IJUMAA WIKI YA 18 YA MWAKA-C
Somo:
Nah 1:15; 2:2; 3:1-3, 6-7
Zab/Kit: Kumb 32:35cd-36ab, 39abcd,
41
Injili:
Mt 16:24-28
Nukuu:
“Zishike
sikukuu zako, Ee Yuda, uziondoe nadhiri zako; kwa maana yule asiyefaa kitu
hatapita kati yako tena kamwe; amekwisha kukatiliwa mbali,” Nah 1:15
“Ole wake mji wa damu! Umejaa mambo ya uongo na unyang'anyi; mateka hayaondoki,” Nah
3:1
“Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mtu ye yote
akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate,” Mt 16:24
“Kwa
kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi
yake kwa ajili yangu, ataiona,” Mt 16:25
“Kwani
atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au
mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?” Mt 16:26
TAFAKARI:
“Salama yetu ipo katika unyofu wetu. Na mtu ye
yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate.”
Wapendwa wana wa Mungu,
penye utaratibu wowote ule ipo akili. Na kinyume chake ni kweli. Maisha adilifu
ni maisha yenye utaratibu na yenye kuona si leo na kesho tu, bali mbali zaidi,
kule tukutamanipo ingawa hatupajui sawa sawa. Na maisha adilifu huongozwa na
dhamiri unyofu. Na hizi ndizo nadhiri Mungu anazo wakumbusha wana wa Israeli.
Na sasa “zishike sikukuu zako, Ee Yuda, uziondoe
nadhiri zako; kwa maana yule asiyefaa kitu hatapita kati yako tena kamwe;
amekwisha kukatiliwa mbali,” Nah 1:15. Maisha bila utaratibu hupoteza lengo
lake, na mwisho wa siku dhana ya kuwajibika upotea. Huu ukiwa ndiyo mfumo wa
maisha, fahari ya maisha hupotea pia. Kuona fahari ya maisha ni kuishi kwa
utaratibu na unyofu. “Kwa maana Bwana
anairudisha fahari ya Yakobo, kama fahari ya Israeli; maana watekao nyara
wamewateka, na kuyaharibu matawi ya mizabibu yao,” Nah 2:2. Utulivu wa maisha
utegemea sana kweli na haki katika jamii husika.
Kweli
na haki inapokosekana au kutolewa kwa ubaguzi, jamii husika kamwe haiwezi
kubaki salama. Na hili ndilo onyo la Mungu kwetu: “Ole
wake mji wa damu! Umejaa mambo ya uongo na unyang'anyi; mateka hayaondoki,” Nah
3:1. Katika hali na mazingira haya, mateso na shida za watu huwa kilio kisicho
koma. Manung’uniko na vitendo vya ukiukwaji wa haki za kibinadamu huonekana
kuwa jambo la kawaida. Na hii ndiyo hali, kwamba, “Kelele
za mjeledi, kelele za magurudumu yafanyayo kishindo; na farasi wenye
kupara-para, na magari ya vita yenye kuruka-ruka; mpanda farasi akipanda, na upanga
ukimeta-meta, na mkuki ukimemetuka; na wingi wa waliouawa, na chungu kubwa ya
mizoga; mizoga haina mwisho; wanajikwaa juu ya mizoga yao,” Nah 3:2-3. Je, hili
ndilo lengo la maisha?
Katika
mazingira hayo Mungu anasema, “Nami
nitatupa uchafu uchukizao juu yako, kukufanya uwe mchafu, nami nitakufanya kuwa
kitu cha kutazamwa kwa dharau,” Nah 3:6. Je, Mungu atakapotuchoka tutakimbilia
wapi? Kwa nini unapenda kuwa sababu ya mateso kwa wengine? Kwa nini hutaki
kukaa kwenye kiti, na badala yake wapenda kukaa vichwani mwa watu kwa mabaya
tu? Kama haya yalitoke Ninawi itashindikanaje kutokea kwetu leo? “Hata
itakuwa, wote wakutazamao watakukimbia, wakisema, Ninawi umeharibika; ni nani
atakayeuhurumia? Nikutafutie wapi wafariji?” Nah 3:7. Haya ni masikitiko
makubwa sana kwa Mungu muumba wetu. Kupoteza dira ya maisha na malengo yake ni
hasara kubwa sana kwa maendeleo ya mwili na roho.
Katika
agano jipya la Mungu na watu wake, chini ya mwanaye mpenzi Yesu Kristo, ili
kuurithi uzima huu wa milele, kila mmoja wetu yampasa kuishi njia hii ya uzima
wa kweli kama Mwanaye Yesu Kristo anavyotuwasa katika injili ya leo: “Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe,
ajitwike msalaba wake, anifuate,” Mt 16:24. Tunamfuata Yesu kwa sababu ‘Yeye
ndiye njia, kweli na uzima,’ Yoh 14:6. Katika ufuasi wetu kwa Kristo, haya
mambo matatu ni muhumu sana: KUJIKANA NAFSI, KUJITWIKA MSALABA, NA KUMFUATA
YESU. Kujikana nafsi ni tendo la kujisalimisha na kuwa tayari kufanya kadiri ya
mapenzi yake Mungu, na siyo tutakavyo sisi au tuonavyo. Ni tendo la kusalimisha
utashi wako kwa Mungu, na kuwa tayari kutumika kadiri ya mpango wa Mungu.
Unafanya tendo hili na kuwa sehemu ya maisha yako kwa kuyachuchumilia yale ya
umilele ukilinganisha na haya ya leo na sasa tu. Ni kuishi ulimwenguni pasipo
kubebwa na malimwengu. Ni kuishi maisha yanayoongozwa na malengo.
Kujitwika msalaba ni kukubali kuwa hapana utukufu pasipo
msalaba. Maisha tunayoyaishi kila mmoja kadiri ya wito wake, si maisha rahisi.
Kuna wakati katika maisha hayo itakupasa kutoa sadaka kubwa ili kuufia umilele
ule aliotuandalia Mungu. Hivyo kujitwika msalaba ni kupokea mateso pasipo shaka
yoyote na bila manung’uniko. Mambo hayo yanaweza kuwa magonjwa, ulemavu,
mahangaiko katika maagano yetu, mfano: ndoa, maisha ya wakfu, aka. Ni kuona
utukufu wa Mungu katika mateso na mahangaiko yetu ya kila siku tunapokabiliana
nayo. Msalaba huo katika maisha utusukume kuubeba kila siku na kusafiri nao
hadi golgota alipowambwa Bwana wetu Yesu Kristo. Ni kuyapokea mateso yote na
kuyabeba mpaka mwisho bila kumwasi Mungu na mwanaye Yesu Kristo. Tukifanya hivi
pasipo shaka yoyote ndipo tutakapo hesabiwa haki na kuushinda mateso hayo.
Mateso hubadilika kuwa ushindi, na msalaba huwa kielelezo cha ushindi huo. Hapa
ndipo tunapoweza kuiokoa nafsi yetu katika majaribu. “Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu
atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona,” Mt 16:25. Je, upo tayari
kuipoteza nafsi yako katika umilele wote?
Kumfuata Yesu ni mwito na matokeo ya kujikana nafsi, na
kujitwika msalaba pasipo shaka. Kumfuata Yesu ni kusafiri naye pasipo shaka
tukijua na kuamini kabisa kuwa ni yeye tu njia ya umilele, ukweli wa umilele,
na uzima wa umilele. Ni kufahamu pasipo shaka na kuamini maneno haya aliyosema
Yesu: “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye
kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni
nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo;
nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa
maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi,” Mt 11:28-30. Hivyo
kitulizo cha mahangaiko na mateso yetu ni YESU TU. Tunapojikana nafsi na
kujitwika msalaba wetu bila kufuatana na Yesu alioshinda mateso na maumivu ya
msalaba ni bure na kupoteza muda. Katika mahangaiko yote tuyapitiayo kamwe
tusimwache Yesu.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Kwa
sababu Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika
zake; ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake,” Mt 16:27
Tusali:-Ee Yesu na
Mkombozi wetu, tuongoze katika kweli yako ili tuweze kuibeba misalaba yetu kila
siku bila manung’uniko. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario