SIKUKUU YA KUNG’ARA KWA BWANA WETU
YESU KRISTO
6/8
Somo I: Dan 7:9-10,
13-14
Zab: 97:1-2, 5-6, 9
Somo II: 2Pet 1:16-19
Injili: Lk 9:28b-36
Nukuu:
“Naye
akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote,
na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita
kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa,” Dan 7:14
“Maana
alipata kwa Mungu Baba heshima na utukufu, hapo alipoletewa sauti iliyotoka
katika utukufu mkuu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye,”
2Pet 1:17
“Ikawa
katika kusali kwake sura ya uso wake ikageuka, mavazi yake yakawa meupe,
yakimeta-meta,” Lk 9:29
“Na
tazama, watu wawili walikuwa wakizungumza naye, nao ni Musa na
Eliya; walioonekana katika utukufu, wakanena habari za kufariki kwake
atakakotimiza Yerusalemu,” Lk 9:30-31
“Petro
na wale waliokuwa pamoja naye walikuwa wamelemewa na usingizi; lakini
walipokwisha amka waliuona utukufu wake, na wale wawili waliosimama pamoja
naye,” Lk 9:32
“Ikawa
hao walipokuwa wakijitenga naye, Petro alimwambia Yesu, Bwana mkubwa, ni vizuri
sisi kuwapo hapa; na tufanye vibanda vitatu; kimoja chako wewe, na kimoja cha
Musa, na kimoja cha Eliya; hali hajui asemalo,” Lk 9:33
“Sauti
ikatoka katika wingu, ikisema, Huyu ni Mwanangu, mteule wangu, msikieni yeye,”
Lk 9:35
TAFAKARI:
“Huyu ni Mwanangu, mteule wangu, msikieni yeye.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo Mama Kanisa anasheherekea Sikukuu ya kung’ara kwa Bwana wetu Yesu Kristo.
Tukio hili la kung’ara kwa Bwana wetu Yesu Kristo linafunua Utukufu na Umungu
ya Yesu kabla na baada ya mateso na kifo chake kama sadaka iliyo hai na yenye
kumpendeza Mungu. Huu ni mpango wa Mungu tangu zamani ili kumkomboa mwanadamu
kutoka utumwa wa dhambi. Nabii Danieli alifunuliwa siri hii katika ndoto, na
leo inatimia ndani na katika Kristo. “Naye
akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote,
na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita
kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa,” Dan 7:14. Tukio hili la
pekee la kung’ara kwa Bwana wetu Yesu Kristo linadhihirisha uwezo na mamlaka
aliyonayo.
Wapendwa
wana wa Mungu, kwa upendo usio na kipimo, wakati ulipotimia, (Ebr 1:1-2),
katika historia hii ya wokovu, Mungu mwenyewe amejimwilisha na kukaa nasi. “Naye
Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama
wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli,” Yoh 1:14. Hivyo
wapendwa katika Kristo, lnjili ya leo inauweka sawa ukweli huu kwa mambo makuu
matatu; Dira yetu ya kufuata kama Wakristo, Utumilifu wa nyakati, na Hatma yetu
iliyojengeka katika agano la umilele. Haya yote yanafanyika katika tukio hili
la kung’ara kwa Bwana wetu Yesu Kristo kadiri ya simulizi la Injili ya leo.
Kwanza, ni dira yetu ya
kufuata kama Wakristo. Heshima na cheo chako kama Mkristo ni utakatifu wako.
Hivyo maisha yetu kama Wakristo kuelekea umilele yatafikika na kuwezekana kama
ni tokeo la utakatifu wetu kwa kuyaona maisha kama ni jukumu la muda fupi hapa
duniani na kama pia sehemu pekee ya maandalizi. Udhihirisho wa utakatifu huu
kama dira yetu ya maisha ni tendo lile la kung’ara Kristo Yesu. “Ikawa
katika kusali kwake sura ya uso wake ikageuka, mavazi yake yakawa meupe,
yakimeta-meta,” Lk 9:29. Kristo anavikwa Utukufu wake ambao ataunyakua rasmi
mara baada ya mateso, kifo na ufufuko huko Yerusalemu. Hivyo Utukufu wa Kristo
hautenganishwi na msalaba/mateso. Kwa maana nyingine hakuna Utukufu pasipo
msalaba. Kama Kristo ndiye njia, kweli na uzima, Yoh 14:6, nasi wafuasi wake
itatupasa kupita njia hiyo ya msalaba, ukweli huu anaotufundisha, ili tuufikie
uzima ule, yaani maisha ya milele. Kristo ni masiha ya Msalaba, nasi twamfuata
Masiha wa Msalaba ili tuifikie taji ile ya Utukufu baada ya kuhesabiwa haki.
Pili, ni ukamilifu wa
nyakati. Katika tendo hili la kung’ara, tunaelezwa tokeo la watu wawili, yaani
Musa na Eliya katika mazungumzano na Yesu. “Na tazama, watu wawili
walikuwa wakizungumza naye, nao ni Musa na Eliya; walioonekana katika
utukufu, wakanena habari za kufariki kwake atakakotimiza Yerusalemu,” Lk
9:30-31. Katika tendo hili, Musa anawakilisha Torati, na Eliya Unabii. Hivyo
leo Yesu anaikamilisha Torati na Unabii. Naye Yesu anatuambia, “Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja
kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu
na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaoondoka, hata
yote yatimie,” Mt 5:17-18. Torati inatimilizwa kwa amri ya upendo kwa Mungu na
jirani. “Basi yo yote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni
vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo torati na manabii,” Mt 7:12. Ni ndani na katika
Kristo tu tunapata neema na kweli kwa mkono wake. “Kwa kuwa
torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu
Kristo,” Yoh 1:17. Na huku ndiko kutimilika kwa sheria na kutamalaki kwa
upendo, kweli, na neema.
Leo pia unabii wote
ulionenwa juu ya Kristo na historia nzima ya wokovu wetu unakamilika. Unabii
huu unafika ukomo wake kwa uwepo wa Kristo ambaye ni UPENDO WA MUNGU kwetu.
Mtume Paulo anasema, “Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali
ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa,
yatabatilika,” 1Kor 13:8. Huyu ndiye Kristo Yesu! Kung’ara kwake Bwana
wetu Yesu Kristo kulikoonyesha Ufukufu wake, kunaamsha furaha ya ndani ya Mtume
Petro na kuyasema ya moyoni mwake. “Petro alimwambia Yesu, Bwana
mkubwa, ni vizuri sisi kuwapo hapa; na tufanye vibanda vitatu; kimoja chako
wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya; hali hajui asemalo,” Lk 9:33.
Hata hivyo hilo halikuwa kusudi la Yesu kubaki mlimani pale. Yesu inabidi
ashuke na kuukumbatia Msalaba kama alama ya ushindi na hapo ndipo wokovu wako na wangu
ulipotundikwa. Hii ndiyo safari kuelekea kilele kile cha wokovu kama
Masiha wa Msalaba.
Tatu, ni hatma yetu
iliyojengeka katika agano la milele. Kristo ndiye kielelezo chetu na wokovu
wetu. Leo Mungu Baba anauweka ukweli huu hadharani na kusema, “Huyu ni
Mwanangu, mteule wangu, msikieni yeye,” Lk 9:35. Hili ndilo agano la milele
kati yetu na Mungu, na Kristo akiwa ndiye daraja na mlango halisi wa sisi
kupitia kwani ni kwake tu tutakuwa salama kama njia, ni kwa Kristo tu
tunalishwa kweli katika kweli, na Kristo tu ndiye uzima halisi. Hivyo hapana
tena ufunuo ulio wa wazi na kamili zaidi ya ufunuo huu wa Mungu kupitia mwanaye
Mpenzi. Tendo hili linathibitishwa na sauti ya Mungu mwenyewe kwa viumbe vyote,
Lk 9:35. Ndugu yangu, Je, unafuata sauti gani katika maisha yako? Sauti hii
kutoka mbinguni inampa Yesu Kristo Heshima, Mamlaka, na Utukufu. “Maana
alipata kwa Mungu Baba heshima na utukufu, hapo alipoletewa sauti iliyotoka
katika utukufu mkuu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye,”
2Pet 1:17. Nasi tunapoisikia sauti hiyo na kuishi kweli hiyo, twajazwa nguvu,
heshima na utukufu kwa kuishi ndani na katika Kristo.
Wapendwa wana wa Mungu, zipo sauti nyingi katika
maisha yetu. Je, sauti hizo zinatupeleka karibu na Kristo Yesu au
zinatutenganisha na ukweli wake? Kusikia sauti hii ni kuyafanya mapenzi yake.
Na kufanya mapenzi yake maana yake ni tuyafanye kila mmoja kadiri ya wito wake.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Ikawa
katika kusali kwake sura ya uso wake ikageuka, mavazi yake yakawa meupe,
yakimeta-meta,” Lk 9:29
Tusali:-Ee
Yesu, tujalie neema ya kuyafanya mapenzi yako. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario