viernes, 9 de diciembre de 2016

TAFAKARI: JUMAPILI YA 3 YA MAJILIO YA MWAKA-A


JUMAPILI YA 3 YA MAJILIO YA MWAKA-A

Somo I: Isa 35:1-6a, 10

Zab: 146:6-7, 8-9, 9-10

Somo: Yak 5:7-10

Injili: Mt 11:2-11

Nukuu:

“Naye Yohana aliposikia huko gerezani matendo yake Kristo, alituma wanafunzi wake, kumwuliza, Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine?” Mt 11:2-3

“Yesu akajibu akawaambia, Nendeni mkamweleze Yohana mnayoyasikia na kuyaona; vipofu wanapata kuona, viwete wanakwenda, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa habari njema,” Mt 11:4-5

 “Nyika na mahali palipo ukiwa patafurahi; jangwa litashangilia na kuchanua maua kama waridi,” Isa 35:1

 “Waambieni  walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama, Mungu wenu atakuja na kisasi, na malipo ya Mungu; atakuja na kuwaokoa ninyi,” Isa 35:4

 Kwa hiyo ndugu, vumilieni, hata kuja kwake Bwana. Tazama, mkulima hungoja mazao ya nchi yaliyo ya thamani, huvumilia kwa ajili yake hata yatakapopata mvua ya kwanza na ya mwisho,” Yak 5:7

“Nanyi vumilieni, mthibitishe mioyo yenu, kwa maana kuja kwake Bwana kunakaribia,” Yak 5:8 

TAFAKARI: “Jipeni moyo, msiogope; tazama, Mungu wenu atakuja na kisasi, na malipo ya Mungu; atakuja na kuwaokoa ninyi.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya tatu ya Majilio, Dominika ya Furuha, “Gaudete.” Ni Dominika ya furaha na kufurahia kwa sababu Bwana Mungu wetu hakuzisahau, hajazisahau, na hatazisahau ahadi zake. Ni wewe na mimi kubaki katika tumaini lake bila kulipoteza.

Somo letu la kwanza linatukumbusha ahadi zile za Mungu kwetu ambazo hazikusaulika. Na hiki ndicho alichokisema Mungu kwa wana wa Israeli; “Waambieni  walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama, Mungu wenu atakuja na kisasi, na malipo ya Mungu; atakuja na kuwaokoa ninyi,” Isa 35:4. Ndugu yangu, kama unakumbuka vizuri, kauli mbiu ya Yesu kwa ile miaka yake mitatu kabla ya mateso kufa na kufufuka kwake ilikuwa hivi;  “Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili,” Mk 1:15.

Kauli mbiu hii ilibeba utimilifu wa ahadi zile za Mungu kwa wana wa Israeli, yaani, “macho ya vipofu yatafumbuliwa, na masikio ya viziwi yatazibuliwa,” Isa 35:5. “Mtu aliye kilema ataruka-ruka kama kulungu, na ulimi wake aliye bubu utaimba,” Isa 35:6a, na “waliokombolewa na Bwana watarudi, watafika Sayuni wakiimba; na furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao; nao watapata kicheko na furaha, huzuni na kuugua zitakimbia,” Isa 35:10. Yesu mwenyewe analithibitisha hili mwanzoni kabisa, ikiwa ndilo lengo na sababu ya uwepo wake. Naye anasema, “Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa,” Lk 4:18-19. Swali ni hili: Je, nini tunacho kifanya wakati huu wa Majilio? Je, hatuamini kuwa Kristo-Masiha kesha kukuja?

Wapendwa wana wa Mungu, ni kweli isiyoshaka kwamba tukifanyacho siyo kwamba hatuzijui habari za huyu Masiha wetu, bali tukifanyacho ni wewe na mimi kumruhusu Masiha huyo, yaani, Neno wa Mungu afanyike mwili ndani yako na yangu. Upendo wa kweli na hai ni pale tu tunapomruhusu Neno huyu wa Mungu kufanyika mwili kwa kila mmoja na kwa kadiri ya agano analoliishi, yaani, wito wako. Hili linapotokea ndani mwa mtu, hakika hapo hakuna hofu kwani nguvu-UPENDO huyasukuma maisha ya mtu. “Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo naya moyo wa kiasi,” 1Tim 1:7.

Kwa hiki alichokijia Yesu, na uwepo wake uliobeba kauli mbiu yake, Yohana Mbatizaji hakuwa na sababu ya kuona shaka juu ya Yesu. Je, hili halikumtosha kusadiki nguvu na uwepo wa Yesu? Mungu anayafunua Mamlaka ya Yesu mbele ya ulimwengu, na mbele ya Yohana Mbatizaji siku ile ya Ubatizo wake Yesu. “Roho Mtakatifu akashuka juu yake kwa mfano wa kiwiliwili, kama hua; sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe,” Lk 3:22. Mungu anathibitisha pia Ukuu na Mamlaka ya Yesu siku ile aliyobadilika sura akiwa na wanafunzi wake, Petro, Yakobo, na Yohana. “Sauti ikatoka katika wingu, ikisema, Huyu ni Mwanangu, mteule wangu, msikieni yeye.” Lk 9:35.

Lakini pamoja na uthibitisho huo wote, bado Yohana Mbatizaji anashaka na uwepo wa Yesu. Bila shaka mazingira aliyokuwa Yohana Mbatizaji, yaani, gerezani, na kuchelewa kwa kutokufanyika kitu juu yake na aliyoyatabiri kunampa wakati mgumu. “Naye Yohana aliposikia huko gerezani matendo yake Kristo, alituma wanafunzi wake, kumwuliza, Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine?” Mt 11:2-3. Matatizo na sintofahamu katika maisha visiwe vigezo vya kulipoteza lile tumaini la kweli aliyotuhaidia Mungu wetu. Badala yake, sintofahamu hizo na mahangaiko hayo, viwe sababu ya kuwa karibu zaidi na Mungu.

Hata hivyo, ujumbe wa Yesu kwa Yohana Mbatizaji unabeba msisitizo wa ahadi ile ya Mungu kwa watu wake. Mungu wetu siyo msaulifu, kiziwi, na wala siyo kipofu. Hutenda yote kwa wakati wake, na inavyompendeza Yeye kufanya hivyo kwa sababu huyajua mahitaji yetu yote: kabla ya kuzaliwa, tungali hai, na baada ya maisha haya mafupi hapa duniani. Naye Yesu anawaambia wanafunzi wa Yohana Mbatizaji hivi; “Nendeni mkamweleze Yohana mnayoyasikia na kuyaona; vipofu wanapata kuona, viwete wanakwenda, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa habari njema,” Mt 11:4-5. Na haya ndiyo Mungu aliyotuhaidia enzi na enzi, na leo yanafanyika chini ya Mwaye Mpendwa Yesu Kristo. Hakika, “Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika. Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu,” Yoh 1:3-4. Je, bado nawe una mashaka juu ya Kristo Yesu? Yesu anakuambia wewe na mimi, “Naye heri awaye yote asiyechukizwa name,” Mt 11:6. Maana yake, tusikwazike pale tunapojisikia upweke. Nyakati hizo za upweke na sintofahamu katika maisha sio wewe utembeaye katika magumu hayo, bali ni Kristo Yesu atembeaye angali kakubeba.

Pamoja na mashaka aliyokuwa nayo Yohana Mbatizaji, Yesu apindishi kweli iliyo ndani ya Yohana Mbatizaji. Naye Yesu anasema, “Huyo (Yohana) ndiye aliyeandikiwa haya, Tazama, mimi namtuma mjumbe wangu Mbele ya uso wako, Atakayeitengeneza njia yako mbele yako,” Mt 11:10. Na ndiyo ilivyokuwa kadiri ya mpango wa Mungu. Mashaka aliyokuwa nayo Yohana Mbatizaji hayana tofauti na mashaka yetu, hasa pale tunapokumbana na sintofahamu katika maisha yetu ya kila siku. Wengine tunakoswa na uvumilivu na subira, na mwisho tunaishia kuaguliwa kwa waganga wa kienyeji, wadanganyifu, na wasio na upeo kuhusu Mungu aliye hai.

Hata hivyo, Yohana anabaki kuwa mfano wa kuigwa hata katika hali ya udhaifu wake. Naye Yesu analithibitisha hilo na kusema, “Amin, nawaambieni, Hajaondokea mtu katika wazao wa wanawake aliye mkuu kuliko Yohana Mbatizaji; walakini aliye mdogo katika ufalme wa mbinguni ni mkuu kuliko yeye,” Mt 11:11. Mwito wa Mungu kwako na kwangu katika hili ni kwamba, ‘tusilipoteze tumaini la kweli hata katika hali ya udhaifu wetu.’ Naye Mungu anasema kwa kupitia Mtumishi wake, Nabii Isaya kwamba, “Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu, yafanyeni imara magoti yaliyolegea,” Isa 35:3. Tunapouishi ubinadamu wetu, na ndivyo ilivyompendeza Mungu na kutuumba, Utukufu wa Mungu ujidhihirisha ndani ya kila mmoja wetu, kwani ndipo ilipo sura na mfano wake. Na tokeo la kuishi ubinadamu wetu kadiri ya mpango wa Mungu kwa kila mmoja wetu, ni kwamba hatupungukiwi neema zake. Na hivi ndivyo itakavyo kuwa; “Nyika na mahali palipo ukiwa patafurahi; jangwa litashangilia na kuchanua maua kama waridi,” Isa 35:1

Huu ni wakati wa kupatanishwa na upendo wa Mungu Baba ambaye yupo tayari kutukomboa kutoka utumwa wa dhambi. Ni huyu tumsubiriaje ambaye, “Nyika na mahali palipo ukiwa patafurahi; jangwa litashangilia na kuchanua maua kama waridi,” Isa 35:1. Anakuja kuuleta uzima pale palipodhoofu, na furaha palipo na ukiwa. “Na hao waliokombolewa na Bwana watarudi, watafika Sayuni wakiimba; na furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao; nao watapata kicheko na furaha, huzuni na kuugua zitakimbia,” Isa 35:10.

Ndugu yangu tunaye safiri sote katika tafakari hii, ili kumjua vizuri Yesu Kristo na uwepo wake katika maisha yako, leo anatupa changamoto na kutufikirisha. Naye anakuuliza wewe na mimi hivi; “Lakini mlitoka kwenda kuona nini? Mtu aliyevikwa mavazi mororo? Tazama, watu wavaao mavazi mororo wamo katika nyumba za wafalme,” Mt 11:8. Maana yake nini? Ni upendo wa ajabu sana kwetu wanadamu kwamba, NENO kafanyika Mwili na kukaa kwetu, Yoh 1:14. Na NENO huyu ni nani? Mwinjili Yohana anatuambia, “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu,” Yoh 1:1-2. Kristo Yesu, ambaye ndiye Neno aliyefanyika Mwili na kukaa kwetu, ni Mungu. Mungu huyu aliwapenda wote bila ubaguzi kwa sababu ndani ya kila mmoja wetu kuna chapa yake, Mwa 1:27. Ni dhambi zako na zangu ndizo zinazotutenga na upendo huu wa Mungu.

Mungu huyu hakuonekana katika majumba ya kifalme wala kuvaa mavazi nyororo, bali alionekana kwa wahitaji, wanyofu wa moyo, na wale wote walioridhia kauli mbiu yake. Marafiki zake wa karibu walikuwa wadhambi, wazinzi, watoto, wanawake, wakoma, watoza ushuru, na wale wote kwa sababu moja au nyingine walitengwa na jamii husika. Mungu huyu alikuwa na ndiye hata leo na umilele wote, ‘sauti ya wasio na sauti.’ Leo Kanisa lapaswa kubeba na kuishi kweli hii ya Kristo Yesu pasipo shaka wala woga. Kanisa hapa nikimaanisha Wabatizwa wote, na wale wote waliopewa dhamana na Mama Kanisa kama viongozi katika ngazi mbalimbali. Naye Yesu anazidi kuzitikisa nafsi zetu na kuuliza, “Lakini kwa nini mlitoka? Ni kuona nabii? Naam, nawaambia, na aliye mkuu zaidi ya nabii,” Mt 11:9. Kwa maana nyingine, ni kipi kinachokusukuma kwa Kristo? Je, wamchukulia Kristo kama shirika ya msalaba mwekundu? Kristo ni nani, na nini katika maisha yako? Je, ni mmoja ya watu maarufu katika historia? Je, leo Yesu kwako ni Yesu wa historia?

Ndugu yangu, Kristo asipokuwa hamu ya moyo wako, na sababu ya kila kitu katika maisha yako, atabaki kuwa Kristo wa matukio, yaani, tutamwona tu kwa hisia zetu siku ya Noeli, Ijumaa Kuu, na Pasaka. Kristo lazima awe shauku yangu kama asemavyo Mtume Yakobo; “Kwa hiyo ndugu, vumilieni, hata kuja kwake Bwana. Tazama, mkulima hungoja mazao ya nchi yaliyo ya thamani, huvumilia kwa ajili yake hata yatakapopata mvua ya kwanza na ya mwisho,” Yak 5:7. Shauku hii iwe maandalizi hai ya Neno huyu kufanyika Mwili ndani yangu, ili niwe ndani na katika Kritso Yesu siku zote za maisha yangu, na mwisho katika uzima wa milele.

Wapendwa katika Kristo, ‘mvumilivu hula mbivu, na siyo mbovu.’ Ila nilivyokwisha kusema, uvumilivu huu bila kulipoteza lile tumaini la kweli iwe nafasi yako ya pekee kujiandaa na kuruhusu Neno kufanyika mwili na kukaa kwako. Hivyo,  “Nanyi vumilieni, mthibitishe mioyo yenu, kwa maana kuja kwake Bwana kunakaribia,” Yak 5:8. Uvumilivu wenye kubeba ufahamu wa kile ukitazamiacho kwa tumaini la kweli, hauna manung’uniko wala kujidharau. “Ndugu, msinung'unikiane, msije mkahukumiwa. Angalieni, mwamuzi amesimama mbele ya milango,” Yak 5:9. Mwamuzi wetu katika kweli na haki yu hai, na anayaona yote yaliyo ndani yetu.

Ndugu yangu, baada ya miaka 27 ya kuugua kwake Josefu Sahani, aliyakabidhi yote mbele ya Mungu, na kuhaidi jambo hili; “baada ya maisha haya ya mateso na kama nitabahatika kukutana na Yesu nitamwambia jambo hili: ‘mbona ulikuwa kimya sana nami nilipokuita katika maumivu yangu makali?’”

Basi kwa vile Kristo alikuwa akisafiri naye ila katika hali ya ukimya, hakuacha kuituliza kiu ya Josefu Sahani. Mara baada ya kifo chake Josefu Sahani alikutana na Yesu, na mara akamuuliza lile swali lake. Yesu akamjibu, “upendo wangu kwako hukuwahi kupungua hata kidogo kwa nyakati zote. Na kadiri ulivyoyasikia mateso makubwa ndivyo nilivyokuwa nawe karibu kupita nyakati zote.”

Je, inawezekanaje hayo uyasemayo Bwana Wangu? Josefu alimuuliza Yesu. Yesu alimwonyesha ramani ya maisha yake ya miaka 27 hapa duniani kama ilivyokuwa. Mara Josefu akamuuliza Yesu, “mbona hapa naona nyayo za watu wawili wakisafiri na ghafla nyayo za mtu wa pili zimepotea na kubaki nyayo za mtu mmoja, tena jangwani na kuna miiba mingi?”

Yesu akamjibu, “Mwanangu, hizo nyayo za watu wawili ni Mimi na wewe tunatembea pamoja, ukiwa upande wangu wa kuume. Hizi ni zile nyakati ambazo uliweza kulala vizuri na hata kusali na kumshukuru Mungu. Unapoona nyayo za mtu mmoja, hizi ni zile nyakati ambazo ulikuwa na maumivu makali sana, na hivyo mimi nilikubeba na nilitembea nawe katika mawe hayo na hiyo miiba. Na ndiyo maana leo umevikwa taji hili lenye kung’ara. Ningekuacha wala leo usingekuwa nami hapa katika furaha hii na maisha haya ya umilele.”

Tumsifu Yesu Kristo!

“Nanyi vumilieni, mthibitishe mioyo yenu, kwa maana kuja kwake Bwana kunakaribia,” Yak 5:8

Tusali: Ee Yesu, tujalie uvumilivu nyakati zote za maisha yetu. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario