baba yenu aliye mbinguni kwamba mmoja wa wadogo hawa
apotee,” Mt 18:14. Hivyo basi, kwa utajiri nilio nao, kwa madaraka niliyo nayo,
kwa umaarufu nilio nao, na kwa kutambulika kwangu katika jamii, iwe sababu na
nguvu ya kuwa sauti ya wasio na sauti.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Majani yakauka, ua lanyauka; Bali neno la Mungu wetu
litasimama milele,” Isa 40:8
Tusali:-Ee Yesu, daima
uwe kimbilio letu kwani kwako kuna uzima wa milele. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario