martes, 27 de diciembre de 2016

TAFAKARI: ALHAMISI, SIKU YA 5 YA OKTAVA, KIPINDI CHA NOELI


ALHAMISI, SIKU YA 5 YA OKTAVA, KIPINDI CHA NOELI

DECEMBA 29

Somo: 1Yoh 2:3-11

Zab: 96:1-2a, 2b-3, 5b-6

Injili: Lk 2: 22-35

Nukuu:

Na katika hili twajua ya kuwa tumemjua yeye, ikiwa tunashika amri zake,” 1Yoh 2:3 

 Lakini yeye alishikaye neno lake, katika huyo upendo wa Mungu umekamilika kweli kweli. Katika hili twajua ya kuwa tumo ndani yake,” 1Yoh 2:5 

 Kisha, zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana, (kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana),” Lk 2:22-23

 Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli,” Lk 2:32 

Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa,” Lk 2:34

“Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi,” Lk 2:35

TAFAKARI: “Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli. Huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi.”

Wapendwa wana wa Mungu, kuishi katika Nuru ya kweli ni kuishi katika KWELI na HAKI. Hii ndiyo mizania au kipimo halisi ndani na katika Kristo. Mizania hii hutuongoza katika kuzishika amri zake kwa sababu tunajua kweli juu ya amri hizo na sababu yake kuelekea umilele. Mizania hii hutupeleka zaidi kwa Kristo, kwani tu huru katika kweli, Yoh 8:32. Na nuru hii ambayo ndiyo uwepo wa Kristo ndani yetu, ni vita isiyo na kikomo dhidi ya giza.

Mkristo amfuataye Kristo Yesu katika kweli na haki ni mtangaza vita dhidi ya mwanga na giza, wema na uovu. Mtihani mkubwa ambao twapambana nao katika hali hii ni pale wewe na mimi ‘ninapoishi upendo kati  yangu na Mungu, kati yangu na jirani, na kati yangu na Mazingira yanayonizunguka.’ Hivyo huu ndio mwaliko wa kuwa chumvi na nuru katika ulimwengu huu; “Ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu. Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima,” Mt 5:13-14. Wote wale walio chumvi na nuru katika ulimwengu huu kamwe Mungu hatovunja ahadi na mategemeo yao.

Hivyo somo letu la kwanza na Injili, yanatutafakarisha juu ya maisha ya nuru ambayo msingi wake ni kuishi katika kweli na haki. Kweli na haki hutuongoza kuzishika amri za Mungu kwa uaminifu. “Na katika hili twajua ya kuwa tumemjua yeye, ikiwa tunashika amri zake,” 1Yoh 2:3. Asiyeishi katika kweli na haki ni vigumu kumwelewa Kristo aliye Haki na kweli. Hakika tutakuwa waongo wakubwa. Hivyo, “Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake,” 1Yoh 2:4. Kweli na haki hutuongoza kwenye neno lake ambalo ndilo uzima. Huku ndiko kukamilika ndani na katika Kristo Yesu. “Lakini yeye alishikaye neno lake, katika huyo upendo wa Mungu umekamilika kweli kweli. Katika hili twajua ya kuwa tumo ndani yake,” 1Yoh 2:5.

Kukaa ndani na katika Kristo ni ukomavu wa kiroho. Hatuendi kwake kwa shuruti  wala kulazimishwa mara tunapoutambua ukweli na nafasi ya Kristo ndani ya maisha yetu. Tunaenda kwake kwa hiari yetu kwa sababu tunajua yeye ndiye kweli, njia na uzima, Yoh 14:6. Hivyo, “Yeye asemaye ya kuwa anakaa ndani yake, imempasa kuenenda mwenyewe,” 1Yoh 2:5. Ukomavu wa Imani ambao ni nuru chini ya msingi wa kweli na haki utuweka karibu sana na Kristo Yesu. Hivyo kila tunayekutana naye twamwona Kristo ndani yake. Hivyo hatuwezi kamwe kuishi katika chuki na yeyote yule kwa sababu twaishi katika nuru ya kweli. “Yeye asemaye kwamba yumo nuruni, naye amchukia ndugu yake, yumo gizani,” 1 Yoh 2:9. Kuishi katika chuki yamaanisha kwamba bado hujakutana na Kristo, na hivyo bado u gizani.

 Matumaini yetu kama binadamu, ingawa hatujui ni lini yatakuwa kweli, Mungu hawezi kuyasahau kwani twaishi kile tunachokiamini katika kweli na haki. Injili ya leo inatupa mfano ulio hai wa yule aliyeishi katika nuru ya kweli chini ya msingi wa kweli na haki. Huyu ndiye Simeoni.

Simeoni anakutana na nuru hii ya kweli na haki wakati Yesu anapotolewa hekaluni kama ilivyo desturi ya Wayahudi kwa kila mzaliwa wa kwanza wa kiume. “Kisha, zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana, (kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana),” Lk 2:22-23. Hata hivyo, kumkomboa huyu mzaliwa wa kwanza kutoka hekaluni iliwapasa wazazi wake kumtolea Bwana sadaka kama shukrani. “Wakatoe na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana, Hua wawili au makinda ya njiwa wawili,” Lk 2:24. Sadaka hii inaonyesha umasikini wa Familia hii Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu.

Ni katika tendo hili pale Hekaluni, Simeoni mtu wa kweli na haki ahadi yake inatimizwa na Mungu. “Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake,” Lk 2:25. Yesu Kristo hapa ndiye nuru halisi na uhuru wa kweli wa wana wa Taifa la Mungu. Kristo ndiye  ile nuru aliyokuwa ikisubiriwa, “Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli,” Lk 2:32.

Mungu anaifunua nuru ya Yesu ndani ya moyo wa Simeoni naye anayaona makuu ndani ya Yesu: “Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa,” Lk 2:34. Kristo ndiye sababu ya kuanguka na kuinuka wengi, kwa sababu ulimwenguni hapa ni vita dhidi ya mwanga ambaye ndiye Kristo, na giza ambayo ndiye yule mwovu shetani. Watainuliwa wale watakaoambatana na mwanga na wataangushwa wale waambatanao na giza, yaani yule mwovu.

Katika vita hii Mama Bikira Maria hatakuwa salama katika maana ya kufurahia tu uwepo wa mwanaye. Ni katika uchungu na kushiriki mateso ya mwanaye nuru ya kweli na haki itafunuliwa ndani yake. Hivyo ni katika msalaba ambao mwanaye anauendea ndipo utakapokuwepo utukufu wake. “Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi,” Lk 2:35. Kwenye Msalaba Mtakatifu na wenye ushindi wa Bwana Yetu Yesu Kristo ndipo penye Utukufu, kufunguliwa kwa mioyo yetu kutoka utumwa wa dhambi, na kuuelekea uzima wa milele. Ndugu yangu, mimi ninao wangu Msalaba. Nawe unao wako Msalaba. Chunguza vizuri. Upo. Hivyo kwa Mkristo na Mfuasi wa Kristo, hakuna UTUKUFU pasipo MSALABA.

Tumsifu Yesu Kristo!

Atamkaye maneno ya kweli hufunua haki; Bali shahidi wa uongo hutamka hila. Nuru ya mwenye haki yang'aa sana; Bali taa ya mtu mbaya itazimika,” Mit 12:7, 13:9

Tusali: Ee Yesu uliyeushinda Msalaba na kuniweka huru, nijalie nami niushinda  wangu msalaba ili niurithi uzima wa milele. Amina

1 comentario: