domingo, 14 de agosto de 2016

TAFAKARI: SIKUKUU YA KUPALIZWA KWA BIKIRA MARIA MBINGUNI

SIKUKUU YA KUPALIZWA MBINGUNI BIKIRA MARIA
Somo I: Ufu 11: 19, 12:1-6, 10
Zab: 45:9-11, 15
Somo II: 1Kor 15:20-26
Injili: Lk 1:39-56
Nukuu:
Na ishara kuu ilionekana mbinguni; mwanamke aliyevikwa jua, na mwezi ulikuwa chini ya miguu yake, na juu ya kichwa chake taji ya nyota kumi na mbili,” Ufu 12:1

Na yule joka akasimama mbele ya yule mwanamke aliye tayari kuzaa, ili azaapo, amle mtoto wake,” Ufu 12:4b 

Naye akazaa mtoto mwanamume, yeye atakayewachunga mataifa yote kwa fimbo ya chuma. Na mtoto wake akanyakuliwa hata kwa Mungu, na kwa kiti chake cha enzi,” Ufu 12:5

Kwa kuwa kama katika Adamu wote wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote watahuishwa,” 1Kor 15:22

Maana sharti amiliki yeye, hata awaweke maadui wake wote chini ya miguu yake,” 1Kor 15:25

Maana sauti ya kuamkia kwako ilipoingia masikioni mwangu, kitoto kichanga kikaruka kwa shangwe ndani ya tumbo langu,” Lk 1:44

Kwa kuwa ameutazama Unyonge wa mjakazi wake. Kwa maana, tazama, tokea sasa Vizazi vyote wataniita mbarikiwa,” Lk 1:48

Amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi; Na wanyonge amewakweza,” Lk 1:52

TAFAKARI: “Utakatifu wetu ndiyo cheo chetu, na ndiyo makusudi ya maisha ya umilele.”

Wapendwa wana na Mungu, leo Mama Kanisa anafanya sikukuu ya kupalizwa mbinguni kwa Mama Bikira Maria. Tendo hili la kupalizwa mbingini kwa Bikira Maria lina vielelezo vyote vya kimazingira na kimaandiko Matakatifu. Kimazingira, kama mwanadamu Bikira Maria alijaliwa neema za Kimungu kushirika kwa ukaribu na undani kabisa fumbo zima la wokovu wetu. Kama Mama na Mzazi, Bikira Maria alikumbana na shuruba nyingi sana za malezi na mahangaiko makubwa kumlea Mtoto Yesu ambaye alikuwa na uwezo mkubwa wa Kimungu, na hata kuwapita wazazi wake. Hakika Bikira Maria alikuwa na mahangaiko makubwa sana katika malezi ya mtoto huyu. Ni ukweli usiotia shaka kabisa, kwa malezi haya, na kwa kushiriki fumbo hili la wokovu tangu kutungwa mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu,  kuzaliwa kwa Yesu, Kukua kwa Yesu, Mateso yake, kifo chake, na ufufuko wake, Bikira Maria alishiriki fumbo hili la wokovu kikamilifu. Kwa kubeba ujauzito, Mama Bikira Maria anashirikishwa utukufu wa Yesu katika ishara hii anaposalimiana na Elizabeth: Maana sauti ya kuamkia kwako ilipoingia masikioni mwangu, kitoto kichanga kikaruka kwa shangwe ndani ya tumbo langu,” Lk 1:44. Elizabeth anatoa ushuhuda huu. Siri kubwa ya mafanikio ya Mama Bikira Maria na mastahili yake ya kupalizwa Mbinguni yapo kwenye unyenyekevu wake. Hivyo Bikira Maria anatambua jambo hilo na kusema, Kwa kuwa ameutazama Unyonge wa mjakazi wake. Kwa maana, tazama, tokea sasa Vizazi vyote wataniita mbarikiwa,” Lk 1:48. Kujinyenyekeza ni jambo la msingi sana na hasa kwa kufunuliwa siri za Mungu. Kujiachilia huku kwa Mama Bikira Maria kuliko kwa chini kabisa, na kubebwa kwa unyenyekevu wake kunaonekana katika maneno haya: Amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi; Na wanyonge amewakweza,” Lk 1:52. Mama Bikira Maria anatufundisha kuhoji na kusema maneno haya: “Je, mimi ni nani Bwana hata kuyatenda haya yote ndani mwangu?”

Kwa mtazamo huo wa kimazingira Bikira Maria anachukua nafasi ya mkombozi mwenza. Ni kwa mantiki hiyo hiyo ushindi wa msalaba ni ushindi wa Bikira Maria pia. Furaha za ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo ni furaha ya Bikira Maria pia. Kupaa kwa Bwana yetu Yesu Kristo mbinguni, hakuwezi kumzuiya mwanaye kumshirikisha furaha hiyo Mama yake kupalizwa mbinguni mwili na roho. Je, nani kama mama? Hali hii inatupa mtazamo wa kimazingira na ushiriki wa Mama Bikira Maria katika fumbo hili la wokovu.

Kwa upande mwingine  Maandiko Matakatifu yanatupa ukweli wa siri hii ya ajabu juu ya kupalizwa Mbinguni kwa Mama Bikira Maria. Kwa kuanguka kwa wazazi wetu wa mwanzo, yaani Adam una Eva, Mungu hakuacha mpango wake wa kumkomboa mwanadamu. Hivyo ujio wa Yesu Kristo ni kielelezo cha Adamu Mpya ambaye kwa kupitia kwake mpango mzima wa wokovu wa mwanadamu unakamilika. Bikira Maria anachukua nafasi ya Eva ambaye kwa kupitia kwake mpango wa kwanza wa kumkomboa mwanadamu ulikwama. Hivyo kadiri ya maandiko matakatifu, Bikira mara ndiye atakayemzaa mtoto wa Kiume, yaani Yesu na kuendeleza mpango wa Mungu. Hivyo, Naye akazaa mtoto mwanamume, yeye atakayewachunga mataifa yote kwa fimbo ya chuma. Na mtoto wake akanyakuliwa hata kwa Mungu, na kwa kiti chake cha enzi,” Ufu 12:5.

Mama huyu alikuwa ndani ya mpango wa Mungu tangu mwanzo. Bikira Maria alishakwisha vikwa taji la ushindi, hivyo ilikuwa ni jambo la wakati tu utakapotia na historia ichukue nafasi yake. Hakuna lisilowezekana kwa Mungu. Na ishara kuu ilionekana mbinguni; mwanamke aliyevikwa jua, na mwezi ulikuwa chini ya miguu yake, na juu ya kichwa chake taji ya nyota kumi na mbili,” Ufu 12:1. Hata pamoja na ishara hii, Mama huyu anaonyeshwa ni kwa namna gani atashiriki mahangaiko ya mtoto wake atakaye mzaa. Maandiko Matakatifu yanachukua Ishara ya Joka, ambalo lipo ili kuzuia uhai wa mtoto huyu. Na yule joka akasimama mbele ya yule mwanamke aliye tayari kuzaa, ili azaapo, amle mtoto wake,” Ufu 12:4b. Uwepo wa Joka hili, twaweza kuufananisha na uovu uliokuwa umemzunguka Yesu, yaani dhambi, na hivyo Yesu itampasa kufa ili kumshinda adui wa mwisho yaani mauti. Maana sharti amiliki yeye, hata awaweke maadui wake wote chini ya miguu yake. Adui wa mwisho atakayebatilishwa ni mauti,” 1Kor 15:26

Ukweli ni kwama kadiri ya maandiko Matakatifu, na kwa kupitia Adamu, wote walikufa, na kwa kupita Yesu wote watahuishwa. Hivyo uzima wa kweli tunaupata kupitia Kristo, na kifo kinabakia tu kama mlango wa kwenda sehemu ya pili yaani uzima wa milele. Kwa kuwa kama katika Adamu wote wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote watahuishwa,” 1Kor 15:22. Tunahuishwa kwa fumbo zima la kifo na ufufuko wake Yesu Kristo. Mastahili haya hayatokani na historia zetu, yaani, familia tulizotoka, koo tulizotoka, wala kabila, wala taifa, bali ni uhaminifu wetu juu ya Kristo na utakatifu wetu ambao ndiyo cheo chetu.

Hivyo hapana shaka yoyote kwamba Bikira Maria kupalizwa Mbinguni. Kama alishiriki mahangaiko na mwanaye ndiyo hivyo hivyo Bikira Maria ilimpasa kushiriki Furaha na Utukufu pamoja na mwanaye. Hiyo ndiyo zawadi kubwa na asante ya Yesu kwa Mama yake. Hakika hatuwezi kulipa waliyotutendea wazazi wetu, na hasa Mama Mzazi.

Kijana Felix aliyemaliza masomo yake ya udaktari alibahatika kumwoa mwanamke mwenye elimu kama yake. Mwanamke huyu alijipenda sana kupita kiasi kutokana na mazingira ya makuzi yake. Ni kweli alitoka familia yenye pesa na tajiri sana.

Felix alitoka familia masikini sana, na soma yake ilikuwa ya shida sana. Felix alifika hapa alipo kwa kutegemea biashara ndogo ndogo za mama yake mzazi. Baba yake Felix alifariki muda mrefu, Felix angali darasa la pili.

Akiwa ameajiriwa na kuwa na mji wake, mama yake mzazi alipenda kumtembelea mtoto wake. Kwa bahati mbaya au nzuri Mama yake Felix alifika na kumkuta mke wa mtoto wake. Kwa namna alivyokuwa mama yake Felix, mke wa Felix alikuwa na mashaka naye kwani alionekana kama ombaomba fulani hivi. Hata kwa kujitambulisha kote kule mke wa felix hakuweza kumpokea vizuri na kulazimika kumwifadhi moja ya vyumba vya stoo.

Alipofika Felix kutoka kazini mkewe alimwambia ujio wa mwanamke mmoja mchafu na waajabu kutokea, na kusema, “eti mama huyo hapa stoo anasema kuwa wewe ni mwanaye.” Felix kwa aibu naye hakumpokea vizuri mama yake, na ndipo ugomvi ulipoanzia. “Kama unasema kuwa wewe ni mama yangu piga mahesabu ya gharama zote ulizonitunza na kunilea nami nitakulipa,” Felix alimwambia mama yake kwa hasiri.

“Naombeni munionyeshe uhani nami nikirudi nitakupa hesabu yangu,” mama yake Felix mjibu Felix. Baada ya muda kidogo mama yake Felix alirudi akiwa amejipaka kinyesi chake mwili mzima na kumwambia Felix, “haya naomba uniogeshe na hii ndiyo gharama yangu kwa siku moja tu katika utoto wako. Kutokana na harufu ile, Felix hakuweza hata kumsogelea Mama yake. Je, Yesu angemlipa nini Mama yake kwa mahangaiko aliyoyapata hadi chini ya msalaba alipokata roho? Yesu anamkabidhi mama yake Kanisa na kusema, “Mama tazama mwanao.”

Tumsifu Yesu Kristo!

Amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi; Na wanyonge amewakweza,” Lk 1:52


Tusali:- Ee Yesu, asante kwa kutupa Mama yako mpenzi na mama yetu. Amina 

No hay comentarios:

Publicar un comentario