JUMATANO
WIKI YA 19 YA MWAKA-C
Somo: Eze 9:1-7, 10:18-22
Zab: 113:1-2, 3-4, 5-6
Injili: Mt 18:15-20
Nukuu
“Waueni
kabisa, mzee, na kijana, na msichana, na watoto wachanga, na wanawake; lakini
msimkaribie mtu ye yote mwenye hiyo alama; tena anzeni katika patakatifu pangu.
Basi, wakaanza kwa wazee waliokuwa mbele ya nyumba,” Eze 9:6
“Nao makerubi wakainua mabawa yao, wakapaa juu kutoka katika
dunia machoni pangu, hapo walipotoka nje, nayo magurudumu yakawa kando yao;
wakasimama mahali pa kuingilia pa mlango wa upande wa mashariki wa nyumba ya
Bwana; na utukufu wa Mungu wa Israeli ulikuwa juu yao,” Eze 9:19
“Na
ndugu yako akikukosa, enenda ukamwonye, wewe na yeye peke yenu; akikusikia,
umempata nduguyo,” Mt 18.15
“Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana
duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye
mbinguni,” Mt 18:19
TAFAKARI: “Na ndugu yako akikukosa, enenda
ukamwonye, wewe na yeye peke yenu; akikusikia, umempata nduguyo.”
Wapendwa
wana wa Mungu, tulitazamapo Agano la kale na Agano jipya, tunaona umbali na
ukaribu wa Mungu. Pamoja na mambo mengi, Agano la Kale linaonyesha Mungu aliye
mbali, na mwenye kutoa adhabu za papo kwa papo licha ya kwamba upendo na huruma
yake huzidi uovu na dhambi za mwanadamu. Na hivi ndivyo ghadhabu ya Mungu
inavyojionyesha katika mazingira na hali ya waja wake wanapokwenda ndivyo
sivyo. Naye anamwambia Nabii Ezekieli, “Waueni
kabisa, mzee, na kijana, na msichana, na watoto wachanga, na wanawake; lakini
msimkaribie mtu ye yote mwenye hiyo alama; tena anzeni katika patakatifu pangu.
Basi, wakaanza kwa wazee waliokuwa mbele ya nyumba,” Eze 9:6.
Ghadabu hizi za Mungu za dhihirisha umbali wa
utukufu wake. “Kisha
huo utukufu wa Bwana ukatoka pale juu ya kizingiti cha nyumba, ukasimama juu ya
makerubi,” Eze 9:18. Agano hili la Kale laonyesha umbali wa utendaji wa Mungu,
ingawa Mungu hakuachana wala kujitenga daima na watu wake katika nyakati zote.
Hili linajidhihirisha utendaji wa Mungu kupitia manabii wake mbalimbali, na
hata waamuzi. “Nao
makerubi wakainua mabawa yao, wakapaa juu kutoka katika dunia machoni pangu,
hapo walipotoka nje, nayo magurudumu yakawa kando yao; wakasimama mahali pa
kuingilia pa mlango wa upande wa mashariki wa nyumba ya Bwana; na utukufu wa
Mungu wa Israeli ulikuwa juu yao,” Eze 9:19.
Na kwa njia hii Mungu aliweza kupatana na watu wake kupitia watumishi wake
waaminifu, kama manabii.
Hata hivyo Agano Jipya
linaonyesha ukaribu wa Mungu. Na huyu ndiye Imanueli, Neno aliyefanyika mwili
na kukaa kwetu, Yoh 1:14. “Kwa
hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa
mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli,” Isa 7:14. Na huu ndiyo unabii uliotabiriwa na kutimia
katika Agano Jipya. “Hayo yote yamekuwa, ili
litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii akisema, Tazama, bikira
atachukua mimba, Naye atazaa mwana; Nao watamwita jina lake Imanueli; Yaani,
Mungu pamoja nasi,” Mt 1:22-23. Huyu ndiye mpatanishi wetu na Mungu. Kristo
ndiye upatanisho wetu na Mungu Baba, naye ndiye kielelezo cha upatanisho sisi
kwa sisi pale tunapokoseana.
Je,
tufanye nini tunapokoseana kama ndugu? Yesu anatufundisha namna ya kufanya.
Naye anasema hivi: “Na ndugu yako
akikukosa, enenda ukamwonye, wewe na yeye peke yenu; akikusikia, umempata
nduguyo,” Mt 18:15. Ni vyema kama umekosana na ndugu yako mkayazungumza mkiwa
naye na kupatana naye. Ni vyema mkayamaliza kama ndugu. Hamuitaji kuyakuza na
kuwafaidia wengine kwa upungufu wenu. Kama hatakusikia na hayupo tayari
kukusikiliza, Yesu anatupa nafasi ya pili. Naye anasema hivi: “Na asipowasikiliza wao, liambie Kanisa; na
asipolisikiliza Kanisa pia, na awe kwako kama mtu wa mataifa na mtoza ushuru,”
Mt 18:17. Kanisa likiwa ndio mwili wa Yesu nasi tukiwa viungo vyake, ndiyo
sehemu muhafaka wa kuyazungumza yale yote yaliyokwenda kinyuma na upendo wa
Mungu. Je, tunatumia nafasi hii vyema kuyamaliza yale yanayotusibu? Kwa nini
basi tunakimbilia mahakamani kwa mambo yetu ya familia? Je, tuupatapo ushindi
huo wa kimahakama utatusaidia kuujenga tena ule undugu wenu ulioingia dosari?
Ndugu yangu, tusipokuwa tayari kulisikiliza Kanisa tunahesabiwa kama watu wa
mataifa.
Wapendwa
wana wa Mungu, yatupasa kuyamaliza mambo yote sisi wenyewe, na pale
tunaposhindwa kufanya hivyo, basi tuliachie Kanisa litusaidie kufikia muhafaka
wa matatizo yetu. Hapa ndipo penye furaha ya Mungu wetu aliye hai. “Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu
watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba
yangu aliye mbinguni,” Mt 18:19. Je, unataka ushindi wa kidunia au upendo wa
Mungu wako aliye hai? Patana na ndugu yako kindugu, naye Mungu atakuneemesha
katika haki na kweli. Na “walipo wawili
watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao,” Mt
18:20. Utulivu na amani ni uwepo wa Mungu.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Tena
nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote
watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni,” Mt 18:19
Tusali:-Ee Yesu uliye
mpatanishi wetu na Mungu Baba, tujalie moyo wa msamaha tunapokosewa na
kuwakosea wengine. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario