martes, 2 de agosto de 2016

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 18 YA MWAKA-C

JUMATANO WIKI  YA 18 YA MWAKA-C
Somo: Yer 31:1-7
Zab/Kit: Yer 31:10, 11-12ab, 13
Injili: Mt 15:21-28
Nukuu:
Wakati huo, asema Bwana, nitakuwa Mungu wa jamaa zote za Israeli, nao watakuwa watu wangu,” Yer 31:1 

Bwana alinitokea zamani, akisema, Naam nimekupenda kwa upendo wa milele, ndiyo maana nimekuvuta kwa fadhili zangu,” Yer 31:3 

 “Na tazama, mwanamke Mkananayo wa mipaka ile akatokea, akampazia sauti akisema, Unirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo,” Mt 15:22 

 “Akajibu, akasema, Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli,” Mt 15:24

 “Akajibu, akasema, Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa,” Mt 15:26

Akasema, Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao,” Mt 15:27 

Ndipo Yesu akajibu, akamwambia, Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yake tangu saa ile,” Mt 15:28 

TAFAKARI:Naam nimekupenda kwa upendo wa milele, ndiyo maana nimekuvuta kwa fadhili zangu.”

Wapendwa wana wa Mungu, licha ya tofauti zetu hapa duniani na ambazo kwa kiasi fulani baadhi yetu huzitumia vibaya kama fimbo ya kuwachapa wengine, utofauti huu ndiyo unaoufunua Utukufu wa Mungu. Ingawa twaonekana kuwa na rangi tofauti, yaani wengine weusi, wengine weupe, wengine wekundu, na wengine maji ya kunde, mwonekano huu ni kama bustani nzuri ya Mfalme yenye kuvutia kwa mchangiko wa maua yenye rangi tofauti. Hakika, bustani hii ya Mfalme isingevutia kama yangekuwepo maua meupe tu. Na ingekuwa hivyo tu, basi kuhimidi weupe wa maua haya kwa muda mrefu kwa kuyatazama ingetupasa kuvaa miwani. Ndivyo hivyo ilivyo kwa maua ya rangi nyingine. Mungu kayafanya haya kama yalivyo kwa sababu ‘anakupenda kwa upendo wa milele, na ndiyo maana amekuvuta kwa fadhili zake,’Yer 31:3.

Ni kwa upendo huu Mungu hakuacha kufanya tena na tena agano na watu wake hapa pale walipo muasi. Na hivi ndivyo tunavyoiona historia ya wokovu wetu. Pamoja na Mungu kuwa Huruma, Upendo, Msamaha, Haki, na Upole, hakuvunja ahadi yake ya kumkomboa mwanadamu pale alipomuasi. Mungu alikuwa na hadi sasa yupo tayari kuanza upya na kila mmoja na kuyajenga maisha ya kila amuelekeaye bila masharti yoyote zaidi ya mtu huyu kuiacha njia yake mbaya na kuishi, Eze 33:11. Na ndivyo Mungu asemavyo, kwamba, nitakuwa Mungu wa jamaa zote za Israeli, nao watakuwa watu wangu,” Yer 31:1. Licha ya kuuthibitisha Ubaba wake kwetu, Mungu huyajenga tena upya maisha yetu yaliyoparanganyika. Naye anasema,Mara ya pili nitakujenga, nawe utajengwa, Ee bikira wa Israeli mara ya pili utapambwa kwa matari yako, nawe utatokea katika michezo yao wanaofurahi,” Yer 31:4. Hii yote Mungu anataka kukuthibitishia kwamba amekuumba ili uishi milele. Kuishi milele huku kunamaanisha pia kuyafurahia matunda ya kazi na uumbaji wake. Naye anasema, Mara ya pili utapanda mizabibu juu ya milima ya Samaria; wapanzi watapanda, nao watayafurahia matunda yake,” Yer 31:5. Kwa hali na kweli hii, kwa nini basi nisimshukuru Mungu kwa ukarimu wake wote?

Kudhihirisha Upendo, Ukarimu, na ukaribu wake kwetu, wakati ulipowadia, Neno alifanyika mwili akakaa kwetu, Yoh 1:14. Ni kwa kupitia tendo hili mimi na wewe leo tu wana wa Mungu na warithi wa ufalme wake. Ingawa ni kweli kwamba Yesu alikuja kwa ajili ya kondoo waliopotea wa Israeli kama Injili ya leo inavyoufunua ukweli huo, ila kwa imani aliyokuwa nayo Mama huyu Mkananayo, wokovu ni kwa kila mtu mwenye hofu ya Mungu. Hivyo Mwanamke huyu anaona hakuna uzima wa kweli nje ya Kristo. Na tazama, mwanamke Mkananayo wa mipaka ile akatokea, akampazia sauti akisema, Unirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo,” Mt 15:22. Imani ya mtindo huu lazima ipimwe.

Yesu anaipima imani ya mama huyu. Wanafunzi wa Yesu wanamwona mama huyu kama kero. Wala yeye hakumjibu neno. Nao wanafunzi wake wakamwendea, wakamwomba, wakisema, Mwache aende zake; kwa maana anapiga kelele nyuma yetu,” Mt 15: 23. Kauli hii inawezekana wanafunzi wake walimtaka Yesu amtimizie hitaji lake mama huyu na awaache kwani ilikuwa usumbufu. Kwa upande mwingine inaonekana kama vile wanafunzi hawa wameudhiwa na hitaji la mama huyu.

Yesu anaweka jambo la muhuhimu sana kuhusu misioni yake hapa duniani na hasa kwa taifa hili la Waisraeli. Naye anasema, “Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli,” Mt 15:24. Tunapoitazama historia ya wokovu wetu hapa duniani, Mungu aliamua kwa makusudi makubwa kuanza na kundi fulani la watu. Hivyo Waisraeli walikuwa chaguo la Mungu katika harakati hizo za ukombozi. Kristo anaweka ukweli huu wazi kwa Wanafunzi wake na huyu Mama Mkananayo. Hata hivyo Yesu anataka kuipima Imani ya Mama huyu Mkananayo na kusema, Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa,” Mt 15:26. Ukweli ni kwamba wale wote ambao walikuwa nje ya mpango huu wa Taifa hili ya Mungu, yaani Waisraeli, walijulikana kama Mbwa, yani watu wa Mataifa.

Hata hivyo pamoja na upendeleo huo, Waisraeli hawakuona ukweli huo na hivyo walikuwa mara kwa mara chukizo kwa Mungu kadiri ya matendo yao. Naye mama huyu Mkananayo, anamjibu Yesu kwa unyenyekevu na hofu ya Mungu, kwa kusema, “ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao,” Mt 15:27. Kwa maneno haya yaliyojaa hofu ya Mungu na Imani ya kweli, Yesu anamuhesabia haki mama huyu. Naye Yesu anamwambia mama huyu, “Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yake tangu saa ile.” Ni kwa Imani ya kweli tunaokolewa licha ya utofauti wetu kiiutaifa, ukabila, kiukoo, na kifamilia. Kwa tendo hili la uponyaji wa binti ya mama huyu mkananayo, Yesu anathibitisha kwamba wokovu huu ni kwa kila mmoja mwenye hofu ya Mungu bila kujali tofauti zetu hapa duniani.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yake tangu saa ile,” Mt 15:28


Tusali:-Ee Yesu na Mkombozi wetu, ondoa tofauti zetu ndani ya mioyo yetu, na utujaze hofu yako na kuenenda katika njia iliyo sahihi ya uzima wa milele. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario