lunes, 29 de agosto de 2016

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 22 YA MWAKA-C

JUMANNE WIKI YA 22 YA MWAKA-C
Somo: 1Kor 2:10b-16
Zab/Kit: 145:8-9, 10-11, 12-13ab, 13cd-14
Injili: Lk 4:34-37
Nukuu
akisema, Acha! Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Umekuja kutuangamiza? Nakujua u nani, Mtakatifu wa Mungu,” Lk 4:34 

Yesu akamkemea, akisema, Fumba kinywa, mtoke. Ndipo yule pepo akamwangusha katikati, akamtoka asimdhuru neno,” Lk 4:35 

 “Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu,” 1Kor 2:10b 

Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu,” 1Kor 2:11b 

 “Maana, Ni nani aliyeifahamu nia ya Bwana, amwelimishe? Lakini sisi tunayo nia ya Kristo,” 1Kor 2:16

TAFAKARI: “Nakujua u nani, Mtakatifu wa Mungu.”

Wapendwa katika Kristo, uwepo wa Kristo na Jina lake, ni tishio kwa roho zile zilizo kinyume na mpango wa Mungu. Pepo wachafu huelewa na kuogopa uwepo wa Kristo. Hakuna roho chafu zinazoweza kuushinda uwepo wa Kristo. Pepo wachafu hawana amani mara litamkwapo jina la Yesu.  Uwepo wa Kristo ni tishio kwa wale wote wampingao Kristo. Mapepo yanasema, Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Umekuja kutuangamiza? Nakujua u nani, Mtakatifu wa Mungu,” Lk 4:34. Utakatifu wa Yesu na Ukamilifu wake ni kielelezo cha maisha yetu na yale yatupasayo kuishi ili kuurithi ufalme wa Mungu.

Ukamilifu na Utakatifu wa Yesu ndio unaompa mamlaka ya kukemea roho chafu na kuwaweka huru wale waliofungwa katika ulimwengu huo wa roho. Ukweli huo hata mapepo yenyewe yanakiri na kusema, “Nakujua u nani, Mtakatifu wa Mungu,” Lk 4:34c. Hata baada ya ukiri huo wa hayo mapepo, Yesu anakemea roho hiyo chafu na kusema, Fumba kinywa, mtoke. Ndipo yule pepo akamwangusha katikati, akamtoka asimdhuru neno,” Lk 4:35. Ndugu yangu, kimbilio lako lipo wapi?

Ni wazi kati yetu mara tupatwapo na changamoto za imani ukimbia hapa na pale, na kushika hiki na kile ili kupata ulinzi. Kwa msukumo na woga huo, wengi ujikuta tumejiweka wenyewe wakfu kwa shetani kwa kupenda au kutokupenda kwa njia mbalimbali. Mfano: wengi wetu ni vinara wa ibada za mitambiko mara kwa mara na zisizo na kikomo.  Wapo pia baadhi yetu huzindika nyumba zao ikiwa ni pamoja na sehemu zao za kazi na biashara. Wengine na walio wengi, huziweka mali na fedha zao wakfu kwa shetani kabla ya kuzitumia, nk. Haya yote ni tokeo la hofu na ujinga.

Hofu na ujinga huu kamwe hauwezi ukawa ndiyo salama yako. Hofu na ujinga huu mwisho wa siku utakuingiza kwenye uovu mwingine na mkubwa zaidi. Ishinde hofu yako kwa kumwamini Kristo Yesu pasipo shaka. Kwa kuwa “hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo,” Mdo 4:12. Je, ndumba, hirizi, na haya mazindiko yako, yanasema chochote kuhusu wokovu wako? Tafakari na chukua hatua mapema!

Wapendwa wana wa Mungu, unavyo yakumbatia yaliyo ya shetani, yaani, ndumba, hirizi, mazindiko na hata wewe mwenyewe kujiweka wakfu kwa shetani na mali zako, Roho yule wa Mungu aliyeko ndani yako huondoka na kukuacha. Ukweli ni kwamba, miili yetu ni hekalu la Roho Mtakatifu, 1Kor 6:19. Na kwa mantiki hiyo, tunapolinajisi hekalu hili ndivyo hivyo hivyo tunavyomfukuza Roho huyo ndani yetu. Kazi ya Roho huyo ndani yetu “huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu,” 1Kor 2:10b. Utawezaje kuyajua mafumbo ya Mungu kama walinajisi hekalu la Roho huyo, yaani, mwili wako? Ndugu yangu tunayesafiri sote katika tafakari hii, mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu,” 1Kor 2:11b. Bila Roho wa Mungu ndani yako ni sawa na kapu tupu licha ya kwamba kapu hilo laweza kubeba chochote kile. Roho Mtakatifu ndani yako ni ulinzi tosha wa Mungu. Ikiwa mwili bila Roho Mtakatifu ndani yake hakuna ulinzi, ni sawa na kapu tupu licha ya uwezo wa kapu hilo kubeba chochote kile.

Pamoja na ulinzi huo wa Roho Mtakatifu ndani yetu, tusifananishe roho hiyo na roho ya dunia. Kwa maana nyingine sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu,” 1Kor 2:12. Utaithamini na kuitunza zawadi  ukijua thamani yake. Uthaminishwaji wa Roho ndani yetu  ndio utupao uwezo wa kusema zaidi ya hekima ya kibinadamu. Nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa na Roho, tukiyafasiri mambo ya rohoni kwa maneno ya rohoni,” 1Kor 2:13. Na hili twalifanya siyo kwa nguvu zetu na werevu wetu, bali yote twawezeshwa kwa neema za Mungu.

Kwa mantiki hiyo ni wazi kwamba mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni,” 1Kor 2:14. Kwa maneno mengine ni kwamba, mtu yule awekaye matumaini yake yote kwenye nguvu nyingine, mfano, kujiweka wakfu kwa shetani, hatoweza kufahamu nguvu ya Roho Mtakatifu ndani yake. Badala yake, mtu wa rohoni huyatambua yote, wala yeye hatambuliwi na mtu,” 1Kor 2:15. Mtu huyu ni yule anayeongozwa na Roho wa Mungu ndani yake, na mwenye hofu hiyo ya Mungu. Maana, Ni nani aliyeifahamu nia ya Bwana, amwelimishe? Lakini sisi tunayo nia ya Kristo,” 1Kor 2:16. Kristo ndiye kielelezo chetu kwa sababu ni katika Yeye tu twaweza kuokolewa Naye.

Tumsifu Yesu Kristo!

Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu,” 1Kor 2:12


Tusali:- Ee Yesu Mwema, tujalie Nguvu ya Roho wako Mtakatifu ili tuyawaze daima yaliyo Matakatifu. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario