domingo, 21 de agosto de 2016

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 21 YA MWAKA-C

JUMATATU WIKI YA 21 YA MWAKA-C
Somo: 2The 1:1-5, 11-12
Zab/Kit: 96:1-2a, 2b-3, 4-5
Injili: Mt 23:13-22
Nukuu
Ndugu, imetupasa kumshukuru Mungu sikuzote kwa ajili yenu, kama ilivyo wajibu, kwa kuwa imani yenu inazidi sana, na upendo wa kila mtu kwenu kwa mwenzake umekuwa mwingi,” 2The 1:3

jina la Bwana wetu Yesu litukuzwe ndani yenu, nanyi ndani yake, kwa neema ya Mungu wetu na ya Bwana Yesu Kristo,” 2The 1:12

Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnawafungia watu ufalme wa mbinguni; ninyi wenyewe hamwingii, wala wanaoingia hamwaachi waingie,” Mt 23:13 

 “Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnazunguka katika bahari na nchi kavu ili kumfanya mtu mmoja kuwa mwongofu; na akiisha kufanyika, mnamfanya kuwa mwana wa jehanum mara mbili zaidi kuliko ninyi wenyewe,” Mt 23:15 

Ole wenu viongozi vipofu, ninyi msemao, Mtu atakayeapa kwa hekalu, si kitu; bali mtu atakayeapa kwa dhahabu ya hekalu, amejifunga,” Mt 23:16 

TAFAKARI:Imetupasa kumshukuru Mungu sikuzote kwa ajili yenu.”

Wapendwa wana wa Mungu, ‘Moyo usio na shukrani ukausha mema yote.’ Tendo la shukrani licha ya kusadifu kile kilichotendwa kiwe kidogo au kikubwa, tendo hilo kama lilivyo ujeuka na kuwa sala au ombi lingine. Unaposema neno ‘asante,’ ni kwa namna hiyo hiyo unafungua ‘uwezekano’ wa kuomba tena. Ni mara ngapi tunasema asante kwa mafanikio tuliyoyafikia au kuyapata hata kama ni kidogo? Lakini badala yake tunapofaulu katika mambo yetu utanguliza nafsi na juhudi zetu binafsi. Na tunaposhindwa kuyafikia malengo yetu ujiweka pembeni na kuwatupia wengine lawama.

 Mtume Paulo na wenzake wanatambua kwamba mafanikio yao katika shughuli za kitume si tokeo la nguvu na juhudi zao wenyewe, bali ni tunda, mchango, na kazi ya kila mmoja katika jumuiya ile ya kwanza ya Kikristo.  Naye anasema, ndugu, imetupasa kumshukuru Mungu sikuzote kwa ajili yenu, kama ilivyo wajibu, kwa kuwa imani yenu inazidi sana, na upendo wa kila mtu kwenu kwa mwenzake umekuwa mwingi,” 2The 1:3. Hii ndiyo picha halisi ya kutumika kama kiongozi na siyo kutumikiwa. Na mazingira haya humjengea kiongozi hali ya kufikika na siyo kuogopwa au kukimbiwa. Hapa tunaona jumuiya inayoongozwa na malengo dhabiti bila kumtenga yoyote. Kristo Yesu ndiye dira halisi ya maisha ya jumuiya hii ya kwanza ya Wakristo, na katika Kristo na ndani ya Kristo wote wanafanywa ndugu. Ikiwa hiki ndicho kiungo na dhamiri halisi ya maisha, Mtume Paulo akosi kusisitiza ukweli huu kwa Wakristo wenzake, na kusema, jina la Bwana wetu Yesu litukuzwe ndani yenu, nanyi ndani yake, kwa neema ya Mungu wetu na ya Bwana Yesu Kristo,” 2The 1:12. Nisipotambua kwamba kuna “zaidi” ya kile nilicho na ambacho kipo nje ya uwezo wangu kama mwanadamu pamoja na hali na nafasi niliyokuwa nayo katika jamii, ni rahisi kukoswa unyenyekevu kama msingi wa fadhila zote.

Pasipo unyenyekevu ni vigumu kuzama kwa yale yaliyo dhaifu ndani yangu kwa lengo la kuyaponya au kuyarekebisha. Pasipo unyenyekevu ni vigumu kujirekebisha, kujikosoa, au kukosolewa. Pasipo unyenyekevu mtu utumia muda mwingi kujitetea na kujilinda hata pale pasipokuwa na sababu ya kufanya hivyo. Na pasipo na unyenyekevu na hasa pale nitumiapo muda mwingi kujitetea na kujilinda, basi kila kisemwacho hata kwa nia njema nitakitafsiri kama ‘sengenyo’ kwangu.

Wapendwa katika Kristo, pamoja na ufahamu wa Maandiko Matakatifu waliokuwa nao waandishi na Mafasisayo, walikoswa unyenyekevu na mwisho wa siku waliyatafakari Maandiko hayo Matakatifu kukidhi hitaji lao na kujikuza kwao. Kwa mtazamo na tabia yao hii, waliinyambua torati kwa kujifaidisha wao ilhali sehemu kubwa ya jamii ilikuwa na mateso makubwa kutoka na tafsiri ile ya Torati. Hivyo tafsiri hii ya Torati (TALMUD), badala ya kuwaweka karibu na Mungu ilizidi kuwaweka mbali na Mungu. Na huu ndio uliokuwa ugomvi kati ya Yesu na hawa Mafarisayo na waandishi. Naye Yesu anawakaripia na kusema, Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnawafungia watu ufalme wa mbinguni; ninyi wenyewe hamwingii, wala wanaoingia hamwaachi waingie,” Mt 23:13

Waandishi na Mafarisayo hawa walitumia upenyo huo wa iliyo tafsiri ya Torati-Talmud na kuiweka pembeni Torati ili kujifaidia kutoka kwa wajane na wasiojiweza. Hakika waliwatiisha mizingo mikubwa na mizito kundi hili la wanyonge ilhali wao wakijiweke pembeni na kujihurumia. Na Yesu anawapasha ukweli na kuwaambia, Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnakula nyumba za wajane, na kwa unafiki mnasali sala ndefu; kwa hiyo mtapata hukumu iliyo kubwa zaidi,” Mt 23:14. Ni sawa na kusema wewe ni rafiki ya masikini, lakini wakikupiga kisogo tu unawaponda migongo yao kwa marungu.

Unafiki huu hauna tofauti na siasa zetu na hasa inchi za bara letu la Afrika. Twawatumia wanyonge kama ngazi, na tukishafika huko juu kwenye magorofa yetu (vyeo tulivyokuwa tunavitaka) tunasahu ngazi zile (wanyonge) bila kujua ipo siku tutawajibika shuka chini (kufikia ukomo wa uongozi). Na ndivyo Yesu alivyo waambia waandishi na mafarisayo, na leo anakuambia wewe na mimi tuliopewa dhamana kwamba, Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnazunguka katika bahari na nchi kavu ili kumfanya mtu mmoja kuwa mwongofu; na akiisha kufanyika, mnamfanya kuwa mwana wa jehanum mara mbili zaidi kuliko ninyi wenyewe,” Mt 23:15. Pasipo na utaratibu hapana akili, na kinyume chake ni sawa, yaani, palipo na akili pana utaratibu. Yesu kwa hakika aliona wazi wazi kujikanyaga kwao, yaani, waandishi na Mafarisayo juu ya Torati.

Hali hii, yaani, kujikanyaga kwa iliyo wazi na kweli Yesu anailinganisha sawa na UPOFU hasa ule wa kujitakia kwa viongozi wanafiki. Naye Yesu anasema, Ole wenu viongozi vipofu, ninyi msemao, Mtu atakayeapa kwa hekalu, si kitu; bali mtu atakayeapa kwa dhahabu ya hekalu, amejifunga,” Mt 23:16. Ni mara ngapi tunawaona na kuwasikia viongozi na watawala wetu kukinzana na Katiba ikiwa ndiyo sheria Mama? Tunatofauti gani kati yetu na waandishi na mafarisayo juu ya kukinzana na torati? Kwa nini basi twapindisha iliyo kweli kwa manufaa na maslahi yetu binafsi au ya vikundi vyetu (vyama vya siasa)? Isipofika mahali tukaona kijiko kama kilivyo kijiko, na badala yake tukaona na kulazimisha wengine waone kijiko kama koleo, hatutaweza kuondokana na vurugu na hata ukandamizaji wa haki za binadamu kwa kigezo cha kuilinda amani. Amani ni tunda la haki. Hivyo siwezi kutumia njia ovu kwa kigezo cha kuilinda amani. Kwa maneno mengine ni kwamba, ‘si vyema na siyo sahihi kulifikia lililo jema na zuri kwa kutumia njia ovu.’ Hapana!

Ni heri kuwa mjinga kwani upo utayari wa kujifunza na kuelewa, kuliko kuwa mpumbavu, yaani, asiye na utayari wa kujifunza akijiaminisha kuelewa kila kitu kumbe hajui chochote. Ndugu yangu tuliyesafiri sote katika tafakari hii, hakuna binadamu yeyote katika ulimwengu huu mwenye kujua moja ya kumi ya mambo yote katika ulimwengu huu. Uwapo katika ulimwengu huu upo “shuleni” kujifunza kutoka kwa wenzako na mazingira yanayokuzunguka hadi siku ya kiama yako. Na ndivyo Yesu anavyowaona viongozi vipofu na kusema,  Wapumbavu ninyi na vipofu; maana ni ipi iliyo kubwa, ile dhahabu, au lile hekalu liitakasalo dhahabu?” Mt 23:17. Kwa maneno mengine ‘yatupasa kuepuka majibu rahisi kwa maswali magumu’ kwa sababu hatutakuwa tunatatua tatizo au kutafuta ufumbuzi wa tatizo, bali kuchochea tatizo na migogoro isiyo na sababu.

Tumsifu Yesu Kristo! 

Ole wenu viongozi vipofu, ninyi msemao, Mtu atakayeapa kwa hekalu, si kitu; bali mtu atakayeapa kwa dhahabu ya hekalu, amejifunga,” Mt 23:16


Tusali:-Ee Yesu Mwema, tuongoze kwa iliyo kweli na haki. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario