miércoles, 10 de agosto de 2016

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 19 YA MWAKA-C

IJUMAA WIKI YA 19 YA MWAKA-C
Somo: Eze 16:1-15, 60, 63
Zab: Isa 12:2-3, 4bcd, 5-6
Injili: Mt 19:3-12
Nukuu
Nami nilipopita karibu nawe, nikakuona ukigaagaa katika damu yako, nalikuambia, Ujapokuwa katika damu yako, uwe hai; naam, nalikuambia, Ujapokuwa katika damu yako, uwe hai,” Eze 16:6 

Nalikufanya kuwa maelfu-elfu, kama mimea ya mashamba, ukaongezeka, na kuzidi kuwa mkubwa, ukapata kuwa na uzuri mno; matiti yako yakaumbwa, nywele zako zikawa zimeota; lakini ulikuwa uchi, huna nguo,” Eze 16:7 

 “Akajibu, akawaambia, Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke, akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja?” Mt 19:4-5 

 “Akawaambia, Musa, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu, aliwapa ruhusa kuwaacha wake zenu; lakini tangu mwanzo haikuwa hivi,” Mt 19:8 

Nami nawaambia ninyi, Kila mtu atakayemwacha mkewe, isipokuwa ni kwa sababu ya uasherati, akaoa mwingine, azini; naye amwoaye yule aliyeachwa azini,” Mt 19:9 

TAFAKARI:Kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu.”

Wapendwa wana wa Mungu, tendo la uumbaji wa Mungu siyo kama mtengeneza saa ambaye akisha maliza kazi yake huiacha saa ikajiendea yenyewe tu. Mungu baada ya kutuumba uendelea kutuumba tukiwa na ushirika naye huku tukiuelekea ule ukamilifu alionao Yeye. Ni katika maana hii, Yesu anatuwasa na kutukumbusha kwamba, “ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu,” Mt 5:48. Huu ni uumbaji endelevu wa nafsi na roho.

Ni katika mwendelezo huu wa uumbaji endelevu wa nafsi na roho, Nabii Ezekieli anatumia lugha ya picha kuelezea ukengeufu na uasi wa wana wa Israeli hasa pale walipo mpiga Mungu kisogo. Na kwa upande mwingine, somo hili la kwanza linaonyesha wazi kwamba Mungu hakuacha kuwa karibu nao kwa kuonyesha huruma na upendo wake kwao. Nami nilipopita karibu nawe, nikakuona ukigaagaa katika damu yako, nalikuambia, Ujapokuwa katika damu yako, uwe hai; naam, nalikuambia, Ujapokuwa katika damu yako, uwe hai,” Eze 16:6. Tatizo walilikuwa nalo wana wa Israeli ni ile  hali ya kuupoteza uhasili wao mara walipokutana na mila na desturi za mataifa mengine. Mchanganyiko huu uliwafanya kuwa uchi kiimani licha ya kwamba Mungu aliwapigania na kuwafanya kuwa Taifa kubwa. Naye anasema, nalikufanya kuwa maelfu-elfu, kama mimea ya mashamba, ukaongezeka, na kuzidi kuwa mkubwa, ukapata kuwa na uzuri mno; matiti yako yakaumbwa, nywele zako zikawa zimeota; lakini ulikuwa uchi, huna nguo,” Eze 16:7. Taifa lolote lile linapovunja misingi yake upoteza uhasili wake na kukosa dira. Hiki ndicho kilio cha waasisi wa mataifa yetu. Pasipo msingi imara kuta za nyumba haziwezi kulibeba paa la nyumba vizuri. Lazima nyufa zitakuwepo tu.

Hata katika hali hiyo ya kuupoteza uhalisi wao na kutokuwa na dira kiimani, Mungu hakuwaacha. Mungu alizidi kuwa karibu nao na kuonyesha upendo na huruma yake. Basi, nilipopita karibu nawe, nikakutazama; tazama, wakati wako ulikuwa wakati wa upendo; nikatandika upindo wa vazi langu juu yako, nikakufunika uchi wako; naam, nalikuapia, nikafanya agano nawe, asema Bwana MUNGU, ukawa wangu,” Eze 16:8. Hizi ni zile nyakati za neema na baraka walipokuwa na mshikamano na Mungu. Mungu hakuchoka kuanza upya na wana wa Israeli hata katika udhaifu wao. Naye Mungu anawakumbusha na kusema, kisha nikakuosha kwa maji; naam, nalikuosha kabisa damu yako, nikakupaka mafuta; nikakuvika nguo ya taraza, nikakupa viatu vya ngozi ya pomboo, nikakufunga nguo ya kitani safi kiunoni mwako, nikakufunika kwa Hariri,” Eze 16:9-10.

Ndugu yangu, hali na mazingira haya kwa upande wako na wangu, ni nyakati zile tubarikiwazo si kwamba tu watakatifu sana kuwazidi wengine, bali Mungu huruhusu neema na baraka zake kwetu katika huruma na upendo wake. Na hivi ndivyo Mtume Paulo anavyotueleza juu ya neema ya Mungu inavyofanya kazi ndani yetu; Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami,” 1Kor 15:10

Mungu hakuzuia neema na baraka kwa wana wa Israeli licha ya udhaifu waliokuwa nao. Upendo wa Mungu kwa taifa hili ulikuwa kama kuku na vifaranga vyake. Naye Yesu anawakumbusha na kusema, “Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii, na kuwapiga kwa mawe wale waliotumwa kwako! Ni mara ngapi nimetaka kuwakusanya pamoja watoto wako, kama vile kuku avikusanyavyo pamoja vifaranga vyake chini ya mabawa yake, lakini hamkutaka!” Mt 23:37.  Na hivi ndivyo Mungu alivyowapenda upeo. Nikakupamba kwa mapambo pia, nikatia vikuku mikononi mwako, na mkufu shingoni mwako,” Eze 16:11.

Mungu aliwapamba na kuwainua juu zaidi ya maitaifa mengine yote, Eze 16:12-13. Mungu aliufunua utukufu wake kwao na kuwatia utukufu huo, Eze 16:14, lakini walijisahau katika fahari na uzuri huo na mwisho kuzama katika ukahaba kwa sababu ya sifa, Eze 16:15. Ukahaba unaozungumziwa hapa ni ile hali ya kila kitu ni ‘ruksa’ bila kujali uhalisi wao na misingi yao kiimani. Hatuwezi kujichanganya kwa kila kitu na mwisho wa siku tukasema kila kitu ni sawa. Katika swala la imani si vizuri kuwa na falsafa ya chura. Huwezi kujua pozi alilokuwa nalo chura ni la kusimama au kuchuchumaa. Ni heri kuwa baridi au moto kiimani, kuliko kuwa vuguvugu.

Mungu kwa kutambua kwamba Israeli ni taifa lake teule, hachoki kufanya tena na tena agano na wana hawa wa Israeli.  “Walakini nitalikumbuka agano langu nililolifanya pamoja nawe, katika siku za ujana wako, nami nitaweka imara agano la milele pamoja nawe,” Eze 16:60. Upendo wa Mungu kwetu ni waajabu sana. Mungu anakupenda kiasi hiki ili siku ya mwisho upate kukumbuka, na kufadhaika, usifumbue kinywa chako tena, kwa sababu ya aibu yako; hapo nitakapokusamehe yote uliyoyatenda, asema Bwana MUNGU,” Eze 16:63. Je, ‘utakuwa na la kujiteteza zaidi ya kilio na kusaga meno?’ Lk 13:28. Haya yote ni kwa sababu ya ugumu wa mioyo.

Na katika Injili ya leo tunaona Mafarisayo wanamtega Yesu kuhusu swala la talaka. Swali ni hili: Je! Ni halali mtu kumwacha mkewe kwa kila sababu? Kwa kujibu swali hili, Yesu anawarudisha kwenye lengo na makusudi ya Mungu la kumuumba mtu mke na mtu mume. Uumbaji huo ulilenga ukweli huu kwamba, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja?” Mt 19:4-5. Kuwa mwili mmoja siyo kitu cha kujibandua tena, wala hakuna hoja ya ubinafsi, yaani, madai ya hiki ni changu.

Kuhusu fumbo hili la kuwa mwili mmoja, Yesu anasisitiza kwa kusema, Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe,” Mt 19:6. Hapa hesabu ya Mungu ni 1+1=1, na siyo 2. Kwa mantiki hiyo, hayo wayafanyayo ambayo wanataka uhalali kutoka kwa Yesu halikuwa kusudi la Mungu wala Yeye Yesu hawezi kubadili mpango huo. Naye anawaambia kwamba swala hilo mlifanyalo liliwezekana kwenu kwa kupitia Musa kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu, aliwapa ruhusa kuwaacha wake zenu; lakini tangu mwanzo haikuwa hivi,” Mt 19:8. Kwa maana nyingine, yalikuwa maamuzi ya kukubaliana kwa kutokubaliana. Na hapa ndipo pale ilipo dhana ile ya Yesu kwamba, “Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka,yodi moja wala nukta moja ya torati haitaoondoka ,hata yote yatimie,” Mt 5:17-18

Fundisho la Yesu ni hili: Kila mtu atakayemwacha mkewe, isipokuwa ni kwa sababu ya uasherati, akaoa mwingine, azini; naye amwoaye yule aliyeachwa azini,” Mt 19:9. Ndugu yangu, mazoea hujenga tabia. Kwa fundisho hili, wanafunzi wake Yesu walikwazika na kumwambia, Mambo ya mtu na mkewe yakiwa hivyo, haifai kuoa,” Mt 19:10. Je, kuna ugumu gani hapa wa kutokuoa kama ni wito wako kufanya hivyo, zaidi ya kuwa na moyo mgumu na wakutokubadukana na mila na desturi zetu zilizo mbaya? Kwa fundisho hili la Yesu, ni wazi hakuna mbadala mwingine zaidi ya kuishi na huyu uliye naye. Maisha ya ndoa kila siku ni kurekebishana na kuumbana. Hapa tuna uumbaji endelevu wa nafsi na roho katika kusaidiana kuelekea utakatifu.

Hata hivyo, Yesu anawatoa wasiwasi na dukuduku wanafunzi wake kuhusu fundisho alilolitoa. Naye anasema, Si wote wawezao kulipokea neno hili, ila wale waliojaliwa,” Mt 19:11. Waliojaliwa hapa ni wale waliopewa uwezo huo. Kwa maana nyingine kuoa au kuolewa siyo ‘kamtindo fulani cha maisha,’ katika maana ya kuiga kwa vile fulani kafanya hivyo na wewe ufanye hivyo katika hali ya kukurupuka na bila maandalizi. Je, umejipima sawa sawa? Kwa kuelezea ukweli wa jambo hili kwa undani, Yesu anasema, wako matowashi waliozaliwa hali hiyo toka matumboni mwa mama zao; tena wako matowashi waliofanywa na watu kuwa matowashi; tena wako matowashi waliojifanya kuwa matowashi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Awezaye kulipokea neno hili, na alipokee,” Mt 19:12.

Kwa maneno mengine, wapo wasio na uwezo huo wa kuoa au kuolewa kwa sababu wamezaliwa hivyo. Wapo walikuwa na uwezo huo wa kuoa na kuolewa lakini walifanywa hivyo na mwisho wa siku kutokuwa na uwezo. Hawa ni wale ambao hasa nyakati zile za wafalme, walifanywa hivyo ili kufanya kazi katika nyumba za wafalme kwa kutokuleta madhara katika familia ya kifalme (hasa katika mahusiano kimapenzi). Wengine walifanywa hivyo ili kutoa burudani nzuri kwa wafalme hasa kwa kuimba na michezo mengine. Na kundi la mwisho ni wale walioamua kutokuoa au kuolewa kwa kuyatoa maisha yao wakfu kwa ufalme wa mbinguni. Hawa ni Watawa wa kiume na kike, Watawa (Makleri), Makleri (wasio watawa).

Tumsifu Yesu Kristo!

Wanafunzi wake wakamwambia, Mambo ya mtu na mkewe yakiwa hivyo, haifai kuoa,” Mt 19:10


Tusali:- Ee Mungu, uniumbie moyo safi, Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu 
Usinitenge na uso wako, Wala roho yako mtakatifu usiniondolee.
Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario