martes, 30 de agosto de 2016

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 22 MWAKA-C

JUMATANO WIKI YA 22 YA MWAKA-C
Somo: 1Kor 3:1-9
Zab/Kit: 33:12-13, 14-15, 20-21
Injili: Lk 4:38-44
Nukuu
Lakini, ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama na watu wenye tabia ya rohoni, bali kama na watu wenye tabia ya mwilini, kama na watoto wachanga katika Kristo,” 1Kor 3:1 

 “Mimi nilipanda, Apolo akatia maji; bali mwenye kukuza ni Mungu,” 1Kor 3:6

Hivyo, apandaye si kitu, wala atiaye maji, bali Mungu akuzaye,” 1Kor 3:7

 “Akasimama karibu naye, akaikemea ile homa, ikamwacha; mara hiyo akaondoka, akawatumikia,” Lk 4:39 

 “Pepo nao waliwatoka watu wengi, wakipiga kelele na kusema, Wewe u Mwana wa Mungu. Akawakemea, asiwaache kunena, kwa sababu walimjua kuwa ndiye Kristo,” Lk 4:41

 “Akawaambia, Imenipasa kuihubiri habari njema ya ufalme wa Mungu katika miji mingine pia; maana kwa sababu hiyo nalitumwa,” Lk 4:43 

TAFAKARI: Hivyo, apandaye si kitu, wala atiaye maji, bali Mungu akuzaye,” 1Kor 3:7

Wapendwa wana wa Mungu, uwepo wa Kristo katika maisha yetu ni habari njema ya ufalme wa Mungu. Habari hii njema ni wokovu na uzima wetu. Ujio wa Yesu kwetu, yaani, Neno kufanyika mwili na kukaa kwetu, Yoh 1:14, siyo ujio wa mwivi mwenye kupora na kuondoka. Naye Yesu anasema, Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele,” Yoh 10:10. Ujio wa Kristo ni uzima kwetu, na tena atutaka tuwe nao wa kutosha. Ukweli huu unajidihirisha katika uponyaji wa Mama mkwe wa Petro Mtume, Lk 4:38. Yesu akasimama karibu naye, akaikemea ile homa, ikamwacha; mara hiyo akaondoka, akawatumikia,” Lk 4:39. Kama tendo la shukrani kwa uponyaji ule, kilichofuata ni kuwajibika kama sehemu ya kuyafanya mapenzi ya Mungu. 

 Kristo anatutaka pamoja na mambo yote tuyafanyayo kila siku tusiache kamwe kuutafuta ufalme wa Mungu. Ufalme huo umeshajidhihirisha hapa hapa duniani kwa matendo ya wokovu ya Kristo mwenyewe. Na jua lilipokuwa likichwa, wote waliokuwa na wagonjwa wenye maradhi mbali mbali waliwaleta kwake, akaweka mikono yake juu ya kila mmoja akawaponya,” Lk 4:40. Alama na ishara hizi zinaufunua Utukufu wa Mungu na Ufalme wake. Pepo nao waliwatoka watu wengi, wakipiga kelele na kusema, Wewe u Mwana wa Mungu. Akawakemea, asiwaache kunena, kwa sababu walimjua kuwa ndiye Kristo,” Lk 4:41. Uwepo wa Kristo unatikisa mfumo mzima wa shetani, na hiki ndicho kiama cha uovu na kushamiri kwa wema ndani na katika Kristo. Ni kwa sababu hiyo Kristo kaja kwetu. Tuushinde uovu kwa wema mara zote katika maisha yetu.

Mambo yote tuyapataya duniani hapa kwayo yenyewe siyo ukamilifu wa yale aliyotuandalia Mungu katika ufalme wake. Ni kwa mantiki hiyo, ishara au miujiza licha ya kuufunua Utukufu wa Mungu, kwayo kama ilivyo siyo mwisho wa kila kitu, bali utusaidia kukua katika Imani. Hata kulipokucha alitoka akaenda mahali pasipokuwa na watu; makutano wakawa wakimtafuta-tafuta, wakafika kwake, wakataka kumzuia asiondoke kwao,” Lk 4:42. Kutaka kumzuia Yesu abaki nao ni kupenda kugaagaa katika miujiza ambayo kwayo kama ilivyo siyo kusudi hasa la ujio wa Kristo kwetu.

Kupenda ishara na kubaki katika ishara ni alama ya kutokukua au kukomaa katika Imani.  Yesu anawaambia wale waliokuwa wanataka kukaa naye tu, “Imenipasa kuihubiri habari njema ya ufalme wa Mungu katika miji mingine pia; maana kwa sababu hiyo nalitumwa,” Lk 4:43. Na kauli mbiu ya Yesu kwako na kwangu ni hii; “Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili,” Mk 1:15. Wapendwa, yatupasa kuinjilishana ili kila mmoja ajue kusudi la Yesu hapa duniani.

Kielelezo cha kazi hii ya kuinjilishana ni Kristo mwenyewe na siyo kujiinua kwetu kuliko kwa kibinadamu. Nafasi yako katika uinjilishaji ni kama chombo cha udongo katika kutimiza wajibu wake kwa yale ipasayo kufanya. Hakika sote tu vyombo vya udongo kama asemavyo Mtume Paulo, Lakini tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwetu,” 2Kor 4:7. Hatuna cha kujisifia zaidi ya kumshukuru Mungu kwa kututumia vyema hata katika udhaifu wetu. Lakini, ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama na watu wenye tabia ya rohoni, bali kama na watu wenye tabia ya mwilini, kama na watoto wachanga katika Kristo,” 1Kor 3:1. Leo na hasa tunapozungumzia uinjilishaji mpya, ni wito kwa kila mbatizwa kuifanya kazi hiyo kuanzia pale alipo.

Leo wengi wetu hatuweki tena mkazo katika mafundisha ya Kanisa na badala yake tumekuwa ‘vidakizi’ wa mambo na mwisho wa siku kukosa mwelekeo thabiti wa imani. Ndugu yangu, mkate usioiva vizuri ni hatari sana kwa tumbo. Wengi wetu leo twatambulika kama Wakrito kwa majina yetu tu. Hili ni jangwa la Imani katika familia. Ukweli ni kwamba, familia ndiyo shule ya kwanza kabisa tunapoweza kujifunza na kuishi imani yetu.

Baba na Mama ndiyo walimu wetu wa Imani. Mtume Paulo anatambua wajibu wake katika kweli hii, na kusema, Naliwanywesha maziwa sikuwalisha chakula; kwa kuwa mlikuwa hamjakiweza. Naam, hata sasa hamkiwezi, kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je! Si watu wa tabia ya mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu?” 1Kor 3:2-3. Kumjua na kumuishi Kristo ni kuwa upande wa mabadiliko, yaani, kutoka kwenye giza na kuingia katika mwanga.

Mabadiliko hayo na katika ngazi tofauti tofauti yasiwe sababu ya mimi au wewe kujisifia na kujikweza. Udakuzi hapa si nani kafanya nini au kamzidi nini mwenzake, bali sote kwa pamoja tumelifikia lengo la kuihubiri habari njema? Maana hapo mtu mmoja asemapo, Mimi ni wa Paulo; na mwingine, Mimi ni wa Apolo, je! Ninyi si wanadamu?” 1Kor 3:4. Je, hayo yote tuyaonayo pamoja na tofauti zetu katika utendaji yapo kama yalivyo kwa nguvu zetu binafsi?  Basi Apolo ni nani? Na Paulo ni nani?” IKor 3:5a. Tofauti zetu katika utendaji ndiyo uzuri wa Mungu. Hatukuumbwa tuwe ‘maroboti,’ bali tuwe wamoja katika tofauti zetu. Hivyo Apolo na Paulo “ni wahudumu ambao kwao mliamini; na kila mtu kama Bwana alivyompa,” 1Kor 3:5b. Na ndivyo ilivyo mpendeza Mungu.

Uzuri wa umoja katika utofauti ukuza ubunifu na utofauti wa yale ya kawaida tuyafanyayo. Katika hili Mtume Paulo anasema, Mimi nilipanda, Apolo akatia maji; bali mwenye kukuza ni Mungu,” 1Kor 3:6. Tunapozitanguliza nafsi zetu kwa kila jambo, tunazikwamisha neema za Mungu ndani yetu. Ni sawa na kubaki katika furaha ya kujichora kwako kusikobeba uhasili wako. Ukweli ni kwamba, apandaye si kitu, wala atiaye maji, bali Mungu akuzaye,” 1Kor 3:7. Je, natambua nguvu hiyo ya Mungu ndani yangu na kwa mwenzangu? Kama natambua kweli hiyo, Je, namshukuru Mungu kwa uwepo wa mwenzangu na mafanikio yake? Ndugu yangu, yeye apandaye, na yeye atiaye maji ni wamoja, lakini kila mtu atapata thawabu yake mwenyewe sawasawa na taabu yake mwenyewe,” 1Kor 3:8. Kufurahia mafanikio ya mwenzako na kumshukuru Mungu ni ukomavu wa imani.

Wapendwa wana wa Mungu, kamwe tusisahau ukweli huu kwamba, sisi tu wafanya kazi pamoja na Mungu; ninyi ni shamba la Mungu, ni jengo la Mungu,” 1Kor 3:9. Umoja katika utofauti wetu ndiyo uzuri wa Mungu na wenye kuufunua Utukufu wake.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Imenipasa kuihubiri habari njema ya ufalme wa Mungu katika miji mingine pia; maana kwa sababu hiyo nalitumwa,” Lk 4:43


Tusali:-Ee Yesu, tutumie vyema kama vyombo vyako vya udongo. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario