JUMAPILI YA 20 YA MWAKA-C
Somo
I: Yer 38:4-6, 8-10
Zab: 40:1, 2, 3, 17
Somo
II: Ebr 12:1-4
Injili:
Lk 12:49-53
Nukuu:
“Ndipo wakuu wakamwambia mfalme, Twakuomba, mtu huyu auawe,
kwa kuwa aidhoofisha mikono ya watu wa vita, waliobaki katika mji huu, na mikono
ya watu wote, kwa kuwaambia maneno kama hayo; maana mtu huyu hawatafutii watu
hawa heri, bali shari,” Yer 38:4
“Basi
wakamtwaa Yeremia, wakamtupa katika shimo la Malkiya, mwana wa mfalme, lililo
katika uwanda wa walinzi; wakamshusha kwa kamba. Na mle shimoni hamkuwa na
maji, ila matope tu; naye Yeremia akazama katika matope hayo,” Yer 38:6
“tukimtazama Yesu,
mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha
iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi
mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu,” Ebr 12:2
“Maana
mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao
dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu,” Ebr
12:3
“Je! Mwadhani ya kwamba
nimekuja kuleta amani duniani? Nawaambia, La, sivyo, bali mafarakano,” Lk
12:51
“Kwa
kuwa tokea sasa katika nyumba moja watakuwamo watu watano wamefarakana, watatu
kwa wawili, wawili kwa watatu,” Lk 12:52
“Watafarakana
baba na mwanawe, na mwana na babaye; mama na binti yake, na binti na mamaye;
mkwe mtu na mkwewe, mkwe na mkwe mtu,” Lk 12:53
TAFAKARI:
“Yesu Kristo aliyestahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa
kuume wa kiti cha enzi cha Mungu, ndiye kielezo chetu katika kweli na haki.”
Wapendwa wana wa Mungu,
Waswahili husema ‘ukiona vinaelea ujue vimeundwa.’ Chochote kile kionekanacho
na kupendeza machoni petu kina historia yake. Na historia kama mang’amuzi yenye
kugusa hisia na maisha ya watu husika, ndiyo msingi wa kile wakiheshimucho na
kukitukuza. Ni kwa maana hii hatuwezi kulitazama Kanisa leo katika uimara wake,
ueneaji wake, uinjilishaji wake, na
kushamiri kwake, bila kutambua sadaka kubwa aliyoitoa Yesu Kristo pale
Msalabani, na wote waliomfuata wakiwemo Mitume wake, na wafiadini Watakatifu
waliomwaga damu zao kwa ajili ya imani ya kweli, na katika kweli na haki. Na
ndiyo maana, “tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza
imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili
msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha
Mungu,” Ebr 12:2. Hili ndilo tumaini letu KUU kama wafuasi wake.
Kutokana na ubinafsi na
umimi uliokithiri miongoni mwetu na kutufanya sanamu za kuabudiwa, ulimwengu
leo siyo sehemu salama pa kuishi. Kila kukicha imekuwa mchezo wa karata wa
kupata na kupoteza. Lakini swali kubwa hapa ni hili; ‘tunapata kwa ajili ya
nini na nani, na tunapoteza kwa ajili ya nini na nani? Ni kweli iliyo wazi
kwamba, kama mimi na wewe leo tutakuwa tayari kuishi Ukristo wetu na kumfanya
Kristo aonekane kwa wengine hasa wanyonge, utawala huo wa kweli na haki
utaingia vitani na utawala wa ubinafsi na umimi wenye kuabudiwa na kutukuzwa.
Jambo la kusikitisha ni kwamba, utawala huu wa kweli na haki hauna Jeshi wala
mahakama kama ulivyo utawala ule wa ubinafsi na umimi. Silaha kubwa ya utawala
huu wa haki na kweli ni UPENDO.
Na sababu ya silaha hii
ni hizi mbili: Moja, ni juu ya lile lililo kuu, “Basi, sasa inadumu
imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo,” 1Kor
13:13. Na la pili ni kuhusu uzito wa sadaka ambayo mtu aweza kuitoa kwa ajili
ya wengine. Kristo ndiye kielelezo chetu katika hili; “Hakuna aliye
na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake,”
Yoh 15:13. Hakuna tutakachopoteza kwa kufanya tendo hili kwa sababu aliyetuweka
huru leo na kupata mastahili ya kuwa wana wa Mungu na warithi wa ufalme wa
Mungu, ndiye Kristo aliyeushinda uovu kwa kifo kile cha Msalaba. “Maana
mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao
dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu,” Ebr
12:3. Na kwa upande wetu katika vita hii dhidi ya uovu, ‘hatujafanya vita
hata kumwagika damu, mkishindana na dhambi,’ Ebr 12:4. Na kama wafuasi wa Kristo
tu askari wa mwanga dhidi ya giza ambalo ndilo uovu.
Upendo kama silaha kuu
ya kweli na haki, utupeleka katika ‘upendo sadaka’ kama tulivyokwisha kuona kwa
Kristo mwenyewe alivyofanya na leo kuwa kielelezo chetu, Yoh 15:13. Licha ya
kwamba leo twajionea fahari kwa Damu Takatifu ya Mitume na Wafiadini
iliyomwagika na kulistawisha Kanisa kama linavyoonekana, miongoni mwetu wapo
wanaoteseka na kuteswa kwa sababu ya kusimama katika kweli na haki. Nabii
Yeremia ni mfano wa wale wanaozibwa midomo yao kutokusema uovu wa utawala.
Yeremia anakumbana na dhiki na kadhia hiyo na maisha yake yapo hatiani. “Ndipo
wakuu wakamwambia mfalme, Twakuomba, mtu huyu auawe, kwa kuwa aidhoofisha
mikono ya watu wa vita, waliobaki katika mji huu, na mikono ya watu wote, kwa
kuwaambia maneno kama hayo; maana mtu huyu hawatafutii watu hawa heri, bali
shari,” Yer 38:4. Shari isemwayo hapa kwa watawala hawa wa nyakati za Yeremia,
leo tungeweza kusema kwamba Yeremia anatuhumiwa kwa ‘kosa la uchochezi
unaosababisha uvunjifu wa amani.’ Kwa kuulinda ufalme wake dhalimu, Mfalme
Sedekia anawajibu waleta mashitaka juu ya Yeremia, “Tazama, yu
mikononi mwenu; maana mfalme siye awezaye kufanya neno lo lote kinyume chenu,”
Yer 38:5. Mfalme anabariki mauaji kwa kuulinda ufalme wake.
Yeremia
anatendwa kwa kadiri ya baraka ya mfalme. “Basi wakamtwaa
Yeremia, wakamtupa katika shimo la Malkiya, mwana wa mfalme, lililo katika
uwanda wa walinzi; wakamshusha kwa kamba. Na mle shimoni hamkuwa na maji, ila
matope tu; naye Yeremia akazama katika matope hayo,” Yer 38:6. Hili
linapotendeka katika jamii yoyote ile iliyo hai na yenye hofu ya Mungu, sauti
za wasio na sauti lazima zitetewe na kulindwa. Kwa kutokufanya hivyo nasi
twashiriki dhambi hiyo moja kwa moja. Hata kama leo tutafunga midomo yetu na
kutokusema chochote pale tulipotakiwa kusema, historia itakuwa hakimu wetu.
Hakika ni swala la wakati tu na historia itatuhukumu.
Ebedmeleki
katika somo hili anawawakilisha wale wote walio sauti ya wasio na sauti katika
jamii yetu. “Ebedmeleki akatoka nyumbani mwa mfalme, akamwambia
mfalme, akisema, Ee bwana wangu, mfalme, watu hawa wametenda mabaya katika
mambo yote waliyomtenda Yeremia, nabii, ambaye wamemtupa shimoni; naye hakosi
atakufa pale alipo, kwa sababu ya njaa; kwa kuwa hapana mkate kabisa katika
mji,” Yer 38:8-9. Ebedmeleki leo katika jamii yetu ni mkusanyiko wa watu wote
wenye hofu ya Mungu, na wenye kupaza sauti zao pale haki za watu zinapokanyagwa
na utawala usio na hofu ya Mungu. Ni wakati pia wa kuzisikia taasisi za kidini
na zisizo za kidini kupaza sauti kutetea kweli na haki. Uhai wa mwanadamu ni
zawadi na mali na Mungu. Tumepewa mara moja tu. Hivyo lazima uhai wa mtu
uheshimiwe na kulindwa kama mboni ya jicho. Ni jambo la kusikitisha sana
unaposikia baadhi yetu wakiongelea umwagikaji wa damu, na wenye kusababishwa na
wao wenyewe kama jambo la kawaida. Ajabu sana!
Sauti
zinapopazwa kwa wasio na sauti, huamsha dhamiri zilizokufa za wale wasio na
hofu ya Mungu. Sauti ya watu ni sauti ya Mungu. Ni kupitia tendo hili la kupaza
sauti, “Ndipo mfalme akamwamuru Ebedmeleki, Mkushi, akisema, Chukua
pamoja nawe watu thelathini; toka hapa, ukamtoe Yeremia shimoni, kabla
hajafa,” Yer 38:10. Kwa nini basi twakaa kimya kama hakuna lolote lile baya
katika jamii yetu leo? Kwa nini tunaingiwa na kigugumizi? Je, twasubiri mambo
yatakapo haribika ndipo tupaze sauti? Kila mwenye hofu ya Mungu huu ni wakati
wakupaza sauti. Kwa mtindo wa ukimya huu kweli
tutaufikia uzima huo wa milele?
Uzima huo
wa milele ndani na katika Kristo Yesu tunausikia leo kutoka katika kinywa chake
mwenyewe hasa kwa maneno haya ya kuchukua hatua tukiwa tunajitathimini maisha
yetu ya kiroho. Naye Yesu anatuambia, “Je! Mwadhani ya kwamba nimekuja kuleta amani duniani? Nawaambia,
La, sivyo, bali mafarakano,” Lk 12:51. Ni mafarakano katika maana ya vita dhidi
ya ubinadamu wetu na uovu. Kumfuata Kristo katika ukamilifu yakupasa kuushinda
ubinadamu wako kwa kulenga ukamilifu ingawa udhaifu upo. Ni kwa kupitia Kristo
aliyeushinda uovu kwa wema, yaani, kuwa tayari kufa kwa ajili yangu na wewe,
nawe waweza kuishinda vita hii. Msalaba ni ishara ya huo ushindi wa wema dhidi
ya uovu. Mimi na wewe, “nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu
Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa
ulimwengu,” Gal 6:14. Je, watambua nguvu ya Msalaba katika maisha na
wokovu wako?
Wapendwa
katika Kristo, kama upo tayari kufanywa upya katika ukamilifu ndani na katika
Kristo Yesu, uwe tayari kupokea sintofahamu kwako na wale waliokuwa nawe karibu
kwa sababu ya ubinadamu wako na yale waliyokuwa wakiyafurahia kutoka kwako.
Ukiwa rafiki wa kweli na karibu wa Yesu, giza la uovu litakuwa na vita kubwa na
mwanga wa Kristo ndani ya maisha yako. Hivyo Yesu anatupatia changamoto hii kwa
kusema, “Kwa
kuwa tokea sasa katika nyumba moja watakuwamo watu watano wamefarakana, watatu
kwa wawili, wawili kwa watatu,” Lk 12:52. Hii ni vita Takatifu ya kiroho yenye
kulenga ukamilifu wa kweli utupelekao kwenye uzima wa milele. Yesu hakuishia
hapo tu. Anatuambia vita hii huenda hata kwa ndugu zetu wa damu. Je, upo tayari
kufarakana na familia yako, Baba, Mama, na ndugu zako katika kweli na haki juu
ya Kristo Bwana na mwokozi wako?
Katika
ukweli huo wa kuelekea ukamilifu na uzima wa milele, Yesu anatuambia, “watafarakana baba na
mwanawe, na mwana na babaye; mama na binti yake, na binti na mamaye; mkwe mtu
na mkwewe, mkwe na mkwe mtu,” Lk 12:53. Unapoamua kumfuata Kristo hakuna
mbadala wake ikiwa ni pamoja na kutazama nyuma. Ni heri kuwa baridi au moto
kuliko kuwa vuguvugu katika Imani. “Nanyi
mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye
kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka,” Mt 10:22. Kwa maana nyingine,
hakuna Utukufu pasipo Msalaba. Mtihani mkubwa kupita yote kwa mwanadamu ni kushindwa
kufanya maamuzi ya kina kuhusu hatma ya maisha yake. Pale tunaposhikwa
kigugumizi cha kuacha mazoea yetu na kufuata njia mpya na mwelekeo mpya katika
maisha, mwanadamu huishia kuwa masikini wa mwili na roho.
Siku moja jioni Baba Nyati na familia yake (Mama na Watoto
wawili), baada ya kutembea takribani heka ishirini za tambarare na zenye ubichi
wa majani laini wakiwa wameshiba, mmoja wa Mtoto Nyati alimshangaa Baba yake na
kumuuliza, “Baba mbona wewe hauna mkia kama sisi?”
Baada ya ukimya kidogo, Baba Nyati alitabasamu na kumuuliza
mwanaye kabla ya kujibu swali lake. “Labda nikuulize mwanangu. Je, katika
matembezi yetu leo na siku zilizopita ulishawahi kukutana na jamaa wale waitwao
simba na fisi katika eneo letu?” Naye akajibu, “hapana Baba. Huwa nawasikia
tu.” Baada ya ukimya tena kidogo, Baba Nyati akasema, “unapoona Baba wa familia
kama mimi yu hai na hana mkia ujue kwamba amepambana na simba na fisi wengi. Ni
kwa sababu hiyo leo familia yetu tuna amani na tunaishi bila hofu yoyote ile
katika himaya yetu hii.”
Ndugu yangu, wakati mwingine kuyaweka mambo katika
utaratibu wake itakupasa kutoa sadaka hai na yenye gharama. Baba Nyati kautoa
mkia wake. Mtume Petro anatuambia, “mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki
wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze,”
1Pet 5:8. Tunayofurahia leo, wapo waliotesaka kwa ajili yetu hata kupoteza
maisha yao au sehemu ya viungo vyao. Na hii ndiyo sababu ya kuwa na siku ya
mashujaa katika taifa letu. Ni wakati wa kukumbuka mazuri waliyotufanyia kama
sababu ya kuwa kama tulivyo. Na walifanya hivyo kwa upendo na bila kujibakiza.
Kamwe tusifumbe macho wala kuifunga midomo yetu pale paliko na uovu. Na kukesha
ni kupaza sauti ikiwa ndiyo hatua ya mwanzo kabisa na muhimu kusema HAPANA kwa
lililo ovu.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Je!
Mwadhani ya kwamba nimekuja kuleta amani duniani? Nawaambia, La, sivyo, bali
mafarakano,” Lk 12:51
Tusali:-Ee
Yesu Mwema, tufanye kuwa vyombo vya haki, kweli, na amani yako. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario