JUMATANO
WIKI YA 20 YA MWAKA-C
Somo: Eze 34:1-11
Zab/Kit: 23:1-3a,
3b-4, 5, 6
Injili: Mt 20:1-16
Nukuu
“Neno
la Bwana likanijia, kusema, Mwanadamu,
toa unabii juu ya wachungaji wa Israeli, toa unabii, uwaambie, naam, hao
wachungaji, Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao wachungaji wa Israeli, wanaojilisha
wenyewe; je! Haiwapasi wachungaji kuwalisha kondoo?” Eze 34:1-2
“Wagonjwa hamkuwatia nguvu, wala hamkuwaponya wenye maradhi,
wala hamkuwafunga waliovunjika, wala hamkuwarudisha waliofukuzwa, wala hamkuwatafuta
waliopotea; bali kwa nguvu na kwa ukali mmewatawala,” Eze 34:4
“kwa sababu hiyo, enyi wachungaji, lisikieni neno la Bwana; Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi
ni juu ya wachungaji; nami nitawataka kondoo zangu mikononi mwao, nami
nitawaachisha hiyo kazi ya kuwalisha kondoo; nao wachungaji hawatajilisha
wenyewe tena; nami nitawaokoa kondoo zangu vinywani mwao, wasiwe tena chakula
chao,” Eze 34:9-10
“Kwa maana ufalme
wa mbinguni umefanana na mtu mwenye nyumba aliyetoka alfajiri kwenda kuajiri
wakulima awapeleke katika shamba lake la mizabibu,” Mt 20:1
“Kulipokuchwa,
yule bwana wa shamba akamwambia msimamizi wake, Waite wakulima, uwalipe ujira
wao, ukianzia wa mwisho hata wa kwanza,” Mt 20:8
“Rafiki,
sikudhulumu; hukupatana nami kwa dinari? Chukua
iliyo yako, uende zako; napenda kumpa huyu wa mwisho sawa na wewe,” Mt 20:13-14
TAFAKARI: “Vivyo hivyo wa mwisho watakuwa wa kwanza, na wa
kwanza watakuwa wa mwisho.”
Wapendwa wana wa Mungu, Mtakatifu Yohane Maria Viane alishawahi kusema
katika maandishi yake kwamba, "acha eneo na sehemu yoyote
bila Padre kwa miaka ishirini, matokeo yake watu wataanza kuabudu
wanyama." Hakika Padre kwa Kanisa ni zawadi kubwa kuliko zawadi zote
zitolewazo. Na hii ndiyo taswira ya Padre kama mchungaji Mwema na akisi la Yesu
Kristo kama Mchungaji. Naye Mtakatifu Franscisco wa Assis anasema hivi juu ya
Padre, "kama ningekutana na malaika pamoja na Padre, ningeweza kumsalimia
kwanza Padre, kwani Malaika ni rafiki wa Mungu, na Padre ni Mhudumu wa
Mungu." Kumbe Padre kama mchungaji utambulika kwa huduma ile aitowayo kama
Kristo mwingine, "Alter Christus."
Nyakati za Nabii
Ezekieli mambo hayakuwa hivyo kwa wale waliopewa wajibu huo kama wachungaji.
Badala ya kuwaongoza watu katika kweli na haki, walichukua nafasi hiyo
kujinufaisha na kuwapoteza kondoo waliokabidhiwa. Naye Mungu kupitia nabii wake
Ezekieli anawapa ujumbe huu wale wachungaji walio kengeuka na kusema, “Mwanadamu, toa unabii juu ya wachungaji wa Israeli,
toa unabii, uwaambie, naam, hao wachungaji, Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao
wachungaji wa Israeli, wanaojilisha wenyewe; je! Haiwapasi wachungaji kuwalisha
kondoo?” Eze 34:1-2. Hawa ni wale wachungaji hata nyakati zetu walio tayari kuwakamua
kondoo bila kuwalisha vizuri. Hawa ni wale wachungaji ambao hutanguliza mambo
yao ya binafsi na fahari zao na kuwaacha kondoo wakiwa wamekondeana ilhali wao
wakiwa wamenawiri.
Je, ni
jambo la ajabu leo kuona mchungaji akiwa hana kitu kabisa na baada ya muda
mfupi tu kuwa tajiri wa kupindukia ilhali kondoo wake wakigaagaa katika wimbi
la umasikini? Mtume Paulo anatupa
taswira halisi ya mchungaji na kusema, “Maana
mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili
yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini
wake,” 2Kor 8:9. Badala yake, Mungu leo anatuambia wachungaji kuwa mmekula
kondoo “walionona, mnajivika manyoya, mnawachinja walionona;
lakini hamwalishi kondoo,” Eze 34:3. Kazi kubwa ya mchungaji ni kuwaongoza wale
anaowachunga katika kweli na haki, na matokeo yake hatakoswa chochote kwa
kutimiza wajibu huo. Naye Yesu katika hili anasema, “ampokeaye nabii kwa kuwa
ni nabii, atapata thawabu ya nabii; naye ampokeaye mwenye haki kwa kuwa ni mwenye
haki, atapata thawabu ya mwenye haki,” Mt 10:41. Kumbe mbele za watu kama
mchungaji yakupasa kuwa kile ukiwakilishacho kwa watu, na wapaswa kuishi hivyo.
Katika hili Mtume Paulo anasema, “kazi ya mtu aliyoijenga juu yake ikikaa,
atapata thawabu,” 1Kor 3:14.
Badala
yake tukiyatanguliza ya ulimwengu huu na ubinafsi wetu, ndicho chanzo cha
kuwapoteza kondoo tulikabidhiwa. Na haya ndiyo matokea yake, na malalamiko ya
Mungu ndani yetu tuliopewa thamana hiyo; “wagonjwa
hamkuwatia nguvu, wala hamkuwaponya wenye maradhi, wala hamkuwafunga
waliovunjika, wala hamkuwarudisha waliofukuzwa, wala hamkuwatafuta waliopotea;
bali kwa nguvu na kwa ukali mmewatawala,” Eze 34:4. Kati yetu wapo wachungaji wasiojitoa kwa chochote
bila kupewa cha juu kwa kile ambacho ni wajibu wao kama wachungaji. Hakika hili
ni sikitiko kubwa sana kwa Mungu. Kumbe wakati mwingine tusishangae kondoo
wakitawanyika na kutafuta malisho kwenye nyumba za sala ambazo leo zinakuwa
kama uyoga pembezoni mwa Makanisa yetu. Kondoo hawa huenda huko si kwa sababu
mafundisho wayasikiayo huko ni sahihi, bali wayasemayo wachungaji huko waendako
huyagusa majereha yao kimwili na kiroho. Hivyo kondoo hawa hutawanyika, “kwa sababu hapakuwa na mchungaji; wakawa chakula
cha wanyama- mwitu, wakatawanyika,” Eze 34:5
Ikiwa Mungu ndiye
aliyekuhesabia haki hiyo ya kuwa mchungaji wa kundi lake, kamwe hatovumilia
utendavyo ndivyo sivyo. Naye Mungu anasema, “kwa
sababu hiyo, enyi wachungaji, lisikieni neno la Bwana; Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi
ni juu ya wachungaji; nami nitawataka kondoo zangu mikononi mwao, nami
nitawaachisha hiyo kazi ya kuwalisha kondoo; nao wachungaji hawatajilisha
wenyewe tena; nami nitawaokoa kondoo zangu vinywani mwao, wasiwe tena chakula
chao,” Eze 34:9-10. Ndugu yangu tunayesafiri sote katika tafakari hii,
mafanikio yako bila Mungu hayana kesho. “Maana, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi
mwenyewe, naam, mimi, nitawatafuta kondoo zangu, na kuwaulizia,” Eze 34:11. Je,
katika hatua hii ya Mungu unalo lako la kujivunia? Tumwogope Mungu na kuwa na
hofu naye!
Wapendwa
wana wa Mungu, kila mmoja wetu mbele ya Mungu ana mizania sawa licha ya
utofauti wetu katika wito na karama tulizojaliwa na kuziishi. Kumbe kila mmoja
wetu yampasa kuishi vyema kile alicho bila kujibakiza. Haijalishi ulianza jana,
leo asubuhi, mchana au jioni, yaani, nyakati zile za mwisho wa uhai wako. Mbele
ya Mungu kutangulia au kuchelewa hakuna nafasi sana zaidi ya kuishi kile
ulichopaswa kuishi kadiri ya wito na karama zako.
“Akatoka mnamo saa tatu, akaona wengine wamesimama sokoni
wasiokuwa na kazi; na hao nao
akawaambia, Enendeni nanyi katika shamba langu la mizabibu, na iliyo haki
nitawapa. Wakaenda,” Mt 20:3-4. Ukarimu wa Mungu hauna kipimo katika mizania
yetu ya kibinadamu. Hivyo, “Akatoka tena mnamo saa sita na saa kenda, akafanya vile
vile,” Mt 20:5. Ndugu yangu, upendo wa Mungu juu yako ni mkubwa sana. Mungu
anachohitaji ni utayari wako tu wa kuelekea upendo wake. Na hivyo, “Hata
kama saa kumi na moja akatoka, akakuta wengine wamesimama, akawaambia, Mbona
mmesimama hapa mchana kutwa bila kazi?” Mt 20:6. Hata hawa ambao hawakuwa na
matumaini tena katika siku ile, Mungu anakuwa matumaini yao. Nao “Wakamwambia,
Kwa sababu hakuna mtu aliyetuajiri. Akawaambia, enendeni nanyi katika shamba la
mizabibu,” Mt 20:7
Mwisho wa siku, yaani,
maisha yetu hapa duniani tutapigwa na mshangao wa ukarimu huu wa Mungu kwa
sababu mahesabu yetu siyo ya Mungu. Ukarimu wa Mungu uzidi mtazamo wetu katika
utoaji haki. Kwa kupenda kwake Mungu hatoacha kutoa kwa wale wamwelekeao katika
kweli na haki. Na ndivyo ilivyokuwa kwamba, “Kulipokuchwa,
yule bwana wa shamba akamwambia msimamizi wake, Waite wakulima, uwalipe ujira
wao, ukianzia wa mwisho hata wa kwanza,” Mt 20:8. Ujira wetu mbele ya Mungu ni
mmoja tu licha ya utofauti wa stadi za maisha na karama tulizojaliwa naye.
Ujira huu ni Utakatifu wako kwa kile ulichoitiwa na kukichuchumilia ambacho
hakipimwi na wingi wa miaka wala masaa uishiyo hapa duniani. Kwa sababu, “Hapana
mfalme aokokaye kwa wingi wa uwezo, Wala shujaa haokoki kwa wingi wa nguvu,”
Zab 33:16. Yote tuliyo nayo tumehesabiwa haki na Mungu mwenyewe. Ni katika
mtazamo ule wa kujihesabiwa haki, “walipokuja wale wa saa
kumi na moja, walipokea kila mtu dinari,” Mt 20:9. Na kinyume chake, na katika
mtazamo wa kibinadamu wa kujihesabia haki “wale wa
kwanza walipokuja, walidhani kwamba watapokea zaidi; na hao pia wakapokea kila
mtu dinari,” Mt 20:10. Huyu ndiye Mungu aliye kweli, haki, na upendo. Na hutoa
yote kadiri ya kile alicho, yaani, upendo usio na kipimo wala mizania ya
kibinadamu.
Pamoja na malalamiko ya watu hao kuona
Mungu hakufanya iliyo haki, Mt 20:11-12, naye anamjibu mmoja wa mlalamikaji na
kusema, “Rafiki,
sikudhulumu; hukupatana nami kwa dinari? Chukua
iliyo yako, uende zako; napenda kumpa huyu wa mwisho sawa na wewe,” Mt
20:13-14. Mimi na wewe ni nani hata kuhoji upendo wa Mungu? Naye Mungu anaamsha
dhamira zetu zilizolala na kuzihoji, “Si
halali yangu kutumia vilivyo vyangu kama nipendavyo? Au jicho lako limekuwa ovu
kwa sababu ya mimi kuwa mwema?” Mt 20:15.
Mbele ya Mungu hupaswi kuishi maisha mlinganisho zaidi ya kuishi kile ulicho na
ulichoitiwa ambacho mwisho wa siku na
kwa kuishi kadiri ya mapenzi yake Mungu
ndipo palipo utakatifu wako kama ujira wako. Na moja ya mshangao mbele
ya Mungu utakuwa huu, “wa mwisho
watakuwa wa kwanza, na wa kwanza watakuwa wa mwisho,” Mt 20:16. Ndugu yangu
ishi vyema wito wako na karama alizokupa Mungu si kwa ajili yako binafsi, bali
kwa kufaidiana.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Rafiki, sikudhulumu; hukupatana nami
kwa dinari? Chukua iliyo yako, uende
zako; napenda kumpa huyu wa mwisho sawa na wewe,” Mt 20:13-14
Tusali:-Ee
Yesu, tujalie neema za kuishi kila siku kile ulichotuita kuishi, na tuishi kwa
uaminifu na bila kujibakiza. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario