JUMATATU
WIKI YA 22 YA MWAKA-C
Somo: 1Kor 2:1-5
Zab/Kit: 119:97, 98, 99, 101, 102
Injili: Lk 4:16-30
Nukuu
“Basi,
ndugu zangu, mimi nilipokuja kwenu, sikuja niwahubiri siri ya Mungu kwa ufasaha
wa maneno, wala kwa hekima,” 1Kor 2:1
“Na
neno langu na kuhubiri kwangu hakukuwa kwa maneno ya hekima yenye kushawishi
akili za watu, bali kwa dalili za Roho na za nguvu, ili imani yenu isiwe katika hekima ya
wanadamu, bali katika nguvu za Mungu,” 1Kor 2:4-5
“Roho
wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari
njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona
tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na
kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa,” Lk 4:18-19
“Akaanza
kuwaambia, Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu,” Lk 4:21
TAFAKARI: “Lakini yeye alipita katikati yao, akaenda zake.”
Wapendwa wana wa Mungu, Yesu
Kristo ndiye mfano hai na halisi kwetu wa kuiga na kufuata hata kama kwa hali
yetu na ubinadamu wetu si rahisi. Leo Yesu katika Sinagogi huko Nazareti,
wanapomjua vizuri anawaacha midomo wazi. Ni kweli walimfahamu Yesu katika maana
ya historia yake. Mara zote tunajisikia vizuri na nyumbani pale tunapofikiri
sawa, na kuwa na maisha yaliyowiyana. Kwa hali hii tunahitaji nguvu ya pekee
kuwa tofauti. Yesu anatufundisha kuwa tofauti na kutokufanya mambo kimazoea. Yesu
kama ilivyokuwa kawaida ya siku ya sabato, anaingia kwenye sinagogi na kulisoma
neno la Mungu, “Roho
wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari
njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona
tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na
kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa,” Lk 4:18-19. Hii ndiyo tofauti ya Yesu
na kauli mbiu yake. Hiki ndicho kinachomtofautisha Yesu na wengine ingawa neno
hili lilishasomwa na wengi waliomtangulia. Kwa kukazia Yesu anasema, “Leo
maandiko haya yametimia masikioni mwenu,” Lk 4:21. Maneno haya ndiyo msukumo wa
mabadiliko yote na mtazamo mpya juu ya Yesu.
Mwana sayansi Isaac
Newton wa Uingereza (1643-1727) alipolichukua jiwa na kulirusha juu na likarudi
ardhini na kugundua nadharia “theory” ya mvutano “gravitation,” hakuwa mwanadamu wa kwanza kurusha
jiwe juu na likarudi ardhini. Ila kwa kwenda zaidi ya mazoea ya urushwaji wa
jiwe na kurudi ardhini ndiko kunakomfanya leo tofauti na wengine
waliomtangulia. Yesu anatualika kutokuishi kwa mazoea, bali tuende zaidi ya
kile kilichozoeleka. Ukweli huu ni kwa hali zote za maisha na kwa namna ya
pekee mahusiano yetu na wenzetu ambayo msingi wake ni Upendo, Kweli na Haki.
Kwenda tofauti na yaliyozoeleka ni mshangao kwa wale wasiopenda kuwa tofauti
katika kile kilichojificha. Hivyo, “wakamshuhudia
(Yesu) wote, wakiyastaajabia maneno ya neema yaliyotoka kinywani mwake,
wakasema, Huyu siye mwana wa Yusufu?” Lk
4:22. Historia ya Mtu siyo kikwanzo cha yeye kuwa vizuri, mzuri, au kufanya
vizuri zaidi hata kama historia ya kule alikotoka kuonekana kuwa mbaya.
Kwa msisitizo Yesu anatutaka tuione
tofauti kati yake na wote waliomtangulia. Naye anasema, “Palikuwa na wajane
wengi katika nchi ya Israeli zamani za Eliya, wakati mbingu zilipofungwa miaka
mitatu na miezi sita, njaa kuu ikaingia nchi nzima; wala Eliya hakutumwa kwa mmojawapo,
ila kwa mjane mmoja wa Sarepta katika nchi ya Sidoni,” Lk 4:25-26. Leo pamoja
na sintofahamu kama hizi tunalo tumaini ndani na katika Kristo. Yesu hatuponji
tu majeraha yetu ya ndani na nje, bali hututakasa pia. Naye anasema, “Tena, palikuwa na wenye ukoma wengi katika
Israeli zamani za nabii Elisha, wala hapana aliyetakaswa ila Naamani, mtu wa
Shamu,” Lk 4:27. Kristo kwa sasa ndiye utakaso
wetu.
Kwa hali ya kawaida hasa kwa yale
tuyoyazoea kuishi na kuyasikia, ujumbe huu wa Yesu hukuwapendeza Mafarisayo na
waandishi walio kuwa vinara wa kudumisha desturi hizo.
“Wakajaa ghadhabu wote waliokuwa katika
sinagogi walipoyasikia hayo,” Lk 4:28. Kwa
vile saa yake ilikuwa bado kufika, ghadhabu ile haikumdhuru. Na mambo yalikuwa
hivi; “Wakaondoka wakamtoa nje ya
mji, wakampeleka mpaka ukingo wa kilima ambacho mji wao umejengwa juu yake,
wapate kumtupa chini; lakini yeye
alipita katikati yao, akaenda zake,” Lk 4:29-30. Chuki na hila za mwanadamu
haziwezi kufanikiwa palipo na mpango wa Mungu.
Unyenyekevu wa Yesu uliobeba
historia yake fupi hapa duniani unakuwa sababu ya hukumu yake. Mara nyingi
tunawahukumu watu ndivyo sivyo kutokana na kujua historia zao, maeneo ya
kijeografia walikotoka, historia za wazazi wao, mazingira ya makuzi yao,
marafiki walioishi nao, na hata mtazamo wao kimaisha. Hili ni kosa kubwa sana
kufanya. Hakuna aliyeko hapa duniani kwa bahati mbaya, au kuzaliwa kwa bahati
mbaya. Sisi tu malengo na makusudi ya Mungu. Mungu anampango na kila mmoja
wetu.
Baada ya Yesu kuwaambia
ukweli Waandishi na Mafarisayo kwa kutokuamini kwao, hawapokei ujumbe ule wa
ukweli na kubadilika, bali wanatafuta njia ya kumwangamiza. Katika hili Yesu
anatujaza ujari kwa kusema, “Hakuna nabii mwenye kukubaliwa katika nchi yake
mwenyewe,” Lk 4:24. Maana yake ni nini? Ukweli ni kwamba, tunaposimama katika
kweli, na kuishi kweli hiyo, twatangaza vita kwa wale wasioipenda kweli hiyo.
Kwa upande wa Imani ni vita, si tu ya nafsi, bali roho pia. Roho ambazo
hazimwelekei Muumba wake zitakuwa kinyume na yote tusemayo na kuyaishi. Kuishi
Ukristo na kumkiri Kristo leo ni vita kubwa ya kiroho. Tulizoea kusikia hadithi
za Mashahidi wa Imani karne na nyakati za nyuma, lakini leo ni nafasi na wakati
wetu kuwa mashahidi wa Kristo. Kuna kila dalili na sababu za kuutoa ushuhuda
huo.
Tunachopaswa kuishi si
maisha ya ushindani wa hoja katika majukwaa, bali zaidi ni kuishi na kutoa
ushuhuda wa ukimya wa maisha ya kweli ya Ukristo wetu. Jambo hili ni muhimu
sana, kwani katika utulivu Mungu yupo na kuonekana. “Na baada ya tetemeko la
nchi kukawa na moto; lakini Bwana hakuwamo katika moto ule; na baada ya moto
sauti ndogo, ya utulivu,” 1Fal 19:12. Huu ni wakati wa mitetemo ya Imani. Nasi
tusienende kadiri ya mitetemo hiyo. Tuitafsiri hiyo mitetemo nako tutakutana na
Mungu katika utulivu.
Ni
wazi katika kutenda lililo la Mungu, yaani lenye kuongozwa na upendo wa kweli,
tujiandae kupata upinzani. Yule mwovu shetani hafurahii yaliyo mazuri na mema
yenye kuufunua Utukufu wa Mungu. Yesu Kristo mwenyewe alipata upinzani nyumbani
mwake mwenyewe. Katika hili Yesu anasema, “Amin,
nawaambia ya kwamba, Hakuna nabii mwenye kukubaliwa katika nchi yake mwenyewe,”
Lk 4:24. Je, kama hatukubaliki nyumbani kwetu
na watu wanaotufahamu iwe sababu ya kutokutenda mema? Jibu ni HAPANA! Tuendelee
kutenda wema na upendo kwa wote, kwa sababu asili ya upendo ni Mungu, uwepo wa
upendo ni Mungu, na Upendo ni Mungu. Kuyaona haya ya Mungu ndani yetu kwahitaji
unyenyekevu na kuepuka kujiinua kusiko na sifa wala siha. Hali hiyo ndani yetu
itatuwezesha kusema toka moyoni maneno haya ya Mtume Paulo; “Basi, ndugu zangu, mimi nilipokuja kwenu, sikuja
niwahubiri siri ya Mungu kwa ufasaha wa maneno, wala kwa hekima,” 1Kor 2:1.
Mungu ndiye anaye wezesha yote ndani yetu. “Na neno langu na kuhubiri kwangu hakukuwa kwa
maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu, bali kwa dalili za Roho na za
nguvu, ili imani yenu isiwe
katika hekima ya wanadamu, bali katika nguvu za Mungu,” 1Kor 2:4-5. Sifa na Utukufu ni kwa Mungu wetu. Amina
Tumsifu Yesu Kristo
“Leo maandiko
haya yametimia masikioni mwenu,” Lk 4:21
Tusali:-Ee
Yesu tujalie ujasiri. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario