ALHAMISI WIKI YA 18 YA MWAKA-C
Somo:
Yer 31:31-34
Zab/Kit: 51:12-13, 14-15, 18-19
Injili:
Mt 16:13-23
Nukuu:
“Angalia,
siku zinakuja, asema Bwana, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na
nyumba ya Yuda,” Yer 31:31
“Bali agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli,
baada ya siku zile, asema Bwana; Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika
mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu,” Yer
31:33
“Basi Yesu akaenda pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi
wake akasema, Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani?” Mt 16:13
“Wakasema,
Wengine hunena u Yohana Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo
wa manabii,” Mt 16:14
“Akawaambia,
Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?” Mt 16:15
“Simoni
Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai,” Mt 16:16
“Tangu wakati huo Yesu alianza kuwaonya wanafunzi wake ya
kwamba imempasa kwenda Yerusalemu, na kupata mateso mengi kwa wazee na wakuu wa
makuhani, na waandishi, na kuuawa, na siku ya tatu kufufuka,” Mt 16:21
“Petro
akamchukua, akaanza kumkemea, akisema, Hasha, Bwana, hayo hayatakupata,” Mt
16:22
“Akageuka,
akamwambia Petro, Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi
yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu,” Mt 16:23
TAFAKARI:
“Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?”
Wapendwa wana wa Mungu,
lengo la kuumbwa kwetu licha ya tofauti zetu hasa kiimani, hakuna shaka kwamba
uwepo wetu kama viumbe unasema zaidi ya kile tulicho na tujuacho kuhusu uwepo
wetu. Ni wazi yule au kile kilichokuwa sababu ya uwepo wetu anaufahamu au
kinaufahamu zaidi yetu. Hivyo kama tujuavyo pasipo shaka kwamba nguvu hiyo ipo
ambayo ni sababu ya uwepo wetu. Na uwepo wa nguvu hiyo wengine ndiye tumwitaye
Mungu, roho kamili. Mungu huyu anajua uwepo wetu ikiwa ni pamoja na mianzo yetu
na miisho yetu. Je, uwepo wetu hapa duniani ni wa bahati mbaya? La hasha!
Tukirudi katika lengo la kuumbwa kwetu ni wazi kwamba tumeumbwa ili tumjue
aliyetuumba, tumpende aliyetuumba, tumtumikia aliyetuumba kupitia ndugu zetu na
viumbe vyake, na mwisho turudi kwake na kuishi naye. Kumbe kupitia Mungu huyu
aliye hai yapo maisha baada ya kifo.
Mungu huyu hakuacha
kuonyesha ukweli huu na ukaribu kwa kile alichokiumba au alivyoviumba.
Mawasiliano hayo yamekuwepo tangu kuumbwa ulimwengu huu kwa njia mbalimbali.
Uwepo wa vile alivyoviumba vinadhihirisha mahusiano hayo na kuufunua utukufu na
furaha hiyo ya Mungu. Kwa kuwa ni Mungu aliye hai na mwenye kujali na
kuwajibika ipasavyo kwa viumbe vyake, Mungu huyu uvitumia viumbe vyake alivyoviumba
kufikisha ujumbe wake. Naye kupitia watumishi wake Manabii analifanya hilo. “Angalia, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapofanya
agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda,” Yer 31:31. Ni kupitia
maagano mbalimbali Mungu anaonyesha umoja na uhusiano wake na viumbe vyake.
Na kwa
namna ya pekee, mara hii anafanya agano la pekee baada ya kuyaona mateso ya
watu wake huko Misri. Agano hili jipya “si
kwa mfano wa agano lile nililolifanya na baba zao, katika siku ile
nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano langu hilo
walilivunja, ingawa nalikuwa mume kwao, asema Bwana,” Yer 31:32. Lengo na
madhumuni ya agano hili ni KUMJUA kama alivyo na hakuna kama Yeye. Naye anasema, “agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli,
baada ya siku zile, asema Bwana; Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika
mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu,” Yer
31:33. Huyu ndiye Mungu tunayepaswa kumwabudu na siyo mwingine au kingine.
Huyu
ndiye Mungu mwenye kusamehe uovu wetu na asiyezikumbuka dhambi zetu mara atoapo
msamaha wake. Huyu ndiye Mungu mwenye mamlaka yote, mbinguni na duniani. Ndani
na katika Mungu huyu, “Wala hawatamfundisha
kila mtu jirani yake, na kila mtu ndugu yake, wakisema, Mjue Bwana; kwa maana
watanijua wote, tangu mtu aliye mdogo miongoni mwao hata aliye mkubwa miongoni
mwao, asema Bwana; maana nitausamehe uovu wao, wala dhambi yao sitaikumbuka
tena,” Yer 31:34. Kuwa ndani na katika himaya ya Mungu huyu kuna uhuru wa
kweli. Mungu huyu ambaye hapo mwanzo alikuwa mbali sana, sasa yupo karibu nasi,
naye ndiye Imanueli, yaani, Mungu pamoja nasi, Mt 1:23. Na huyu ndiye Kristo Yesu ambaye leo katika Injili
anataka kujua wewe na mimi tunayejiita wafuasi wake twasema nini juu yake. Je,
tunamjua?
Injili ya leo kwa namna nyingine inatupa wasifu wa Petro
kwa undani na kutuelekeza nini hasa maana ya kiti chake na nafasi yake kati ya
Mitume. Mtume Petro ndiye pekee aliyejibu swali ya Yesu kwa ufasaha, licha
kwamba kwa mujibu wa Yesu jibu lile ni ufunuo kutoka kwa Mungu. Yesu
anapowauliza wanafunzi wake, Je, Nanyi
mwaninena mimi kuwa ni nani?,
Petro anajibu baada ya ukimya mkuu (tafakari): “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai,” Mt 16:16. Yesu
anaridhika na jibu hili, na hapo hapo anamnyenyekesha Petro kwa kusema, “Heri
wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba
yangu aliye mbinguni,” Mt 16:17. Ufahamu huu wa Petro, na kufunuliwa huku kwa
siri hii juu ya Kristo, kunamhesabia haki juu ya kiti kile alichokikalia hadi
leo, Petro kama halifa wa kwanza, na Mababa Watakatifu waliomfuata kama maalifa
wa Kristo. Yesu mwenyewe anaweka kiti hiki rasmi kwa kusema, “wewe ndiwe Petro,
na juu ya mwamba huu nitalijenga Kanisa langu; wala milango ya kuzimu
haitalishinda,” Mt 16:18. Wapendwa, Kanisa letu linamisingi yake. Moja ya
misingi yake hiyo ni uongozi Imara usio wa kuyumbishwa.
Wapendwa wana wa Mungu, baada ya kuwekwa rasmi kiti hicho
kama alama ya uongozi imara kichungaji, anayekalia kiti hicho anapewa mamlaka
kamili juu ya wale watakao kuwa chini ya uongozi huo. Yesu anayatoa mamlaka
hayo kwa kusema, “Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa
mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na
lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni,” Mt 16.19.
Kwa kupitia kiti na mamlaka haya, Kanisa linakuwa rasmi chombo cha msamaha na
huruma ya Mungu. Na hii ndiyo maana ya Kanisa kama Sakramenti ya wokovu. Kanisa
pia linapewa mamlaka ya kufundisha, kuonya, kukataza na hata kufungia yale
yanayoenda kinyume cha Imani na ufuasi wa Kristo.
Hata hivyo pamoja na
ukweli huu anaoufunua Yesu na Masiha mbele ya Mitume wake, hapendi jambo hilo
lisikike kwa mtu ye yote zaidi yao akijua saa ile bado kutimia, yaani,
atakapoutoa uhai wake kwa ajili yako na yangu ili tuwe huru. “Ndipo
alipowakataza sana wanafunzi wake wasimwambie mtu ye yote ya kwamba yeye ndiye
Kristo,” Mt 16:20. Yesu anauficha Umasiha wake akisubiri kuufunua wazi katika
saa ile, ya mateso na kifo chake. Na ni kwa mantiki hiyo, “tangu
wakati huo Yesu alianza kuwaonya wanafunzi wake ya kwamba imempasa kwenda
Yerusalemu, na kupata mateso mengi kwa wazee na wakuu wa makuhani, na
waandishi, na kuuawa, na siku ya tatu kufufuka,” Mt 16:21. Ukweli huu
haukupendeza masikioni mwa wanafunzi wake.
Lakini
hii ndiyo njia aliyoichagua Yesu kukuweka wewe na mimi huru kutoka utumwa wa
dhambi.
“Petro akamchukua (Yesu pembeni), akaanza kumkemea,
akisema, Hasha, Bwana, hayo hayatakupata,” Mt 16:22. Ukiwa huu ndio mpango
wenyewe na ndivyo ilivyompendeza Mungu, na kwa Yesu kujitoa bila kujibakiza,
Yesu “Akageuka, akamwambia Petro, Nenda
nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya
wanadamu,” Mt 16:23. Hatuwezi kufika pale alipo Kristo hasa katika thamani ya
sadaka yake pale Msalabani, na kuishi maisha ya Ufufuko kama tutaendelea kuwaza
yaliyo ya wanadamu. Kwayo kama yalivyo, yaani, ya wanadamu, hayana umilele. Na
ndiyo maana Mtume Paulo anatusihi nini maana ya kuishi maisha ya Ufufuko. Naye
anasema, “ikiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo
aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo
katika nchi,” Kol 3:1-2. Ndugu yangu, yaliyo katika nchi ni yale ya wanadamu
kadiri ya ufahamu wao wa kibinadamu.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Akageuka,
akamwambia Petro, Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi
yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu,” Mt 16:23
Tusali:-Ee Yesu; uliye
Njia, Kweli, na Uzima wetu, tujalie neema yako tukujue kila siku ya maisha
yetu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario