JUMAMOSI, SIKU YA 7 YA OKTAVA YA NOELI
DECEMBA 31
Somo: 1Yoh 2:18-21
Zab: 96:1-2, 11-12, 13
Injili: Yoh 1:1-18
Nukuu:
“Watoto,
ni wakati wa mwisho; na kama vile mlivyosikia kwamba mpinga Kristo yuaja, hata
sasa wapinga Kristo wengi wamekwisha kuwapo. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni
wakati wa mwisho,” 1Yoh 2:18
“Nanyi mmepakwa
mafuta na Yeye aliye Mtakatifu nanyi mnajua nyote,” 1Yoh 2:20
“Hapo mwanzo kulikuwako
Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu,” Yoh 1:1
“Vyote vilifanyika kwa
huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika,” Yoh 1:3
“Ndani yake ndimo
ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu,” Yoh 1:4
“Nayo nuru yang'aa
gizani, wala giza halikuiweza,” Yoh 1:5
“Alikuwako ulimwenguni,
hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua,” Yoh 1:10
“Alikuja
kwake, wala walio wake hawakumpokea,” Yoh 1:11
“Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika
watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa
damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa
Mungu,” Yoh 1:12-13
“Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi
tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa
neema na kweli,” Yoh 1:14
“Kwa kuwa katika
utimilifu wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema,” Yoh 1:16
“Kwa kuwa torati
ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo,”
Yoh 1:17
“Hakuna mtu aliyemwona
Mungu wakati wo wote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye
aliyemfunua,” Yoh 1:18
TAFAKARI: “Nanyi
mmepakwa mafuta na Yeye aliye Mtakatifu.”
Wapendwa
wana wa Mungu, tunaishi katika siku za mwisho. “Watoto, ni
wakati wa mwisho; na kama vile mlivyosikia kwamba mpinga Kristo yuaja, hata
sasa wapinga Kristo wengi wamekwisha kuwapo. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni
wakati wa mwisho,” 1Yoh 2:18. Hata hivyo si
wakati wa kujawa hofu na wasiwasi. Wanafunzi wa Yesu pia walitaka kujua hasa
siku hiyo itakuwa lini. Yesu “Akawaambia, Si kazi yenu kujua nyakati
wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe,” Mdo 1:7. Kwa muda
tulibaki nao kila mmoja wetu atimize vyema utume wake kadiri ya wito na karama
alizojaliwa na mwenyezi Mungu.
Matokeo ya utume wako
yatadumu milele kuliko matokeo ya kazi zako. Hivyo Yesu anawaambia wafuasi wake,
“Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi
mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria,
na hata mwisho wa nchi,” Mdo 1:8. Hili ndilo tunalopaswa kufanya sote tulio
mpokea Roho huyu Mtakatifu kwa Sakramenti ya Ubatizo na Kipaimara.
Kwa maana nyingine siku
ya mwisho ni mpaka pale dunia yote itakapofikiwa na habari njema ya wokovu. Ni
pale yote yatakapofikia ukamilisho wake katika umoja ule Yesu aliyotuombe, Yoh
17:18-23. Hivyo kuharakisha siku hii ya mwisho ni sawa na kusema kila mmoja
wetu atimize utume wake vyema na habari hiyo ifike kila kona ya dunia. La sivyo
ni kupoteza muda bure kubashiri siku ya mwisho. Hakuna ajuaye siku hiyo. Naye
Yesu anasema, “Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata
malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake,” Mt 24:36. Neno, yaani, Yesu kesha fanyika mwili na kesha
ushinda ulimwengu, ila tunatembea katika siku zetu za mwisho. Hata hivyo
udhihirisho ulio wazi na kamili wa ushindi wa Yesu upo unakuja.
Katika safari hii kuelekea udhihirisho huo wazi na kamili kati yetu wapo mbwa
mwitu waliovaa ngozi ya kondoo. Katika mtazamo huu, kuishi ni vita. Wapinga
Kristo sio wale wazushi tu, bali ni mtindo pia wa kuishi.
Sote
tu wapinga Kristo katika maana ya kwamba maisha yetu yasipo akisi ukweli na
upendo wa Kristo. Haya ndiyo ayasemayo Mtume Paulo, “Basi
Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani,
wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani; kwa unafiki wa watu wasemao uongo,
wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe; wakiwazuia
watu wasioe, na kuwaamuru wajiepushe na vyakula, ambavyo Mungu aliviumba
vipokewe kwa shukrani na walio na imani wenye kuijua hiyo kweli,” 1Tim 4:1-3.
Leo si jambo la ajabu kusikia dini za waabudu mashetani, wajenzi
huru-free-masons.
Lakini pamoja na ukweli
huo, Kristo ndiye “Nguvu upendo” yenye
kuyashukuma na kuyaratibisha yote kuelekea ukamilifu wake, yaani, kusudi la
kila kilichoumbwa. Na kusudi la kuumbwa kwetu wanadamu ni kuishi milele. Kuishi
ndani na katika Kristo ndiyo sehemu salama na ngome imara. “Mungu wa Bwana wetu
Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika
kumjua yeye; macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi
lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo;
na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadiri ya
utendaji wa nguvu za uweza wake; aliotenda katika Kristo alipomfufua katika
wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho; juu sana kuliko
ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si
ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; akavitia vitu vyote chini ya
miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo ndilo
mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote,” Efe 1:17-23.
Kristo kesha shinda ila
vita inaendelea dhidi ya wema na uovu. Wale watakaokuwa katika kweli watakuwa
katika hatua ya ukomavu na utakaso. Kuzaliwa kuliko kwa kweli kunatoka juu,
ambako ndiko kupakwa mafuta kwetu kupitia Sakramenti ya Ubatizo na Kipaimara. “Nanyi
mmepakwa mafuta na Yeye aliye Mtakatifu nanyi mnajua nyote,” 1Yoh 2:20. Hivyo
kuishi Ukristo ni vita dhidi ya mpinga Kristo. Utaielewa vizuri vita hii
unapofanya tafiti moyo.
Injili ya leo mada kuu
ni hii, “Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote; Mungu Mwana pekee aliye
katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua,” Yoh 1:18. Yesu, Mwana, ni
dhihirisho la Baba. Kwa hiyo kwa maneno haya, “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye
Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu,” Yoh 1:1, kati yetu uwazi wa
utufuku wake unawezesha uelewa wetu wa maneno haya, “Naye Neno alifanyika
mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee
atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli,” Yoh 1:14.
Ni kwa mantiki hilo
kwamba katika mwili Mungu ni kama Baba, Yoh 1:1-3. Ye yote yule amtazamaye
mwana, Yesu Kristo, amwona Baba. “Yesu
akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo?
Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuonyeshe Baba?” Yoh 14:9. Ni katika tendo hili la “kuona,” upewa
tu yule asikiaye neno, ni yule kwa imani kupitia mwili anaona Utukufu wa Baba. “Bali
wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale
waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi
ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu,” Yoh 1:12-13.
Kwa hiyo ujio wa Kristo ni mgogoro
katika maana ya mtengano wa wanaoishi katika mwanga na wale waishio katika giza,
Kristo akiwa ndiye mwanga wa ulimwengu. Watakao upokea mwanga huu, watapokea
kwa imani zawadi zilizo kubwa atakazo kuja nazo. “Bali
wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale
waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi
ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu,” Yoh 1:12-13
Wapendwa katika Kristo,
pona yetu katika siku hizi za mwisho ni kuishi katika mwanga wa Kristo. Sote
tuliobatizwa yatupasa kuziishi ahadi zetu za ubatizo kwa uaminifu. Pia tuwe
makini kwa mafundisho ya uongo juu ya kweli na haki ya Kristo, kwani wengi
watakuja kwa jina lake.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Wapenzi, msiiamini kila roho, bali
zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo
wengi wametokea duniani,” 1Yoh 4:1
Tusali:
Ee Yesu Mwema, nasadiki pasipo shaka yoyote Wewe ndiye Njia, Kweli, na Uzima wa
maisha yangu. Amina
Ahsante sanaaa kwa tafakari hii Mungu aendelee kukupigania katika utume wako. Tumsifu Yesu Kristo
ResponderEliminar