JUMAMOSI
WIKI YA 20 YA MWAKA-C
Somo: Eze 43:1-7
Zab/Kit: 85:9ab-10,
11-12, 13
Injili: Mt 23:1-12
Nukuu
“na
tazama, huo utukufu wa Mungu wa Israeli ulitokea kwa njia ya mashariki; na
sauti yake ilikuwa kama mshindo wa maji mengi, nayo nchi iling'aa kwa utukufu
wake,” Eze 43:2
“Mwanadamu, hapa ni mahali pa kiti changu cha enzi, na mahali
pa nyayo za miguu yangu, nitakapokaa kati ya wana wa Israeli milele; na nyumba
ya Israeli hawatalinajisi jina langu takatifu tena, wao, wala wafalme wao, kwa
mambo yao ya kikahaba, na kwa mizoga ya wafalme wao, katika mahali pao pa juu,”
Eze 43:7
“Waandishi
na Mafarisayo wameketi katika kiti cha Musa; basi, yo yote
watakayowaambia, myashike na kuyatenda; lakini kwa mfano wa matendo yao,
msitende; maana wao hunena lakini hawatendi,” Mt 23:2-3
“Wao
hufunga mizigo mizito na kuwatwika watu mabegani mwao; wasitake wenyewe kuigusa
kwa kidole chao,” Mt 23:4
“Bali ninyi msiitwe
Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu,” Mt 23:8
“Naye aliye
mkubwa wenu atakuwa mtumishi wenu,” Mt 23:11
“Na
ye yote atakayejikweza, atadhiliwa; na ye yote atakayejidhili, atakwezwa,” Mt
23:12
TAFAKARI: “Naye aliye mkubwa wenu atakuwa mtumishi wenu.”
Wapendwa wana wa Mungu, kuwa na uwezo wa kuzaa kwa weza kukufanya mama
au baba, ila siyo kigezo cha wewe kuwa Mama au Baba katika maana ya MZAZI. Wapo
wengi kati yetu wenye watoto ila bado hayajawa Baba wala Mama. Kumbe
kutambulika kwako kuwa Mama au Baba haijalizi uwezo ule tu ukupelekeao kuwa na
familia, bali zaidi ni kutumika kwako na pasipo kujibakiza kama Mama au Baba
kwa nafasi hiyo ya pekee katika familia yako. Kwa mantiki hii, huitaji kujivika
‘BANGO’ lenye maandishi “mimi ndiye mama au baba wa familia hii.” Wana familia,
yaani, watoto mlio nao, na mengine mnaowajibika kwao kama walezi wao,
huwatambua kwa kuwajibika kwenu kila mmoja (Baba au Mama) kwa nafasi yake.
Ni vyema tukajua kwamba, kila aliye na nafasi ya kuwa “Mzazi” ni
mshiriki wa pekee kama kiumbe shirikishwa cha Mungu katika kazi takatifu ya
uumbaji. Nafasi hii na upekee huu hata malaika hawakupewa na Mungu. Haya yote,
yaani, ‘UUMBAJI WA MUNGU katika ujumla wake,’ na yale yote ashirikishwayo mzazi
na yenye uhusiano na uumbaji wa pili, yaani, uumbaji endelevu wa Mungu, na
wenye kumshirikisha mwanadamu katika ujumla wake, uifunua Furaha ya Mungu,
Utukufu wa Mungu, na Uwepo wa Mungu. Na ndivyo ilivyo kama asemavyo Mzaburi
kwamba, “Wewe, MUNGU, Bwana wetu Jinsi lilivyo tukufu jina lako
duniani mwote! Wewe umeuweka utukufu wako mbinguni,”
Zab 8:1.
Tukizama
ndani zaidi, uumbaji huu wa Mungu katika ujumla wake waufunua Utukufu wa Mungu.
“Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu, Na anga
laitangaza kazi ya mikono yake,” Zab 19:1. Kazi kubwa ya mwanadamu mwenye
ufahamu wa kutosha na hofu ya Mungu ndani yake, hana cha kujivunia wala
kujikweza, zaidi ya kumpa Mungu sifa na utukufu kadiri anavyopumua. “Mpeni Bwana utukufu wa jina lake; Mwabuduni
Bwana kwa uzuri wa utakatifu,” Zab 29:2. Lakini mbona basi tunakuwa na kiburi
na majivuno ya Jogoo? “Na ye yote
atakayejikweza, atadhiliwa; na ye yote atakayejidhili, atakwezwa,” Mt 23:12. Jogoo bila
shaka ufikiri asipowika mapema alfajiri, hakutopambazuka. Hii ni faraja tu kwa
mpumbavu!
Kwa
mjinga na katika maana ya kujifunza, kinywa chake mara zote kitatamka haya; “Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu, Na juu ya nchi
yote uwe utukufu wako,” Zab 57:5. Tusipotaka kuuona utukufu huu wa Mungu, Mungu
huyu huyu utuonyesha kwa namna nyingine. Na hivi ndivyo ilivyokuwa kwa wana wa
Israeli nyakati zile za Nabii Ezekieli, “na
tazama, huo utukufu wa Mungu wa Israeli ulitokea kwa njia ya mashariki; na
sauti yake ilikuwa kama mshindo wa maji mengi, nayo nchi iling'aa kwa utukufu wake,”
Eze 43:2. Tukumbuke maneno ya Yesu alivyokuwa anaingia mjini Yerusalemu kabla
ya saa ile ya kuteswa kwake juu ya Mafarisayo walio mtakaka Yesu awakanye
wanafunzi wake wanyamaze, Lk 19:37-39. Naye “akajibu, akasema, Nawaambia ninyi,
wakinyamaza hawa, mawe yatapiga kelele,” Lk 19:40.
Ni kwa
nini basi twajitwalia mamlaka ya kuwaziba watu wengine midomo wanapotaka
kuyatoa yaliyo ndani ya mioyo yao tena kwa utaratibu kubalika? Je, tunakuwa na
hofu gani kama tunajiamini kwa kile tukifanyacho kama viongozi au wazazi na
ndivyo tulivyo? Utukufu wa Mungu kama tokeo la Mungu kuushirikisha kwa viumbe
vyake, hatutaweza kuuzuia utukufu huo hata kama tutawekeza nguvu zetu zote. Na
hii ndiyo maana ya maneno haya kwamba, “Na
huo utukufu wa Bwana ukaingia ndani ya nyumba, kwa njia ya lango lile
lielekealo upande wa mashariki,” Eze 43:4. Na hapa ndipo waja wa Mungu hujazwa
na Roho ya ujasiri wa ajabu na kufanya hata yale ambayo kwa uwezo wetu wa
kibinadamu hubaki kuwa fumbo. Na hili
linatokea kwa Nabii Ezekieli na kusema, “Kisha
Roho ikaniinua, ikanichukua mpaka ua wa ndani; na tazama, utukufu wa Bwana
uliijaza nyumba,” Eze 43:5. Mungu akishasema ‘NDIYO’ kwa watu wake, mwanadamu
kwa ‘HAPANA’ yake, atakesha bure.
Wapendwa katika Kristo,
tuelewe kwamba, “Utukufu wa mfalme ni wingi wa watu wake; Bali uchache wa watu
ni uharibifu wa mkuu wao,” Mit 14:28. Kunapo tokea utengano na wenye
kusababishwa na wewe binafsi ambaye ulitakiwa kuwa alama ya umoja kama kiongozi
au mzazi pale ulipo, hakika lazima ujiandae kwa uharibifu. Elewa kwamba dhamana
na nafasi uliyo nayo kwa ajili ya watu na kwa watu, inaufunua Furaha ya Mungu,
Uwepo wa Mungu, na Utukufu wa Mungu, endapo UTATUMIKA vyema, na siyo
KUTUMIKIWA. Na huu ndio ujumbe wa Mungu kwa wana wa Israeli, na kwetu leo pia; “Mwanadamu, hapa ni mahali pa kiti changu cha
enzi, na mahali pa nyayo za miguu yangu, nitakapokaa kati ya wana wa Israeli
milele; na nyumba ya Israeli hawatalinajisi jina langu takatifu tena, wao, wala
wafalme wao, kwa mambo yao ya kikahaba, na kwa mizoga ya wafalme wao, katika
mahali pao pa juu,” Eze 43:7. Hiki kiburi cha kuchukua nafasi ya Mungu
tunakitoa wapi?
Ndugu
yangu tunayesafiri sote katika tafakari hii, “Kichwa
chenye mvi ni taji ya utukufu, Kama kikionekana katika njia ya haki,” Mit
16:31. Na pasipo haki hakuna amani hata kama nikifoka kwa nia njema kwa watu
niliopewa dhamana kwao. Ukweli ni kwamba, “Haifai
kula asali nyingi mno; Vile vile mtu kutafuta utukufu wake mwenyewe si
utukufu,” Mit 25:27. Siwezi kamwe kuutafuta utukufu wangu binafsi na kufika
kileleni kwa kutumia migongo ya watu kama ngazi. Kwa kufanya hivi nafuta kabisa
dhana ile ya KUTUMIKA na siyo KUTUMIKIWA. “Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja
kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi,” Lk 10:45.
Katika Injili yetu ya
leo, Yesu anatoa angalizo kwa wanafunzi wake akisema wawe macho juu ya
waandishi na mafarisayo kwa kujihesabia haki na kukaa katika kiti cha Musa. Wapendwa
wana wa Mungu, Musa anawakilisha sheria. Mafarisayo na waandishi kukaa katika
kitu cha Musa ni kuwa juu ya Sheria za Mungu. Wanajichukulia mamlaka yasiyo
yao, na kuwabebesha watu mizigo mizito isiyo bebeka.
Ushauri wa Yesu kwetu
kuhusu Mafarisayo na Waandishi, ni kutenda na kuishi wasemayo, ila kwa mfano wa
matendo yao tusitende. Yesu Kristo anaona kasoro ya watu hawa na anawakemea kwa
kusema, “ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnawafungia watu
ufalme wa mbinguni; ninyi wenyewe hamwingii, wala wanaoingia hamwaachi
waingie,” Mt 23:13. Wanausema na kuusifia utakatifu bila kuuishi.
Badala yake, Yesu
anatutaka kufanya hili, “Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja,
nanyi nyote ni ndugu,” Mt 23:8. Mwalimu wetu ni Yesu Kristo, na katika Yeye
sote kwa kupitia Sakramenti ya Ubatizo tumerudishiwa urithi (Ufalime ule wa
Mbinguni) wetu na kuwa wana wa Mungu. Kwa tukio hili la kupatanishwa na Mungu
Baba kupitia Mwanaye Mpenzi Yesu Kristo, sisi sote leo ni ndugu. Kwa upatanisho
huo, Yesu Kristo anayo mamlaka ya kusamehe dhambi. “Lakini mpate kujua ya
kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (amwambia yule
mwenye kupooza) Ondoka, ujitwike kitanda chako, uende nyumbani kwako,” Mt 9:6
Ndugu yangu, nani aliye
tabibu zaidi ya Bwana wetu Yesu Kristo? Ni kwa Yesu Kristo tunaweza kuponywa na
kuwa huru tukiwa na haja hiyo. “Na makutano walipojua walimfuata;
akawakaribisha, akawa akisema nao habari za ufalme wa Mungu, akawaponya wale
wenye haja ya kuponywa,” Lk 9:11. Je, mwenzangu humuitaji Yesu? Kuponywa huku
na Yesu ni matokeo ya kuziungama dhambi na kuomba uponyaji huo. Tendo hili
linatupelekea kuwa na haja ya kuponywa. “Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi,
na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa
bidii,” Yak 5:16. Amina
Tumsifu Yesu Kristo!
“Bali
ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu,” Mt 23:8
Tusali:-Ee
Yesu, tujalie unyenyekevu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario