miércoles, 24 de agosto de 2016

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 21 YA MWAKA-C

ALHAMISI WIKI YA 21 YA MWAKA-C
Somo: 1Kor 1:1-9
Zab/Kit: 145:2-3, 4-5, 6-7
Injili: Mt 24:42-51
Nukuu
 “Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo,” 1Kor 1:3

Namshukuru Mungu sikuzote kwa ajili yenu, kwa sababu ya neema ya Mungu mliyopewa katika Kristo Yesu,” 1Kor 1:4

 “Mungu ni mwaminifu ambaye mliitwa na yeye mwingie katika ushirika wa Mwanawe, Yesu Kristo Bwana wetu,” 1Kor 1:9

Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu,” Mt 24:42

Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa,” Mt 24:34 

TAFAKARI:Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu.”
Wapendwa wana wa Mungu, leo tutafakari kuhusu maisha ni jukumu la muda mfupi. Na ndiyo dhima ya Injili ya leo kwa maneno haya ya Yesu, Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu,” Mt 24:42. Ndugu unayesafiri nami katika tafakari hii, ni ukweli usiofichika kwamba maisha duniani ni jukumu la muda mfupi. Je, unabisha? Maandiko Matakatifu hufundisha na kutukumbusha maisha yetu duniani yalivyo mafupi na yasiyodumu. Maisha yanaelezwa kama ukungu, mkimbiaji, pumzi, na mvuke.  "Kwani sisi tu wa jana tu, wala hatujui neno, kwa kuwa siku zetu duniani ni kivuli tu." Ayu 8:9

Ndugu, ili kutimiza vizuri maisha yako hupaswi kusahau ukweli wa aina mbili: Kwanza, yakilinganishwa na umilele, maisha ni mafupi sana. Pili, dunia ni makazi ya muda tu. Hatuwezi kukaa hapa kwa muda mrefu, hivyo usijishikamanishe sana nayo.Fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa,” Mt 24:34. Tumwombe Mungu atusaidie kuyaona maisha ya duniani kama anavyoyaona yeye mwenyewe. Mfalme Daudi aliomba, "Bwana, nijulishe mwisho wangu, na kiasi cha siku zangu ni kiasi gani; nijue jinsi nilivyo dhaifu," Zab 39:4

Ndugu yangu hapana shaka wa mfahamu vizuri "inzi!" Mdudu huyu kadiri ya utafiki wa kisayansi huishi siku saba tu. Ni wiki moja kati ya wiki 52 katika mwaka mmoja. Tazama fujo na papara za inzi. Hutua kila mahali kwa siku hizo saba; kwenye vyakula (vilivyo chacha na visivyo chacha), kwenye vinjwaji, kwenye vidonda, kwenye vinyesi, nk. Tazama anavyoongea kwa ishara akiwa amenyanyua miguu yake ya nyuma na kusema, "yaliyopita yeshapita." Na anapoinua miguu ya mbele husema hivi, "yajayo na yaje, ponda mali, furahia yote, haya ndiyo maisha."

Ndugu yangu, tulio wengi leo maisha yetu hayana tofauti na haya ya inzi. Hutaka kufanya yote na kujaribu yote katika maisha. Hakuna muda wa maandalizi wala tafakari kuhusu umilele wetu kama zawadi ya pekee tuliyopewa sisi wanadamu. Katika kweli hii Yesu anakuambia wewe na mimi kwamba, Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja,” Mt 24:44

Ona! tunavyoishi na jirani zetu! Unaweka wigo "fence" kiasi kwamba unamzuiya hata jirani yako kufungua mlango. Ona! tusivyo wajali wengine afya zao! Tunaelekeza maji taka kwenye makazi yao bila huruma. Eti kwa vile unapesa, na unajulikana hadi usalama wa Taifa. Eti kwa vile wewe ni kiongozi wa ngazi za juu kwenye utawala dhalimu. Eti kwa vile wewe ni mfanya biashara maarufu nchini. Je, hili ndilo kusudio la Mungu kwa maisha yako hapa duniani? Yesu anatutaka kila mmoja wetu tutafakari swali hili; Ni nani basi yule mtumwa mwaminifu mwenye akili, ambaye bwana wake alimweka juu ya nyumba yake, awape watu chakula kwa wakati wake?” Mt 24:45. “Ambaye Bwana wake alimweka juu ya nyumba yake,” kwa maanisha utumiaji mzuri wa mali, karama na vipaji ulivyojaliwa na Mungu. Huku ni sawa na kuwa ‘mtumwa mwaminifu.’ Naye Yesu anasadifu utumwa huu na kusema, Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta akifanya hivyo,” Mt 24:46. Mwenye kuwekeza vizuri katika haya atawekwa juu kabisa machoni mwa Mungu. Amin, nawaambieni, atamweka juu ya vitu vyake vyote,” Mt 24:47 

Ndugu yangu, usisahau kuwa maisha ya hapa duniani ni sawa na kuwa ugenini. Haya si makazi yako ya kudumu, au hatma yako ya mwisho. Unapita tu! Unatembea tu duniani. Mfalme Daudi anatukumbusha, "Mimi ni mgeni katika nchi, usinifiche maagizo yako," Zab 119:19, na Mtume Petro anasema,  "na ikiwa mnamwita Baba, yeye ahukumuye kila mtu pasipo upendeleo, kwa kadiri ya kazi yake, enendeni kwa hofu katika wakati wenu wa kukaa hapa kama wageni." 1Pet 1:17. Waamini wa kweli wanafahamu wazi kwamba kuna mambo mengi ya maisha kuliko hii miaka michache tunayoishi hapa duniani.

Ndugu yangu, kitambulisho chako kiko katika umilele, na nchi yako ni mbinguni. Unapofahamu ukweli huu, utaacha kuwa na wasiwasi wa "kupata kila kitu" hapa duniani. Mungu yupo wazi kabisa kuhusu habari za kuishi kwa ajili ya "hapa" na "sasa" tu huku ukijifananisha na watu wa dunia hii katika kipaumbele na mtindo wa maisha.

Tunapochezacheza na majaribu ya dunia hii, Mungu anaita hali hiyo uzinzi wa kiroho.  "Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki ya dunia ni kuwa adui wa Mungu?" Yak 4:4. Karipio hili kwa maana nyingine la tuambia kwamba 'twajidanganya mbele za Mungu iwapo tunachotaka ni mambo yetu, kuchezacheza na ulimwengu kwa kila nafasi tunayopata mwisho wetu ni kuwa maadui wa Mungu na njia yake.' Rejea mfano wa inzi hapo juu. Tukichukua mfano wa mtumwa wa Injili ya leo, Yesu anamfananisha na Mtumwa mbaya, yaani asiye tumia vyema mali, karama na vitaji vyake. Ni mtumwa yule asemaye moyoni mwake ‘kula maisha kifa chaja.’ Ni mtumwa yule mbaya akisema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia; akaanza kuwapiga wajoli wake, na kula na kunywa pamoja na walevi; bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyodhani, na saa asiyojua, atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wanafiki; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno,” Mt 24:48-51

Mimi na wewe "tu wajumbe kwa ajili ya Kristo..." 2Kor 5:20. Cha kusikitisha, wakristo wengi tumemsaliti mfalme wetu na ufalme wake. Katika hali ya upumbavu tumeamua kwamba kwa sababu tunaisha hapa duniani, basi hapa ndiko nyumbani kwetu. "Wapenzi, nawasihi kama wapitaji na wasafiri, ziepukeni tamaa za mwili zipinganazo na roho." 1Pet 2:11. Tunasahau ukweli huu kwamba, hata tukiwa katika kila jambo tulitajirika katika Yeye Yesu Kristo, 1Kor 1:5. Kristo ndiye anayethibitika kwetu tunapomwamini, 1Kor 1:6. Na katika Kristo Yesu hatupungukiwi kitu na hatutapungukiwa kitu,1Kor 1:7. Mungu hubaki kuwa mwaminifu ambaye tumeitwa na Yeye tuingie katika ushirika na Mwanaye, Yesu Kristo Bwana wetu na Mwokozi wetu, 1Kor 1:9.

Mungu pia anatuonya tusijishikamanishe sana na vitu vinavyotuzunguka kwa kuwa si vya kudumu. "Na wale wautumiao ulimwengu huu, kama hawautumii sana; kwa maana mambo ya ulimwengu huu yanapita." 1Kor 7:31. Ni wazi yatupasa kufanya kazi na kujipatia mahitaji yetu ya kila siku. Ila yote hayo tuyapatayo hatupaswa hata mara moja kujilinganisha nayo. Utu wetu na watu wengine ni zaidi ya mali hizo. Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo,” 1Pet 1:18-19. Ndugu yangu, ni ukweli usiotia shaka kwamba kwa mivuto ya hali ya juu, na vyombo vya mawasiliano vyenye kutia upofu, na mambo mengi ya anasa yaliyopo siku hizi, ni rahisi kusahau kwamba maisha si kufanya raha tu. Ndugu sikuonei gere bali nakukumbusha tu!

Ni pale tu tunapokumbuka kuwa maisha ni jukumu la muda mfupi ndipo mvuto wa mambo ya anasa utakapokosa nguvu maishani mwetu. Hili likifikiwa twaweza kujiandaa kwa jambo jingine ambalo ni bora zaidi. "Kwa maana vinavyoonekana ni vya muda tu; bali visivyoonekana ni vya milele. "2Kor 4:18b. Ukweli kwamba dunia si makazi yetu ya kudumu huelezea kwa nini, kama wafuasi wa Kristo, tunapatwa na magumu, huzuni, na kukataliwa (Yoh 15: 18-19; 16:20; 16:33). Ukweli huu pia hueleza kwa nini baadhi ya ahadi za Mungu huonekana kutotimizwa, baadhi ya sala hazijajibiwa, na baadhi ya mazingira kuonekana kutokuwa na haki. Huu si mwisho wa mambo.

Ili kutufanya tusijifungamanishe na ulimwengu sana, Mungu huruhusu tusikie hali fulani ya kutokuridhisha na kutosheka katika maisha-hitaji ambalo "haliwezi" kutoshelezwa kamwe hapa duniani. Hatuna furaha kabisa hapa kwa sababu hatutakiwi! Dunia si makazi yetu ya milele, tumeumbwa kwa ajili ya kitu bora zaidi. Ndugu yangu, samaki hawezi kuwa na furaha kuishi nchi kavu, kwa sababu ameumbwa kwa ajili ya kuishi majini. Tai kadhalika asingefurahi kama asingeruhusiwa kupaa angani. Hatuwezi kamwe kujisikia kutosheka kabisa hapa duniani, kwa sababu tumeumbwa kwa mambo mengine zaidi. Utakuwa na vipindi vya furaha hapa, lakini hakuna cha kufanana na kile Mungu amepanga kwa ajili yako.

Kwa kutambua kwamba maisha ni jukumu la muda mfupi tu ni lazima kubadili kabisa mambo unayoyaona ya muhimu maishani mwako. Mambo ya milele, yasiyo ya muda mfupi, yapasa yawe vigezo vya maamuzi yako. Kama C. S. Lewis anavyosema, "Kila kisicho cha milele hakifai milele."Tusiviangalie vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Kwa maana vinavyoonekana ni vya muda tu; bali visivyoonekana ni vya milele," 2Kor 4:18.

Ndugu, ni kosa kubwa kudhani kuwa mpango wa Mungu kwa ajili ya maisha yako ni mafanikio ya mali au mafanikio ya siku hizi, katika ulimwengu unavyoyaona. Maisha tele hayana uhusiano na mali tele, na uaminifu kwa Mungu hautuhakikishii kuwa na mafanikio ya kazi au huduma, usitazamie taji zisizodumu (1Pet 2:11). Pia, "usiogope mtu atakapopata utajiri, na fahari ya nyumba yake itakapozidi. Maana atakapokufa hatachukua chochote; utukufu wake hautashuka ukimfuata," Zab 49:16-17.

Paulo aliyeitwa kuwa mtume wa Yesu Kristo kwa mapenzi ya Mungu,” 1Kor 1:1, baada ya kuongoka kwake alikuwa mwaminifu lakini alijikuta gerezani. Yohane Mbatizaji alikuwa mwaminifu lakini alikatwa kichwa. Mamilioni ya watu waaminifu wameuawa, wamepoteza kila walichokuwa nacho, au maisha yao yamekoma wakiwa hawana kitu. Lakini mwisho wa maisha haya si mwisho, bali mwanzo wa maisha mapya ya umilele.

Ndugu niliyesafiri nawe katika tafakari hii, naomba nisikuchoshe.  Katika macho ya Mungu, mashujaa wa imani sio wale waliopata mali, wenye mafanikio na nguvu katika maisha haya, bali ni wale wanaoyaona maisha kama jukumu la muda mfupi na kutumia uaminifu, wakitumaini kupokea thawabu yao katika umilele. "Hawa wote wakafa katika imani, wasijazipokea zile ahadi, bali wakaziona tokea mbali na kuzishangilia, na kukiri kwamba walikuwa wageni, na wasafiri juu ya nchi. Lakini sasa waitamani nchi iliyo bora, yaani, ya mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni haya kuitwa Mungu wao, maana amewatengenezea mji," Ebr 11:13, 16. Asante kwa kusafiri nami. Tafakari na chukua hatua. Na mara zote tujitazamapo katika hali zote kama yalivyo majira ya mwaka na tusema kama Mtume Paulo, Namshukuru Mungu sikuzote kwa ajili yenu, kwa sababu ya neema ya Mungu mliyopewa katika Kristo Yesu,” 1Kor 1:4.

Tumsifu Yesu Kristo!

Mungu ni mwaminifu ambaye mliitwa na yeye mwingie katika ushirika wa Mwanawe, Yesu Kristo Bwana wetu,” 1Kor 1:9


Tusali: Neema na iwe kwetu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario