miércoles, 31 de agosto de 2016

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 22 YA MWAKA-C

ALHAMISI WIKI YA 22 YA MWAKA-C
Somo: 1Kor 3:18-23
Zab/Kit: 24:1-2, 3-4ab, 5-6
Injili: Lk 5:1-11
Nukuu
Mtu asijidanganye mwenyewe; kama mtu akijiona kuwa mwenye hekima miongoni mwenu katika dunia hii, na awe mpumbavu, ili apate kuwa mwenye hekima,” 1Kor 3:18 

Maana hekima ya dunia hii ni upuzi mbele za Mungu. Kwa maana imeandikwa, Yeye ndiye awanasaye wenye hekima katika hila yao,” 1Kor 3:19 

 “Akaingia katika chombo kimoja, ndicho chake Simoni, akamtaka akipeleke mbali kidogo na pwani. Akaketi, akawafundisha makutano ali chomboni,” Lk 5:3 

Hata alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki,” Lk 5:4 

 “Simoni Petro alipoona hayo, alianguka magotini pa Yesu, akisema, Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi, Bwana,” Lk 5:8 

 “Yesu akamwambia Simoni, Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu,” Lk 5:10b

Hata walipokwisha kuviegesha pwani vyombo vyao, wakaacha vyote wakamfuata,” Lk 5:11 

TAFAKARI: Nanyi ni wa Kristo, na Kristo ni wa Mungu. Tweka mpaka kilindini.”

Wapendwa wana wa Mungu, kwa uzoefu aliokuwa nao Simoni kama mvuvi wa samaki, isingekuwa rahisi kuuchukua ushauri wa Yesu wa kurudi tena ndani ya maji na kuvua samaki. Elewa kwamba usiku kucha Simoni na wenzake walikesha wakivua bila kupata chochote. Usiku ndio muda muhafaka wa kuvua samaki. Leo kwa namna ya kushangaza Yesu anamwambia Simoni azitupe nyavu zake ndani ya maji mchana kweupe, na kwenda kinyume kabisa na utaratibu wa uvuvi. Hata alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki,” Lk 5:4. Simoni akitambua alichokifanya usiku kucha bila kupata chochote, akajibu akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu,” Lk 5:5. Maneno haya ya Simoni “lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu,” yanaonyesha kujisalimisha kwa Simoni pasipo shaka mbele ya Yesu. Ni kwa njia ya neno hili: Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika. Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu,” Yoh 1:3-4. Je, bado unamashaka na Neno wa Mungu, yaani Yesu Kristo?

Maneno hayo ya Simoni yenye kuonyesha kujisalimisha kwake, ndiyo roho na uzima. Katika hili Yesu anasema, Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima,” Yoh 6:63. Na neno lile Yesu alilomwambia Simoni “tweka mpaka kilindini,” ndiyo uzima na ponya yake Simoni. Ndugu yangu tunayesafiri sote katika tafakari hii, tuzame kidogo ndani na tuone maana halisi ya kujisalimisha kama siri na ufunguo wa mfanikio yote katika maisha yako.

Kujisalimisha ni neno lisilotumiwa sana, halipendwi kama vile neno kunyenyekea. Lina maana ya kupoteza, na hakuna mtu yeyote anapenda kupoteza. Kujisalimisha kunaonyesha picha isiyopendeza ya kukubalika kushindwa katika vita, kupoteza katika michezo, au kukubali kushindwa na mpinzani mwenye nguvu zaidi. Neno hili linatumiwa mara nyingi katika hali isiyokubalika. Wahalifu waliotekwa hujisalimisha kwa mamlaka.

Katika mila ya leo ya ushindani tunafundishwa kutokuacha au kutokukubali tu. Hivyo hatusikii sana kuhusu kujisalimisha. Kama kushinda ndiyo kila kitu, basi kujisalimisha hakupo. Labda tuongelee kushinda, kufanikiwa, kuzidi nguvu, na kushinda vita kuliko kujitoa, kunyenyekea, kutii, na kujisalimisha. Lakini kujisalimisha ni kiini cha kuabudu. Ni mwitikio wa asili wa huruma na upendo wa ajabu wa Mungu. Tunajitoa nafsi zetu kwake, si kwa hofu au kwa kuwa ni wajibu. Lakini kwa upendo, “kwa sababu alitupenda kwanza.” I Yn 4:9-10, 19.

Kujisalimisha kwa Mungu si kujiuzulu na kukaa tu kusubiri, au kuamini kuwa yote yameandikwa binadamu hana hiari, au kuwa na udhuru na wivu. Siyo kukubali hali hiyo hiyo uliyo nayo. Inaweza kumaanisha kinyume cha haya; kujitoa sadaka maisha yako au kuteseka ili kubadilisha yanahitajika kubadilishwa. Mara nyingi Mungu huwaita watu waliojisalimisha kwake kupiga vita kwa jina lake. Kujisalimisha sio kwa uoga au mazulia. Mungu asingependa kupoteza akili alizokupa! Mungu hapendi watu wawe kama mitambo (robots) ili kumtumikia.

Kujisalimisha siyo kukomesha utu wako. Badala ya kukomesha utu wako, kujisalimisha huutia nguvu. C. S Lewis alisema, “kadiri tunavyomruhusu Mungu atutawale ndivyo tunavyozidi kuwa sisi wenyewe-kwa sababu yeye ndiye aliyetuumba. Alibuni namna mbalimbali za watu wote tofauti ambao mimi na wewe tulikusudiwa kuwa…. Ni pale ninapomgeukia Kristo, ninapojikabidhi nafsi yangu kwake, ndipo ninapokuwa na ule utu wangu halisi.” Naye Mtume Paulo anasema, nanyi ni wa Kristo, na Kristo ni wa Mungu,” 1Kor 3:23

Kujisalimisha kunadhihirika vyema katika kutii. Unasema ‘ndivyo, Bwana’ kwa chochote anachokueleza. Kusema “hapana, Bwana” ni kutamka vinyume. Hatuwezi kumwita Yesu Bwana na wakati huo huo hatutaki kumtii. Baada ya usiku kucha bila kupata samaki, Simoni alionyesha kujisalimisha pale Yesu alipomwambia kujaribu tena” “Bwana tumefanya kazi kwa bidii usiku wote na hatujakamata samaki yeyote. Lakini kwa sababu umesema, nitatia nyavu majini.” Lk.5:5. Watu waliojisalimisha hutii neno la Mungu hata kama linaonekana kutokuwa na maana.

Hapa Simoni Petro anauvua uelewa wake, anaweka pembeni uzoefu katika jambo analolijua tangu udogo wake, na kuruhusu hekima ya Mungu ifanye kazi ndani yake. Kwa maneno mengine, Simoni anaiweka pembeni hekima na busara yake ya kibinadamu na kuruhusu neema na hekima ya Mungu ifanye kazi ndani yake. Maana hekima ya dunia hii ni upuzi mbele za Mungu. Kwa maana imeandikwa, Yeye ndiye awanasaye wenye hekima katika hila yao,” 1Kor 3:19. Kuiacha hekima ya dunia na kuruhusu hekima ya Mungu ndani yako kutakuhitaji ujisalimishe.

Jambo lingine katika kujisalimisha ni IMANI. Ibrahimu alifuata maelekezo ya Mungu bila kujua alikokuwa akienda. Hana alisubiri wakati wa Mungu bila kujua ni lini. Mariamu alitarajia muujiza bila kufahamu utatendekaje. Yusufu aliamini lengo la Mungu bila kujua kwa nini mazingira yalikuwa hivyo. Kila mmoja wa watu hawa alikuwa amejisalimisha kwa Mungu alipomtegemea. Katika kweli hii Mtume Paulo anatuambia, Mtu asijidanganye mwenyewe; kama mtu akijiona kuwa mwenye hekima miongoni mwenu katika dunia hii, na awe mpumbavu, ili apate kuwa mwenye hekima,” 1Kor 3:18. Kuwa mpumbavu ili upate kuwa mwenye hekima kutakuhitaji kujisalimisha. 

Utafahamu umejisalimisha kwa Mungu unapomtegemea Mungu akutengenezee mambo yako badala ya kujaribu kuwafanyia hila wengine, ukapitisha jambo lako, na mwisho ukatawala mazingira hayo. Unamwachia Mungu afanye, Huhitaji wakati wote kuwa, “mwangalizi.” Maandiko matakatifu yanasema, “Jisalimishe nafsi yako kwa Bwana, na umsubiri kwa uvumilivu.” Zab. 37:7a. Baada ya kujaribu sana, umwamini zaidi. Pia unafahamu kwamba unajisalimisha unapokuwa huchukizwi na lawama na kukimbilia kujitetea. Mioyo iliyojisalimisha huonyesha mahusiano mazuri na wengine. Huwatupilii mbali wengine, hudai haki zako, na hutumikii nafsi yako kama umejisalimisha.

Na tazama huu ndio uzima juu ya neno lile la Yesu na kujisalimisha kule kwa Simoni: Basi, walipofanya hivyo walipata samaki wengi mno, nyavu zao zikaanza kukatika; wakawapungia mikono washirika wao waliokuwa katika chombo cha pili, waje kuwasaidia; wakaja, wakavijaza vyombo vyote viwili, hata vikataka kuzama,” Lk 5:6-7. Ndugu yangu, yawezekana umekata tamaa kabisa katika maisha yako kutokana na jambo fulani ambalo kwa uelewa wako na uzoefu wako hakuna pa kutokea. Leo Yesu anakuambia neno hili, “‘tweka mpaka kilindili,” yaani jaribu tena kile kilichobaki katika ukamilifu wake, na hadi mwisho wake kabisa, nawe utaona uwezo wangu.’ Hakika hakuna jambo lolote linaloweza kumshinda Mungu.

Yawezekana wakati fulani ulikuwa tajiri sana kwa kuwa na mali na pesa nyingi, na leo huna chochote. Usijifungie ndani kwa kuona aibu au kuchekwa na watu, na wala usiendelee kuishi jana ambayo ilishapita. Itazama kwa kina leo yako ambayo ndiyo uliyo nayo ili iwe tumaini lako la kesho. Jana yako ya ‘utajiri wa mali na pesa’ ibaki kuwa kumbukumbu tu na rejea ya kuwa karibu zaidi na Mungu. Jana yako iliyokuwa na mafanikio mengi ikukumbushe kiini halisi cha maisha, yaani, Maisha ni jaribu, Maisha ni dhamana, na Maisha ni jukumu la muda mfupi.

Matokeo ya nguvu na uwezo wa Yesu katika muujiza huu, unamfanya  Simoni kuyaona maisha yake ya ndani. Simoni Petro alipoona hayo, alianguka magotini pa Yesu, akisema, Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi, Bwana,” Lk 5:8. Ndugu yangu, hutoweza kujiona ulivyo kama hutojiachia ndani na katika Kristo Yesu. Kuiona vizuri chunusi iliyoko kwenye paji la uso wako, yakupasa kusimama mbele ya kioo. Kumbe kujiachia mbele ya kioo kunakuwezesha kujiona vizuri. Yesu ni kioo kwetu, na ndivyo Simoni alivyojigundua kuwa yu mdhambi.

Pamoja na udhaifu ule aliokuwa nao Simoni bado Mungu anampango na maisha yake. Tena mpango mahususi kabisa. Naye “Yesu akamwambia Simoni, Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu,” Lk 5:10b. Yesu anaifanya njia katika maisha ya Simoni. Huyu ndiye baadaye aliyejulikana kama Simoni Petro, na juu yake ndipo lilipo jengwa Kanisa. Mtume Paulo anatuambia, Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili,” 1Kor 10:13. Amina! Mruhusu Yesu ndani yako pasipo shaka naye atayatengeneza maisha yako upya.

Wapendwa wana wa Mungu, ukiyatazama maisha yako na jinsi Mungu alivyoendelea kuwa upendo na huruma kwako, hakika yote ndani yako ni kwa neema ya Mungu. Hakika, “Bwana, kama Wewe ungehesabu maovu, Ee Bwana, nani angesimama?” Zab 130:3. Ndugu yangu, mahangaiko katika maisha yako ya kila siku yasiwe ukuta wa kutokuona uwepo na nguvu ya Kristo Yesu ndani ya yale uyafanyayo hata kama uzoefu wako unathibitisha kutokuwezekana tena.

Kama kweli wasadiki Kristo ndiye Mwokozi, basi ni kwa namna hiyo hiyo huyaweza yote yaliyo chini ya miguu yake kwa sababu, “amevitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya Kanisa; ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote,” Efe 1:22-23. Yesu Kristo analiweka jambo hili hadharani anapowakuta Simon Petro na wenzake waliokuwa mahodari wa kuvua samaki usiku kucha bila kupata chochote. Ni Kristo Yesu huyo huyo aliye hai atakayeyabadilisha maisha yako. Jisalimishe kwake mara!

Tumsifu Yesu Kristo!

Hata walipokwisha kuviegesha pwani vyombo vyao, wakaacha vyote wakamfuata,” Lk 5:11


Tusali:-Ee Yesu Mwema, yatengeneze upya maisha yangu. Naamini pasipo shaka yoyote, Wewe kwangu ndiye Njia, Kweli, na Uzima. Amnia

No hay comentarios:

Publicar un comentario