domingo, 7 de agosto de 2016

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 19 YA MWAKA-C

JUMATATU WIKI YA 19 YA MWAKA-C
Somo: Eze 1:2-5, 24-2:1a
Zab: 149:1-2, 11-12ab, 12c-14a, 14bcd
Injili: Mt 17:21-26
Nukuu
Kama kuonekana kwa upinde wa mvua, ulio katika mawingu siku ya mvua, ndivyo kulivyokuwa kuonekana kwa mwangaza ule pande zote. Ndivyo kulivyokuwa kuonekana kwake mfano huo wa utukufu wa Bwana. Nami nilipoona nalianguka kifudifudi, nikasikia sauti ya mmoja anenaye,” Eze 1:28

Akaniambia, Mwanadamu, simama kwa miguu yako, nami nitasema nawe,” Eze 2:1 
Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga,” Mt 17:21 

Nao walipokuwa wakikaa Galilaya, Yesu akawaambia, Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa katika mikono ya watu, nao watamwua, na siku ya tatu atafufuka. Wakasikitika sana,” Mt 17:22-23 

Naye alipoingia nyumbani, Yesu alitangulia kumwuliza, akisema, Waonaje, Simoni? Wafalme wa dunia hutwaa kodi ama ushuru kwa watu gani? Kwa wana wao au kwa wageni?” Mt 17:25 

Naye aliposema, Kwa wageni, Yesu alimwambia, Basi, kama ni hivyo, wana ni mahuru,” Mt 17:26

TAFAKARI:Mwanadamu, simama kwa miguu yako, nami nitasema nawe.”

Wapendwa wana wa Mungu, tunapolitazama somo hili la kwanza kutoka kwa Nabii Ezekieli tunapigwa na mshangao mkubwa hasa pale Ezekieli anapojaribu kuelezea kisichoelezeka, yaani, muonekano wa Utukufu wa Bwana. Nabii Ezekieli anaelezea viumbe vinne, huku kila kiumbe kikiwa na sura nne na mabawa manne. Katikati ya viumbe hivi kuna moto na mwanga uangazao. Jambo lingine la ajabu la hawa viumbe ni kwamba kila kiumbe alikuwa na tairi ndani ya tairi. Hivyo viumbe hivi vilipotaka kutembea na matairi nayo yalitembea navyo. Sauti za mbawa za viumbe hawa ilikuwa kama tufani, kama sauti ya jeshi kuu. Juu ya viumbe hawa kulikuwa na mduara na wenye kung’ara, na juu ya mduara huu kulikuwa kuna kitu kama kiti. Na hapa ndipo alipokuwepo Bwana.

Hata hivyo Nabii Ezekieli hasemi kwamba alimwona Bwana, bali aliona Utukufu wa Bwana, Eze 1:28. Ni kwa namna hii tunaona pasipo shaka kwamba Ezekieli analazimika kutumia taswira hii ya ajabu kuelezea maono haya. Ugumu upo hapa; utawezaje kuelezea kitu ambacho unachotaka kukieleza hakina nukuu ya vipimo halisi? Ni sawa na kumwelezea kipofu juu ya rangi nyekundu ambaye hakuwahi kuona rangi. Hili ndilo tatizo analokutana nalo Ezekieli anapojaribu kueleza juu ya utukufu wa Mungu. Ezekieli anatumia taswira ya vitu ambavyo tumeshaviona. Kwa maana nyingine Ezekieli anajaribu kueleza kisichoelezeka, yaani, Utukufu wa Mungu.

Wapendwa wana wa Mungu, hata kama hatuwezi kuelezea Utukufu wa Mungu kama ulivyo, hatuwezi kupinga kwamba hakuna Utukufu huo. Mimi na wewe, pamoja na vyote tunavyoviona na tusivyoviona vinaufunua Utukufu wa Mungu. Kumbe jambo la msingi ni mimi kutambua Utukufu wa Mungu upo, na kwa wakati huohuo nimezungukwa na Utukufu wa Mungu. Hapa ndipo tunapoona wajibu wa pekee wa mwanadamu kuyatunza na kuyalinda mazingira yanayomzunguka kama wakili pekee wa Mungu, Mwa 1:28, 2:15, na 3:17-19. Ni wajibu msingi kwako na kwangu kuifanya dunia yetu hii mahali pazuri na salama kwa kuishi, tukitambua ndiye ‘Mama yetu,’ atupaye kila kitu tungali hapa dunia. Nafasi na umuhimu wa kila mmoja wetu katika kweli hii, imezungumzwa vizuri katika ‘Waraka ule maalumu’ wa Baba Mtakatifu Francis, “Shukrani kwako, Ee Bwana wangu,”-Laudato si, mi signore, 66-70.

Hivyo ndugu zangu, kuelewa Utukufu huu wa Mungu yatupasa kujua wajibu wetu na kuwa waaminifu kwa yale yote tunayokirimiwa bure, ikiwepo hewa hii tunayoitumia. Na hii ndiyo maana ya maneno haya, Mwanadamu, simama kwa miguu yako, nami nitasema nawe,” Eze 2:1. Kusimama huku ni kujua wajibu wako pale ulipo. Na kwa kufanya hivyo uwepo wa Mungu utaonekana. Mfano tukiendelea kukata miti hovyo tutaweza kweli kupata hewa nzuri kwa afya yetu? Na ingekuwa ni kulipa kodi ya hewa tunayoitumia ni wangapi kati yetu wangehimili pigo hilo?

Yesu katika Injili yetu ya leo anatupa mfano wa kuwajibika hasa pale watozao nusu-shekeli walipomwendea Petro na kujua kama  Mwalimu wao, Yesu Kristo hulipa nusu-shekeli. Kwa mtazamo wa leo tungeweza kusema kwamba ‘mamlaka ya mapato na ukusanyaji wa kodi, TRA,’ walitaka kujua kama Yesu/Kanisa analipa kodi au linalipa kodi. Na kabla ya Petro kupeleka taarifa ile kwa Yesu, alikwisha jua habari ile kabla. Na ndipo alipomuuliza Petro; “Waonaje, Simoni? Wafalme wa dunia hutwaa kodi ama ushuru kwa watu gani? Kwa wana wao au kwa wageni?” Mt 17:25. Jibu la Simon Petro lilikuwa, ‘ushuru ama kodi hulipwa kwa wageni.’ Naye Yesu anamjibu, “basi kama ni hivyo, wana ni mahuru,” Mt 17:26. Neno “mahuru,” la maanisha kutokutozwa kodi au ushuru, isiyotozwa. Je, mambo yalikuwa hivyo? Jibu ni hapana! Kwa kawaida na ndivyo ilivyokuwa, kodi walilipa wageni katika maana ya hali ile ya kuwa utumwani. Mshangao ni kwamba pamoja na kuwa katika nchi yao wanalazimika kulipa kodi. Na ukweli ni kwamba ikiwa Petro ni mwana wa Daudi, Mfalme wa Israeli, alikuwa ni mmoja wa nyumba na familia ya Mfalme, na kwa heshima hii, isingestahili kulipa kodi.

Hata hivyo wanawajibika kulipa nusu shekeli kama tozo la kidini kuhusiana na huduma ile itolewayo kwa kuabudu kwenye Hekalu. Hapa haikumaanisha kununua huduma bali lilikuwa swala la uratibishaji wa shughuli za hekalu. Na mwisho wa siku Yesu ataamuru zoezi hilo lifanyike huku akiitazama ile saa yake, yaani, mateso na kifo chake pale msalabani, Mt 17:22-23. Ni wazi fedha zilizokuwa zinatozwa wengi walifaidika nazo na ndiyo maana Mafarisayo na Waandishi walikuwa wakali sana Yesu alipokuwa anaongelea juu ya Hekalu na kuwaambia, ‘Livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha,’Yoh 2:19. Hapa hawakumwelewa ingawa Yesu alikuwa anaongelea habari za mwili, Yoh 2:21. Ndugu yangu, kama kodi ni wajibu wetu kulipa, basi kusiwe na ujanja ujanja katika wajibu huu. Hata hivyo uzoefu waonyesha kwamba watu wenye kipata kidogo ndiyo walipaji kodi kuliko wenye kipato kikubwa. Kwa ukubwa wao imekuwa rahisi kuwatia upofu wahusika na nguvu yote ya kukusanyaji kodi kuwalemea wanyonge. Lazima kuwa makini sana katika eneo hili. Na kila mtu atimize wajibu wake.

Tumsifu Yesu Kristo!

Naye aliposema, Kwa wageni, Yesu alimwambia, Basi, kama ni hivyo, wana ni mahuru,” Mt 17:26


Tusali:-Ee Yesu, pamoja na Umungu wako, hukuacha kuwajibika kwa yale yahusuyo ubinadamu wetu. Tukumbushe wajibu wetu kila siku. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario