DECEMBA 22, WIKI YA 4 YA MAJILIO
Somo: 1Sam 1:24-28
Zab: 1Sam 2:1, 4-5, 6-7, 8abcd
Injili: Lk 1: 46-56
Nukuu:
“Naliomba
nipewe mtoto huyu; Bwana akanipa dua yangu niliyomwomba; kwa sababu hiyo mimi
nami nimempa Bwana mtoto huyu; wakati wote atakaokuwa hai amepewa Bwana. Naye
akamwabudu Bwana huko,” 1Sam 1:27-28
“Mariamu akasema, Moyo
wangu wamwadhimisha Bwana,” Lk 1:46
“Na roho yangu
imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu,” Lk 1:47
“Kwa kuwa ameutazama
Unyonge wa mjakazi wake. Kwa maana, tazama, tokea sasa Vizazi vyote wataniita
mbarikiwa,” Lk 1:48
“Amewaangusha wakuu
katika viti vyao vya enzi; Na wanyonge amewakweza,” Lk 1:52
TAFAKARI: “Kwa
kuwa ameutazama Unyonge wa mjakazi wake. Kwa maana, tazama, tokea sasa Vizazi
vyote wataniita mbarikiwa.”
Wapendwa
wana wa Mungu, masomo ya leo yanatualika kuyatafakari Makuu ya Mungu kwa
wanyenyekevu wake wa Moyo. Taswira hii na fadhila hii ya unyenyekevu
inajionyesha katika wimbo ule wa Ana na Bikira Maria. Ana ana kila sababu ya
kumshukuru Mungu kwa kumrudishia heshima yake kama Mama kwa kumpatia Mtoto,
Samweli. Kwa kutokuwa na mtoto alidharaulika sana na kuonekana hafai.
Hivyo
inamlazimu kumrudishia Mungu sifa na shukrani kama alivyokwisha kuhaidi mbele
ya Eli, Kuhani huko Shilo. “Naliomba nipewe mtoto huyu; Bwana akanipa
dua yangu niliyomwomba; kwa sababu hiyo mimi nami nimempa Bwana mtoto huyu;
wakati wote atakaokuwa hai amepewa Bwana. Naye akamwabudu Bwana huko,” 1Sam
1:27-28. Ndugu yangu, nawe hauna kitu cha kumshukuru Mungu kama Mama huyu Ana?
Ukweli ni kwamba, ‘moyo usio na shukrani ukausha mema yote.’
Tenzi hizi zote mbili,
yaani wmbo wa Ana na Bikira Maria zinatuonyesha utendaji wa Mungu katika
historia ya wokovu. Kwa kuikamilisha safari hii ya wokovu, Mungu aliwachagua
baadhi ya watu, na wakati mwingine wale waliodharauliwa na hata kutokujaliwa
katika jamii. Watu hawa ni kama Ana mama yake Samweli aliyekuwa tasa, Elizabeti
mama yake Yohane Mbatizaji, Mama Bikira, na wengine wengi tu katika historia
hii ya wokovu.
Utenzi wa Bikira Maria,
“Magnificat,” wenye maana ya “Wamtukuza,” unaonyesha kutukuza na kuinuliwa kwa
hali ya juu roho na nafsi ya binti wa Sioni. “Moyo wangu wamwadhimisha Bwana,”
Lk 1:46. Utenzi huu unaonyesha matumaini mapya na furaha mpya kwa kujibiwa kwa
sala ambayo ilifanywa muda mrefu na wana wa Mungu waliokuwa wakisubiri kujibiwa
kwao. “Amemsaidia Israeli, mtumishi wake; Ili kukumbuka rehema zake; Kama
alivyowaambia baba zetu, Ibrahimu na uzao wake hata milele,” Lk 54-55. Machozi,
furaha na matumaini ya watu yamefungwa katika
mioyo yao. Hivyo Mungu ndiye mwenye kutukuzwa kwa sababu kamjibu mjakazi
wake. Huruma ya Mungu imefanywa milele ndani ya mjakazi wake. “Kwa kuwa
ameutazama Unyonge wa mjakazi wake. Kwa maana, tazama, tokea sasa Vizazi vyote
wataniita mbarikiwa,” Lk 1:48.
Kwa maana hiyo, Neno
kufanyika mwili ni neno la kinabii ambalo huharibu na kutengeneza, hung’oa na
kupanda, Yer 1. Yesu Kristo ndiyo hitimisho la historia, nguvu inayokamilisha
ahadi za kale. “Agano langu nitalifanya imara
kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, na vizazi vyao, kuwa agano la
milele, kwamba nitakuwa Mungu kwako na kwa uzao wako baada yako,” Mwa 17:7.
Binti Sioni alitoa jina letu kwa “Ndiyo”
yake kwa Mungu, na Neno akafanyika mwili, 1Sam 2:1-10.
Wapendwa
katika Kristo, unyenyekevu na kule kujishusha ni silaha kubwa sana katika
maisha, kuzijua njia za Mungu, na mwisho kutumika naye kwa mambo makubwa na
hata kupita uwezo wetu kama wanadamu. Unyenyekevu ni mama wa fadhila zote. Anza
sasa kwa kutambua mipaka yako ikiwa ni pamoja na madhaifu yako.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Kijapo kiburi
ndipo ijapo aibu; Bali hekima hukaa na wanyenyekevu,” Mit 11:2
Tusali:- Ee Yesu Mwema,
tuondelee ukuta wa kiburi na majivuno, ili tufikie makuzi yale yalio kusudi ya
kuumbwa kwetu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario