ALHAMISI
WIKI YA 19 YA MWAKA-C
Somo: Eze 12:1-12
Zab: 78:56-57, 58-59, 61-62
Injili: Mt 18:21-19:1
Nukuu
“Mwanadamu,
wewe unakaa kati ya nyumba iliyoasi, watu ambao wana macho ya kuona, ila
hawaoni, wana masikio ya kusikia, ila hawasikii; kwa maana ni nyumba iliyoasi,”
Eze 12:2
“Sema, Mimi ni ishara kwenu; kama mimi nilivyotenda, wao nao
watatendwa vile vile; watahamishwa, watakwenda kufungwa,” Eze 12:11
“Kisha Petro akamwendea akamwambia, Bwana, ndugu yangu
anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba?” Mt 18:21
“Yesu
akamwambia, Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini,” Mt 18:22
TAFAKARI:
Baba yangu wa mbinguni atakavyowatenda ninyi, msiposamehe kwa mioyo yenu kila
mtu ndugu yake
Wapendwa
wana wa Mungu, ni ukweli kwamba katika maisha yetu tumeumizwa na kuwaumiza
wengine. Kwa mantiki hii kila mmoja wetu anayo maumivu yake ya ndani. Ili
kuponya maumivu haya ya ndani yatupasa kusamehe tukitambua pia katika maisha
tuliwaumiza watu wengine pia. Injili ya leo inatuwasa kusamehe. Tendo hili si
ombi ila ni amri ya Mungu mwenyewe. Sala yetu ya Baba yetu, inaeleza tendo hili
la kusamehe kama sharti ya yale tuyaombayo kwa Mungu, “utusamehe sisi kama
tunavyo wasamehe wale walio tukosea.” Mfano alioutoa Yesu kwenye Injili ya leo
unaonyesha ni kwa namna gani yatupasa kuwa na utu wa kweli na kusamehe pasipo
sharti. Pili, yatupasa kuishi na watu vizuri. Kwa kufanya tendo hilo, tutajua
kweli ni nani tunayemtumikia na kumfuata.
Je,
kipimo cha kusamehe ni kipi? Mtakatifu Augustino anatuambia kipimo cha upendo
ni kupenda bila kipimo. Hivyo basi, kipimo cha kusamehe ni kusamehe bila
kipimo. Habari njema yetu ya leo, yaani, Injili, inafafanua ulazima wa kutoa msamaha. Yesu
akamwambia Petro, “Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini.” Mt
18:22. Ndugu yangu, lazima tufahamu msingi wa swali la Petro. Petro anamwambia
Yesu, “Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba?”
Mt 18:21. La kujiuliza ni kwamba, kwa nini Petro ajikite kwenye mara saba?
Wapendwa katika Kristo, kadiri ya Maandiko Matakatifu, namba saba inamaanisha
UKAMILIFU, ILIYOKAMILIKA, YAKUTOSHA. Kwa Petro mara hizo saba za tosha na za
pendeza machoni mwa Mungu.
Yesu katika hili
hatengui ukamilifu na utoshelevu wa mtazamo huo, bali anaupa maana zaidi na
kuutimiliza, kwani Yeye mwenyewe anasema, “Msidhani ya kuwa nilikuja kuitangua
torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza,” Mt 5:17. Tunapotoa
msamaha yatupasa kuzama ndani katika tendo la kusamehe na kusamehewa. Ni
kuvivaa viatu vya wale waliotusamehe na kujirudi ndani kwa wale tuliowakosea.
Unaposamehe kumbuka pia nawe umesamehewa mara nyingi tu.
Ni mangapi unafanya
kinyume na mapenzi ya Mungu, lakini yeye amekupa muda wa kujirudi? Je, angetoa
adhabu za hapo kwa hapo ungebaki salama kweli? Kwa nini wasubiri kupigiwa
chetezo ndio utoe msamaha? Kwa nini tunawazungusha watu wanapotaka kusamehewa?
Kwa nini tunaweka vikwazo ili tuwasemehe watu waliotukosea hata kama weshakiri
makosa yao? Jumuiya ya wakristo, na Kanisa kwa ujumla lisilotoa msamaha ni wazi
jumuiya hiyo na Kanisa hilo halimwakilishi Yesu Kristo. Mkusanyiko huo
utakakuwa mkusanyiko usio na mwelekeo na mbele yake kuna giza kubwa sana!
Kwa Habari Njema hii ya
leo, Yesu anatoa simulizi la kuvivaa viatu vya wale waliotusamehe na kujirudi
ndani ya nafsi zetu kwa wale tuliowakosea. Hii ndiyo namna ya uzito na ulazima
wa kusamehe. Mara nyingi Yesu ameonyesha hali hiyo, na hata umauti wake kwa
ajili ya dhambi zetu walisemea jambo hili. Yesu alipoletewa mwanamke mzizi,
aliyasema haya, baada ya kulitafakari tukio lile kwa kuandika chini, “Yeye
asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza kumtupia jiwe,” Yoh 8:7. Wote
tunajua kilichofuata baada ya maneno haya ya Yesu.
Kuomba msamaha kama
tendo la kujirudi hujenga uhusiano binafsi kati yako na Muumba wako. Mungu
kamwe afurahii kuangamia kwa mtu mwovu, bali aiache njia yake mbaya na
kumfuata, Eze 33:11. Kutokuwa na uhusiano mzuri na Mungu ni sawa na kuasi. Naye
Mungu anasema, “Mwanadamu, wewe unakaa kati ya nyumba iliyoasi, watu
ambao wana macho ya kuona, ila hawaoni, wana masikio ya kusikia, ila hawasikii;
kwa maana ni nyumba iliyoasi,” Eze 12:2. Upofu huu usababishwa na majivuno. Ni vigumu sana kwa mtu kwenye
majivuno kuyaona madhaifu yake. Huu ni upofu mbaya sana kwa maisha ya kiroho.
Wapendwa wana wa Mungu,
Bwana wetu Yesu Kristo ni kielelezo sahihi cha Msamaha wa Mungu. Ndugu yangu,
“Mtu huyo Mungu amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe Mkuu na Mwokozi, awape
Waisraeli toba na msamaha wa dhambi,” Mdo 5:31. Na katika Kristo “tuna ukombozi,
yaani, msamaha wa dhambi; naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa
kwanza wa viumbe vyote,” Kol 1:14-15.
Ndugu yangu, msamaha ni
Ukristo wetu na maisha yetu kama wafuasi wake Kristo. Msamaha ni tendo la Mungu
mwenyewe na sababu ya wokovu wetu. Hakuna anayeishi kwa sababu yake mwenyewe. Hakika
tusipowasamehe wale waliotukosea katika mtazamo wa Kimungu na Uwana wake
tulioumbwa kwa sura na mfano wake, Mungu huyu tunayemwamini hatakuwa tayari
kutusamehe makosa yetu. Yesu anaweka wazi ukweli huu anaposema, “Ndivyo na Baba yangu wa mbinguni atakavyowatenda
ninyi, msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake,” Mt 18:35. Ndugu
yangu, nani wewe usiye samehe?
Tumsifu Yesu Kristo!
“Sikuambii
hata mara saba, bali hata saba mara sabini,” Mt 18:22
Tusali:-Ee Yesu,
nijalie moyo wa msamaha. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario