JUMANNE WIKI YA 18 YA MWAKA-C
Somo:
Yer 30:1-2, 12-15, 18-22
Zab: 102:16-18, 19-21, 29, 22-23
Injili:
Mt 14:22-36
Nukuu:
Maana
Bwana asema hivi, Maumivu yako hayaponyekani, na jeraha yako ni kubwa. Hapana mtu wa kukutetea; kwa jeraha
yako huna dawa ziponyazo,” Yer 30:12-13
“Wote
wakupendao wamekusahau; hawakutafuti; maana nimekujeruhi kwa jeraha ya adui,
kwa adhabu ya mtu mkatili; kwa sababu ya ukubwa wa uovu wako, kwa sababu dhambi
zako zilikuwa zimeongezeka,” Yer 30:14
“Nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu,” Yer
30:22
“Na kile chombo kimekwisha kufika katikati ya bahari,
kinataabika sana na mawimbi; maana upepo ulikuwa wa mbisho,” Mt 14:24
“Wanafunzi walipomwona akienda juu ya bahari, wakafadhaika,
wakisema, Ni kivuli; wakapiga yowe kwa hofu,” Mt 14:26
“Mara
Yesu alinena, akawaambia, Jipeni moyo ni mimi; msiogope,” Mt 14:27
“Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe
mwenye imani haba, mbona uliona shaka?” Mt 14:31
TAFAKARI:
“Nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu
wenu.”
Wapendwa wana wa Mungu,
Mungu wetu aliye hai anatuambia, ‘ninyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu
wenu.’ Maneno haya ya Mungu pamoja na ukuu wake, yanafafanua Mungu wetu ni wa
aina gani, na zaidi yanaonyesha uhusiano wa Mungu huyu na viumbe vyake. Uhusiano
wa Mungu wetu si ule wa mtumwa na mtwana, bali ni uhusiano wa Baba mwenye
kujali na kuwajibika ipasavyo. Ni Mungu mwenye kujali na asiyesahau ahadi zake
hata pale tunapokumbana na sintofahamu nyingi katika maisha ya kila siku. Kamwe
Mungu hawezi kuisahau sura na mfano wake katika tendo zima la uumbaji wetu sisi
wanadamu, Mwa 1:27.
Kwa mwonekano huu wa
Mungu wetu, ni wazi Mungu wetu “ni mpole wa
hasira, mwingi wa rehema, mwenye kusamehe uovu na makosa, naye hatamfanya
mwenye hatia kuwa hana makosa kwa njia yo yote; mwenye kuwapatiliza wana kwa
uovu wa baba zao, katika kizazi cha tatu na cha nne,” Hes 14:18. Hata hivyo,
upole na wingi huu wa rehema za Mungu siyo halalisho la sisi kufanya
kama tutakavyo, bali ni mwaliko wa sisi kufanana naye katika ukamilifu wake, Mt
5:48. Tunaposhindwa kuzifuata njia za Mungu, ni dhahiri tutakayo kutana nayo mbele ya safari yatakuwa tokeo matakwa yetu, na siyo ya
Mungu. Huu ndio uovu tutesekao kama tokeo la ufahamu na utashi wetu. “Maana Bwana asema hivi, Maumivu yako hayaponyekani, na
jeraha yako ni kubwa. Hapana mtu
wa kukutetea; kwa jeraha yako huna dawa ziponyazo,” Yer 30:12-13. Mateso na
mahangaiko ya Taifa lile teule la wana wa Israeli kwa kiasi kikubwa yalitokana
na uasi wao kwa kumsahau Mungu na kuenenda kadiri ya ubinafsi na matakwa yao
yasiyo na hofu ya Mungu ndani yake.
Mungu
hubaki kama Mungu, na katika nafasi yake kama Mungu. Jambo la ajabu na
kusikitisha ni pale mwanadamu anapojifananisha na Mungu, na kutoa maneno mazito
ambayo huzidi upole na wingi wa rehema za Mungu. Mwanadamu huyu ambaye hata
sekunde moja ya uhai wake haiijui, hujijengea himaya ya juu kuliko hata
makerubi. Hujikuza na hata kujiona kuwa zaidi ya Mungu unapoyatazama matendo
yake. Vita yoyote ile dhidi ya Mungu na watu wake mwanadamu mwenye mifupa na
nyama hawezi kuishinda hata kidogo. Kuendelea kushindana na Mungu kwa mtindo
huu ni dhihirisho la ufinyi wetu wa kufikiri uliojaa mbwembwe za hapa na pale
kama mvua za vuli.
Na hii
ndiyo maana ya kutegemea nguvu zetu na urafiki wa kibinadamu wenye kupotoshana
kama asemavyo Mungu kupitia kinywa cha Nabii Yeremia, “Wote
wakupendao wamekusahau; hawakutafuti; maana nimekujeruhi kwa jeraha ya adui,
kwa adhabu ya mtu mkatili; kwa sababu ya ukubwa wa uovu wako, kwa sababu dhambi
zako zilikuwa zimeongezeka,” Yer 30:14. Katika majivuno na hali hii ya
kujihesabia haki, Mungu hubaki kama alivyo na ukuu wake si kwa ubaya, bali kwa
vile umejitenga naye. Hivyo kulia kwako na lawama zako juu yake hukurudia mwenyewe
hadi pale utakapoifuata njia yake na kukutana naye. Naye Mungu anakuambia, “Mbona unalilia maumivu yako? Hayaponyeki maumivu
yako; kwa sababu ya ukubwa wa uovu wako, kwa sababu dhambi zako zimeongezeka,
nimekutenda haya,” Yer 30:15. Ponya yako katika hali na mazingira haya ni
kumrudia Mungu kwa toba ya kweli na majuto.
Unapomrudia
Mungu katika toba ya kweli na majuto, Mungu hurudisha ahadi zake zote, neema na
baraka. Na hivi ndivyo atakavyofanya kwa wana wa Israeli. “Bwana
asema hivi, Tazama, nitarudisha tena hema za Yakobo zilizohamishwa, na
kuyahurumia makao yake; nao mji huo utajengwa juu ya magofu yake wenyewe, nalo
jumba litakaliwa, kama ilivyokuwa desturi yake,” Yer 30:18. Huyu ndiye Mungu
aliye hai na mwenye kututakia mema muda wote. Naye anasema, “Tena
kwao itasikiwa shukrani, na sauti yao wachangamkao; nami nitawazidisha, wala
hawatakuwa wachache; tena nitawatukuza, wala hawatakuwa wanyonge,” Yer 30:19.
Tukiwa na Mungu aliye hai hatuna cha kuogopa wala kufishwa. Licha ya kutupa
yale tunayohitaji, Mungu utulinda dhidi ya
adui na watesi wetu.
Na
katika hili Mungu anasema, “Watoto wao nao
watakuwa kama zamani, na kusanyiko lao litathibitika mbele zangu, nami
nitawaadhibu wote wawaoneao,” Yer 30:20. Katika usalama huu na amani, Mungu
humwinua mmoja katika kundi kuliongoza kundi hilo katika kweli na haki. “Na
mkuu wao atakuwa mtu wa kwao wenyewe, naye mwenye kuwatawala atakuwa mtu wa
jamaa yao; nami nitamkaribisha, naye atanikaribia; maana ni nani aliye na moyo
wa kuthubutu kunikaribia? Asema Bwana,” Yer 30:21. Ndugu yangu, ukizitazama
siasa za Bara letu la Afrika na sehemu nyingine kusipokoma vita na mateso ya
watu, karibia wote waliohodhi mamlaka hawakuwa na siyo matakwa ya Mungu kupitia
watu wake kwa sanduku la kura. Kinachofanyika ni mchezo wa kuigiza.
Wengi
hujitokeza kuchagua wampendaye na mwenye mastahili hayo kadiri ya hitaji la
wakati, ila watu wachache na tena wasiozidi kumi huamua nani awe kiongozi. Hii
ni dhambi kubwa sana, na ndiyo chanzo cha mateso ya watu. Ni vyema kuheshimu sauti
ya Mungu kupitia watu wake walio huru na wenye utashi katika maamuzi. Naye
Mungu anasema, “Nanyi mtakuwa watu wangu,
nami nitakuwa Mungu wenu,” Yer 30:22. Tunapokosa hofu ya Mungu katika matendo
yetu, Mungu hujitenga nasi hadi pale tutakapo mtafuta. Leo badala ya kuwa na
hofu ya Mungu, wengi tumekuwa na hofu isababishwayo na ubinadamu wetu, na hofu
ya wachache wanaojitwalia umungu watu.
Ndugu yangu, hofu ni
kitu kibaya sana katika maisha. Ikiwa maisha ya kawaida ya mtu hujengwa katika
msingi wa Imani, hofu kwa upande mwingine hubomoa msingi huu. Ukiwa na hofu
huwezi kufikiri sawasawa, huwezi kupanga mipango yako sawasawa, huwezi kukua
kimwili na kiroho, huwezi kuabudu vizuri. Hofu hutujengea shaka kwa kila kitu
tufanyacho. Hatuwezi kumwendea Mungu katika hali ya hofu. Tukiwa na hofu ni
vigumu kuelewa fumbo la Kristo katika maneno yake yale matatu: “mimi ndiye
njia, kweli na uzima,” Yoh 14:6. Hivyo Yesu anapowaacha wafuasi wake wenyewe
katika boti, wanaingiwa na hofu wanapomwona akitembea juu ya baharí. Wote
wanadhani kuwa yeye ni kivuli. “Wanafunzi
walipomwona akienda juu ya bahari, wakafadhaika, wakisema, Ni kivuli; wakapiga
yowe kwa hofu,” Mt 14:26. Wanafunzi wa Yesu wanashindwa kufahamu ukuu wa
Kristo na mamlaka aliyokuwa nayo. “Nao walipomwona, walimsujudia; lakini baadhi yao
waliona shaka. Yesu akaja kwao,
akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani,” Mt
28:17-18. Tukiwa ndani na katika Kristo hatuna sababu yoyote kuwa na mashaka
juu ya utendaji wake.
Hata katika hali hii ya
hofu na sintofahamu katika maisha, Kristo anatuambia kama alivyowaambia
wanafunzi wake, “Jipeni moyo ni mimi; msiogope,” Mt 14:27. Ila ukweli
ni kwamba kwa Mkristo yule anayejitamba kuwa ni mfuasi wa Kristo, na akawa na
mashaka juu ya utendaji wa Kristo katika maisha yake, huwa sikitiko kubwa kwa
Yesu Kristo. Hivyo ndivyo
ilivyokuwa kwa wanafunzi wa Yesu. “Mara
Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona
uliona shaka?” Mt 14:31. Je, wamwamini Kristo
wakati mambo yako yakikunyookea tu? Ni kweli kwamba Yesu hawezi kuongea nawe
katika shida? Je, Yesu anamaanisha nini anaposema yeye ndiye NJIA? Ndugu yangu
labda nikukumbushe kidogo. Njia ya kweli aliyoichagua Yesu kukukomboa kutoka
utumwa wa dhambi, ni njia ile aliyoichukua, yaani, njia ya mateso. Hivyo Yesu
anatuambia hata katika mateso tunawekwa huru katika kweli. Ni kwa namna hiyo
hiyo kwamba hakuna Utukufu pasipo Msalaba.
Wapendwa katika
Kristo, ni katika Imani ya kweli Kristo anaendelea kutuponya majeraha yetu ya
mwili na roho. “nao wakamsihi waguse hata pindo la vazi lake tu; na wote
waliogusa wakaponywa kabisa,” Mt 14:36. Hili ni tendo la Imani. Uwe na Imani,
Usiogope.
Tusifu
Yesu Kristo!
“Jipeni
moyo ni mimi; msiogope,” Mt 14:27
Tusali:-Ee Yesu, uliye
tumaini letu, kwako kuna amani ya kweli. Litazame taifa letu katika mapito
yake. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario