viernes, 5 de agosto de 2016

TAFAKARI: JUMAPILI YA 19 YA MWAKA-C

JUMAPILI YA 19 YA MWAKA-C
Somo I: Hek 18:6-9
Zab: 33:1, 12, 18-19, 20-22 (K) 12
Somo II: Ebr 11:1-2, 8-19
Injili: Lk 12:32-48
Nukuu:
“kwa hiyo watu wako waliutazamia wokovu wa wenye haki na uharibifu wa adui. Madhali uliwalipia kisasi watesi wale, na kwa njia ileile ulitutukuza ukituita ili tukujie,” Hek 18:7-8

“watoto watakatifu wa watu wema walitoa dhabihu kwa siri, na kwa moyo mmoja walijitwalia agano la torati ya dini, ya kwamba watashirikiana katika mambo mema na vilevile katika hatari,” Hek 18:9abc

"Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana,” Ebr 11:1

 “Hawa wote wakafa katika imani, wasijazipokea zile ahadi, bali wakaziona tokea mbali na kuzishangilia, na kukiri kwamba walikuwa wageni, na wasafiri juu ya nchi,” Ebr 11:13

 “Msiogope, enyi kundi dogo; kwa kuwa Baba yenu ameona vema kuwapa ule ufalme,” Lk 12:32
 “Lakini fahamuni neno hili, Kwamba mwenye nyumba angalijua saa atakayokuja mwivi, angalikesha, wala asingaliacha nyumba yake kuvunjwa,” Lk 12:39 

TAFAKARI: “Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana. Na kwa njia ileile ulitutukuza ukituita ili tukujie. Hivyo, viuno vyenu na viwe vimefungwa, na taa zenu ziwe zinawaka.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya 19 ya mwaka “C,” wa Kanisa. Leo Mama Kanisa kwa njia ya pekee anatualika kutafakari mambo makuu matatu; kwanza, ‘imani katika maisha na sintofahamu zake tukilenga lile tumaini la kweli, yaani, uwepo wa Mungu.’ Jambo la pili, ‘upi mwelekeo sahihi wa kukua katika imani kulielekea lile tumaina la kweli.’ Na tatu, ‘ni mastahili yapi yatuwezeshayo kudumu katika imani ya kweli tukilielekea tumaini lile la kweli, yaani,  maisha baada ya kifo-maisha ya umilele.’ Haya mawazo makuu matatu ambayo ndiyo kiini na mapaswa yetu kama Wakristo na wafuasi wa Kristo, ndiyo yaliyobeba masomo yetu ya leo tuliyokwisha yasikia.

Wazo kuu la kwanza, yaani, ‘imani katika maisha na sintofahamu zake tukilenga lile tumaini la kweli, yaani, uwepo wa Mungu, tunalipata kutoka somo letu la pili la leo, yaani, waraka ule kwa Waebrania kama tulivyosikia. Maisha kama zawadi ya Mungu kwetu na mali yake, yana changamoto zake. Maisha ni changamoto kwa sababu yanatuwajibisha kuishi kadiri ya kile tulichoitiwa na ndani ya hicho kitu, yaani, wito huo, ndipo penya ule utakatifu ambalo ndilo tumaini lako mara baada ya maisha ya hapa duniani. Maisha ni changamoto katika maana ya kwamba, tupo hapa duniani kwa muda mfupi tu. Hivyo, maisha yamaanisha ‘kuzaliwa, kustawi, na mwisho wa siku kunyauka.’

Hivyo kama nataka kulifikia tumaini lile, yaani, uzima wa milele, yanipasa kuishi kadiri ya mapenzi ya Mungu, na wakati huo huo kujiandaa vyema kwa sababu siijui siku wala saa ya kutwaliwa kwangu katika ulimwengu huu. Na Yesu katika hili anasema, Lakini fahamuni neno hili, Kwamba mwenye nyumba angalijua saa atakayokuja mwivi, angalikesha, wala asingaliacha nyumba yake kuvunjwa,” Lk 12:39. Kumbe huu ndio wito wa kuishi kadiri ya mapenzi ya Mungu, na ndiyo maana halisi ya kukesha. Kukesha tu haitoshi kama sintojiandaa vyema kwa sababu siri ile ya siku ya mwisho imefichwa kwangu. Hivyo Yesu anasema,  Nanyi jiwekeni tayari, kwa kuwa saa msiyodhani ndipo ajapo Mwana wa Adamu,” Lk 12:40 

Hata hivyo kuzikabili sintofahamu za maisha kadiri ya wito wangu, na wakati huo huo kukabiliana nazo, yanipasa kuwa na uelewa sahihi wa imani ya kweli. Somo hili la pili la tuelezea "imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana,” Ebr 11:1. Kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo ni ‘kutokuwa na shaka yoyote ilhali ukiwa umeyakabidhi yote mikono mwa Mungu katika maana ya ufahamu wa kweli wa kile ukiaminicho, na wakati huo huo umaana wake (rationality and significativity).’ Imani tu bila kubeba ufahamu wake na umaana wake ni kishawishi kikubwa cha kuanguka kwenye ujinga na upumbavu. Ni kwa mantiki hii ‘imani siyo ushuhuda tu uliobebwa katika miujiza na alama nyingine kama hizo.’ Imani ni zaidi ya hayo licha kwamba kama yapo katika kweli uimarisha imani changa. Imani ni zaidi ya ishara tuzionazo kwa sababu, Imani “ni bayana ya mambo yasiyoonekana,” Ebr 11:1b.

Maisha huwa na maana kwa kila changamoto tunayokutana nayo kwa sababu maisha hayo yamepewa maana kwa imani ile ya kweli ibebayo maisha yako kama nilivyokwisha sema kuhusu imani. Muono huu wa imani ndiyo utupao tumaini hata pale tunapozungukwa na changamoto katika maisha na sintofahamu zake. Ni ndani ya maisha haya yenye maana Kwa imani Ibrahimu alipoitwa aliitika, atoke aende mahali pale atakapopapata kuwa urithi; akatoka asijue aendako,” Ebr 11:8. Ibrahimu hakushikamana na mali na mazingira yake aliyoyazoea kwa sababu aliona maisha mengine kwa imani na tumaini la kweli hata kama hayakuwa yamefunuliwa wazi kwake kwa wakati ule. Ni mara ngapi kwa kukosa maana ya maisha na imani ya kweli twafa kwa shinikizo la damu tunapoamuriwa kuhama vituo vyetu vya kazi tulivyovizoea? Ibrahimu ni tofauti kabisa kwa sababu, Kwa imani alikaa ugenini katika ile nchi ya ahadi, kama katika nchi isiyo yake, akikaa katika hema pamoja na Isaka na Yakobo, warithi pamoja naye wa ahadi ile ile,” Ebr 11:9. Kumbe kitu cha maana katika maisha yetu si pale tulipo, bali maisha ya pale tulipo. Mtu wa kuyaboresha yawe mazuri zaidi na sehemu nzuri zaidi ya kuishi ni wewe mwenyewe kwa sababu hu kiumbe shirikishwa cha Mungu katika uumbaji wa pili. Maisha yasiyo na maana hata kama utakuwa huru, ni sawa na kuishi gereza lisilokuwa na kikomo.

Ni katika ufahamu huu na umaana wake katika maisha yabebwayo na imani ya kweli na tumaini la kweli, Sara mwenyewe alipokea uwezo wa kuwa na mimba; alipokuwa amepita wakati wake; kwa kuwa alimhesabu yeye aliyeahidi kuwa mwaminifu,” Ebr 11:11. Tukumbuke kuwa Sara alibeba mimba akiwa na umri wa miaka 90, na Ibrahimu akiwa na miaka 100, Mwa 17:17, kitu ambacho kwa hali ya kawaida ni vigumu kutokea, ila kwa Mungu vyote vyawezekana tunapojisalimisha kwake. Hata pale Mungu alipoyafanya yale yasiyowezekana, yaani, kuipatia familia hii mtoto-Isaka, Ibrahimu hakukosa utii mbele ya Mungu kwa sababu imani yake ilimfanya ayaweke matumaini yake yote kwa Mungu. Hivyo, Kwa imani Ibrahimu alipojaribiwa, akamtoa Isaka awe dhabihu; na yeye aliyezipokea hizo ahadi alikuwa akimtoa mwanawe, mzaliwa pekee,” Ebr 11:17. Kwa uhakika Ibrahimu anatambua kwamba,  “Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, Dunia na wote wakaao ndani yake,” Zab 24:1. Ibrahimu hapati maana ya maisha yake kwa utajiri aliokuwa nao, bali tumaini lile alilokuwa nalo kwa Mungu mwenye milki zote na kila kitu kwake. 

Kujisalimisha kwa Mungu katika ufahamu na umaana wake ndiyo maisha yenyewe kuelekea lile tumaini la kweli, yaani, maisha ya umilele. Ni katika kujisalimisha huku na katika maana hiyo, Hawa wote (Ibrahimu na Sara) wakafa katika imani, wasijazipokea zile ahadi, bali wakaziona tokea mbali na kuzishangilia, na kukiri kwamba walikuwa wageni, na wasafiri juu ya nchi,” Ebr 11:13. Ndugu yangu, “Mungu ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya; ndiye aliyeifanya imara; hakuiumba ukiwa, aliiumba ili ikaliwe na watu,” Isa 45:18, na mwisho wa siku wale wote walio yasalimisha maisha yao kwake pasipo shaka, kwa ufahamu na umaana wake, waitamani nchi iliyo bora, yaani, ya mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni haya kuitwa Mungu wao; maana amewatengenezea mji,” Ebr 11:16. Ugoto wa maisha yetu hapa duniani ni mwanzo wa maisha ya milele mbinguni kwa sababu tumeumbwa ili tuishi milele.

Wapendwa wana wa Mungu, wazo kuu la pili, yaani, ‘upi mwelekeo sahihi wa kukua katika imani kulielekea lile tumaina la kweli.’ Ndugu yangu, mwelekeo sahihi katika maisha ya kiroho ni kuitafuta sura ya Mungu. Kama uhai unaye Mungu, ni wazi Mungu ndiye sababu ya kila kitu katika maisha yetu. Huyu ndiye yatupasa kumtafuta kila siku ya maisha yetu kwa sababu anajua jana yetu, leo yetu, na kesho yetu. “kwa hiyo watu wako waliutazamia wokovu wa wenye haki na uharibifu wa adui. Madhali uliwalipia kisasi watesi wale, na kwa njia ileile ulitutukuza ukituita ili tukujie,” Hek 18:7-8. Ndugu yangu hakuna maana yoyote ya kufahamu haya ya leo na kesho bila ya kufahamu yule ayaratibishaye hayo ya leo na kesho. Huyu ndiye Mungu, Mtakatifu, na mwenye Utakatifu na katika yeye sote tu watoto watakatifu kwa mastahili yake na siyo yetu. Na ndani na katika Yeye ndiye mwenye kustahili yote yatuhusuyo leo na kesho tusiyoijua. Na ndivyo ilivyo kwamba, “watoto watakatifu wa watu wema walitoa dhabihu kwa siri, na kwa moyo mmoja walijitwalia agano la torati ya dini, ya kwamba watashirikiana katika mambo mema na vilevile katika hatari,” Hek 18:9abc. Mungu aliye alfa na omega, ndiye sababu ya kila kitu katika maisha yetu.

Wapendwa wana wa Mungu, jambo la tatu leo katika tafakari yetu ni juu ya ‘ni mastahili yapi yatuwezeshayo kudumu katika imani ya kweli tukilielekea tumaini lile la kweli, yaani, maisha baada ya kifo-maisha ya umilele.’ Stahili la jambo lolote lile huakisi uhasili wa kitu hicho. Ni swala la vitendo zaidi kuliko nadharia. Na moja ya kuwa huru ili kutumika vizuri kadiri ya matakwa ya Mungu ni kuipokea kweli hii kwamba, Viuzeni mlivyo navyo, mtoe sadaka. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, akiba isiyopungua katika mbingu, mahali pasipokaribia mwivi, wala nondo haharibu,” Lk 12:33. Sababu na maana ya maisha yetu haipo kwa yale tuyamilikiyo, bali katika tumaini la kweli la kile tukitegemeacho kwa sababu yapo maisha baada ya haya. Angalizo ni hili; Kwa kuwa hazina yenu ilipo, ndipo itakapokuwapo na mioyo yenu,” Lk 12:34. Je, furaha yangu ipo katika utajiri nilio nao wa leo na kesho, au kwa tumaini lile la milele?

Ni vyema wewe na mimi kuelewa vyema chanzo cha uhai wetu. Kumbe ni jambo la busara kabla ya yote kujua uwezo wako binafsi dhidi ya vita vile uvipiganavyo, na kusimama kwa yale yote yakutiayo nguvu. Ni katika kweli na mazingira haya Yesu anakwambia wewe na mimi leo kwamba, Viuno vyenu na viwe vimefungwa, na taa zenu ziwe zinawaka,” Lk 12:35. Ufahamu wa kitu ujengwa katika kujua asili ya kile kitu utakacho kukijua. Hivyo viuno vyetu vyapaswa kuwa vimefungwa kwa maanisha kutumia vyema milango yetu ya ufahamu, yaani, kusikia, kunusa, kuonja, kugusa, na kuona. ‘Na taa yetu iwe inawaka,’ kwa maanisha uhai wa dhamira ile iliyoko ndani yako yenye kuona kweli kama ilivyo na sivyo kama ulivyo. Ni katika mantika hiyo twaweza kuelewa maana ya maneno haya, kwamba, nanyi iweni kama watu wanaomngojea bwana wao, atakaporudi kutoka arusini, ili atakapokuja na kubisha, wamfungulie mara,” Lk 12:36. Bila dhamiri hii njema ndani yangu, hakuna sababu ya kukesha kwa kile nisichokijua. Hapa ndipo penye ile heri ya mtumwa na kwenye uhai wa dhamiri hii ndani yake. Hakika, Heri watumwa wale, ambao bwana wao ajapo atawakuta wanakesha. Amin, nawaambieni, atajifunga na kuwakaribisha chakulani, atakuja na kuwahudumia,” Lk 12:37. Kuna maana kubwa kukesha kwa kile ujuacho na chenye kubeba maana ya maisha yako.

Bila dhamiri hai na njema ni vigumu kuijua siri ya Mungu ndani ya maisha yako na moyo wako. Na kukesha hakuna maana yoyote bila kujua sababu ya kufanya hivyo na maana yake hasa tukilitazama tumaini lile, yaani, uzima ule wa milele. Kuififisha dhamiri hii, na hasa kwa dhambi ni kuua uzima ndani yako. Lakini fahamuni neno hili, Kwamba mwenye nyumba angalijua saa atakayokuja mwivi, angalikesha, wala asingaliacha nyumba yake kuvunjwa,” Lk 12:39. Usalama wako na wangu wa kuishi katika kweli hii na sintofahamu hii katika maisha ni kuwa tayari kwa kila kitu katika maana ya kuishi mapenzi ya Mungu. Nanyi jiwekeni tayari, kwa kuwa saa msiyodhani ndipo ajapo Mwana wa Adamu,” Lk 12:40. Ni katika kuwa tayari kwa kweli hii, Yesu anatuhoji na kututaka kufikiri zaidi ya yale tuyaonayo kwa macho yetu, kwamba,  Ni nani, basi, aliye wakili mwaminifu, mwenye busara, ambaye bwana wake atamweka juu ya utumishi wake wote, awape watu posho kwa wakati wake?” Lk 12:42. Kuwa wakili wa kitu chochote kile, na ili kukabiliana na changamoto zake lazima kuwa na ufahamu wa kile ulicho kama wakili.

Hata hivyo Yesu anatupa angalizo, hasa pale tunapochukulia mambo kutokana na mazoea. Naye anasema,  Lakini, mtumwa yule akisema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia kuja, akaanza kuwapiga wajoli wake, wanaume kwa wanawake, akila na kunywa na kulewa; bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyodhani na saa asiyojua, atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wasioamini,” Lk 12:45-46. Hapa ndipo pale penye kulia na kusaga meno, na kama hauna meno, ndugu yangu hakika jiandae kusaga fizi. Usicheke! Kuna kulia na kusaga meno kwa sababu Mungu aliye kweli, haki, huruma, msamaha, na upendo, siye Mungu mwenye kuificha kweli yake, na hasa pale tunapokuwa tayari kujifunua kwake. Ni kwa mantiki hiyo kwamba,  Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake, atapigwa sana,” Lk 12:47. Hiki ni kipigo cha kujichagulia kwa sababu kwa hiari yako hukupenda kuenenda njia ile ya haki na kweli. Kinyume chake ni kwamba, yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi,” Lk 12:48. Ndugu yangu, uwapo mwaminifu kwa yale ya kawaida na madogo madogo, ni mizania hiyo hiyo itakayo kusogeza kwa yale makubwa na wakati mwingine hubaki kama fumbo katika maisha yako. Mungu asemapo “ndiyo,” hakuna mamlaka yoyote chini ya jua yenye uwezo wa kusema “hapana.”

Andrea cha Usiku, mkazi wa mwenda pole, na mtoa habari wa Tarafa ya Jumuikeni, alikuwa na ujumbe wa dharura katika kijiji cha Mwenge Mshindo. Hivyo ilimpasa kufikisha ujumbe huo jioni ile ingawa ilimlazimu kusafiri usiku ambao kwa mazingira yale haikuwa salama kutokana na mazingira hatarishi ya wanyama pori.

Andrea cha Usiku alianza safari ile kuelekea kijiji kile cha Mwenge Mshindo majira ya saa kumi na mbili ya jioni. Baada ya kusafiri kwa takribani masaa mawili, kwa mbali alisikia sauti ya Simba. Kadiri ya uzoefu, wataalamu wanasema unaposikia sauti ya simba kwa mbali ujue kwamba simba huyo yupo karibu, na kinyume chake ni kwamba simba huyo yupo mbali. Hivyo kwa ufahamu huu, Andrea cha usiku ilimpasa kutafuta mti mrefu wa karibu na ulio mwepesi kukwea ili kujiepusha na simba yule aliye kuwa karibu.

Baada ya kuukweya mti ule, alisikia mtikisiko wa nyasi, na mara simba yule aliyeonekana kushiba alijilaza chini ya mti ule. Hadi jua linachomoza kesho yake, simba yule hakuonekana kutoka chini ya mti ule, zaidi ya kupiga miayo na kutanua kucha zake kwa kujinyoosha na kuonyesha umahiri wake. Hapa ndipo Andrea alipoanza kusali na kuomba Mungu amwondoe simba yule mahali pale.

Ndani ya moyo wake aliisikia sauti ikisema, “achia tawi hilo uliloshika nawe utakuwa salama.” Baada ya sauti hii kujirudia zaidi ya mara tatu, Andrea alianza kupingana na sauti ile na kusema, “hivi wewe wanifanya mimi ni mjinga wa mchana kweupeee kukubali kujiachi na kutua kwenye meno haya ya simba huyu na kucha hizi na kuwa kifungua kinywa chake?” Na baada ya robo saa, alisikia tena sauti ile ndani ya moyo wake ikisema, “usalama wako upo pale tu utakapo jiachia.” Kwa vile hakuweza kulala usiku kucha kwa hofu ya simba yule, aliingiwa na usingizi wa hapa na pale. Hali hii ilimpelekea kushtuka shtuka. Na ndipo bila kujijua alijiachia na kutua tumboni mwa simba yule kwa ghafla!

Kwa hofu ile, simba alikurupuka na kukimbia alipokujua kusalimisha maisha yake, naye Andrea cha usiku alitimka vikwake bila tone la usingizi. Na hivi ndivyo ilivyokuwa salama na pona yake Andrea. Je, wamwamini Mungu?

Tumsifu Yesu Kristo!

Kwa kuwa hazina yenu ilipo, ndipo itakapokuwapo na mioyo yenu,” Lk 12:34

Tusali:-Ee Yesu, tujalie imani ya kweli. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario