viernes, 26 de agosto de 2016

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 21 YA MWAKA-C

JUMAMOSI WIKI YA 21 YA MWAKA-C
Somo: 1Kor 1:26-31
Zab/Kit: 33:12-13, 18-19, 20-21
Injili: Mt 25:14-30
Nukuu
Maana, ndugu zangu, angalieni mwito wenu, ya kwamba si wengi wenye hekima ya mwilini, si wengi wenye nguvu, si wengi wenye cheo walioitwa,” 1Kor 1:26

 “Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika Kristo Yesu, aliyefanywa kwetu hekima itokayo kwa Mungu, na haki, na utakatifu, na ukombozi,” 1Kor 1:30

 “Akampa mmoja talanta tano, na mmoja talanta mbili, na mmoja talanta moja; kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake; akasafiri,” Mt 25:15 

 “Kwa maana kila mwenye kitu atapewa, na kuongezewa tele; lakini asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang'anywa,” Mt 25:29 

TAFAKARI:Kila mwenye kitu atapewa, na kuongezewa tele; lakini asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang'anywa.” 

Wapendwa wana wa Mungu, ‘maisha ni dhamana’ ni mfano mwingine ambao  Maandiko Matakatifu yanatufunulia kuhusu maisha. Hivi karibu tulitafakari kwa undani ‘maisha ni jukumu la muda mfupi. Leo niwaombe tusafiri pamoja katika tafakari hii tukiyatazama maisha kama dhamana. Muda wetu hapa duniani na nguvu zetu, akili, nafsi, mahusiano, na mali zetu zote ni zawadi toka kwa Mungu ambazo ametukabidhi tuvitunze na kuvitumia vizuri. Sisi ni mawakili wa yale Mungu atupayo. Wazo hili la uwakili huanza na utambuzi wa kuwa Mungu ndiye mmiliki wa kila kitu na kila mtu duniani. "Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, dunia na wote wakaao ndani yake." Zab 24:1. Masomo ya leo, na hasa somo la Injili linafunua ukweli huu kuwa maisha ni dhamana.

Hakika "hatumiliki" chochote kwa wakati wetu mfupi wa kuishi duniani. Mungu "hutukopesha" dunia tunapoishi hapa. Ilikuwa mali ya Mungu kabla hujaja, na Mungu anamkopesha mtu mwingine ukifa. Na hivi ndivyo ilivyokuwa kwamba, maisha ni “mfano wa mtu atakaye kusafiri, aliwaita watumwa wake, akaweka kwao mali zake,” Mt 25:14. Je unabisha? Ndugu yangu, ukweli ni kwamba unaifurahia dunia hii kwa muda mfupi tu.

Mungu alipowaumba Adamu na Hawa, aliwakabidhi uangalizi wa uumbaji wake na akawaweka kuwa mawakili wa uumbaji wa mali yake. "Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi," Mwa 1:28. Hapa Mungu aliwaumba na kuwaita wazazi wetu wa kwanza na kuwapa wajibu wa kufanya. Wajibu huu haukuwaondolea dhana ya kuwa mawakili wa kile walichokabidhiwa. Maisha yao yalifungamanishwa na dhamana ya kile walicho. Kwa maneno mengine iliwawajibisha kutumia hekima na busara katika kutumiza wajibu huo. Maana, ndugu zangu, angalieni mwito wenu, ya kwamba si wengi wenye hekima ya mwilini, si wengi wenye nguvu, si wengi wenye cheo walioitwa,” 1Kor 1:26. Na ndivyo kila mmoja watu na kadiri ya wito wake impasavyo kuishi.

Ndugu unayesafiri nami katika tafakari hii, kazi ya kwanza ambayo Mungu aliwapa wanadamu ni kuangalia na kutunza "vitu" vya Mungu duniani. Wajibu huu haujaondolewa kamwe. Ni sehemu ya malengo yetu leo. Kila kitu tunachokifurahia yapasa tukione kama dhamana ambayo Mungu ameiweka mikononi mwetu. "Hapo tena inayohitajiwa katika mawakili, ndiyo mtu aonekane kuwa mwaminifu." 1Kor 4:2

Yesu mara kwa mara na hasa katika Injili ya leo anaonyesha kuwa maisha ni dhamana na anatoa mfano wa talanta, mfanya biashara alikabidhi watumishi utajiri wake alipo safiri. Akampa mmoja talanta tano, na mmoja talanta mbili, na mmoja talanta moja; kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake; akasafiri,” Mt 25:15. Aliporudi alitathmini kazi ya kila mtumishi na kumpa ujira sawasawa na kazi yake. Yule tajiri anasema,  "vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya Bwana wako," Mt 25:21.

Ndugu yangu, mwisho wa maisha yako duniani utatathminiwa kulingana na ulivyotumia yale Mungu aliyokukabidhi. Hii inamaana mambo yote unayofanya, hata yale mambo madogo madogo ya kila siku, yana matokeo ya umilele. Kwa maana kila mwenye kitu atapewa, na kuongezewa tele; lakini asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang'anywa,” Mt 25:29. Tunapoongelea alichokuwa nacho mtu, ni pamoja na karama na vipaji vyake. Yanipasa kuvitumia vyema na kwa faida ya wengine pia. Hivyo kama utaona mambo yote kuwa dhamana, Mungu anaahidi zawadi tatu katika maisha ya milele. Kwanza, utapewa "uthibitisho". Atasema, "kazi nzuri! umefanya vyema." Kisha "utapandishwa" daraja na utapewa jukumu kubwa katika umilele: "nitakuweka uwe mwangalizi wa vitu vingi." Na mwisho utakaribishwa katika "karamu." "Njoo ushiriki katika furaha ya Bwana wako.

Jambo lingine ni kwamba watu wengi wanashindwa kufahamu kuwa pesa ni jaribu na dhamana toka kwa Mungu. Mungu anatumia pesa kutufundisha kumtegemea; na kwa watu wengi fedha ni jaribu kuu kupita yote. Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi,” 1Tim 6:10. Mungu anaangalia jinsi tunavyotumia pesa ili kupima jinsi gani tunaaminika. "Basi, kama ninyi hamkuwa waaminifu katika mali ya udhalimu, ni nani atakayewapa amana mali ya kweli?" Lk 16:11. Huu ni ukweli wa muhimu sana. Mungu anasema kuna uhusiano wa moja kwa moja baina ya ninavyotumia pesa zangu na hali yangu ya kiroho. Jinsi ninavyotawala pesa zangu "utajiri wa dunia" ni kigezo cha kiasi gani Mungu anaweza kunikabidhi baraka za kiroho, "utajiri wa kweli".

Hebu jiulize ndugu yangu, Je, namna ninavyotumia fedha zangu yaweza kumzuia Mungu kufanya mambo zaidi maishani mwangu? Je, ninaweza kuaminiwa katika utajiri wa kiroho? Wapo watu wachache katika mazingira na maisha yetu, waliweza kuthibitisha uhusiano wa moja kwa moja baina ya walivyotumia pesa zao na hali ya kiroho ya maisha yao. Pesa au utajiri wao havikuwa kipao mbele katika maisha yao. Watu na maisha yao ya dhiki ilikuwa kero zake na mara zote alijitahidi kutafuta suluhu ya kero hizo za watu. Mtu wa namna hii ndiye tunayeweza kuumpa dhamana ya kusimamia mali ya umma. Alilolisema ndilo alilolifanya. Dhima hii ndiyo iliyompa nguvu ya Kimaadili. Mfano wa mtu huyu ni Baba yetu wa Taifa; Julius Kambarage Nyerere, aliyetutangulia katika haki. Mungu amlaze mahali pema peponi. Sina shaka katika maisha yake. Ipo siku atapewa uangalizi mkubwa zaidi na Mama Kanisa na kuwa Mwombezi wetu-Mtakatifu.

Ndugu yangu, kuwa na utajiri iwe wa kiroho na ule wa kushikika na wakati huo huo kubandukana nao, kutakuhitaji unyenyekevu wa hali ya juu. Na waliofanikiwa sana katika maisha ni wale waliojinyenyekeza sana katika maisha hana kama palikuwa na fursa ya wazi kufanya vinginevyo. Na wakati mwingine tunashangazwa na tabia hizi za wachache wetu kuishi maisha ya chini na ya kawaida kabisa licha ya mwamba mazingira na nafasi aliyokuwa nayo katika jamii ni kubwa na ya kuheshimika. Hapa ndipo tunapoona mkono wa Mungu ukifanya kazi pamoja na wale walio mridhia. Wakati mwingine na kwa mshangao mkubwa, Mungu huchagua mambo mapumbavu ya dunia awaaibishe wenye hekima; tena Mungu alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu,” 1Kor 1:27.

Huyu ndiye Mungu na tena uvichagua vitu vinyonge vya dunia na vilivyodharauliwa, naam, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko,” 1Kor 1:28. Na watu wa mtindo huu pamoja na mambo yote, hutambua maisha ni dhamana na hakuna cha kujivunia zaidi ya kuwa mawakili wa kweli kwa kile walichokabidiwa kadiri ya wito na nafasi zao katika jamii. Na katika hili Mtume Paulo anasema, mwenye mwili awaye yote asije akajisifu mbele za Mungu,” 1Kor 1:29. Jambo hili linawezekana tu pale tunapokuwa tayari na kwa moyo thabiti kuishi ndani na katika Kristo Yesu. Kwake ‘yeye tumepata kuwa katika Kristo Yesu, aliyefanywa kwetu hekima itokayo kwa Mungu, na haki, na utakatifu, na ukombozi,’ 1Kor 1:30. Hivyo aonaye fahari na aone fahari juu ya Bwana,” 1Kor 1:31. Fahari hii utuongoza kuyaona maisha yetu kuwa dhamana. Yesu Kristo anasema, "na yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi." Lk 16:48. Maisha ni dhamana. Na kadiri Mungu anavyokupa zaidi, ndivyo anakutaka uwajibike zaidi.

Tumsifu Yesu Kristo!

Na mtumwa yule asiyefaa, mtupeni mbali katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno,” Mt 25:30


Tusali:- Ee Yesu, tuongoze vyema ili tuyaone maisha ni dhamana. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario