JUMANNE
WIKI YA 19 YA MWAKA-C
Somo: Eze 2:8-3:4
Zab: 119:14, 24, 72, 103, 111, 131
Injili: Mt 18:1-5, 10, 12-14
Nukuu
“Bali
wewe, mwanadamu, sikia neno hili ninalokuambia; usiwe wewe mwenye kuasi kama
nyumba ile yenye kuasi; funua kinywa chako, ule nikupacho,” Eze 2:8
“Akalikunjua
mbele yangu; nalo lilikuwa limeandikwa ndani na nje; ndani yake yalikuwa
yameandikwa maombolezo, na vilio, na ole!” Eze 2:10
“Akaniambia,
Mwanadamu, kula uonacho; kula gombo hili, kisha enenda ukaseme na wana wa
Israeli,” Eze 3:1
“Akaniambia, Mwanadamu, lisha tumbo lako, ulijaze tumbo lako
kwa hili gombo nikupalo. Ndipo nikalila, nalo kinywani mwangu lilikuwa tamu,
kama utamu wa asali,” Eze 3:3
“akasema,
Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika
ufalme wa mbinguni,” Mt 18:3
“Basi, ye yote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu,
huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni,” Mt 18:4
“Angalieni msidharau mmojawapo wadogo hawa; kwa maana
nawaambia ya kwamba malaika wao mbinguni siku zote huutazama uso wa Baba yangu
aliye mbinguni,” Mt 18:10
TAFAKARI: “Kuifahamu siri ya Mungu na kutumika vyema kama chombo chake,
yanipasa kujiadabisha na kujinyenyekeza.”
Wapendwa wana wa Mungu, ili tuzame vizuri katika tafakari yetu ya leo,
na hasa somo letu la kwanza ni vyema tungeanza na mstari ule wa nne. Ni dhahiri
leo tunahitaji
viongozi kama Nabii Ezekieli aliyesimama na kusema kweli bila kupepesa macho.
Mungu anasimamia haki za wanyonge wake kwa kuwatumia watu wenye hofu ya Mungu
kama Nabii Ezekieli na kusema: “Na wana hao wana
nyuso zisizo na haya, na mioyo yao ni migumu. Mimi nakutuma kwa hao; nawe
utawaambia, Bwana MUNGU asema hivi. Nao, kwamba watasikia, au kwamba hawataki
kusikia, (maana ndio nyumba ya kuasi hao), hata hivyo watajua ya kuwa nabii
amekuwako miongoni mwao,” Eze 2:4-5
Siri
ya hofu ya Munga aliye nayo Nabii Ezekieli ni tokeo la kulisikia neno la Mungu,
kulipokea, kulitafakari, kulishirikisha, na mwisho akawa shahidi na shuhuda na
neno hili, Eze 2:8; 3:1-3. Na hivi ndivyo Nabii Ezekieli alivyolisikia neno na
kulipokea, “Bali wewe, mwanadamu, sikia
neno hili ninalokuambia; usiwe wewe mwenye kuasi kama nyumba ile yenye kuasi;
funua kinywa chako, ule nikupacho,” Eze 2:8. Ili kulishirikisha neno lile la
Mungu katika kufundisha na kuonya, ilimpasa kulitafakari neno hilo la Mungu kwa
kina. Neno hili ambalo kwalo lipo kwenye
gombo la chuo, Ezekieli anaamuriwa kulila. Kulila neno la Mungu ni kuzama ndani
ya neno hilo na kuwa sehemu yake, kama vile tunavyonawiri kwa kula lishe bora.
Ni ndani ya neno
tunafunuliwa mengi yaliyojificha. Ezekieli “akalikunjua
mbele yangu; nalo lilikuwa limeandikwa ndani na nje; ndani yake yalikuwa
yameandikwa maombolezo, na vilio, na ole!” Eze 2:10. Na hivi ndivyo Mungu
alivyo mwamuru na kumwambia, “Mwanadamu,
kula uonacho; kula gombo hili, kisha enenda ukaseme na wana wa Israeli,” Eze
3:1. Ni pale tunaposhibishwa vizuri na neno la Mungu ndani yetu, Eze 3:2-3a,
ndivyo hivyo tunakuwa imara kulishirikisha neno hili katika kulifundisha na
kuonya.
Tushibishwapo
vizuri na neno la Mungu, neno lile huwa na matokeo mawili. Kwanza kabisa neno
linatupa furaha, katika maana ya utamu wa neno. Na hivi ndivyo ilivyokuwa kwa
nabii Ezekieli. “Ndipo nikalila, nalo kinywani mwangu lilikuwa tamu, kama utamu
wa asali,” Eze 3:3b. Na pili, neno la Mungu linatupa utayari katika maana ya
kulishirikisha neno la Mungu bila woga. Naye Mungu akamwambia Ezekieli, “Mwanadamu, haya! Waendee wana wa Israeli
ukawaambie maneno yangu,” Eze 3:4. Kuifikia hatua hii kwahitaji kujiadabisha kunakoendana na kujinyenyekeza. Wapo viongozi
wengi wenye maona mazuri ila pale wanapokosa tunu hii ya ‘kujiadabisha na
kujinyenyekeza,’ yote waliyo nayo husambaratika.
Ni
ukweli usiopingika kwamba hakuna mwanadamu aliyekamilika. Kila mmoja wetu, na
hata viongozi wetu tulio nao wanamadhaifu yao kama wanadamu. Tatizo kubwa
tulilonalo ni pale tunapohalalisha udhaifu wetu, na kuwasadikisha wale
waliotuweka madarakani kuwa huo ndio mtindo wa maisha. Ni vyema tunapotambua
udhaifu wetu iwe dawa ya kujirekebisha na kufanya vizuri zaidi. Hii ndiyo sifa
mojawapo ya kiongozi, yaani “kujisahihisha.” Na hii ndiyo tunu ya kujiadabisha.
Kiongozi asiyejisahihisha au kujiadabisha, ni hatari sana kwa wale
anaowaongoza. Kama viongozi, katika shughuli zetu si kila mara
mambo yatakwenda vema. Tunaweza kukosea hapa na pale. Basi tuwe tayari
kusahihishwa na kujisahihisha. Tujisahihishe kweli. Tunajifunza kutoka makosa
yetu na ya wenzetu. Zaidi ya hayo tusiyaache makosa yatokee kwa makusudi.
Tujitahidi kuzuia makosa na mapungufu mengine yoyote yasitokee. Tulenge kwenye
ukamilifu ingawa udhaifu upo.
Udhaifu wenye mwono wa
kujisahihisha na kusimama katika kweli, ndiyo Mtume Paulo anauzungumzia kama
“Mwiba.” Mtume Paulo anamwomba Mungu mara tatu amwondolee mwiba huu. Baada ya kulifahamu tatizo lake, Mtume Paulo
anatumia tatizo hilo kujiimarisha zaidi katika kweli. Jibu la tatizo lake ni
UNYENYEKEVU katika kutenda. “Na makusudi
nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nalipewa mwiba katika
mwili, mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi,” 2Kor
12:7. Ndugu yangu, je, unaliona jambo hili ndani yako, na kwa viongozi tulionao
sasa? Tuposhindwa kufanya maamuzi yenye tija na hasa kuanzia kwako na kwangu,
baada ya miaka 50 au 100 ijayo, watu wote wa Taifa hili la Tanzania tutakuwa
watumwa katika nchi yetu wenyewe. Neema na baraka alizotujalia Mungu zitakuwa
sababu ya mateso yetu yasiyokuwa na kikomo.
Wapendwa wana wa Mungu,
mnyenyekevu husimamia haki katika kweli kwa sababu msingi wa fadhila zote ni
unyenyekevu. Mnyenyekevu hawezi kudongoka katika laana ya uovu wo wote. “Laana ya Bwana i katika nyumba ya waovu, Bali
huibariki maskani ya mwenye haki. Hakika
yake huwadharau wenye dharau, Bali huwapa wanyenyekevu neema,” Mit 3:33-34.
Unyenyekevu hutujengea nidhamu ya hali ya juu. Unyenyekevu utupelekea kupokeana
kama tulivyo na kusaidiana kufikia malengo tarajiwa kwa kila mmoja wetu.
Unyenyekevu utufikirisha kabla ya kutenda jambo lo lote katika maisha.
Unyenyekevu hutufanya kuwa watii na wapole hata pale mantiki ya ufahamu wetu
inaposhindwa kukubaliana na ukweli kama ulivyo hasa katika joto la ujana wetu. “Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam,
ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu
huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema,” 1Pet 5:5.
Unyenyekevu wa mtu ni ukweli wa Mungu ndani ya mtu huyo.
Wapendwa wana wa Mungu,
ni katika mtizamo huu tunaweza kuona pale ambapo hapana unyenyekevu binadamu
alijifanyia yake, na Mungu alijiweka pembeni. Kiburi cha mwanadamu ni chukizo
kubwa sana kwa Mungu. Kuishi katika kiburi siyo makusudio ya uumbaji wetu. Wana
wa Israeli wanatambua tatizo hili na kwa vinywa vyao wanasema, “Tumemwasi,
wala hatukuitii sauti ya Bwana Mungu wetu, kwenda katika sheria zake
alizoziweka mbele yetu. Bali tulikwenda kila mtu katika mawazo ya moyo wake
mbaya, kutumikia miungu ya kigeni na kufanya yaliyo maovu machoni pa Bwana
Mungu wetu,” Bar 1: 18, 22. Hakuna neema na baraka pale tunapotawaliwa na
kiburi. Mwenye kiburi ni vigumu sana kujipokea na kuupokea ukweli ambao
hauendani na mfumo mzima wa kufikiri kwake.
Katika
Injili ya leo, Yesu anamfananisha mtu mwenye unyenyekevu kama mtoto. Mtoto
mdogo hana cha kujikuza zaidi ya kuyaona yote na katika yote kwa wazazi wake.
Mtoto huweka uaminifu mkubwa sana kwa wazazi wake. Wazazi wake huwa kila kitu
kwake. Ni katika mtazamo huu Mungu wetu ni kila kitu kwetu. Hatuna cha
kujikweza mbele zake “kwa sababu upumbavu wa Mungu una hekima zaidi ya
wanadamu, na udhaifu wa Mungu una nguvu zaidi ya wanadamu,” 1Kor 1:25. Ni
katika ukweli huu Yesu anawaambia wanafunzi wake maneno haya mazito, “akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa
kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni,” Mt 18:3. Tusipojivua
kujua kwetu kusikokuwa na maana yo yote zaidi ya mbwembe zetu, hatutaweza
kufunuliwa siri za mbinguni.
Unyenyekevu
wenye mfano wa utoto ndio huo unaotufanya wakubwa mbele ya uso wa Mungu. Ukubwa
huo siyo ule wa kufanya tutakayo sisi na kuzirithisha nafsi zetu, bali
kuyafanya yote kadiri ya mpango wa Mungu. Kuujua mpango wa Mungu ni pale tu
unapokuwa tayari kujinyenyekeza mbele zake. Hivyo, “ye
yote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika
ufalme wa mbinguni,” Mt 18:4. Katika ufalme huu wa mbinguni hakuna maguvu ya
kutalawa au kutawaliwa, bali nguvu ya UPENDO wa kweli.
Wapendwa
wana wa Taifa la Mungu, wanyenyekevu wana sauti kubwa sana mbele za Mungu. Mtu
ye yote anayemdharau mtu mnyenyekevu kwa vile anayafanya yote hayo kwa
kujishusha yu na hatia kubwa sana mbele za Mungu. Yesu anatuambia, “Angalieni
msidharau mmojawapo wadogo hawa; kwa maana nawaambia ya kwamba malaika wao
mbinguni siku zote huutazama uso wa Baba yangu aliye mbinguni,” Mt 18:10. Hivyo
tujiadhari sana na jeuri yetu ya pesa, madaraka, umaarufu na kutambulika kwetu
katika jamii, na kutumia hali hizo kama fimbo ya kuchapa wengine. Haya yote
mwisho wa siku hayana msaada wo wote katika umilele wako. “Vivyo hivyo
haipendezi mbele za Baba yenu aliye mbinguni kwamba mmoja wa wadogo hawa
apotee,” Mt 18:14. Hivyo basi, kwa utajiri nilio nao, kwa madaraka niliyo nayo,
kwa umaarufu nilio nao, na kwa kutambulika kwangu katika jamii, iwe sababu na
nguvu ya kuwa sauti ya wasio na sauti.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Angalieni
msidharau mmojawapo wadogo hawa; kwa maana nawaambia ya kwamba malaika wao
mbinguni siku zote huutazama uso wa Baba yangu aliye mbinguni,” Mt 18:10
Tusali:-Ee Bwana
tujalie fadhila ya unyenyekevu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario