JUMAMOSI
WIKI YA 19 YA MWAKA-C
Somo: Eze 18:1-10, 13b, 30-32
Zab: 51:12-13, 14-15, 18-19
Injili: Mt 19:13-15
Nukuu
“Neno
la Bwana likanijia tena, kusema, Je! Maana yake ni nini hata mkatumia mithali
hii katika Israeli, mkisema, Baba wamekula zabibu mbichi, nao watoto wakatiwa
ganzi la meno?” Eze 18:1-2
“Kama
mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hamtakuwa na sababu ya kuitumia tena mithali
hii katika Israeli,” Eze 18:3
“Basi, nitawahukumu ninyi, nyumba ya Israeli, kila mmoja kwa
kadiri ya njia zake, asema Bwana MUNGU. Rudini, mkaghairi, na kuyaacha makosa
yenu yote; basi hivyo uovu wenu hautakuwa uharibifu wenu,” Eze 18:30
“Tupilieni
mbali nanyi makosa yenu yote mliyoyakosa; jifanyieni moyo mpya na roho mpya,”
Eze 18:31a
“Maana
mimi sikufurahii kufa kwake afaye, asema Bwana MUNGU; basi ghairini, mkaishi,”
Eze 18:32
“Lakini Yesu akasema, Waacheni watoto wadogo waje kwangu;
wala msiwazuie; kwa maana walio mfano wa hao, ufalme wa mbinguni ni wao,” Mt
19:14
TAFAKARI:
“Maana mimi sikufurahii kufa kwake afaye, asema Bwana MUNGU; basi ghairini,
mkaishi.”
Wapendwa wana wa Mungu, maisha ya kiroho na yenye furaha ni kuishi
bila hatia. Mtu anayeisha katika hatia, hutumia muda wa maisha
yake yote kupekua lawama na kuficha aibu. Hivyo watu wanaoongozwa na hatia
wanaonewa sana na kumbukumbu. Wanaruhusu mambo yaliyopita kutawala mambo yao ya
usoni. Wanajiadhibu bila kujua kwa kuharibu mafanikio yao. Kaini alipotenda
dhambi, hatia yake ilimtenga na Mungu, na Mungu akasema, "utakapoilima
ardhi haitakupa mazao yake; utakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani,"
Mwa 4:12. Hii inawaeleza jinsi watu wengi walivyo siku hizi-wanatangatanga
katika maisha bila lengo. Mfano mzuri angalia katika vyama vyetu vya kitume.
Wapo walio wengi huama chama kimoja cha kitume kwenda kingine na mwisho huishia
katika nyumba za sala. Nyumba za sala hapa ninamaanishisha vijikanisa
vinavyojiibua na kujiinua kwa wachungaji wao kuwa manabii.
Ndugu yangu, sisi ni
matokeo ya muda wetu uliopita lakini hatupaswi kuwa wafungwa wa muda huo.
Kusudi la Mungu halifungwi na muda wako uliopita. “Neno
la Bwana likanijia tena, kusema, Je! Maana yake ni nini hata mkatumia mithali
hii katika Israeli, mkisema, Baba wamekula zabibu mbichi, nao watoto wakatiwa
ganzi la meno?” Eze 18:1-2. Ona!
Alimbadilisha muuaji Musa na kuwa kiongozi mzuri; akambadilisha Gidioni
aliyekuwa mwoga akawa shujaa na hodari; anaweza kufanya mambo ya ajabu na
maisha yako yaliyobaki. “Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hamtakuwa na
sababu ya kuitumia tena mithali hii katika Israeli,” Eze 18:3. Kila mtu lazima
awajibika kwa kile alichokifanya na siyo kuuzunguka mbuyu. Tazama pia maisha ya Mt.
Augustino wa Hippo kabla na baada ya kuongoka kwake. Alitumia muda mrefu
kumtafuta Mungu nje kumba Mungu aliwa naye. Ni pale tu alipomwelekea naye akawa
na amani ndani yake.
Mungu ni mtaalam wa
kutupa mawazo mapya. "Heri aliyesamehewa dhambi, na kusitiriwa makosa
yake," Zab 32:1. Kwa maana nyingine twaweza kusema, "wana furaha
kubwa wale waliosamehewa hatia zao. Na wana amani wale waliotubu dhambi zao na
Mungu amefuta mashtaka yao." “Bali
kama mtu ni mwenye haki, na kuyatenda yaliyo halali na haki; hakula juu ya milima, wala
hakuviinulia macho vinyago vya nyumba ya Israeli, wala hakumtia unajisi mke wa
jirani yake, wala hakumkaribia mwanamke wakati wa kutengwa kwake; wala hakumdhulumu mtu, bali
amemrudishia mdeni wake rehani yake, wala hakumnyang'anya mtu mali yake kwa
nguvu, naye amewapa wenye njaa chakula chake, na kuwavika nguo walio uchi,” Eze
18:5-7. Bila kubadilika na kuziacha njia mbaya, hatutaweza kuwa na amani ndani
yetu. Naye Mungu anasema, “Tazama, roho zote ni mali yangu; kama vile roho
ya baba ni mali yangu, ndivyo ilivyo roho ya mwana mali yangu; roho ile
itendayo dhambi itakufa,” Eze 18:4
Kwa namna hii tunamwona
Nabii Yoha anajihukumu na kuchagua kufa kwa sababu ya kuhisi Mungu amemtenga na
kumwacha. Hata hivyo Nabii Yona anajua kwa uhakika Mungu anayemtumikia jinsi
alivyo, na kusema, “nalijua ya kuwa wewe u Mungu
mwenye neema, umejaa huruma, si mwepesi wa hasira, u mwingi wa rehema, nawe waghairi
mabaya,” Yon 4:2c. Hata pamoja na kujua ukweli huu, bado Yona haoni uwepo wa
Mungu katika shida zake. Hivyo kwa kukata tamaa anaamua afe. “Basi,
sasa, Ee Bwana, nakuomba, uniondolee uhai wangu; maana ni afadhali nife mimi
kuliko kuishi,” Yon 4:3. Uhai huo ambao Yona anaotaka kuuondoa siyo mali yake.
Uhai ni mali ya Mungu na zawadi ya Mungu. Kujiua kwa kukimbia matatizo siyo
njia sahihi ya kufanya. Na kukata tamaa ni kumkufuru Roho Mtakatifu. Dhambi hii
haisamehewi. “Kwa sababu hiyo nawaambia, Kila dhambi na kila neno la kufuru
watasamehewa wanadamu, ila kwa kumkufuru Roho hawatasamehewa,” Mt 12:31
Kuishi katika kweli na haki ndiyo salama yako. Na mfano wa mtu huyu ni
yule “ambaye hakumkopesha mtu ili apate faida, wala hakupokea ziada
ya namna yo yote; naye ameuepusha mkono wake na uovu, na kufanya hukumu ya haki
kati ya mtu na mwenzake,” Eze 18:8. Na huyu
ni yule, "azishikaye hukumu za Mungu;
mtu huyu ni mwenye haki; hakika ataishi, asema Bwana MUNGU,” Eze 18:9. Kinyume
na mpango huu wa Mungu, mtu huyo hatakuwa na maisha hata kama atafanikiwa sana
katika njia zake mbaya. Kuhusiana na dhambi za kurithishana Mungu anasema, “Walakini
mtu akizaa mwana aliye mnyang'anyi, mmwaga damu, atendaye mambo hayo mojawapo.
La, hataishi; amefanya machukizo hayo yote; hakika atakufa; damu yake itakuwa
juu yake,” Eze 18:10. Hili huwezekana katika mtindo huu tu. Kwa maana hiyo,
Mungu anasema, “nitawahukumu ninyi, nyumba
ya Israeli, kila mmoja kwa kadiri ya njia zake, asema Bwana MUNGU. Rudini,
mkaghairi, na kuyaacha makosa yenu yote; basi hivyo uovu wenu hautakuwa
uharibifu wenu,” Eze 18:30. Toba na majuto ya kweli ndiyo njia sahihi ya
kuurudisha uhusiano ule ‘haribika’ kati yetu na muumba wetu. “Tupilieni
mbali nanyi makosa yenu yote mliyoyakosa; jifanyieni moyo mpya na roho mpya;
mbona mnataka kufa, enyi nyumba ya Israeli?” Eze 18:31
Ndugu
yangu, Mungu wetu anasema, “Mimi
sikufurahii kufa kwake afaye, asema Bwana MUNGU; basi ghairini, mkaishi,” Eze
18:32. Wito wetu ikiwa ndio uhusiano wetu na Mungu ni kuwa na unyenyekevu kama
watoto wadogo. Ni husiano usio na shaka, yaani, wa mtoto na mzazi wake. Mtoto
huamini yote yawezekana kwa mzazi wake na hakuna cha kumshinda. Ni kwa mantiki
hiyo Yesu anasema, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu; wala msiwazuie; kwa
maana walio mfano wa hao, ufalme wa mbinguni ni wao,” Mt 19:14. Ndugu yangu
tujifunze kwa watoto wadogo.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Tupilieni
mbali nanyi makosa yenu yote mliyoyakosa; jifanyieni moyo mpya na roho mpya,”
Eze 18:31a
Tusali:-Ee Yesu uliye
mwingi wa huruma na rehema, tujalie utulivu wa ndani. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario