martes, 16 de agosto de 2016

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 20 YA MWAKA-C

JUMANNE WIKI YA 20 YA MWAKA-C
Somo: Eze 28:1-10
Zab/Kit: Kumb 32:26-27ab, 27cd-28a, 30, 35cd-36ab
Injili: Mt 19:23-30
Nukuu
 “Mwanadamu, mwambie mkuu wa Tiro, Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa moyo wako umeinuka, nawe umesema, Mimi ni Mungu, nami nimeketi katika kiti cha Mungu, kati ya bahari; lakini u mwanadamu wala si Mungu, ujapokuwa umeweka moyo wako kama moyo wa Mungu,” Eze 28:2 

Tazama, una hekima kuliko Danieli; hapana neno la siri watu wawezalo kukuficha; kwa hekima yako na kwa fahamu zako umejipatia utajiri, nawe umepata dhahabu na fedha katika hazina zako; kwa hekima yako nyingi, na kwa biashara yako, umeongeza utajiri wako, na moyo wako umeinuka kwa sababu ya utajiri wako,” Eze 28:3-5 

 “Yesu akawaambia wanafunzi wake, Amin, nawaambieni, ya kwamba itakuwa shida tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni,” Mt 19:23 

 “Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza,” Mt 19:30

TAFAKARI:Kwa wanadamu hilo haliwezekani; bali kwa Mungu yote yawezekana.” 
Wapendwa wana wa Mungu, mafanikio katika maisha ikiwa ni pamoja na kupata mali na utajiri, havipaswi kuwa sababu ya kufuru na kujiinua kwetu. Mali na utajiri aliyotujalia Mungu vyapaswa kuwa sababu ya kutumika zaidi kwa sababu “na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana viti vingi, kwake huyo watataka vingi,” Lk 12:48b. Hivyo hatuna sababu ya kujiinua kutokana na mafanikio au utajiri wetu. Vyote hivyo ni mali ya Bwana nasi hatuna kilicho chetu, Zab 24:1.

Kwa watu wengine utajiri wao wameutumiwa vibaya na kujiinua katika hali ya kimungu. Watu hawa wameziabudu mali na wao wenyewe kuwa sehemu ya kuabudiwa katika jamii. Na hili ndilo onyo analopewa Mkuu wa Tiro na Mungu kupitia Mtumishi wake Nabii Ezekieli; Mwanadamu, Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa moyo wako umeinuka, nawe umesema, Mimi ni Mungu, nami nimeketi katika kiti cha Mungu, kati ya bahari; lakini u mwanadamu wala si Mungu, ujapokuwa umeweka moyo wako kama moyo wa Mungu,” Eze 28:2. Ni wazi Mkuu huyu wa Tiro alikirimiwa vingi kutoka kwa Mungu ikiwa ni pamoja na hekima. Kosa lake kubwa ni kujifananisha na vitu hivyo kiasi cha kusahau kuwa yeye bado ni mwanadamu. Naye Mungu anamwambia, Tazama, una hekima kuliko Danieli; hapana neno la siri watu wawezalo kukuficha; kwa hekima yako na kwa fahamu zako umejipatia utajiri, nawe umepata dhahabu na fedha katika hazina zako; kwa hekima yako nyingi, na kwa biashara yako, umeongeza utajiri wako, na moyo wako umeinuka kwa sababu ya utajiri wako,” Eze 28:3-5. Je, neno hili la Mungu linasema chochote kuhusu maisha yako? Ipekue nafsi yako, nawe utagundua.

Mafanikio yetu bila Mungu, mwisho wake ni majanga tu. Shetani anaweza kukusaulisha na akakupandisha hadi kileleni. Ukiwa katika furaha za hapo kileleni, shetani huyo huyo hukuachia mzima mzima hadi chini. Hakika kishindo chake ni kikubwa mno. Na hii ndiyo maana ya maneno haya ya Yesu,  Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake?” Mk 8:36. Mara tunapojithaminisha na haya ya ulimwengu, Mungu aliye vyote katika vyote hujitenga nasi katika maana hii: kwanza, anaheshimu uhuru aliotupa kama kipimo cha upendo wetu kwake katika ufahamu na umaana wa kumfuata bila shuruti. Pili, Mungu asingependa kututumia kama “maroboti,” na kwa maana hiyo anataka tuwajibike kwa kila tendo tulitendalo. Kwa mantiki hii, hatuna sababu yoyote ya kulala mwisho wa siku kwa yale mabaya yatakayo tukuta, kwani hayo yote yatakuwa changuo letu wenyewe. Na hivi ndivyo itakavyokuwa, kwamba, Kwa kuwa umeweka moyo wako kama moyo wa Mungu; basi, tazama, nitaleta wageni juu yako, watu wa mataifa wenye kutisha; nao watafuta panga zao juu ya uzuri wa hekima yako, nao watautia uchafu mwangaza wako,” Eze 6-7 

Ukiwa rafiki na ulimwengu huu kwa wakati mfupi sana utapata yote uyatamaniyo. Ila ukweli ni kwamba, baada ya muda mfupi, watakushusha hata shimoni; nawe utakufa kifo chao waliouawa kati ya baharí,” Eze 28:8. Je, katika hali na mazingira hayo ndugu yangu, utazidi kusema mbele yake huyo akuuaye, Mimi ni Mungu? Lakini u mwanadamu, wala si Mungu, mkononi mwake akutiaye jeraha,” Eze 28:9. Katika ukengemfu huu hakika utakufa kifo cha hao wasiotahiriwa, kwa mikono ya wageni; kwa maana mimi nimenena neno hili, asema Bwana MUNGU,” Eze 28:10. Haya ndiyo yaliyompata Mkuu wa Tiro na wale wote leo wenye kiburi cha mali na utajiri wao.

Suala ya utajiri na mali bila uwepo wa Mungu na hofu yake, analisema vizuri sana Yesu bila kupepesa macho. Naye anawaambia wanafunzi wake, amin, nawaambieni, ya kwamba itakuwa shida tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni,” Mt 19:23. Utajiri anausema hapa Yesu, bila shaka siyo mali tu za kushikika, bali yale yote tuliyojaliwa kwa ziada ikiwa ni pamoja na karama na vipaji vyetu. Hayo tumepewa ili yawe faida kwa wengine. Tumepewa ili tufaidiane katika kweli na haki. Na “kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana,” IKor 12:7. Vipaji na karama hizi zenye kulenga nafsi tu bila kufaidiana ni ngumu sana kuufikia ule ufalme wa Mungu aliyotuandalia kwa kila mmoja wetu. Na hii ndiyo maana ya maneno haya ya Yesu, nawaambia tena, Ni rahisi zaidi ngamia kupenya tundu ya sindano, kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu,” Mt 19:24. Mkazo huu na mafundisho haya ya Yesu haukuwa habari njema kwa wanafunzi wake. Hivyo,  Wanafunzi waliposikia, walishangaa mno, wakisema, Ni nani basi awezaye kuokoka?” Mt 19:25. Hata hivyo palipo na nia ya kweli yote huwezekana. Naye  Yesu akawakazia macho, akawaambia, Kwa wanadamu hilo haliwezekani; bali kwa Mungu yote yawezekana,” Mt 19:26. Katika hali ya kibinadamu na yenye kuangalia faida tu,  ndipo Petro akajibu, akamwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi?” Mt 19:27. Wapendwa wana wa Mungu, hakuna aliyeacha yote kwa ajili ya Kristo akawa masikini. Naye,  Yesu akawaambia, Amin, nawaambia ya kwamba ninyi mlionifuata mimi, katika ulimwengu mpya, atakapoketi Mwana wa Adamu katika kiti cha utukufu wake, ninyi nanyi mtaketi katika viti kumi na viwili, mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli,” Mt 19:28. Unapoacha yote kwa ajili ya Kristo na ndani ya Kristo, upatapa yote ndani na katika Yeye.

Faida kubwa ya kuyaacha yote kwa ajili ya Kristo, siyo tu kupata furaha na faida ya leo na sasa, bali zaidi ni kwamba, Na kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu wa kiume au wa kike, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili ya jina langu, atapokea mara mia, na kuurithi uzima wa milele,” Mt 19:29. UZIMA WA MILELE ndiyo lengo la maisha yetu hapa duniani. Hakuna maana yoyote ile ya kuyapata yote hapa duniani na kukosa lengo hili, yaani, kuufikia uzima ule wa milele. Yote yanawezekana utakapo kuwa tayari kujinyenyekeza. Na kujinyenyekeza huku ni kwamba, wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza,” Mt 19:30. Je, upo tayari kujinyenyekeza?

Tumsifu Yesu Kristo!

Ndipo Petro akajibu, akamwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi?” Mt 19:27


Tusali:- Ee Yesu, tupe neema ya kuona furaha ya kweli zaidi ya yale tuliyo nayo ya leo na sasa. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario